- Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa binadamu wanaweza kutambua bayoanuwai kupitia kuona na kusikia, na mitazamo hiyo inahusiana na bayoanuwai halisi ya maeneo ya asili.
- Wanajamii wa asili katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameelezea uzoefu wao ambao unathibitisha kile ambacho watafiti walibaini.
- Utafiti huu unaongeza maarifa kwenye hazina ya tafiti zinazokua kuhusu utambuzi wa bayoanuawai na uhusiano wake na afya ya akili ya binadamu na ustawi.
Katika kina kirefu na chenye kupendeza cha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo sauti za ndege zilizoambatana na msukosuko wa majani, watu kadhaa wa jamii za asili wanathibitisha matokeo ya utafiti uliochapishwa mwezi Julai. Wanasayansi wa bayoanuwai, waliovutiwa na jinsi binadamu wanavyotambua mazingira ya asili, walianzisha utafiti wenye kichwa cha habari; “Bayoanuwai inayoonekana: Je, kile tunachokipima ndicho tunachokiona na kukisikia?”
Wazo lililokuwa nyuma ya utafiti huo lilikuwa rahisi: Katika awamu ya kwanza, washiriki waliombwa kusikiliza sauti zilizorekodiwa msituni kutoka maeneo yenye viwango tofauti vya bayoanuwai. Katika awamu nyingine, washiriki walionyeshwa picha za mazingira ya asili.
Lengo ? Ili kujua kile ambacho watu hutambua pale wanapoona au kusikia viwango tofauti vya bayoanuwai, na ni kwa kiwango gani bayoanuwai halisi inalingana na ile inayotambulika na binadamu. Inavutia, siyo?
Ili kulifumbua fumbo hili, watafiti walichunguza washiriki 48 katika kila kikundi ambao walionyeshwa alama za kuona (picha 57 zilizopigwa kwenye misitu yenye viwango tofauti vya bayoanuwai) au vidokezo vya sauti (rekodi 16 za sekunde 10 kila moja kutoka katika mazingira ya asili), kisha wakatakiwa kuainisha picha na sauti kulingana na kiwango cha bayoanuwai waliyoitambua.
Kevin Rozario, mmoja wa waandishi wa utafiti huo, katika ujumbe wa sauti kwa Mongabay, alieleza hivi; “Tuliwaambia tu, ‘Tazama picha hizi, sikilizeni sauti hizi. Tuambieni mnaona nini na mnasikia nini’ Na wao wakaanza kulinganisha kwa uhuru, wakitumia kumbukumbu na uzoefu wao binafsi.”

Matokeo ya utafiti huo yalibainisha kuwa mitazamo ya watu ililingana kwa karibu na bayoanuwai halisi ya kibayolojia. Sauti za msitu, vilio vya wanyama, mivumo ya majani: Haya yote yanaunda lugha ambayo washiriki waliielewa. Watafiti walipiga hatua zaidi kwa kutumia viwango vya hisabati kupima mitazamo hiyo kulingana na vichocheo vya kuona na kusikia.
“Bayoanuwai inayoonekana na ya kusikia iliyotambuliwa na washiriki ilihusisiana kwa kiasi kikubwa na bayoanuwai halisi ya kuona na kusikia” Rozario alisema.
Lakini zaidi ya maabara, pia katika hadithi na uzoefu wa wazee wa jamii za asili, msitu hufichua siri zake za ndani kabisa.
Katika taifa la Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo DRC, mbali na kelele za magari na viwanda, katika kisiwa cha Idjwi chenye amani na kijani kibichi, Rwankumkumba Kamanzi Athanase, mkulima na mchungaji mwenye umri wa miaka 70 kutoka kijiji cha Bwiru, ambaye hakuhusika na utafiti, alitoa ushuhuda wake kwa Mongabay kupitia njia ya simu, akisema; “Kwenye msitu wetu wa Nyamusisi, tulikuwa tumewazoea nyani, kiasi kwamba hata bila kuwaona, tuposikia kelele zao , tulijua kinachoendelea msituni. Wengine waliishi katika mapango na mashimo, na kulipokuwa au kuwepo kwa dalili za maporomoko ya ardhi au maafa ya asili, tuliweza kujua kwa sababu tulisikia vilio vyao vinavyoashiria tahadhari.”
Aliendelea kusema kwamba hali hii imebadilika sana tangu wakimbizi wa Rwanda walipoingia wakikimbia vita na mauaji ya halaiki ya mwaka 1994: “Walikata miti kwa ajili ya mbao za kujengea nyumba.… Lakini kabla ya hapo, sauti za ndege zilibadilika kulingana na wakati: Asubuhi, mchana, jioni – na hiyo ilitusaidia kujua ilikuwa saa ngapi bila kuwa na saa mikononi mwetu.”

Kwa baadhi ya jamii za watu wa asili, msitu huzungumza, hucheza na kupumua. Majani yanapovuma kwa nguvu , wanajua kuwa wanyama wapo na wanabeba ujumbe. Kwenye msimu wa kiangazi, wanyama hujificha kwenye miamba na wakati mwingine hukaribia mikondo ya maji nyakati fulani.
Mnamo mwaka 2015, Kambale Nganga, chifu wa kijiji cha Kamandi katika dola ya Lubero kaskazini mwa mji wa Kivu, alisafiri hadi jiji kuu la Goma, akitembea kando ya barabara iliyojipinda na yenye ngazi za msururu wa milima ya Virunga inayojulikana kama Kabasha katika Hifadhi ya Kitaifa ya Virunga. Akikumbukia tukio hilo, alisimulia kwamba mtazamo wa hisia ulikuwa muhimu kwa uelewa wake wa mazingira. “Katika msururu huu wa milima, ilikuwa rahisi kwangu kuona uwepo wa Mto Semliki, kutokana na uoto wa kijani kibichi ambao ulionekana kwa mbali kwenye kingo zake. Rangi hii iliashiria afya ya uoto unaozunguka mto huo kwa kuutazama tu,” alisema wakati alipopigiwa simu na Mongabay. “Na mara nyingi, pale penye msitu wa kijani kibichi namna hiyo, ni rahisi pia kupata ndege na wanyama wanaokuja kunywa maji na wengine hata kuwinda wakati wa kiangazi. Hapo, basi, kwa mbali, ni sauti inayotoka ambayo husaidia kujua kama kuna wanyama au la,” aliongeza kusema.
Batundi Hangi Vicar, ni mratibu wa kitaifa wa shirika la FDAPID, kituo cha maendeleo cha Kivu Kusini na Kaskazini ambacho kinafanya kazi na jamii asilia na watu wanaohitaji, aliiambia Mongabay kupitia barua pepe kuwa watu jamii za asili wanatambulika kama wafuatiliaji wa kipekee wa masuala ya mazingira na kwamba mitazamo yao huko msituni inawafanya kuwa wataalam wazuri sana katika eneo hilo.
“Kwa msaada wa harufu kali inayopeperushwa na upepo unaopita msituni, kilomita chache kutoka hapo, Mbilikimo huweza kujua iwapo kuna mtu amekata mti msituni,” alisema Batundi. “Na kwa kutumia hali ya joto wanayohisi kwa kawaida chini ya kivuli cha mti, wanaweza kusema iwapo siku hiyo mvua itanyesha au la. Zaidi ya hayo, kwa kulala chini na kuweka masikio yao chini kwenye ardhi ya msituni, hata wakiwa umbali wa kilomita chache (kama kilomita moja au mbili), wanaweza kusikia uwepo wa wanyama, hasa wanapokuwa katika makundi makubwa kama sokwe, tembo na hata aina fulani ya nyati.”
Matukio ya uzoefu huu, na matokeo ya utafiti, ni sehemu ya ushahidi unaoongezeka kuhusu namna binadamu wanavyotambua bayoanuwai na uhusiano wake na afya ya akili. “Bayoanuwai ni muhimu kwa afya na ustawi wa binadamu,” waandishi wa utafiti wanaandika, na “bayoanuwai inayotambulika – yaani uzoefu wa kibinafsi wa watu kuhusu bayoanuwai, inaonekana kuwa na uhusiano wa karibu na ustawi wa akili.”

Mbali kabisa, katika sehemu ya kusini mwa Marekani, katika mji mkuu wa Georgetown huko Guyana, utafiti mwingine uliochapishwa mnamo mwaka 2021, kwa kutumia mbinu tofauti za utafiti, ulisisitiza matokeo haya, sio tu kwa kusisitiza umuhimu wa mtazamo wa watu kuhusu bayoanuwai lakini pia kwa kuonyesha nafasi ya bayoanuwai kwa ustawi wa akili ya mwanadamu. “Tulitathmini usahihi wa mitazamo hii ya tovuti kwa vipimo vya kimazingira kama vile sauti (kwa kutumia kipimo cha sauti za asili), utajiri wa spishi za ndege, na asilimia ya ufunikaji wa uoto, maji, na maeneo yaliyofunikwa na yasiyoruhusu kupenya,” waandishi waliandika. “Matokeo yalionyesha kuwa iwapo maeneo yaliyotambuliwa kama spishi tajiri, zenye sauti za asili kama vile wimbo wa ndege, kuwa na asili badala ya bandia, na kuwa salama, yalionekana kuwa ya kurejesha zaidi, na hivyo kusababisha ustawi bora.”
Ni vyema kunakili kuwa vichocheo vya hisia za kila mtu ni tofauti kulingana na uzoefu wao. Athari chanya ya bayoanuwai inayotambulika kwenye afya ya akili inaweza kuwa chombo cha thamani, ingawa mara nyingi hupuuzwa, ni kifaa cha kuimarisha ufahamu wa uhifadhi wa asili.
“Kwenye utafiti huu, tunawasilisha viashiria vya kuona na viashiria kadhaa vya utofauti wa sauti vinavyopima vipengele vya bayoanuwai inayotambulika na ile halisi. Fahirisi hizi zinaweza kutumika kama zana za gharama nafuu za kusimamia na kupanga nafasi za kijani ili kukuza bayoanuwai na ustawi wa akili,” Rozario aliongeza kusema.
Picha ya bango: Euphonia wa kiume aliyeungwa mkono na mzeituni (Euphonia gouldi) ukiimba kwa sauti kamili katika msitu wa mvua wa Costa Rica. Watafiti walichunguza mitazamo ya watu kuhusu bayoanuwai kulingana na kile wanachoona kwenye picha na kusikia katika rekodi za asili. Picha na Andy Morffew kupitia Wikimedia Commons (CC BY 2.0).
Nukuu:
Rozario, K., Shaw, T., Marselle, M., Oh, R.R.Y., Schröger, E., Botero, M.G., … Bonn, A. (2025). Perceived biodiversity: Is what we measure also what we see and hear? People and Nature, 7(8). doi:10.1002/pan3.70087
Fisher, J.C., Irvine, K.N., Bicknell, J.E., Hayes, W.M., Fernandes, D., Mistry, J., & Davies, Z.G. (2021). Perceived biodiversity, sound, naturalness and safety enhance the restorative quality and wellbeing benefits of green and blue space in a neotropical city. ScienceDirect, 755(2). doi:10.1016/j.scitotenv.2020.143095
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 04/09/2025