- Katika miaka kumi iliyopita, maelfu ya kasuku wa kijivu wa Afrika yamesafirishwa nje ya nchi hiyo licha ya kupigwa marufuku kuwa bidhaa mojawapo ya kimataifa.
- Mwaka 2016 Kasuku aina ya Psittacus erithacus ambao wako hatarini kutokweka waliingizwa katika Kiambatanisho Namba 1 cha Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Biashara ya Wanyama na Mimea Ambayo iko Hatarini Kutoweka (CITES), jambo ambalo lingekomesha biashara hiyo lakini serikali ya Kongo ilikataa hatua hiyo.
- Serikali ikatakiwa kufanya uchunguzi wa ndege hao ili kujiridhisha na msimamo wao lakini mpaka sasa haijachukua hatua yoyote. Ukamataji na usafirishaji wa ndege hao nje ya nchi umekuwa ukiendelea lakini hatimaye serikali ya Kongo imezuia biashara ya ndege hao wa aina ya kipekee.
LUBUMBASHI, DRC — Idadi ya kasuku wa kijivu wa Afrika inaendelea kupungua maeneo ya katikati na kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Takwimu zilizokusanywa wakati wa doria na Lukuru Foundation katika eneo la Lomami Luidjo, jimbo la Maniema zinaonyesha kuwa idadi ya ndege hao aina ya Psittacus erithacus imepungua kati ya mwaka 2016 na 2021. Hali hii inatia wasiwasi. Mwezi Agosti mwaka 2023, aliyekuwa waziri wa Mazingira wa nchi hiyo, JKK (DRC), Eve Bazaïba, alitia saini amri ya kuwalinda aina ya ndege hao kwa namna yoyote ile.
Kupungua kwa idadi ya ndege hao kunawiana na ongezeko la biashara ya ndege wanaotumika kama mapambo ya majumbani. Biashara hiyo imekuwa ikiongezeka kuanzia mwaka 2012 na ongezeko hili linasababishwa na udhaifu wa usimamizi na uangalizi wa biashara ya kimataifa na rushwa miongoni mwa maafisa ambao wanatakiwa kusimamia biashara hiyo chini ya mkataba wa CITES.

Kasuku wa aina hii waliingizwa katika Kiambatanisho Namba 1 cha CITES (CITES Appendix I in 2016) na hii ilikuwa na maana kuwa mamlaka zilitakiwa kufanya usimamizi mkali wa biashara ya kimataifa ya ndege hao. Hata hivyo serikali ya Kongo ilipinga ndege hao kuingizwa kwenye Kiambatanisho hicho kwa madai kwamba ndege hao hawakutishiwa uhai kiasi cha kuwekwa katika jedwali hilo, jambo ambalo liliungwa mkono za serikali ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu ambao ndiyo walikuwa wanunuzi wakubwa wa ndege hao. Kwa sasa, serikali za Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu haziungi tena mkono hoja ya Kongo kwamba ndege hao hawako hatarini kutoweka.
Serikali ya Kinshasa ilitakiwa kufanya uchunguzi na kubaini idadi ya ndege hao ili kuthibitisha hoja yake kuwa biashhara ya kimataifa ya ndege hao ingeweza kuendelea lakini bila kuathiri uwepo wao, lakini uchunguzi huo haujafanyika.
Mratibu wa CITES aliyeko katika Taasisi ya Kuhifadhi Mazingira ya Asili (ICCN) Jeff Mapilanga, aliithibitishia Mongabay kwamba biashara ya kimataifa ya kasuku imesitishwa mpaka hapo uchunguzi utakapofanyika ili kujua idadi yao, lakini ukweli ni kwamba biashara hiyo inaendelea.
Biashara isiyo endelevu ya kasuku wa porini
Kila mwaka kuanzia mwezi Juni mpaka Agosti ni wakati wa kutega ndege kwa wingi kwani wakati huo matunda mengi huwa yameiva na kuwavutia ndege, alieleza Papy Matoandayayi ambaye huwafundisha watu wengine kuwanasa kasuku kwa kutumia gundi inayotokana na aina maalumu ya miti.
Emmanuel Boselo, mtaalamu wa ikolojia aliyepata mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Kisangani alieleza kuwa wakati mwingine wawindaji huchukua vifaranga vya kasuku kutoka katika viota vyao. Alisema kuwa uwindaji wa kasuku unachochewa na ongezeko la soko la kimataifa ambapo ndege hao huuzwa kati ya dola za Marekani 6 na 30 huko Maniema na dola za Marekani kati ya 75 na 00 mjini Kinshasa ambako biashara hiyo imeshamiri. Biashara hiyo pia hufanyika kupitia mitandao ambako ndege mmoja anaweza kuuzwa hadi dola za Marekani 1,500 kwa masoko yaliyopo Umoja wa Falme za Kiarabu.
Baada ya kukamatwa kasuku hao husafirishwa kwa ndege au kwa usafiri wa majini kupitia kwenye mito hadi Kinshasa na kupelekwa nje ya nchi, wakiwa wamerundikwa kwenye makreti. Wengine hufanya safari ndefu kwenye mitumbwi isiyo salama. Wanaosafirishwa kwa ndege wakati mwingine hukosa hewa na wengi hufa kabla hawajafikishwa sokoni.
Takriban asilimia 70 ya ndege wanaosafirishwa hufia njiani kabla hawajafika katika vituo vikuu vya biashara hiyo vilivyoko mijini. Hii ni kulingana na taarifa iliyotolewa na wataalamu kutoka ICCN na Lakuru Foundation. Hali hii ina maana kuwa iwapo ndege waliokamatwa na kupelekwa Kinshasa kati ya mwaka 2016 na 2022 ni takriban 86,000, zaidi ya kasuku robo milioni walikamatwa lakini walifariki kabla ya kufikishwa sokoni.
Ufuatiliaji wa misafara ya biashara haramu ya kasuku inaweza kuwa migumu sana kwani, hata wale wanaosafirishwa kwa ndege ambako mizigo yote lazima iandikwe kwenye orodha na hivyo kuwepo na udhibiti mkubwa. Mongabay ilipata nafasi ya kuangalia kitabu cha orodha ya mizigo katika kiwanja kimoja cha ndege katika jimbo la Sankuru lakini walichoona ni jina la kwanza na jina la ukoo la msafirishaji. Hapakuwa na taarifa nyingine yoyote.
“Adhabu inayotolewa kwa wasafirishaji haramu ni dhaifu, haisaidii kupunguza uhalifu,” alisema Mpo Diamba kutoka Asasi ya Action for the Promotion of Indigenous Peoples and Local Communities for the Promotion of Natural Resources (APPACOL-RN), mwaka 2024.

JKK yachukua hatua
Mapema mwaka 2025, serikali ya jimbo la Maniema ilikamata kasuku 35 ambao walipatikana kwa njia haramu kutoka katika kisiwa cha Kituhu. Ndege hao walikabidhiwa kwa bustani ya wanyama ya Kindu ili kuwarudisha katika hali yao ya kawaida kabla hawajarudishwa porini.
Mji mkuu wa jimbo la Maniema, Kindu, na Kisangani, jiji lililopo katika jimbo la kaskazini la Tshopo, ndiyo sehemu maarufu kwa biashara haramu ya kasuku kwa miaka kumi iliyopita. Lakini wafanya biashara wamefika hata maeneo yaliyohifadhiwa katika majimbo ya Lualaba, Tshuapa na Sankuru.
Ripoti ya utafiti iliyowasilishwa katika mkutano wa Kigali na mkurugenzi wa sayansi wa Lukuru Foundation na kwa niaba ya ICCN, John Hart, ilieleza kuwa kati ya mwaka 2017 na 2022 takriban kasuku wa kijivu 68,000 walisafirishwa kutoka Kisangani hadi Kinshasa ili kuingizwa katika masoko ya kimataifa. Kati ya hao, takriban 50,000 walitambuliwa kuwa walitokea Maniema.
Kuna kila dalili kwamba biashara hii haramu na isiyo endelevu haipungui kwani Mwezi Machi mwaka 2024, gavana wa mpito wa Maniema aliruhusu usafirishaji wa nchi za nje wa kasuku 400.
Mwnaharakati wa mazingira, Jean-Claude Sefu ambaye pia ni mwanachama wa asasi ya SOCEARUCO anasema kuwa mpaka hivi karibuni wafanyabiashara haramu walipata kibali cha kufanya biashara hiyo kutoka kwa mamlaka za majimbo. “Waliwanunua kasuku kwa bei ya chini sana. Wakati mwingine wao wenyewe walikwenda msituni kuchagua aina wanayotaka. Lilikuwa janga kubwa!”
Serikali za majimbo hatimaye zilichukua hatua kupambana na biashara hiyo haramu. Mwezi Machi mwaka 2025, jimbo la Tshopo lilipiga marufuku ukamataji na uuzaji wa kasuku wa kijivu. Asasi ya ICCN imeanzisha kituo cha kuhifadhi kasuku kwenye bustani ya wanyama iliyopo katika mji mkuu wa jimbo hilo. Taarifa hii ilitolewa na Gentil Kisangani, mkurugenzi wa uhifadhi katika jimbo hilo. Kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti, kituo hicho kilikuwa kimepokea kasuku 100 waliokamatwa kutoka kwa wafanya biashara haramu.
Lakini kituo hicho kina upungufu wa rasilimali watu hasa inapokuja kuwaokoa ndege walioko kwenye hatari, na kutokana na hali hiyo ndege wengi hufa.
“Tunapata changamoto linapokuja suala la kushirikiana na baadhi ya idara za serikali kwani hawaelewi ukubwa wa tatizo.Bado tunaendelea kuwajengea ufahamu na ni matumaini yetu kuwa hatimaye wataelewa,” alieleza Geni Kisangani.
Katika hatua inayoonyesha kuongezeka kwa ufahamu juu ya tatizo hilo, mwishoni mwa mwezi Julai, waziri wa mazingira alitia saini amri ya kupiga marufuku utegaji, usafirishaji na uuzaji nchi za nje wa kasuku isipokuwa kwa kibali cha wizara ambacho kitaruhusu kwa ajili ya shughuli zisizo za kibiashara kama utafiti, au ufugaji.
Makala hii ilichangiwa na Saïbe Kabila aliyeko Kisangani.
Picha ya bango: Kasuku wa kijivu wa Afrika. (Picha: Robert01 kupitia Wikimedia (CC BY-SA 3.0).
Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kifaransa mnamo Septemba 2, 2025.