- Wahifadhi barani Afrika wanakabiliana na vitisho, kutengwa na ufadhili usiotosheleza, kama ilivyoonyeshwa na mhifadhi wa Nigeria Itakwu Innocent, ambaye alinusurika jaribio la kuuawa na amevumilia miaka mingi ya vurugu na kutengwa kwa sababu ya kulinda wanyamapori na kupinga ujangili katika jamii yake.
- Wanawake na wanasayansi vijana hukabiliana na vikwazo vya kimfumo katika sekta ya uhifadhi, ikijumuisha ubaguzi wa kijinsia na upatikanaji mdogo wa ufadhili na kutambuliwa, licha ya kubeba majukumu ya uongozi na kuendesha miradi ya jamii katika maeneo kama Kenya, Uganda na Nigeria.
- Tofauti za ufadhili na kuvunjwa kwa ahadi za mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa, vimedhoofisha imani katika juhudi za uhifadhi, na hivyo kufanya iwe vigumu kwa wanasayansi wa ndani kama Owan Kenneth kupata msaada kutoka kwa jamii bila motisha za kifedha.
- Licha ya changamoto hizi, utambuzi na hadithi za mafanikio vimeanza kuonekana, na fursa kama ufadhili wa masomo na mageuzi yanayoongozwa na jamii ya kusaidia watu kama vile Adekambi Cole, Bashiru Koroma na Asuquo Nsa Ani, vinaleta mafanikio halisi katika uhifadhi na kuwatia moyo wengine.
Jioni ya Mei 9, 2019, mhifadhi na mwalimu Itakwu Innocent alinusurika jaribio la mauaji nje ya nyumba yake huko Kubong-Bette, kijiji kidogo cha wakulima katika jimbo la Cross River kusini mashariki mwa Nigeria.
“Baba! Bunduki!” Innocent anakumbuka mwanawe akipiga kelele sekunde chache kabla ya risasi kufyatuliwa. Risasi hiyo ilipasua nyumba yake na kuchana sikio lake na kuliacha likiwa vipande vipande vinavyoning’inia.
“Walidhani nimekufa,” Innocent anasema.
Jaribio la kumaliza maisha ya Innocent linatoa muhtasari wa vitisho vinavyowakabili wanasayansi wa Kiafrika walio mstari wa mbele katika uhifadhi vijijini.
Ushirikishwaji unaotatanisha wa Innocent kwenye mfumo wa ikolojia wa maeneo ya vijijini mashinani humpa ufahamu wa kina kuhusu ardhi na watu wanaomzunguka. Hata hivyo, uhusiano huu unamweka kwenye mashambulizi na vitisho. Tofauti na wanasayansi wa kigeni au wa mijini, yeye anakosa mbinu za kukabiliana na hatari hiyo.
“Mtu hawezi kutoroka kutoka nyumbani kwake,” anasema. “Hii ndiyo nyumba yangu pekee. Na nisipoihifadhi, nani ataihifadhi?”
Zaidi ya ukosefu wa usalama, wanasayansi kama Innocent wanakabiliwa na changamoto nyingi zaidi za kitaaluma, anasema Babafemi Ogunjemite, profesa wa usimamizi wa wanyamapori katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Akure, kusini magharibi mwa Nigeria. Kwa kiasi kikubwa wanasahaulika na wanafadhiliwa kidogo. Uwakilishi, nafasi za kupata ushauri na mchango wao kuonekana, viko chini na zaidi ya hayo, ubaguzi wa kijinsia ni kikwazo cha ziada kwa wanawake. Kutokana na hilo, Ogunjemite anasema, “vipaji vyetu bora havitumiwi ipasavyo na sekta ya uhifadhi.”

Anaonekana kama ‘mwendawazimu’
Mapenzi ya Innocent kwa masuala ya mazingira asili yalidhihirika kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 16, alipokuwa akihusishwa sana na ndege aina ya horbill aliyenusurika na manati yake. Miezi mitatu baadaye, alikumbwa na huzuni kufuatia kifo cha ndege huyo.
Uhusiano wake na korongo – pamoja na kusikitishwa kwake na kuwasili kwa msumeno katika misitu iliyo karibu, kukutana na wanasayansi wa uhifadhi wa Magharibi, na kuonekana kwa chui karibu na nyumba yake – kulimfanya aingie kwenye njia iliyompeleka kwenye kazi ya uhifadhi.
Kwa zaidi ya muongo mmoja, kuanzia mwaka 2003, Innocent alifanya kazi katika shamba la mifugo la Drill, kituo cha hifadhi na ukarabati wa wanyamapori. Mnamo mwaka 2004, alianza kufunga biashara ya bunduki ya familia yake ya karne na karne, ambayo aliamini ilikuwa ikichochea ujangili na ukosefu wa usalama kwa kutoa silaha za bei nafuu kwa wawindaji na wahusika wa migogoro.
Uamuzi huo, anasema Innocent, uliwakera ndugu na jamaa zake: Walimwona kuwa “mwendawazimu” kwa kutanguliza wanyama wa mwituni dhidi ya mali. Alipotengwa na familia yake mwaka 2012, Innocent pia alinyang’anywa ardhi ya kurithi, mashamba na jina la familia.
Innocent anakumbuka jaribio la kumuua miaka iliyopita hadi mgogoro uliopo sasa. Mtu aliyekamatwa kwa kumpiga risasi – ambaye alifukuzwa na kupigwa na wanakijiji wengine – alikuwa mwanajeshi wa Nigeria ambaye alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na dada yake Innocent.
Kesi ya mauaji dhidi ya mtuhumiwa huyo ilishindwa kuendelea mahakamani, lakini upelelezi wa tukio hilo uliofanywa na mamlaka za kimila za kijiji hicho ulisababisha adhabu ya viwango tofauti kwa ndugu na jamaa wa Innocent, kuanzia faini ya fedha taslimu na kreti za bia hadi kifungo cha uhamisho cha miaka kumi.
Zaidi ya kaya yake, Innocent bado anazua maoni yaliyogawanyika. Anaendelea kuheshimiwa sana na mahali alipokuwa akifanya kazi awali, ambako bado huchangia chakula cha nyani mara kwa mara. Kampeni yake ya msimu dhidi ya moto wa porini, inayolinda mashamba dhidi ya moto, imemfanya apendwe na wakulima na wale anaowafundisha.
Hata hivyo, zaidi ya mara moja, Innocent anasema, wawindaji wametishia kumuua kwa kung’oa mitego yao na kusaidia kufichua uhalifu wao kwa wachunguzi. Wakati wa kufanya kazi na timu ya doria ya uharibifu wa misitu mwaka wa 2014, umati wa wakataji miti ulimpiga hadi akapoteza fahamu na kuzivunja kucha zake kwa jiwe la simiti kwa kuwazuia kupita kwenye kituo cha ukaguzi.
“Nusura waniuwe usiku huo,” Innocent anakumbuka, akiinua vidole vyake vilivyokuwa na makovu.

Kisiwa cha Sokwe
Miaka mingi iliyopita, Innocent alianza kuwazia kujenga kituo cha ujuzi ambacho kingewapa vijana ujuzi katika masuala ya kidijitali, ujuzi utakaoweza kutumika duniani kote.
Lakini maono hayo yalipunguzwa kasi na ukosefu wa fedha – kikwazo kilichoripotiwa sana na wanasayansi wengine waliohojiwa na Mongabay, ikiwa ni pamoja na Koroma Bashiru, ambaye anaishi zaidi ya kilomita 2,200 (kama maili 1,400) katika jiji la Bo, nchini Sierra Leone.
Alizaliwa wakati wa kilele cha vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1988, hali iliyomfanya Bashiru asifurahie maisha rahisi ya utotoni. “Tulitumia muda wetu mwingi msituni kujaribu kuvitoroka vikosi vya waasi,” Bashiru anasema. “Nilihisi kiwewe kuona watu wakiuawa.”
Kutazama angani wakati wa usiku wa giza alipokuwa akisoma na kuona nyota, kulimvutia Bashiru , jambo lililompelekea kusomea Shahada ya Sayansi ya Mazingira mwaka 2012, na hiyo ikawa njia ya kuelekea kwenye kazi ya uhifadhi wa mazingira. Mwaka wa kuhitimu kwake, Bashiru alitembelea Viata Sewa, kisiwa kilicho karibu na Bo ambacho kina msitu wenye utajiri wa mimea na makundi ya vipepeo na ndege.
Bashiru anasema pia kuna ushahidi kuwa sokwe wa Magharibi (Pan troglodytes verus), nyani diana (Cercopithecus diana) na nyani mbega wa rangi nyeusi na nyeupe Colobus spp.) wanaishi kisiwani.
Alipopendekeza kwa mara ya kwanza kwamba kisiwa hicho kibadilishwe kuwa kituo cha utalii na uhifadhi, Bashiru anasema wenyeji walipokea wazo hilo kwa furaha. Hata hivyo, hakuwa na fedha za kufanya utafiti wa awali kuthibitisha uwepo wa nyani kisiwani humo, wala kulipa fidia kwa wakaazi waliotegemewa kuhamishwa au kushawishi wabunge ili eneo hilo litangazwe rasmi kuwa hifadhi. Mradi huo bado haujatekelezwa, ingawa Bashiru bado anaendelea kutamani hilo ndoto yake itimie.
Ukosefu wa rasilimali kwa wahifadhi wa ndani mara nyingi hutofautiana sana na ukarimu wa mashirika ya kimataifa.

Owan Kenneth, ambaye sasa ana miaka 36, alikuwa mtoto wakati wa kile ambacho mara nyingi huelezewa kama “enzi ya dhahabu ya uhifadhi wa Cross River.” Hapo awali sokwe wakubwa wa Cross River (Gorilla gorilla diehli) walidhaniwa kutoweka kabisa nchini Nigeria, lakini waligunduliwa wakiwa porini katika miaka ya 1980, jambo ambalo lilisababisha wanasayansi na wahifadhi kutoka Magharibi kuanza kumiminika eneo hilo.
Akiwa mtoto wa kiongozi wa eneo hilo, Kenneth alishuhudia mashirika yasiyo ya kiserikali ya kigeni yakiahidi ufadhili wa masomo, shule, hospitali, visima vya maji na barabara ili kuwashawishi wanajamii walio karibu kukubali jukumu kubwa katika uhifadhi wa mfumo wao wa ikolojia.
“Walitoa ahadi kupita kiasi. Walijionyesha kama waokozi waliokuja kutatua matatizo yote ya watu kwa kubadilishana na uhifadhi wa msitu,” anasema Kenneth.
Kwa muda, “pesa kwa ajili ya uhifadhi” ikawa kawaida katika eneo hilo, na ikawatenga wanasayansi chipukizi wa vijijini waliokosa ufadhili wa kushindana na mbwembwe hizo. Hatimaye, ahadi zilizovunjwa zilianza kuondoa imani ya wenyeji kwa wahifadhi wapya kama Kenneth.
“Sasa watu wetu wanaamini kuwa uhifadhi wowote usioambatana na kutupiana pesa haustahili kupewa muda wala kuzingatiwa,” Kenneth aliiambia Mongabay. “Na mtazamo huu ni kikwazo kikubwa. Lazima ubadilike.”
Katika miaka ya hivi karibuni, ametumia muda na rasilimali kupambana na fikra hiyo kupitia kampeni na ushirikishwaji wa jamii – njia ya kujenga tena imani ya wenyeji na uwajibikaji, unaochochewa na upendo kwa mazingira yao wenyewe, si kwa ajili ya pesa zinazopatikana humo.

Vikwazo kwa uongozi wa wanawake
Katika Msitu wa Embobut nchini Kenya, umbali wa kilomita 4,500 (maili 2,800) kutoka kijiji cha Kenneth, Kuto Naomi mwenye umri wa miaka 24 anakabiliwa na changamoto zake lukuki anapojitahidi kusaidia kurejesha usimamizi wa jadi wa msitu huo.
Wafukuzi wanaoungwa mkono na serikali, wakiongozwa na Huduma ya Misitu ya Kenya (KFS), wamechoma mamia ya nyumba za Wasengwer huku wakipiga marufuku makazi katika ardhi ya mababu ya Wasengwer.
Miaka mingi iliyopita, wakati kufukuzwa kulipoanza, masuala ya haki za ardhi na uhifadhi yalionekana kuwa ya wanaume pekee. Lakini siku hizi, wanawake kama Naomi wamejitokeza si kama washirika tu, bali pia kama viongozi katika harakati za Wasengwer. Kwao, Embobut si tu msitu wenye miti ambayo wanaume wanapaswa kuitetea, bali ni mzizi unaounganisha ukoo wa Wasengwer na lugha yao, ujuzi wao wa jadi, na imani yao ya kiroho.
Naomi ni mmoja wa wanakikundi cha wanawake 30 wa Wasengwer kinachoitwa “Berur”, kinachofanya kazi ya kujumuisha maarifa ya asili na mbinu za jadi katika juhudi za kuhifadhi misitu. Wanatoa semina zinazolenga uhifadhi kwa wanawake, wanaratibu shughuli za kupanda miti ili kurejesha mifumo ya ikolojia iliyoharibika, na kuhakikisha usalama wa chakula kwa kukusanya na kuhifadhi mbegu za asili.
Ingawa jamii inapongeza kazi yao, wanaume wengi bado wanapinga ushiriki kamili wa wake zao na binti zao, wakiuona kama usumbufu kwa majukumu ya nyumbani. Na kwa kuwa wanaume, wakisaidiwa na mila na dini, bado wana ushawishi mkubwa katika jamii ya Wasengwer, baadhi ya wanawake wanalazimika kulinganisha jitihada zao za kisayansi na majukumu ya nyumbani — au kuachana kabisa na juhudi hizo.
“Hawana ruhusa kamili kutoka kwa waume zao kufanya shughuli hizi za uhifadhi,” Naomi anasema, akizungumzia changamoto wanazopata baadhi ya wanachama wa kikundi cha Berur.

Katika nchi jirani ya Uganda, mtaalamu wa uhifadhi Aol Nancy anasema ubaguzi wa kijinsia dhidi ya wanawake katika sekta ya uhifadhi umeota mizizi na uko katika sura mbalimbali. “Uhifadhi katika tamaduni za Kiafrika siku zote umechukuliwa kama jukumu la wanaume,” anasema Nancy, ambaye ni afisa anayehakikisha ushirikishwaji wa kijinsia katika shirika la Friends of Zoka, mfuko unaoongozwa na wanawake unaosaidia wanawake wanaoishi katika maeneo ya misitu kuboresha vyanzo vyao vya mapato.
Nancy anasema pia kuna wasiwasi kuhusu usalama na madhara ya kimwili. Kuongezeka kwa hatari ya kubakwa, kushambuliwa au kupigwa risasi, pamoja na mazingira hatarishi ya kazi katika maeneo ya mbali na yenye miinuko, kunafanya familia zisikubali binti zao kuingia katika taaluma hiyo.
Nancy kidogo aache kazi yake ya uhifadhi alipoanza kupokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa watu wasiojulikana. Wanawake ni wachache katika umiliki wa ardhi na misitu katika jamii nyingi, jambo ambalo hupunguza ushawishi wao katika juhudi za uhifadhi.
“Ardhi ni ya wanaume, na uongozi wa jadi uko mikononi mwao,” anasema Nancy. “Katika jamii inayosema nafasi ya mwanamke ni jikoni, anawezaje kuwa kiongozi?” Anasema hali hii imesababisha hali ya kutojali na kukata tamaa miongoni mwa wanawake.
Licha ya changamoto hizo za kihistoria, Nancy anasema jamii kwa sasa inaanza kutambua uwezo na ubora wa wanawake katika uhifadhi wa rasilimali. Na katika baadhi ya jamii, hata uongozi wa jadi wenye misingi ya mfumo dume sasa unawakubali wanawake kama wadau muhimu katika sayansi ya uhifadhi.
Hata hivyo, Nancy anaongeza kuwa kazi ya hawa wanawake wa kizazi kipya katika uhifadhi mara nyingi hairekodiwi wala kupewa kipaumbele, hivyo kuwafanya wasionekane katika jukwaa la kimataifa, wakose ufadhili na nafasi za kushirikiana mitandao ya kitaaluma.

Njia za kutambuliwa
Licha ya vikwazo vingi, baadhi ya wanasayansi vijana wa Kiafrika sasa wanapata kutambuliwa kimataifa na kupata fursa za kazi, jambo linaloashiria matumaini kwa sekta ya uhifadhi.
Adekambi Cole, mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Calabar kilichopo Cross River, amekuwa akivutiwa kwa muda mrefu na sokwe mkubwa wa Cross River, mnyama adimu zaidi duniani na mwenye tabia ya kujificha sana, ambaye inakadiriwa kuwa kuna takriban 300 tu waliobaki porini.
Mwaka 2023, Cole alipewa ufadhili wa masomo kupitia mpango wa Cross River Gorilla Initiative, unaoendeshwa na Wilder Institute-Calgary Zoo kwa kushirikiana na Nigerian Conservation Foundation, ukilenga kutoa mafunzo na msaada kwa viongozi chipukizi katika sayansi ya sokwe.
Cole alishirikiana na walinzi wa wanyamapori na wawindaji wa zamani kuchora mipaka ya Afi Mountain Wildlife Sanctuary kwa kuigawanya katika seli za gridi. Kisha akaweka zaidi ya kamera 12 katika maeneo yaliyokuwa na dalili za shughuli za sokwe. Kazi hiyo ilizaa matunda: mara tatu mwaka 2024, kamera zake zilinasa picha mjongeo za madume wakubwa aina ya silverback. Habari hiyo ilisambaa kwa kasi ndani na nje ya nchi.
“Ilikuwa mafanikio makubwa kwangu na ya kuvutia sana. Nilihisi kuwa na nafasi muhimu katika taaluma hii,” anasema Cole akikumbuka alipoona picha hizo kwa mara ya kwanza. “Unajisikia kuwa na bahati, kwa sababu ni nadra kuona vijana wa Nigeria wenye nguvu na ari kupata msaada katika sekta hii.”
Mwaka 2012, Bashiru, kama Cole, alipata “wakati wa kipekee” kama huo alipochaguliwa kwa ufadhili kutoka U.S. Fish and Wildlife Service, uliolenga hasa kuwawezesha wanasayansi chipukizi wa sokwe barani Afrika.
Leo hii, kuna programu chache, ikiwemo zile zinazoendeshwa na African Wildlife Foundation na Society for Conservation Biology, zinazofanana na mfano huo. Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, programu hizi zinaunga mkono makumi ya wahifadhi wa Kiafrika wanaochipukia ambao wanatafuta njia bunifu za kutatua changamoto za mazingira.

Ushindi mdogo
Ingawa changamoto zinatawala vichwa vya habari, ushindi mdogo unaleta athari ndogo lakini zinazokua kwa kasi. Katika jamii ya Owan Kenneth ya Okwa, kwa mfano, uvuvi unaotumia kemikali ulikuwa ukisababisha uchafuzi wa maji na uhaba wa samaki, jambo lililolalamikiwia na kujadiliwa katika baraza la wenyeji.
Mwaka 2010, wakati wa muhula wa pili wa baba yake kama kiongozi wa jamii, Kenneth alitoa pendekezo lenye ushawishi mkubwa la kupiga marufuku uvuvi wa kutumia kemikali na kuweka ratiba za msimu za uvuvi kwa mito maalum. Baba yake alikubaliana naye, na tamko la kimila likatolewa kuunga mkono mabadiliko hayo.
Leo hii, mito hiyo imerejea kuwa na wingi na utofauti wa samaki. “Sasa kuna samaki wengi katika mito kila mahali,” anasema Kenneth. Lakini mafanikio makubwa kwake si tu idadi ya samaki, bali ni ya kiitikadi: kwamba wamiliki wa misitu ndio wanaoongoza juhudi za uhifadhi, wakichochewa na mapenzi ya kweli kwa mazingira, na si tamaa ya pesa.
Na ni aina hii ya mapenzi ambayo yamemweka Asuquo Nsa Ani kazini kwa zaidi ya miaka ishirini katika Drill Ranch, ambako anawatunza sokwe pori wa aina ya drill (Mandrillus leucophaeus) ambao ameunda nao urafiki wa karibu. “Kuna zaidi ya sokwe kumi na wambili, na najua hadithi za kila mmoja,” Nsa Ani aliambia Mongabay.
“Kila kitu hapa kinahusu mapenzi kwa mazingira,” anasema Nsa Ani. “Hii si kazi ya kila mtu. Mshahara si mkubwa. Bila upendo, shauku, na uvumilivu, huwezi kuwatunza wanyama.” Hivyo basi, alipopokea Tuzo ya Siddle-Marsden ya 2024, inayotambua raia wa Afrika wanaofanya kazi ya kipekee katika vituo vya hifadhi au makazi ya wanyamapori. Ilikuwa ni mshangao mzuri sana.
Wakurugenzi wa mradi huo, pamoja na wafanyikazi wengine na washirika, walikuwa wamemteua kwa siri.
“Ina maana kubwa kwangu. Niliheshimiwa. Ilikuwa nzuri sana,” anasema Nsa-Ani, ambaye ni mzungumzaji mpole na mwenye ustadi thabiti. “Iliongeza ari yangu. Inaweza pia kuwatia moyo wengine.”
Akiwa ameketi kwenye benchi la mbao, anakumbuka upekee wa siku hiyo alipopanda jukwaa, akisindikizwa na watu mashuhuri wa uhifadhi kutoka kote Afrika na nje ya nchi. Anakumbuka picha na shangwe, kupeana mikono kwenye sherehe, taa zinazomulika, na ukumbi wa kifahari.
“Huo ulikuwa wakati mkubwa zaidi maishani mwangu,” anasema.
Picha ya bango: Marafiki wa Nancy Aol huwasaidia wanawake wa vijijini katika jamii za misituni kubadilisha vyanzo vyao vya mapato kupitia kilimo na ufundishaji wa kuweka akiba na uwekezaji. Picha kwa hisani ya Nancy Aol.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kingereza mnamo tarehe 03/06/2025