- Shirika lisilo la kiserikali la uhifadhi la African Parks limewahamisha faru weupe 70 kutoka Afrika Kusini hadi Hifadhi ya Taifa ya Akagera iliyoko nchini Rwanda.
- Faru hawa ndio wa kwanza kuhamishwa toka taifa moja hadi lingine, chini ya mpango wa African Parks wa Rhino Rewild, ambao unatazamia kusambaza faru 2,000, au hata zaidi, kutoka operesheni ya ufugaji wa kudhibitiwa ambao shirika hilo liliazimia mwaka wa 2023.
- Mwaka 2021, African Parks ilihamisha faru 30 kwenda Akagera. Pia imesema Rwanda itahakikisha faru hao wana makazi salama, yanayoweza kukaliwa na idadi kubwa zaidi – kwa sababu kuna uwezekano wa kuhamisha faru weupe wengine wengi kutoka hapo kwenda Afrika Mashariki na Kati.
Faru weupe 70 wamekamilisha safari yao kwa mafanikio kutoka Afrika Kusini hadi Hifadhi ya Taifa ya Akagera nchini Rwanda. Hii ni mara ya kwanza kwa faru kuhamishwa kimataifa kutoka Platinum Rhino, mradi mkubwa wa ufugaji faru uliopitwa mnada mwaka 2023, baada ya kukumbwa na matatizo ya kifedha kwa miaka mingi. Baada ya kukosa wanunuzi, shirika la African Parks lilinunua eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 7,800, lililopo kilomita 160 kusini mashariki mwa Johannesburg, pamoja na faru wake 2,000 — twiga, pundamilia, na wanyama wengine — kwa kiasi cha fedha ambacho hakikutajwa. Platinum Rhino ilibadilishwa jina na kuitwa Rhino Rewild.
Hii idadi ya faru waliokuwa African Parks inawakilisha takriban asilimia 15 ya idadi ya faru weupe wote duniani (Ceratotherium simum). Mpango wa African Parks wa Rhino Rewild unalenga kuwasambaza wanyama hao kwenye maeneo salama na yenye usimamizi mzuri kote Afrika, ili kuanzisha maeneo mapya ya kuwalinda na kuimarisha idadi ya waliopo tayari.
Mwanzoni, faru 40 walihamishwa kutoka Rhino Rewild hadi Munywana Conservancy, ambayo ni hifadhi binafsi ya wanyamapori iliyoko mkoa wa KwaZulu Natal nchini Afrika Kusini. Hivyo uhamisho huu wa faru 70 kwenda Akagera ulikuwa wa pili.

“Akagera inaweza kuhifadhi idadi kubwa ya faru weupe,” alisema Donovan Jooste, meneja wa mradi wa Rhino Rewilding wa African Parks. “Hii, pamoja na ukweli kwamba Rwanda ni nchi thabiti na serikali yake inaunga mkono kazi zetu, inamaanisha kwamba kundi hili la faru linaweza kuwa na umuhimu sana katika mafanikio ya spishi hii kwa muda mrefu. African Parks ilihamisha faru 30 kwenda Akagera mwaka 2021, ambao tunafurahi kuongezeka kwao. Tunapata faraja kujua faru hawa wana uwezo wa kustawi hapa. Eneo la Rwanda katika bara la Afrika ni muafaka kwa upanuzi wa baadaye wa idadi ya faru weupe kuelekea Afrika Mashariki na Kati.”
Dave Balfour, mtaalam huru na kiongozi wa Kundi la Wataalam wa Faru wa Afrika katika IUCN, mamlaka ya kimataifa ya uhifadhi wa wanyamapori na ambaye si sehemu ya Mpango wa Rhino Rewild, anasema: “Ingawa uhifadhi unahitaji faru wawe salama, kuna mambo mengi zaidi ya kuzingatia wakati uhamishaji unapopangwa.
“Uhamisho wa faru weupe wa kusini hadi Hifadhi ya Taifa ya Akagera unabadili uzoevu wao na eneo lao la kihistoria la hivi karibuni. Ingawa wanaweza kuepuka tisho la ujangili, kuna hatari nyingine ambazo zinatulazimisha kuwa waangalifu,” alisema Balfour. “Mifano ya hatari ni kama vile athari mbaya kwenye makazi wanakopokelewa, kukabiliwa na magonjwa yasiyozoeleka, au faru kushindwa kuzoea mazingira mapya.”
Uhamisho una changamoto, na unaweza kusababisha vifo. Mnamo Mei 2018, faru wanne kati ya sita waliokuwa katika hatari kubwa ya kutoweka (Diceros bicornis), na ambao African Parks waliwahamisha kutoka Afrika Kusini kwenda Hifadhi ya Taifa ya Zakouma nchini Chad, walishindwa kuzoea kula mimea katika makazi yao mapya na mwishowe wakafa.


Uhamisho wa hivi karibuni ulifanywa kwa hatua mbili, kila moja ikihusisha faru 35. Kundi la kwanza lilianza kusafiri Juni 4, huku lile la pili likisafirishwa kuanzia Juni 7, na kufuatiliwa mfululizo na timu za mifugo. Hapo awali faru hao walihamishwa kutoka eneo la Rhino Rewild hadi Munywana ili kuwatayarisha kwa kuhimili magonjwa ya asili, na hali ya hewa, kabla ya wao kupelekwa Akagera. Safari yao ya mwisho ya kilomita 3,400 (maili 2,100) kwa kila kundi ilichukua siku mbili.
Walibebwa kwenye lori kutoka Munywana hadi Durban, kisha wakasafirishwa kwa ndege hadi Kigali, mji mkuu wa Rwanda, kabla ya kupelekwa Akagera kupitia barabarani.
Kuhamishwa kwa faru hao kulikuwa kilele cha miezi kadhaa iliyozingatia upangaji na ushirikiano kati ya Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB), African Parks na Munywana Conservancy.
“Tuna uhakika faru hawa watazoea makazi yao mapya Akagera,” Jooste alisema. “Kama ilivyo kawaida katika uhamishaji wa wanyama na hatua za usimamizi, hatari haziwezi kukosa. Hata hivyo tuna taratibu za kupunguza hatari, na pia tutakuwa tukifuatilia ustawi wa kila mnyama mara kwa mara.”
Uhamishaji wa wanyamapori kutoka Rhino Rewild utaendelea mwaka huu na miaka ijayo. Kwa sasa, mpango wa Rhino Rewild umebaki kusherehekea hatua hii muhimu.
Jooste alisema: “Tunafurahia hii hatua na kuiona kama fursa kubwa ya kulinda mustakabali wa faru weupe. Ni mchakato mgumu, lakini yote yatafaa faru watakapokuwa salama na kustawi kule Akagera.”
Picha ya bango: Uhamishaji wa faru weupe kutoka hifadhi moja hadi nyingine, licha ya kuwa mchakato mgumu, unachukuliwa kuwa fursa muhimu ya kulinda mustakabali wa wanyama hao.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya kiingereza mnamo tarehe 10/06/2025.