- Mpango kuanzisha mashamba ya msituni na kuboresha maisha Kenya (PELIS)unaruhusu jamii kulima mashamba katika ardhi kubwa huku wakisaidia kupanda tena miti, ikilenga kuongeza uoto wa miti na kuimarisha kipato vijijini.
- Mfumo huu, ambao umechukua nafasi ya mpango wa shamba, umeonyesha matokeo mchanganyiko: kuongeza uhai wa miche na ushirikiano wa jamii katika baadhi ya maeneo, lakini pia umechochea rushwa, uvamizi wa ardhi na upotevu wa bioanuai pale inaposimamiwa vibaya.
- Wakosoaji, hasa vikundi vya Wenyeji asili kama Ogiek, wanabishana (PELIS) inaondoa misitu ya asili yenye aina nyingi na kuweka mashamba ya miti ya aina moja ya kigeni, jambo ambalo linaharibu mifumo ikolojia na kudhoofisha maisha ya asili ya misitu.
- Licha ya kusimamishwa kazi hapo awali, Rais William Ruto alifufua mpango wa PELIS mwaka wa 2022 ili kuunga mkono lengo kuu la Kenya la kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032, na hivyo kuzidisha mjadala kuhusu iwapo misitu ya mashambani inaweza kuchukua nafasi ya urejeshaji wa misitu asilia.
KAKAMEGA, Kenya — Msitu wa mvua wa kitropiki ulienea mashariki kutoka Bonde la Kongo hadi eneo ambalo sasa ni magharibi mwa Kenya. Hayo karibu yote yamepita sasa, ingawa bado kuna miti mingi ya kuonekana karibu na kitongoji cha Turbo, kaunti ya Kakamega. Mji uko kwenye ukingo wa Hifadhi ya Msitu wa Nzoia, hekta 5,000 (Takriban ekari 12,400) wa miti aina moja ya kigeni ya mikaratusi na misonobari.
Kwa miaka 20 iliyopita, wakati Kenya ikihangaika na jinsi ya kupunguza na kurejesha nyuma upotevu wa haraka wa miti, swali finyu la jinsi ya kudhibiti mashamba mengi ya mbao nchini limejitokeza katika mfumo unaolenga kuboresha maisha, unaojulikana kama Plantation Establishment and Livelihood Improvement Scheme, au PELIS. Mpango huo umesifiwa na kulaaniwa, ukichukuliwa na baadhi ya watu kama njia bora na ya gharama nafuu ya kupanua wigo wa miti huku ikichangia mapato ya ndani na uwekezaji wa jamii katika kulinda misitu; na kukosolewa vikali na wengine kwa kuhimiza ufisadi, kuwezesha uvamizi wa mashamba kwenye ardhi yenye misitu, na kupunguza bioanuai.

Ukianzishwa mwaka 2007, mpango wa PELIS ni mrithi wa mfumo wa shamba, ambao uliwapa Wakenya wanaoishi karibu na mashamba ya miti mashamba madogo ya kulima katika sehemu za hifadhi za misitu ambazo zilihitaji kupandwa tena baada ya miti kuvunwa au kuharibiwa na moto. Wakulima walitakiwa kupanda miche ya miti katikati ya mazao waliyolima kwa matumizi yao wenyewe, kutunza miche hadi ilipokuwa mirefu ya kutosha kutengeneza dari, na kuondoka kwenye mashamba, na kuacha miti kufikia ukomavu.
Lakini mfumo huu ulikosa mfumo wa utawala ulio wazi na hivyo kusababisha matumizi mabaya na Maofisa wa Huduma ya Misitu ya Kenya (KFS) pamoja na watu wenye uhusiano mzuri na wanasiasa wenye ushawishi, kujinyakulia maeneo makubwa ya ardhi – wakati mwingine kuwalazimu wakulima wa eneo hilo ambao waliokuwa wamepewa mashamba kufanya bila malipo kwenye ardhi ambayo maafisa mafisadi walikuwa wamejimilikisha.
Katika hali nyingi, wakulima wa mfumo wa mashamba walibaki kwenye mashamba ya miti muda mrefu hata baada ya muda wao wa kuondoka kupisha ukuaji wa miti kwisha. Wanamazingira, wakikumbuka kwamba mashamba haya ya mbao hapo awali yaliwahi misitu ya mvua ya kitropiki iliyojaa mimea ya kiasili na wanyama, walikosoa zaidi mfumo huo wa ukuzaji miti ya kigeni. Mikalatusi inayokua kwa haraka (Eucalyptus globulus na E. saligna), misonobari ya kulia (Pinus patula) na miberoshi ya Mexico (Cupressus lusitanica) ni ya thamani kibiashara, lakini hutoa makazi haba kwa wanyamapori wa asilia huku ikipunguza uwezo wa mazingira kuhifadhi maji.


Mpango wa PELIS ulianzishwa kushughulikia uwajibikaji katika matumizi na ugawaji wa ardhi kwa kuyakabidhi majukumu hayo kwa mashirika ya jamii ya usimamizi wa misitu, (CFAs), vilivyosajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Misitu ya Kenya ya mwaka 2005. Chini ya mpango huo, vyama vya jamii CFA katika eneo husika, huhakikisha kwamba ni kiwango kilichowekwa tu cha ardhi kinagawiwa kwa wanajamii wanaostahili na walio karibu na mashamba. Kadhalika huhakikisha wakulima wanafuata utaratibu uliokubaliwa: katika mwaka wa kwanza, wanachama wa CFA wanapanda mazao; katika mwaka wa pili, wanapanda miche ambayo wataitunza kwa muda wa miaka miwili ijayo pamoja na kuendesha kilimo chao cha msimu, na baada ya hapo wanalazimika kuondoka eneo hilo ili miti ikue.
Shirika la KFS pia limechapisha miongozo ya kina ya utendaji kazi kwa maafisa ugani wake.
“Mpango wa PELIS [unakidhi] malengo pacha ya kuongeza misitu ya mashamba makubwa na kuboresha maisha ya jamii za vijijini zinazoishi karibu na misitu,” anasema , Naibu Mhifadhi Mkuu wa Mashamba ya Misitu nchini Kenya. Anthony Musyoka, Alisema mfumo huo umeboresha viwango vya kuishi kwa miche ya miti kati ya asilimia 75 hadi 80, ikilinganishwa na asilimia 40 tu kwa maeneo yaliyopandwa tena kwa njia nyingine.
“Kupitia mfumo wa PELIS, kumekuwa na uboreshaji wa ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa jamii za vijijini, jambo linaodhihirishwa na kupungua kwa umaskini na migogoro,” aliiambia Mongabay.

Waangalizi wengine wameelekeza mahali ambapo mfumo wa PELIS umeleta matokeo yaliyotarajiwa. Mradi wa kurejesha mandhari ya msitu wa WWF-K uitwao BENGO ulishirikiana na shirika la KFS mwaka wa 2021 kutekeleza mpango wa PELIS katika eneo la hifadhi ya mbao lililotangazwa rasmi katika eneo la Aberdare Range, eneo linalokumbwa na moto, malisho ya mifugo na viwango vya chini vya maisha ya miti iliyopandwa upya, hasa miche ya asili ya Juniperus procera, katika eneo la Kinangop Kusini.
Kulingana na muhtasari wa WWF-K, mpango wa PELIS ulitoa mfumo muhimu wa kujenga uaminifu kati ya wanajamii, miungano ya CFA ya eneo hilo na shirika la huduma ya misitu kufanya kazi pamoja ili kupunguza uharibifu wa mashamba ya mbao na kusimamia vyema miti mipya iliyopandwa. Shirika la WWF-K lilisema mafanikio ya mpango huo katika mazingira yoyote yanatokana na kuwasiliana kwa uwazi masharti ya kubadilishana – upatikanaji wa ardhi kwa muda kwa malipo ya ulinzi wa jumla wa shamba na kusaidia kurejesha miti – ili shughuli zote katika msitu ziwiane na malengo ya mpango huo.
Lakini miaka mitano tu baada ya kuanzishwa kwake, mpango wa PELIS ulisimamishwa katika mashamba mengi kutokana na wasiwasi wa mashirika ya kijamii kwamba wakulima, hasa wa sehemu ya magharibi mwa Kenya, walikuwa hawazingatii sheria, na walipanda mazao kama mahindi, ambayo yalifunika miche ya miti michanga, na hivyo kupunguza nafasi zao za kuishi. (Mpango huu uliruhusiwa kuendelea katika maeneo yanayokuza viazi kama vile Nyanda za Juu na Kaskazini mwa Bonde, ambako Taasisi ya Utafiti wa Misitu ya Kenya ilirekodi viwango vya maisha vya asilimia 75 kwa miti iliyopandwa mseto na viazi.)
Swali la kimazingira kuhusu namna mpango huo unavyofanya kazi, hasa unapoendeshwa kama ilivyokusudiwa, lilirejeshwa wakati Rais wa Kenya William Ruto aliporuhusu kuendelea kwa mpango wa PELIS mwaka 2022, akisema mpango huo unaweza kuchangia mpango wa kitaifa unaolenga kupanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka 2032.
Mpango wa Rais Ruto, unaolenga kufikia asilimia 30 ya miti katika muongo mmoja, hautofautishi kati ya urejeshwaji wa misitu, misitu asili, na upanuzi wa aina nyingine za miti.
Kuondolewa kwa zuio hilo kunakumbusha hatua muhimu ya kihistoria katika usimamizi wa misitu nchini Kenya, alisema Dominic Walubengo, mtaalamu wa Kenya katika utawala na usimamizi wa misitu: kukamilika kwa reli inayounganisha bandari ya Bahari ya Hindi ya Mombasa na mji wa Kisumu kwenye Ziwa Victoria mwaka 1901.

“Injini za mvuke zilihitaji kuni nyingi kuendesha, na kusababisha uharibifu wa misitu ya asili,” Walubengo alisema. “Mwaka 1910, serikali ya kikoloni [ya Uingereza] ilipitisha sheria ambayo ililipa Shirika la Reli la Kenya umiliki wa angalau kilomita 5 [maili 3] za ardhi upande wa njia ya reli, ambapo miti ya asili ilikatwa na mahali pake pamewekwa aina za miti ya kigeni inayokua kwa kasi kama vile Eucalyptus globulus na Eucalyptus saligna.”
Kwa ghafla, watu waliokuwa wakiishi katika misitu iliyotengwa kwa ajili ya reli walifukuzwa wakiwa wamenyooshewa bunduki. Mwaka 1942, serikali ya kikoloni ilikwenda mbali zaidi, ikitangaza kwamba misitu yote na mashamba ya miti ni mali ya serikali, na hivyo kufanya kuwa kosa la jinai kwa Waafrika kutumia mazao yoyote ya misitu. Baada ya Vita Kuu Pili ya Dunia, maveterani wa Uingereza walialikwa kuishi kwenye maeneo makubwa ya misitu; wengi wa walowezi hawa waliikata miti ya asili kwa ajili ya mbao za thamani kwa ajili ya kuuza nje, na badala yake wakaipanda miti ya kigeni inayokua haraka au mazao ya msimu, hasa mahindi na ngano.
Tamko hili, ambalo lilirithiwa na serikali ya ukoloni, limesalia kuwa mwiba kwa jamii za wenyeji ambao maisha yao, riziki na tamaduni zao zilitegemea misitu, kama vile misitu ya Ogiek ya Mau na msitu wa Mlima Elgon.
Idara ya Misitu enzi za ukoloni ilikuwa imeanzisha upandaji wa miti mingine inayokua kwa kasi, hasa misonobari na miboreshi ya Mexico, ambayo, pamoja na mikaratusi, bado ndiyo spishi kuu zinazopandwa na Huduma ya Misitu ya Kenya ya leo.
“Hiyo ilikuwa mwanzo wa misitu iliyopandwa nchini Kenya,” alisema Walubengo, ambaye shahada yake ya uzamivu, yaani Ph.D., ilichunguza historia ya misitu nchini Kenya.

Kulingana na Mpango wa Clearing House (CHM), jukwaa la serikali la kubadilishana taarifa za Mkataba wa Biolojia Anuai, karibu hekta milioni 4.5 (ekari milioni 11), au asilimia 7.8 ya eneo la ardhi la Kenya, limefunikwa na miti. Hii inajumuisha eneo lote la misitu ya asili na eneo lililopandwa kama vile mashamba ya miti ya kibiashara. Misitu ya kiasili iliyofungwa dari hufunika takriban hekta milioni 1.24 (ekari milioni 3.1); mashamba makubwa ya biashara ya umma hufanya karibu hekta 152,000 (ekari 375,600).
Naibu Mhifadhi Mkuu wa shirika la KFS wa Mashamba ya Misitu Anthony Musyoka, anasema vituo 85 vya misitu kote nchini vinatekeleza mpango wa PELIS katika eneo la jumla la hekta 6,224 (ekari 15,380), na hii inatarajiwa kuongezeka katika miaka ijayo.
“Katika miaka miwili tu, zaidi ya hekta 8,000 [kama ekari 20,000] za mashamba zimeanzishwa kupitia mpango wa PELIS, hivyo kusaidia shirika la KFS kupunguza mrundikano wa upandaji pamoja na kuanzisha upya mashamba ya kibiashara katika maeneo yaliyokatwakatwa,” Musyoka alisema.
Baada ya kupata uhuru kutoka kwa Waingereza mwaka 1963, serikali ya Kenya ilidumisha udhibiti wa ardhi yote yenye misitu, lakini hivi karibuni ilibaini kuwa usimamizi wa mashamba umekuwa mzigo. Majibu yake yalikuwa kuanzisha mfumo wa shamba, ambao ulilenga kupunguza gharama ya kupanda upya maeneo yaliyovunwa au yaliyoharibiwa na kuhusisha jamii zilizo karibu kufanya hivyo ili kubadilishana na upatikanaji wa ardhi kwa muda ya kulima mazo katika maeneo hayo.
“Nilikuwa mmoja wa walengwa wa kwanza wa mfumo huu wa kilimo kisicho cha wakazi,” Walubengo alisema.
Aliendelea kuwa mtu mashuhuri katika siasa za usimamizi wa misitu nchini Kenya, ikiwa ni pamoja na kuandaa Sheria ya Misitu ya mwaka 2005. Walubengo pia ni mbunifu wa Mpango wa PELIS ulioondoa mfumo wa shamba.

Wilfred Mulindi ni mwenyekiti wa chama cha msitu wa jamii cha Nzoia, ambacho huwaleta pamoja wakulima 965 kutoka jamii zinazozunguka shamba hilo. Alisema mpango wa PELIS ni rasilimali muhimu sana kwa jamii nzima.
“Tunaelewa umuhimu wa bayoanuwai, lakini kwa mpango wa PELIS, wanachama wanaweza kupata riziki, ambayo inawapa sababu ya kulinda shamba dhidi ya ukataji miti ovyo na moto wa nyika miongoni mwa changamoto nyingine,” aliiambia Mongabay.
Kwa sasa hifadhi hiyo inasimamiwa na shirika la KFS tawi la Kaunti ya Kakamega kwa ushirikiano na mashirika ya jamii ya CFA ya eneo hilo. Mtandao wa barabara unapita katikati yay mashamba hayo, kupitia safu nadhifu ya miti na mashamba ya kilimo katika vitalu. Wanyamapori wengi wanaoweza kuzoea kuishi katikati ya miti ya kigeni, na ambao ni wakubwa kiasi sha kuonekana kwa urahisi, wamefukuzwa kutoka kwenye mfumo huu wa ikolojia uliokuwa umestawi hapo awali; Nzoia leo hii ni mandhari ya kibiashara.
Nchini Kenya kote, kuna mashirika ya kijamii ya CFA 233 yaliosajiliwa yanayoshiriki katika mpango wa PELIS. Musyoka alisema makazi 200,000 yanafanya kazi katika eneo la jumla la hekta 6,000 (karibu ekari 15,000).
Iwapo maswali ya utawala na ufisadi yameshatatuliwa, lakini swali la kuendelea na mradi ulioanza na reli ya enzi ya ukoloni – ya kupanda tena spishi za kigeni maeneo ambayo kulikuwa na misitu ya asili – halijapatiwa majibu. Kama mkuu wa Mtandao wa Shughuli za Misitu (FAN), Walubengo alishirikiana na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel na mwanzilishi wa Green Belt Movement, hayati Wangari Maathai, kupinga unyanyasaji wa mfumo wa shamba pamoja na athari za bioanuai za upandaji wake uliowekwa wa spishi za kigeni.
Walubengo alikiri kwamba mpango wa PELIS unalenga kupanda tena miti ya kigeni inayokua kwa kasi ili kuzalisha mbao, ambazo zinapokoma huuzwa kwa kampuni ambazo lazima zipate leseni kutoka kwenye ofisi ya mkurugenzi wa shirika la KFS ili kuvuna mbao katika misitu iliyoteuliwa.
Mradi wa pamoja wa shirika lisilo la kiserikali la WWF-Kenya na shirika la serikali la KFS huko Kinangop Kusini, wa kurejesha hekta 22,000 (ekari 54,400) ambazo ziliathiriwa na ukataji miti haramu, uvamizi na moto wa mwituni, ulifanikisha kupandwa kwa spishi kama vile misanduku, misonobari na mikaratusi. Mradi huo pia ulijaribu kuchanganya miti ya asili ya mireteni ya Kiafrika, lakini aina hiyo haikufanya kazi vyema kama ilivyotarajiwa.

Msitu Nzoia, ambako mashirika ya jamii CFA ya Mulindi yanalima mahindi na maharage karibu na miche michanga ya misonobari na misanduku, ulikuwa msitu wa asili katika enzi ya kabla ya ukoloni, uliofunikwa na spishi asilia zinazofanana na zile zilizosalia katika Msitu wa Kakamega ulio karibu. Kaunti ya Kakamega imeathiriwa na uvamizi, ikiwa ni pamoja na tukio la mwaka 1985, ambapo makazi kadhaa yalihamishwa kutoka ardhi ya mababu zao katika kaunti ya Vihiga hadi Kaunti ya Kakamega ili kutoa nafasi kwa ujenzi wa makao makuu ya kaunti.
Kesi za ukataji haramu wa miti ya asili pia zimeripotiwa, lakini msitu unabaki na sifa nyingi za miaka 100 iliyopita: kuna aina mbalimbali za miti zinazozalisha mwavuli wa tabaka nyingi na safu nene ya vichaka, wapandaji miti na nyasi. Msitu uliobakia ni makazi ya aina ya ndege wa kipekee kama vile Ansorge’s greenbul (Eurillas ansorgei), (Merops muelleri), Chapin’s flycatcher (Fraseria lendu) na Turner’s eremomela (Eremomela turneri).
Kilomita 36 (maili 22) kaskazini, kuna bioanuai hii kidogo katika mistari iliyopangwa ya miti ya mbao zilizopandwa huko Nzoia, na hakuna hadithi ya chini ya kuzungumzia, zaidi ya mazao ya wakulima katika sehemu zinazopandikizwa na mpango wa PELIS.
Hata ilipogubikwa na ufisadi, jamii nyingi zinazoishi karibu na hifadhi za misitu ya miti ya mbao ambako ziliendesha shughuli zake zilifurahia upatikanaji wa ardhi iliyotolewa. Miongoni mwa tofauti hizo kulikuwa na jamii zinazoishi msituni kama vile Sengwer na Ogiek, ambao hawana shauku na mpango wa PELIS .
“Kama jamii ya asili ya wenyeji, tunaamini tu katika kuzaliwa upya kwa misitu, ili bioanuai ihifadhiwe iwezekanavyo, na sio kupanda miti ambayo hairuhusu kitu kingine chochote kukua chini ya mwavuli,” alisema Peter Kitelo, mwanachama wa jamii ya Ogiek huko Chepkitale, Msitu wa Mlima Elgon, na mkuu wa Mpango wa Maendeleo ya Watu asili Wenyeji wa Chepkitale.

Alisema kuwa licha ya madai ya mafanikio kwa mfumo wa PELIS, katika hali nyingi kile kinachotokea chini kinafanana kidogo na nadharia. Aliiambia Mongabay kwamba wakulima wanaotumia mpango wa PELIS kwenye mashamba karibu na Msitu wa Mlima Elgon wamepanua mashamba yao waziwazi zaidi ya nusu ya hekta (ekari 1) ya mipaka yao, na kuvamia msitu wa asili kwa “baraka” za maafisa wa misitu.
“Tumeona katika maeneo kama vile Msitu wa Chesokwo ndani ya Mlima Elgon, ambako watu walivamia msitu wa asili, na kuharibu mamia ya hekta, na baadaye shirika la serikali la KFS walitumia uharibifu huo kama kisingizio cha kubadilisha eneo lililostawi kama mfumo wa ikolojia wa asili kuwa shamba ambalo mpango wa PELIS sasa unatumika,” Kitelo aliiambia Mongabay.
Kitelo alisema jibu la kurejesha misitu ya asili iliyoharibika mara nyingi ni kuiacha tu. Alidokeza kuwa ardhi yenye misitu kwa kawaida huwa na mbegu nyingi ardhini. Nyasi mbalimbali, vichaka na miti zikiachwa bila kusumbuliwa, na miti itapona, na kurejesha dari na sehemu ya chini ambayo inaweza kusaidia viumbe hai na maisha kama vile ufugaji nyuki, na uwindaji.
“Huwezi kulinganisha mapato ya kila mwaka ambayo jamii inaweza kunufaika kutokana na nyuki wanaofugwa kwenye shamba la ekari moja katika msitu wa asili, na kurudi kwa mahindi yaliyopandwa kwenye shamba kama hilo katika shamba la mbao ambalo limechukua nafasi ya msitu wa asili unaostawi,” alisema.
“Ili kukabiliana na changamoto zinazokabili misitu yetu, ni muhimu kutumia maarifa asilia ya jamii ambazo zinaingiliana na misitu katika maisha yake yote,” Kitelo aliongeza. “Kutegemea suluhu za kinadharia kama mpango wa PELIS ni kama kutibu nyati katika makazi yao ya asili kama ambavyo ungewattibu ng’ombe wa kufugwa – haiwezi kufanya kazi.”
Picha ya bango: Joseph Lijodi, mmiliki wa kitalu cha miti, akiwa mche wake wa Kiafrika wa Prunus. Picha na Isaiah Esipisu wa Mongabay.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 09/09/2025