- Licha ya mkataba wa kimataifa wa biashara ya wanyamapori, CITES, kupiga marufuku kuuzwa kwao, chui ni wa pili kati ya paka mwitu ambao biashara yao imeshamiri.
- Uwindaji unaofanywa kwa ajili ya burudani au ushindani, na biashara ya viungo vya tembo kama vile ngozi, kucha, mifupa na meno ndivyo vina wateja wengi, kulingana na takwimu za CITES. Hata hivyo, taarifa zingine zimeonyesha kuwa biashara haramu ya ngozi na viungo vya chui imeenea barani Asia na Afrika.
- Kusini mwa bara la Afrika, hasa Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe, ndiko uuzwaji wa viungo vya chui umeenea sana, huku Marekani ikiwa ndiyo soko kubwa zaidi ulimwenguni. China pia imedhihirika kuwa kitovu cha biashara haramu ya ngozi na kucha za chui.
- Biashara halali na isiyo halali, ikiwa pamoja na kupotea kwa makazi na mawindo ya wanyama hao, imesababisha kupungua kwa idadi ya chui barani Asia na Afrika kwa kasi.
Chui ni mnyama anayependa faragha, mwenye tabia ya kuficha mambo, anayependa kuwinda usiku, huku akijitenga na jamii. Kimaumbile, ana manyoya ya rangi ya dhahabu yenye madoadoa meusi. Mnyama huyu ni mmoja kati ya paka wakubwa wa porini, na wameenea sana kote duniani. Kwa mara nyingi, chui waanapatikana katika mazingira kama vile misitu ya mvua, milima yenye miamba, nyika, nyanda na hata jangwani, katika hali ya joto na pia hata baridi. Kwa jumla, kuna aina ndogo nane za chui duniani, zilizogawanywa kulingana na maeneo wanayoishi na muonekano wao.
Kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kuwa chui walienea Asia na Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, lakini kwa sasa, eneo lao limepungua zaidi. Chui (Panthera pardus) sasa wanapatikana Asia ya Kati, Kusini mwa Asia, Afrika, na maeneo madogo Mashariki na Kusini-Mashariki mwa Asia. India pia ina idadi ya chui wengi zaidi duniani, takriban 14,000, ambao wanaishi porini.
Licha ya kuwepo kwao kwenye kiambatisho cha CITES (Huu ni mkataba wa kimataifa wa biashara ya wanyamapori na mimea pori vilivyo hatarini kutoweka) — ambao umepiga marufuku biashara ya kimataifa ya mnyama huyu — chui wamethibitishwa kuwa paka mwitu wa pili kuuzwa zaidi duniani, wakitanguliwa na simba, ambao biashara yao inadhibitiwa. Hata hivyo, vitisho dhidi ya chui havijapewa kipaumbele, licha ya tamaa kubwa ya viungo vyao, ambayo imechochea biashara na uwindaji haramu.
“Serikali nyingi zinatoa taarifa zaidi kuhusu chui milia (tigers) kuliko chui wa kawaida,” anasema Debbie Banks, ambaye ni kiongozi wa kampeni dhidi ya uhalifu wa wanyamapori kwenye shirika la Environmental Investigation Agency (EIA) la Uingereza – ambalo linachunguza uhalifu wa mazingira. “Chui ndio wanyama wanaokamatwa kwa wingi zaidi kwenye biashara haramu.” Takwimu za EIA zinaonyesha kuwa kwa kila chui milia mmoja anayewindwa, kuna chui watatu, au hata watano, wanaouawa.
Viungo vyao kama vile ngozi, meno, kucha na mifupa vinapendwa sana, hasa nchini China na Asia ya Kusini-Mashariki, ambapo vinachukuliwa kama alama ya utajiri na kutumika kama mapambo majumbani. Mifupa ya chui hutumika zaidi kwenye tiba za jadi, ambazo pia huzingatia mifupa ya chui milia. Mara nyingi pia ngozi ya chui huwa sehemu ya mavazi ya jadi katika jamii nyingi Afrika. Ngozi hii pia ilikuwa sehemu ya vazi la kitamaduni kule Tibet, lililoitwa chuba. Pia kuna biashara ya uwindaji wa nyara za chui, ambayo huhalalishwa na kusajiliwa chini ya mkakata wa CITES.
Biashara ikilinganishwa na takwimu
Takwimu za CITES zinaonyesha kwamba kutoka mwaka 2000 hadi 2024, jumla ya vibali 8,303 vya biashara ya chui vilitolewa, idadi iliyofanya chui kuwa mnyama aliyeuzwa zaidi kwenye kiambatisho cha CITES. Uwindaji unaofanywa kwa ajili ya burudani au ushindani ulipokea sehemu kubwa ya vibali hivyo (4,165), ukifuatiwa na vibali 1,099 vya ngozi na 933 vya fuvu. Kumbuka kuwa kibali kimoja kinaweza kuhusisha viungo zaidi ya kimoja.
Ripoti iliyochapishwa na shirika la International Fund for Animal Welfare (IFAW) mwaka wa 2016 ilibaini kuwa kati ya mwaka 2004 na 2014, zaidi ya nyara 10,000 za chui ziliuzwa kihalali. Ripoti hiyo pia ilibaini kuwa chui ndiyo waliouzwa zaidi, wakilinganishwa na paka mwitu wote.
Takwimu zaidi kutoka CatByte, ambayo huzingatia biashara ya paka mwitu inayofanywa kihalali na kinyume cha sheria, inaonyesha kuwa kati ya mwaka 2000 na 2023, takriban bidhaa 60,830 za chui ziliuzwa. Karibu asilimia 91 ya bidhaa hizo (55,583), zilitoka kwenye chui wa porini, na asilimia 5 pekee kwa chui wa kufugwa kwenye mashamba au hifadhi za wanyama.
CatByte pia inaonyesha kuwa asilimia 32 ya biashara halali na isiyo halali ilihusisha bidhaa zilizotengenezwa kwa viungo vya chui. Kucha, ambazo hutumika kwa tiba za jadi, zilikuwa asilimia 17, nyingi zikiwa zimepatikana kwa njia isiyo halali. Ngozi ilikuwa asilimia 6, nyingi pia zikiwa zimetoka kwa biashara haramu.
Kulingana na takwimu za taasisi inayofuatilia uhalifu wa kimataifa wa wanyamapori, (Global Environmental Crime Tracker), tangu mwaka 2000, takriban chui 5,995 au viungo vyake vilikamatwa. Kwa takwimu kutoka India, Debbie Banks anakadiria kuwa angalau chui 6,400 walikamatwa. Takwimu zaidi ya CatByte zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2020 na 2025, bidhaa 738 za chui zilinaswa, nyingi zaidi zikiwa kucha, zikifuatiwa na ngozi na kisha mifupa.
Ofir Drori, ambaye ni mkurugenzi mwanzilishi wa EAGLE Network, shirika lisilo la kiserikali lililobobea katika uchunguzi wa masuala ya wanyamapori na utekelezaji wa sheria, anasema kuwa bara la Afrika lina wanunuzi wengi wa viungo vya chui. “Kila mwaka tunakamata ngozi 30 za chui Afrika Magharibi, Kati na Mashariki, lakini hiyo ni kiasi kidogo tu cha biashara halisi,” alisema Drori. Kulingana na utafiti mmoja uliofanyika huko Ivory Coast, mwaka wa 2025, karibu nusu ya masoko 46 yaliyofanyiwa uchunguzi, yalikuwa yameuza viungo vya chui, ikiwepo ngozi.

Maeneo hatari ya biashara
Kulingana na CITES, idadi ya vibali vinaonyesha kuwa Marekani ndiyo ina soko kubwa la kihalali la chui, ikifuatiwa na Afrika Kusini kisha Ufaransa. Nchi za Kusini mwa Afrika zikiwemo Zimbabwe na Namibia zimetajwa kama wauzaji wakuu.
Hata hivyo, Banks anasema kuwa China hununua viungo vya chui kwa wingi kwa lengo la kuvitumia kwenye matibabu ya jadi. “Tumebaini kuwa China ina mahitaji ya kudumu ya ngozi, mifupa, meno na kucha za chui,” alisema.
Idadi kubwa ya mahitaji ya viungo nya chui nchini China inatokana na tiba za jadi, huku kitabu cha hivi karibuni cha dawa nchini humo kikiruhusu matumizi ya sehemu za chui katika tiba zilizoidhinishwa. Utafiti wa EIA umebaini kuwa angalau kampuni 24 za dawa nchini China zinajumuisha mifupa ya chui miongoni mwa viungo vya dawa zao za jadi.
Asia ya Kusini-Mashariki na A.atari kubwa ya kutoweka. Utafiti uliofanyika nchini Indonesia mwaka 2021, uligundua matukio 24 ya ukamataji wa chui wa Javan ambao wako hatarini. Matukio hayo yalihusu chui takriban 51. Kwa mujibu wa utafiti huo, ngozi, kucha na meno ndio bidhaa zilizokamatwa zaidi.
Chris Shepherd, mmoja wa watafiti hao, alisema: “Chui wa Indonesia wako hatarini sana. Hawapati mawindo yao ya asili, hivyo kulazimika kula mifugo, jambo linalofanya wauawe. Pia, viungo vya chui vina faida vya kifedha.”
Kwingineko India, biashara haramu ya chui imekithiri. Katika miaka mitano iliyopita, vibali 2,527 vya ukamataji vimeripotiwa. Ripoti ya 2022 kuhusu mitego ya paka mwitu Asia ilibaini kuwa chui 245 walikamatwa kwenye mitego kati ya mwaka 2012 na 2021, ambapo asilimia 93 ya mitego yote hiyo ilikuwa nje ya maeneo ya hifadhi.
“Nina hofu kubwa kuhusu chui walio Asia, hasa Kusini-Mashariki na Kusini mwa nchi hiyo, kwani wanatoweka kimya kimya,” alisema Banks. “China ikiamua kusitisha matumizi ya mifupa ya chui kwenye dawa za jadi, idadi ya chui wa porini itaongezeka.”

‘Paka aliyesahaulika’ anayetoweka kimya kimya
Licha ya kuenea kwake, kwenye orodha ya Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Asili yaani, IUCN, chui wameorodheshwa kwenye alama nyekundu kwa sababu ya upotevu wa makazi, kupungua kwa mawindo, na biashara ya viungo vyao. Chui ndiye paka mwitu pekee ambaye hali yake ya uhifadhi imedorora — kutoka karibu kutoweka mwaka wa 2008, hadi katika hatari mwaka wa 2015.
Kulingana na utafiti, chui wamepoteza karibu theluthi mbili ya maeneo yao Afrika, na asilimia 84 barani Asia. Spishi ya chui wa Indo-China imekaribia kufutika kabisa kwenye makazi yake asili. Jinsi makazi yao yanavyozidi kudidimia ndivyo chui wanavyozidi kuingia kwenye maeneo yanayomilikiwa na kuishi binadamu, na kuwaua mifugo, jambo ambalo pia limesababisha kuuawa kwao kama njia ya kulipiza kisasi. Kati ya spishi nane zimebainika kuwa hatarini zaidi, ilhali mbili zimo hatarini.
Drori kutoka EAGLE Network aliita hali hii kutoweka kwa chui “kutoweka kimya kimya” kwa vile habari hizi hazipati “vichwa vya habari, wala watu kujua.” Hali hiyo inatokana na uhaba wa takwimu kuhusu idadi ya chui na biashara inayowagusa.
“Paka mwitu huyu ameachwa nyuma,” alisema Banks, “amezungukwa na fumbo.”
Ripoti iliyotolewa baada ya mkutano wa 2023 wa kamati ya CITES ilibaini upungufu mkubwa wa taarifa kuhusu ukamataji wa chui wa Asia. Ilipendekezwa kwamba nchi wanachama zitoe ripoti maalum kabla ya mkutano uliofuata baadaye Februari iliyopita.

Banks alisema taarifa zilizowasilishwa mapema mwaka huu zilikuwa “duni sana” na hazikujumuisha takwimu zote zilizoko. “Muda na juhudi za kushughulikia ukosefu wa utekelezaji wa sheria au kupunguza tamaa ya viungo vya chui hazitoshi,” aliongeza, huku akitazamia kuwa mkutano mkuu wa CITES COP20 wa mwezi Novemba utangeleta mabadiliko.
“Tangu mwaka wa 1999, CITES imekuwa ikitoa onyo kwamba chui walioko Asia wako kwenye hatari sawia na ile ya chui milia. Hii imedhihirika,” alisema Banks. “Swali ni: Je, wajumbe wa CITES COP20 mwaka 2025 watachukua hatua kwa wakati unaofaa?”
Picha ya bango: Chui akiwa ametulia katika Hifadhi ya Taifa Panna, nchini India. Picha: Harsh Tank – kupitia Unsplash (kikoa cha Umma).
Nukuu
Gomez, L., & Shepherd, C. R. (2021). The illegal exploitation of the Javan leopard (Panthera pardus melas) and Sunda clouded leopard (Neofelis diardi) in Indonesia. Nature Conservation, 43, 25-39. doi:10.3897/natureconservation.43.59399
Jacobson, A. P., Gerngross, P., Lemeris Jr., J. R., Schoonover, R. F., Anco, C., Breitenmoser-Würsten, C., . . . Dollar, L. (2016). Leopard (Panthera pardus) status, distribution, and the research efforts across its range. PeerJ, 4, e1974. doi:10.7717/peerj.1974
Rostro-García, S., Kamler, J., Ash, E., Clements, G., Gibson, L., Lynam, A., … Paglia, S. (2016). Endangered leopards: Range collapse of the Indochinese leopard (Panthera pardus delacouri) in Southeast Asia. Biological Conservation, 201, 293-300. doi:10.1016/j.biocon.2016.07.001
Williams, S. T., Williams, K. S., Lewis, B. P., & Hill, R. A. (2017). Population dynamics and threats to an apex predator outside protected areas: Implications for carnivore management. Royal Society Open Science, 4(4). doi:10.1098/rsos.161090
Viollaz, J. S., Thompson, S. T., & Petrossian, G. A. (2021). When human-wildlife conflict turns deadly: Comparing the situational factors that drive retaliatory leopard killings in South Africa. Animals, 11(11), 3281. doi:10.3390/ani11113281
Horion, R., Aglissi, J., Pickles, R., Ouattara, A., & Drouilly, M. (2025). Fading roars? A survey of the cultural use and illegal trade in wild felid body parts in Côte d’Ivoire. Animals, 15(3), 451. doi:10.3390/ani15030451
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya kiingereza mnamo tarehe 26/06/2025.

