- Kenya inafikiria kujenga kiwanda cha nishati ya nyuklia katika Kaunti ya Kilifi, kwenye pwani ya nchi hiyo, eneo linalopakana sana na mikoko ya Mida Creek, Hifadhi ya Msitu wa Arabuko Sokoke na Hifadhi ya Bahari ya Taifa ya Watamu, maeneo ambayo yanatambulika kwa wingi wa bayoanuwai, zikiwemo spishi asilia na miamba ya matumbawe.
- Tayari wataalamu wameonya kuwa mfumo huo wa kupooza mitambo una uwezo wa kuzidisha joto majini, na kuathiri vibaya viumbe wa baharini, licha ya kusababisha kuendelea kwa ufifiaji wa matumbawe na uvurugaji wa planktoni, na spishi nyingine muhimu. Wanasema jambo hili litaathiri mlolongo mzima wa chakula kwa muda mrefu.
- Wakazi na wanaharakati wa mazingira hayo, mmojawao akiwa mwanabiolojia wa baharini Peter Musila, wameilaumu serikali kwa kutohakikisha uwepo wa mawasiliano ya kutosha kuhusu mradi huo, kwa kutoshauriana na umma kikamilifu, au hata kutoa taarifa kuhusu jinsi taka za nyuklia zitakavyoshughulikiwa.
- Musila anasema Kenya haihitaji nishati ya nyuklia, kwa kuwa tayari ina rasilmali nyingi ya nishati jadidifu. Kwa maoni yake, mradi huu wa nyuklia utazua wasiwasi kuhusu vitisho kama vile ajali zinazoweza kutokea, athari za muda mrefu kwa ikolojia na upotezaji wa riziki kwa jamii za wenyeji.
Kenya iko katika mchakato wa kujenga kituo chake cha kwanza kabisa cha nishati ya nyuklia. Kwa mujibu wa makadirio ya Shirika la Nguvu za Nyuklia na Nishati la Kenya (NuPEA), ujenzi unatarajiwa kuanza ifikapo mwaka 2027 na kituo hicho kitazalisha megawati 1,000 za umeme. Mji wa Uyombo, ulioko katika kaunti ya Kilifi, pwani ya Kenya, ni moja ya maeneo matatu yanayofikiriwa na NuPEA kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho. Lakini tayari kuna pingamizi. Wananchi wakijitokeza kwa sauti moja na kusema kuwa hawataki umeme ya nyuklia. Walisema, “Sitaki Nuclear”. Maandamano yalizuka kabla ya kesi ya kisheria kuwasilishwa mahakamani na wananchi hao. Kesi hiyo ilitupiliwa mbali. Ombi la mtandaoni pia halikufaulu kukomesha mradi huo, kwa kuwa unaendelea mbele, jambo ambalo linawatia wasiwasi wakazi na baadhi ya wanaharakati wa mazingira nchini Kenya.
Kijiji cha Uyombo kimezungukwa na mikoko ya Mida Creek, na kiko umbali wa kilomita chache tu kutoka Hifadhi ya Msitu wa Arabuko Sokoke – msitu mkubwa zaidi wa pwani uliosalia Afrika Mashariki, na ambao unatambulika kama kitovu cha bioanuai nchini, kwa sababu ya wingi wa spishi asilia na upotevu wa makazi ya viumbe kwingineko. Uyombo pia imepakana na Hifadhi ya Bahari ya Taifa ya Watamu, ambayo inatambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kama Hifadhi ya Biosfera (Biosphere Reserve) ikizingatiwa kwamba ina miamba ya matumbawe na wingi wa viumbe wa baharini, kama vile papa wakubwa nyangumi (Rhincodon typus) na samaki wakubwa aina ya manta (Manta alfredi).
Je, mradi huu unaweza kuwa na athari gani kwa bioanuai? Mwanabiolojia wa masuala ya baharini na mratibu wa programu katika shirika lisilo la kiserikali la A Rocha Kenya, Peter Musila, anasema anafuatilia hali ya matumbawe ya eneo hilo, huku akishiriki kwenye juhudi za kuyarejesha. Kama mtaalamu wa matumbawe, Musila hafurahishwi na mipango ya serikali ya kujenga kituo cha nyuklia.
Mongabay ilikutana naye mjini Watamu, na kumhoji.

Mongabay: Uliposikia kwamba kituo cha nishati ya nyuklia kitajengwa Uyombo, ulipata hisia gani?
Peter Musila: Nilisikia kwa mara ya kwanza kuhusu ujenzi wa kiwanda hiki mwaka 2022. Kwangu, jambo hili halina maana kwa sababu eneo wanalopanga kutumia kuweka kiwanda hiki ni eneo safi mno na la asili lenye wanyamapori wa aina nyingi, wakiwemo wale wa nchi kavu na hata ndege. Mida Creek ni eneo muhimu sana kwa ndege, hasa wale wa kuhama, na wanaokuja hapa kuzaliana. Hapa ndani kuna viumbe wengi mno.
Eneo hilo pia ni la muhimu sana kwa wanyama wa baharini kama vile pomboo, nyangumi, papa na samaki wakubwa wa “rays.” Wote hao hutumia eneo hili kuzaliana na kutaga mayai. Hatutaki kiwanda cha nyuklia katika eneo letu.
Mongabay: Kama ulivyosema kuwa eneo hili la bahari ni muhimu, kwani linawapa makao mamalia. Je hali ya matumbawe iko vipi kwa sasa?
Peter Musila: Kabla ya miaka ya 1990, miamba ya matumbawe ilikuwa safi na ya kupendeza, ingawa sikuiona kwa macho yangu. Kwa wakati mmoja kulikuwa na zaidi ya familia 200 za matumbawe. Tatizo lililoathiri eneo hili zaidi ni kufifia kwa matumbawe (bleaching). Mara ya kwanza tukio hili kutokea ilikuwa mwaka 1997. Baada ya hapo matumbawe yalipungua kwa kiwango kikubwa. Yalikuwa yamehifadhiwa kwa asilimia 60 kabla ya hapo, lakini ilipofika 1998, yaliporomoka hadi asilimia 10 tu. Jambo hili lilikuwa baya. Tangu hapo yamejaribu kupona, lakini pia yameendelea kufifia kila uchao, hasa miaka ya 2005, 2007, 2013, 2016, na 2020.
Mwaka 2024 tulishuhudiwa tukio lingine kubwa la kufifia kwa matumbawe. Tukio hilo lilikuwa baya kama lile la mwaka 1997. Ingawa ufunikaji wa matumbawe yaliyosalia kwenye laguni bado uko chini, kuna matumaini, kwani matumbawe mengi yanaonyesha uimara na uwezo wa kuhimili changamoto.
Hali hii imechangiwa na sababu nyingi ambazo zikijumlishwa huleta tatizo kubwa zaidi. Chanzo kikubwa ni kuongezeka kwa joto majini – jambo linalosababishwa na ongezeko la joto duniani. Tatizo hili haliwezi kutatuliwa kwa hatua za ndani pekee. Sababu nyingine ni ubora wa maji kutokana na virutubisho vinavyotiririka kutoka maeneo jirani. Kwa sasa miji mingi na hoteli zinazoibuka zinaathiri ubora wa maji.
Lengo kubwa ni kupunguza changamoto za ndani ili kuhakikisha zile za kimataifa hazileti madhara makubwa.
Mongabay: Kwanini NuPEA inataka kujenga kiwanda karibu na Bahari ya Hindi? Na kitakuwa na athari gani kwa matumbawe?
Peter Musila: Mimi nilisoma kwenye nyaraka zao kuwa mtambo unahitaji maji baridi. Hii ndio sababu wamechagua Uyombo. Mradi huu pia unahitaji maji mengi sana. Hayo maji yatatumika kupooza reaktori, na hayo yanaweza kuwa na madhara makubwa. Nina uhakika yataongeza joto la maji. Maji yanaporudishwa baharini baada ya kutumika, yatakuwa na joto kali, kuliko vile yalivyotolewa humo. Bila shaka hii itapandisha joto la maji baharini na kuathiri matumbawe zaidi. Yanaweza kufifia zaidi. Hili linanifanya nijiulize: ‘Kuna haja gani tena ya kulinda eneo hili?’
Isitoshe, maji yanayovutwa huja na viumbe wadogo wengi sana – planktoni – ambao hawawezi kuonekana kwa macho tu, lakini huwa muhimu sana kwa wanyama wakubwa kama papa nyangumi. Kila wanapovutwa na kuingizwa kwenye reaktori, hawawezi kuishi tena. Hali hii inanihuzunisha mno.

Tayari nimewasilisha ripoti. Kuna timu ambayo inatengeneza vipeperushi kueleza umma athari zinazoweza kujitokeza. Pia kuna ripoti zingine nyingi, hadi serikalini na bungeni.
Licha ya hayo, nimeshiriki katika kuripoti aina za bioanuai zilizopo, na jinsi ambavyo zitaathiriwa, na kwa nini siyo chaguo bora kwao kuutekeleza mradi wa kujenga kituo cha nyuklia. Hizi taarifa zote ziko mtandaoni, lakini serikali imeziba masikio. Kuna makundi mbalimbali, makundi ya uhamasishaji, na hata makundi ya WhatsApp katika jamii. Taarifa nzito.
Mongabay: Matumbawe yana umuhimu gani kwa mfumo wa ikolojia?
Peter Musila: Kwa kawaida miamba ya matumbawe haithaminiwi ipasavyo. Wengi hawajaelewa umuhimu wake. Lakini bila matumbawe, hakutakuwa na uhai duniani. Ni mfumo muhimu sana, kwani unabeba bayoanuwai nyingi. Kote ulimwenguni, miamba ya matumbawe huwa inabeba zaidi ya asilimia 25 ya bayoanuwai zote zilizo baharini, ilhali yenyewe ni chini ya asilimia moja ya bahari. Jambo hili pekee linaonyesha umuhimu wake.
Zaidi ya hayo, matumbawe yana thamani ya kiuchumi, kwa sababu yanatoa chakula kwa jamii za pwani, pamoja na kipato kupitia shughuli za utalii. Aidha, matumbawe hulinda jamii kutokana na mawimbi makubwa ya bahari. Bila matumbawe, hali ya dunia ingekuwa tofauti zaidi.
Mongabay: Mwezi Januari mwaka 2023, NuPEA ilitoa rasimu ya tathmini ya kimkakati ya mazingira na kijamii (SESA). Lengo lilikuwa kushughulikia masuala ya usimamizi wa mazingira na kijamii yanayohusu mpango wa nyuklia. Uliichukulia vipi ripoti hiyo?
Peter Musila: Tuliiangalia kwa makini, na kugundua kuwa ilikuwa na makosa mengi. Walipunguza uhalisia wa madhara kabisa. Walipaka sukari mambo mabaya. Lakini ilipitiwa upya na Tume ya Uholanzi ya Tathmini ya Mazingira. Sina uhakika kama serikali imezingatia maoni hayo. Wamekuwa wakipiga danadana bila kuwaeleza wananchi ukweli kuhusu umuhimu wa kiwanda cha nyuklia.
Licha ya hayo, elimu kwa umma haijatolewa vya kutosha. Na bado wananchi wanasukumiwa mradi huu bila kuambiwa taka zitatupwa wapi, nani atazisimamia, na atafanya hivyo kwa njia gani. Huu ukosefu wa uwazi unasababisha kutokuaminiana, na utazidisha upinzani.
Mongabay: Hadi sasa, ni rasimu tu ya tathmini ya kimazingira na kijamii (SESA) ndiyo ipo kwenye tovuti ya NuPEA. Uwazi wa jinsi taka za nyuklia zitakavyosimamiwa haujadhihirika, isipokuwa tu imetaja kwamba itazingatia mapendekezo ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Nyuklia (IAEA). Una mawazo gani kuhusu hili?
Peter Musila: Tatizo kubwa limekuwa mawasiliano hafifu. Hadi sasa hawajaeleza jinsi taka hatari zitakavyotupwa, na wapi hasa. Wamewahi kusema kuwa zitapelekwa angani – ambalo si jambo la maana. Wakati mwingine wamependekeza kuchimbiwa kwa taka hizo kwenye eneo la Turkana. Jamii wanafaa kujulishwa mambo haya mapema. Wananchi wanapaswa kufahamu aina ya taka zinazozalishwa na mchakato mzima kabla ya kuafiki chochote.
Kwa kuzingatia gharama ya mradi na pato litakalotokana nao, ukilinganisha na vyanzo vya nishati jadidifu vilivyopo, kiwanda cha nyuklia hakitaleta faida.

Mongabay: Ajali ikitokea kwenye kiwanda hiki, unadhani athari zitakuwaje?
Peter Musila: Hata sitaki kufikiria jambo hilo. Kuvuja kwa taka za nyuklia kunaweza kuwa janga kubwa, kwani eneo hili ni muhimu sana kwa viumbe wote, kuanzia ndege, nyangumi, papa, samaki, matumbawe na jamii. Madhara kama hayo yanaweza kuwa makubwa mno.
Unakumbuka tukio la Fukushima? Je likitokea hapa hali itakuwaje? Linaweza kuwa sawa na mauaji ya kimbari. Taka za nyuklia zikiingia majini, mlolongo mzima wa chakula utaathirika – kuanzia planktoni hadi papa na nyangumi, na hatimaye wanaokula samaki.
Hata lijengwe kwa viwango vya juu, bado lina uwezo wa kuharibika. Kwingineko duniani, nchi kubwa zimeacha kutegemea nyuklia kwa sababu si nishati endelevu. Kwa sasa hatuwezi kuelewa kwa nini Kenya inazingatia mradi huo, ilhali kuna teknolojia zingine rahisi na endelevu za kuzalisha nishati.
Picha ya bango: Wanawake wakipanda mikoko Uyombo. Picha na: Elodie Toto wa Mongabay.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 29/08/2025