- Vifo vya wavuvi wawili wasiokuwa na leseni katika eneo la Ziwa Navaisha nchini Kenya, vinavyodaiwa kufanywa na Shirika la Huduma la Walinzi wa Pwani ya Kenya, vinazua maswali kuhusu mbinu zinazotumiwa kudhibiti uvuvi haramu.
- Jayne Kihara, mbunge wa Naivasha, anawashutumu maafisa walinzi wa pwani katika eneo hilo kwa “kuwaua vijana wetu kila mahali, na kuwazamisha majini wanapokwenda kutafuta riziki yao.”
- Oparesheni nzito za silaha kali za walinzi wa pwani na madai ya hapo awali ya kutumia nguvu kupita kiasi vimewaacha wengi katika eneo hilo wakihoji iwapo kikosi kama hicho kweli kiko kwa maslahi yao.
- Mongabay liliwasiliana na Shirika la Huduma la Walinzi wa Pwani ya Kenya kuhusu matukio hayo lakini halikupata majibu. Shirika hilo pia halikujibu ombi la Mongabay kutaka data kuhusu matukio kati ya walinzi wa pwani na wavuvi ambayo yalisababisha majeraha au vifo.
NAIVASHA, Kenya — Ilikua bado ni giza simu ilipoingia.
Grace Nyambura, anayejulikana kwa majirani zake eneo la Karagita Naivasha, kama Mama Chuma, alikuwa amelala alipopigiwa simu na binti yake. Ilikuwa yapata saa 11 alfajiri. Alimwambia Nyambura kuwa kuna jambo limemkumba Chuma, ambaye ni mtoto wa tano wa kiume wa Nyambura. Alimwomba mama yake afike Ziwa Naivasha haraka iwezekanavyo.
Nyambura alitii wito huo. Kamau, mwanawe mkubwa, alimchukua kwa pikipiki na wakaendesha kwa kasi katika mji uliokuwa kimya, kuelekea ufuo wa ziwa. Aliyoyakuta asubuhi hiyo miaka minne iliyopita, yanampa kumbukumbu ya kuhuzunisha sana: mwanae, Samuel Mwangi Kimani – jina la utani Chuma kwa wale waliomfahamu – mwenye umri wa miaka 25 na baba wa watoto wawili, alikuwa amekufa kando ya ufukwe wa ziwa.
“Alionekana kapigwa risasi mgongoni, ikiashiria kuwa alikuwa akikimbia,” Nyambura anaiambia Mongabay, akiwa ameketi kwenye sofa iliyochakaa ndani ya sebule yake yenye mwanga hafifu. “Walikuwa wakikimbia walinzi wa pwani. Walikuwa wakielekea upande mwingine.”
Tukio hilo lilitokea mwezi wa Septemba mwaka 2021. Maandamano kuhusu mauaji hayo yalizuka baadaye katika makazi ya Karagita. Lakini katika kusimulia mauaji ya mwanae, Nyambura haonekani kufadhaika. Anaonekana kusumbuliwa zaidi na hilo, si kifo chake tu, bali pia miaka iliyotangulia, ambapo alishuhudia mtoto wake akihangaika kutafuta riziki.
Kwa muda wa miaka miwili, Kimani alikuwa akivua samaki na kupata vibarua vya ujenzi sehemu mbalimbali mjini. Uvuvi, alisema, umekuwa hatari kila wakati.
“Walikuwa wakipigwa,” Nyambura anasema. “Walinyanyaswa na maafisa wa ulinzi wa pwani.”
Mongabay iliwasiliana na Shirika la Huduma ya Walinzi wa Pwani ya Kenya kuhusu tukio hilo, lakini halikuweza kuthibitisha undani wa kifo hicho. Shirika hilo pia halikujibu ombi la data kuhusu makabiliano kati ya walinzi wa pwani na wavuvi, ambayo yalisababisha majeraha au vifo.

Mongabay ilipata ripoti ya tukio la walinzi wa pwani, ambayo ilitoa picha tofauti, ikieleza maafisa wake walivyofyatua risasi kujibu makabiliano makali na wavuvi haramu.
Kimani hakuwa na leseni ya uvuvi au mashua. Yeye na vijana wengine mara kwa mara walikuwa wakifanya kazi kwa maagizo ya wamiliki wa mashua ambao walitoa vifaa vya kuvulia. Mwanzoni alikamatwa na walinzi wa pwani lakini aliachwa huru baada ya wamiliki wa boti kuingilia kati. Mama yake alimuonya kukaa mbali na maji na alitii onyo hilo, ila kwa muda tu. Baadaye alianza kufanya vibarua vya ujenzi. Lakini kazi hizo hazikuwa za kuaminika na malipo hayakutabirika. Hatimaye, ziwa, pamoja na hatari zake zote, lilimrudisha nyuma.
Miezi mitano baada ya Kimani kukutwa amefariki, Februari 2022, familia nyingine ilipata hasara sawa na hiyo. Priscilla Njeri, mama wa watoto wanne, alikuwa ameanza shughuli zake asubuhi wakati jirani yake alipofika na kumbishia hodi mlangoni kwake.
“Mume wako amepigwa risasi,” mgeni huyo alisema.
Mumewe, Simon Thuku Mbugua, mwenye umri wa miaka 38, mvuvi na mmiliki wa boti, alikuwa amekwenda kwenye ufukwe wa ziwa kufanya mazungumzo ya kuachiliwa kwa mashua yake, ambayo ilikuwa imekamatwa na kuzuiliwa na walinzi wa pwani, kulingana na Njeri.
Alikimbizwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya kaunti ndogo ya Naivasha. Anakumbuka majeraha hayo waziwazi: “Alikuwa amepigwa risasi mara sita; kwenye mbavu, viganja vya mikono, miguu, na risasi moja mbaya ya moyo.”
Uchunguzi wa maiti ulithibitisha baadaye kuwa alikuwa amepoteza damu nyingi na kuumia kwa viungo vya tumbo.
Shirika la Huduma ya Walinzi wa Pwani la Kenya lilibuniwa mnamo mwaka 2018, kwa madhumuni ya kulinda fukwe za bahari za Kenya, maji yake ya pwani na vyanzo vya maji vya pwani. Shirika lina kambi kando ya fukwe za mwambao wa Ziwa Naivasha, ambayo ilianzishwa ili kutekeleza kanuni za uvuvi na kulinda mfumo wa ikolojia wa ziwa hilo.

Operesheni za kikosi cha walinda fukwe wenye silaha kali na madai ya hapo awali ya kutumia nguvu kupita kiasi – ikiwa ni pamoja na mauaji ya wavuvi wanaofanya kazi katika ziwa hilo, yamewaacha wengi wanaoishi karibu na mji wa Navaisha wakihoji iwapo kikosi kama hicho kiko kwa ajili yao ama la. Huku baadhi ya wakaazi wakiwapongeza walinzi hao wa pwani kwa kurejesha hali ya utulivu katika ziwa lililojaa shughuli haramu, wengine wanawalaani kwa madai ya ukatili.
Jayne Kihara, mbunge wa eneo la Naivasha, hana shaka kuhusu msimamo wake.
“Kwa kuanzia, sijui hata ni kwa nini waliwaleta maafisa walinzi wa Pwani katika Ziwa Naivasha,” anaiambia Mongabay. “Hili ni ziwa la ndani. Unalilinda dhidi ya nani? ”
Ingawa walinzi wa pwani wamepewa mamlaka rasmi ya “kuwakamata na kuwashtaki watu wanaoshukiwa kufanya makosa katika eneo la maji ya Kenya na bara,” Kihara anasema mamlaka hii imetumiwa vibaya katika Ziwa Naivasha. Anasema kuwa badala ya kulinda uvuvi wa ziwa hilo kwa manufaa ya umma, matumizi ya nguvu ya walinzi wa pwani yamefanya uvuvi kuwa harakati hatari.
Katibu wa Baraza la Mawaziri wa wakati huo, Prof. Kithure Kindiki, akihutubia katika bunge la Kenya mwaka wa 2023, Kihara aliwashtaki maafisa wa ulinzi wa pwani wanaolinda ziwa hilo, akisema “wamekuwa wakiwaua vijana wetu katika kila pembe ya Ziwa Naivasha, na kuwazamisha majini wanapokwenda kutafuta riziki zao.”
“Watoto hawa hawana chakula,” Kihara, ambaye sasa ana umri wa miaka 70, aliiambia Mongabay. “Wanapokwenda kuvua samaki, wanapigwa risasi – hata nje ya ziwa. Mtu anakimbia, lakini bado wanampiga risasi.”
Lakini si kila mtu anakubali. Patrick Sankale, Naibu Mwenyekiti wa ufuo wa bandari ndogo ya Karagita, chama cha usimamizi wa ufuo kinachoendeshwa na wavuvi wa ndani na wafanyabiashara, ambaye pia ni mvuvi, ana mtazamo tofauti.
“Wavuvi hawana shida kabisa na walinzi wa pwani,” anasema. “Badala yake, wavuvi wanajivunia kuwa nao karibu.”
Sankale, ambaye pia anaendesha shirika la utalii wa mazingira na duka sehemu hiyo, anasema kwamba tangu kuwasili kwa walinzi wa pwani mnamo mwaka 2021, wavuvi wa kweli, wenye leseni wamefanikiwa. Anataja jitihada za hivi karibuni za wavuvi ambao alisema walijaza tena ziwa hilo na samaki wachanga wenye thamani ya shilingi za Kenya 700,000 (sawa na dola za Marekani 5,400) bila msaada wowote wa serikali.
“Kabla ya walinzi wa pwani, ni walaghai tu waliokuwa wanafaidika. Wangetunyanyasa kwa mapanga. Sasa, hilo limeisha,” Sankale anasema.
Kuhusu upigaji risasi, huku akionyesha kufikiria kwa makini, alisema; “Nilisikia kuhusu mauaji hayo,” anasema, “lakini siwezi kusema kwa uhakika. Mimi sikuwepo huko. ”

Anaongeza kwamba katika baadhi ya matukio, wafanyakazi wa walinzi wa pwani pia wamekuwa waathirika – ambapo hushambuliwa na makundi yenye hasira ya wavuvi haramu, na wakati mwingine kuishia hospitalini.
Kikosi cha walinzi wa pwani kilianza shughuli zake katika Ziwa Navaisha baada ya idara ya serikali inayohusika na uvuvi, ufugaji samaki na uchumi wa samawati kubaini kupungua kwa samaki na uwepo wa idadi kubwa ya wavuvi haramu katika ziwa hilo.
“Uvuvi haramu umekithiri sana katika ziwa hilo. Idadi ya wavuvi wasio na leseni kando ya ufukwe, na kwa bahati mbaya, kwenye maeneo ya kuzaliana samaki, imeongezeka kwa miaka mingi tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000 na wakati mwingine wanavua samaki wengi zaidi kuliko wenzao waliopewa leseni,” aliyekuwa afisa mkuu wakati huo katika kaunti ya Nakuru ambayo Ziwa Naivasha linapatikana aliliambia Shirika la Habari la serikali la Kenya News Agency wakati alielezea uamuzi wa kuwaita walinzi hao.
Uvuvi katika maji ya ndani ya Kenya unahitaji mtu kuwa na leseni halali ya wavuvi wa ndani au kuwa mfanyakazi wa mmiliki wa meli maalum ya uvuvi iliyoidhinishwa na mamlaka. Kibali kinagharimu shilingi za Kenya 500 (sawa na dola za Marekani 4) kwa mvuvi kwa mwaka. Leseni hutolewa kwa wanachama wa vitengo vya usimamizi wa ufuo, yaani (BMUs), kama ile inayoongozwa na Sankale, kupitia mkurugenzi wa uvuvi katika kaunti.
Baadhi ya viongozi wa eneo hilo wanadai leseni hizo zimebanwa na watu wachache na hazitolewi kwa haki na hivyo kusababisha uvuvi haramu ukanda huo.
Kwa wavuvi Ishmael Ongata na Samuel Karanja, wanaofanya kazi kwa wamiliki wa boti katika Ufuo wa Karagita, mlinzi wa pwani si mlinzi wala mwathirika, bali ni mwindaji.
“Watu hawa hawakuja hapa kutusaidia kwa njia yoyote,” Ongata anasema. “Wanachofanya ni kukiuka haki na kutunyanyasa.”

Wanaume hao wawili wanazungumza na Mongabay kando ya ziwa Naivasha, karibu na mahali ambapo mwili wa Kimani ulipatikana. Ongata anawaelezea walinzi wa pwani kama mafisadi, mara nyingi wakifanya kazi kwa kushirikiana na wamiliki wa boti huku wakiwalenga wavuvi wadogo kama yeye.
“Ikiwa ni boti kubwa, hawajali. Lakini ikiwa ni mtu kama mimi, kuna shida,” anasema.
Wote wawili wanasema kuwa wamewahi kukamatwa na kushambuliwa na walinzi wa pwani. Karanja anasimulia kisa cha hivi karibuni ambapo mvuvi alipigwa vibaya sana kiasi cha kujichafua. “Walimpiga kikatili sana, hata kumpiga teke tumboni alipokuwa amelala chini,” anasema.
“Hata wanatuua,” Ongata anaongeza, akionyesha maeneo mawili yaliyo karibu ambayo anasema wavuvi waliuawa kwa kupigwa risasi. “Tuliwakashifu, tukawakaripia, ‘Angalieni mlichokifanya!’ Lakini waliondoka tu.”
Wavuvi wanasema mara nyingi wanashutumiwa vikali kwa kuvua samaki wachanga, kosa kubwa la kiikolojia. Lakini hata wakati samaki ni wakubwa, unyanyasaji unaendelea.
“Wao hudai tuwape shilingi 10,000 ya Kenya kutoka kwenye samaki wenye thamani ya shilingi 2,000,” Karanja anasema. “Kama hauwalipi, wanakukamata.”
Mbunge Kihara anaiambia Mongabay kwamba maafisa wa walinzi wa pwani wanauza samaki waliowanyakua kinyume cha sheria.
Josiah Odongo, Naibu Kamishna wa Naivasha, anapinga vikali madai haya. Yeye anaongoza kamati ya usalama na ujasusi ya eneo hilo, ambayo inaleta pamoja mashirika yote ya serikali yanayofanya kazi katika kutekeleza sheria ndani ya Kaunti ndogo ya Naivasha – ikiwa ni pamoja na walinzi wa pwani.
“Uhusiano kati ya walinzi wa pwani na jamii ni mzuri sana,” Odongo anaiambia Mongabay. “Hatujapata matatizo yoyote.”
Odongo anakiri kuwepo kwa umuhimu wa Ziwa Naivasha kwa uchumi wa ndani, lakini anasisitiza kuwa uchimbaji wote wa rasilimali lazima uzingatie sheria za mazingira.
“Kama mtu anataka kushiriki katika uvuvi haramu, usitarajie mtu huyo kuunga mkono sera yoyote inayolinda ziwa,” anasema. “Hatujapata hata kesi moja ya kuwashtaki walinzi wa pwani kwa mateso katika mwaka uliopita.”
Odongo anakataa katakata kutoa maoni yake kuhusu matukio ya mwaka 2021 na mwaka 2022, akiiarifu Mongabay kwamba hakuwa akihudumu katika serikali ya kaunti ndogo ya Naivasha wakati huo.
Mongabay iliikagua ripoti ya walinzi wa pwani ya mwezi wa Septemba 22, mwaka 2021, kuhusu tukio ambalo Kimani aliuawa. Inasema maafisa walikabiliwa na “wavuvi haramu waliokuwa na silaha” saa kumi na nusu alfajiri, ambao walikataa amri ya kusimama na badala yake wakakimbia kuelekea eneo la Karagita. Ripoti hiyo inasema kundi la wavuvi haramu, wakiwa wamejihami kwa mapanga, walipiga kelele “choma, choma” walipokuwa wakikimbia mbele. Koplo mmoja alifyatua bunduki yake aina ya M4 na kumuua Kimani.

Mapanga mawili yaliripotiwa kupatikana.
Hakuna mtu aliyekamatwa. Pia hakuna mashtaka.
Punde tu baada ya kifo chake, mjane wa Kimani aliondoka na kuolewa tena. Njeri, mjane wa mwathiriwa mwingine, Simon Thuku, bado anamuomboleza mumewe. Sasa anasimamia kile kilichosalia kwenye biashara ya uvuvi ya familia.
“Kwa watu ambao jamaa zao waliangushwa na mtutu wa bunduki kutoka kwa maafisa ambao walitarajiwa kulinda vyanzo vya maji, hii ilikuwa bahati mbaya ikizingatiwa kwamba haya ni maisha ya binadamu yaliyopotea kutokana na kuvua samaki,” Willy Dennis Njiru, mwanahabari aliyefuatiliwa mauaji ya Kimani kwenye kituo cha runinga cha TV47, anaiambia Mongabay.
“Ingeweza kutekelezwa kwa njia nyepesi, lakini hii ilikuwa ya kikatili,” anasema.
Licha ya kauli zinazopinga vikali ya matukio yanayohusu mauaji katika Ziwa Naivasha, ukweli unabakia kuwa: watu waliuawa. Na hadi sasa, hakuna mtu ambaye amewajibishwa hadharani kutokana na vifo hivyo.
Nyambura, ambaye ni mamake Kimani, alishirikiana na wakili kushughulikia suala hilo. Lakini mawasiliano yamepungua tangu wakati huo, na Nyambura, ambaye amelemewa na kazi na kukatishwa tamaa na urasimu, hakuweza kufuatilia. Anasema watoto wake wengine hawawezi kupata muda wa kutoka kazini ili kuhudhuria vikao vya mahakama. Hajui tena hali ya kesi hiyo.
Kwa Njeri, kutochukua hatua za kisheria katika mauaji ya mumewe lilikuwa chaguo gumu. “Hakuna njia unaweza kushindana na serikali,” anasema.
Nyambura anasema hata wakili wake aliacha kujibu simu zake. Lakini hilo halijamaliza utafutaji wake wa majibu kuhusu kifo cha mwanawe.
“Kijana wangu hakuwa akiiba. Na hata kama aliiba, kuna utaratibu kamili unaofaa,” anasema. “Lau wangemuacha, angelea watoto wake. Nimepoteza mtoto wangu, nahitaji haki itendeke.”
Picha ya Bango: Boti kwenye Ziwa Naivasha, Kenya. Picha kwa hisani ya ISB0210 kupitia Wikimedia Commons (CC-BY-SA-4.0)
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 21/08/2025