- Huku ukitambuliwa kama “Jiji la Miti Duniani,” Mji Mkuu wa Uganda, Kampala, umeanza safari ya kubadilisha msitu wake wa mjini kuwa mandhari imara yenye miti mingi asilia.
- Kile kilichoanza kama mwitikio wa kutatua tatizo la miti kuanguka, sasa kimekuwa mkakati mkubwa wa kimazingira unaoshughulikia masuala ya afya, usawa na mabadiliko ya tabianchi.
- Hivi karibuni, Kampala imepanua wigo wa malengo yake kwa kuongeza maeneo ya kijani ili kujumuisha uhifadhi wa viumbe hai na kuunganisha njia za wanyamapori jijini kote.
KAMPALA — Miaka kumi iliyopita, Mji Mkuu wa Uganda, Kampala, ulikuwa ukikabiliwa na tatizo la ajabu – miti ilikuwa ikianguka barabarani, kujeruhi watu na kusababisha uharibifu wa magari na mali nyingine. Halmashauri ya Jiji ilifanya uchunguzi na kugundua kuwa chanzo kikubwa cha tatizo hilo kilikuwa ni miti ya zamani iliyozeeka.
Kufuatia hali hiyo, Mamlaka ya Jiji la Kampala (KCCA) ilianzisha mpango uliosaidia si tu kutatua tatizo la miti kuanguka, bali pia kuleta maboresho ya muda mrefu katika miundombinu ya kijani ya jiji na ustahimilivu wake dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Mwaka 2016, KCCA ilizindua zoezi la miaka miwili la kuhakiki miti katika jiji lote, ambapo wataalamu wa misitu 10 na wataalamu wa takwimu wawili walihesabu na kufanya tathmini ya kila mti kwenye wilaya nne kati ya zile zilizoko katika jiji hilo. Wilaya zilizohusishwa kwenye mpango huo ni; Kololo, Nakasero, Mulago na Makerere.
“Hatukuwa na takwimu za awali. Hatukujua tulicho nacho wala tunapotoka,” alisema mtaalamu wa misitu ya mijini kutoka KCCA, Padde Daniel, alipokuwa akizungumza na Mongabay wakati wa Mkutano wa Misitu ya Mijini uliofanyika Johannesburg, Afrika Kusini, mapema mwaka huu.

Daniel alikuwa mmoja wa wahitimu wapya katika taaluma ya masuala ya misitu walioitwa na KCCA kuongoza juhudi hizo. Yeye na wenzake walihesabu miti kwa njia ya kawaida katika maeneo ya umma na binafsi, zikiwemo hifadhi za mijini. Walikusanya taarifa kwa kutumia vigezo 23, vikiwemo ukubwa wa mti, mahali ulipo, aina ya spishi na hali ya kiafya. Kwa mwaka 2016 pekee, walikagua takriban miti 53,000 ya spishi zaidi ya 300. Kati ya hiyo miti yote, asilimia 80 ilikuwa ya spishi za kigeni, na asilimia 20 pekee ndiyo ilikuwa ya asili ya eneo hilo.
Wakati huo, suala la uboreshaji wa mazingira ya kijani mijini halikuwa linatiliwa mkazo sana katika mijadala ya umma jijini Kampala. Kutokana na ukosefu wa ufadhili kwa ajili ya zana za kidijitali, Daniel na timu yake walitekeleza kazi yao kwa mikono wakitumia kalamu na karatasi.
“Tulilazimika kuwaelezea maana ya mtaalamu wa misitu ya mijini, kazi tunayofanya, na jinsi kazi hiyo itakavyosaidia jiji,” alisema mtaalamu wa misitu na uhifadhi wa mazingira, Marvin Kibalama Bogere, ambaye kwa sasa anasoma shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Tokyo (NODAI), Japan. “Hapo awali, wafanyakazi wengi wa jiji hawakuelewa kwa nini miti ilikuwa ikikaguliwa,” Padde alisema. “Kwa upande wa sayansi, tunaliita zoezi hili hesabu ya rasilimali — miti ni mali yetu.”
Takribani muongo mmoja baadaye, mtazamo huo unazidi kubadilika. Kadri misitu ya mijini na maeneo ya kijani yanavyozidi kutambuliwa kama yenye mchango muhimu katika ustawi wa mazingira, kijamii na kiuchumi kwenye miji duniani kote, Kampala imekuwa mfano bora wa namna ya kutekeleza jambo hili kwa mafanikio.
Mwaka 2021, Jiji la Kampala lilichaguliwa kuwa jiji la kwanza barani Afrika kutambuliwa kama “Jiji la Miti Duniani’’ na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). Tuzo hii inatambua dhamira ya halmashauri za majiji katika kuhifadhi miti na misitu ya mijini.
“Hakuna jiji kuu lingine barani Afrika lililofanya vizuri zaidi ya Kampala katika kusoma na kuweka kumbukumbu za misitu ya mijini,” alisema mshauri mwandamizi katika Kituo cha Utafiti wa Misitu wa Kimataifa (CIFOR) na Agroforestry ya Dunia (ICRAF), Catharine Watson, alipozungumza na Mongabay. “Hata hivyo, wanakabiliwa na changamoto kubwa katika kulifanya jiji kuwa la kijani. Miti ya zamani inaendelea kukatwa kila mara kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Kadhalika, majengo marefu yanayojengwa hayaangalii sehemu ya eneo inayopaswa kubaki kuwa kijani,” aliongeza.
Kama ilivyo kwa miji mingine barani Afrika, Kampala — jiji kubwa zaidi nchini Uganda lenye wakazi wapatao milioni 1.8, linakabiliwa na changamoto ya ukuaji wa haraka wa miji, jambo ambalo linasababisha maeneo ya kijani mijini kutokuwa na nafasi ya kutosha.

“Miti ni sehemu ya mkakati wa afya ya umma, ni njia ya kuhifadhi aina za viumbe, na pia ni chanzo cha ajira,” alisema Watson, akiongeza kuwa wanasiasa na watumishi wa serikali wanahitaji kutambua manufaa mengi ya misitu ya mijini.
Kwa mujibu wa Daniel, Kampala imefaidika kutokana na kuungwa mkono na Serikali, hasa kutoka kwa Meya wa Jiji. “Kwa sasa tunapata uungwaji mkono wa kisiasa kwa ngazi ya meya, jambo linalotupa nguvu ya kuendelea kufanya kazi tunayoifanya.”
Tangu juhudi za kuhesabu miti zilipoanza mwaka 2016, Kampala imepima hekta 200 (takriban ekari 500) za maeneo ya kijani kibichi, imepiga picha za kijiografia miti 134,000 katika wilaya nne za jiji, na kujitolea kupanda miti 8,000 kila mwaka. Sehemu kubwa ya kazi hii inafanywa kwa kutumia zana za ramani za kijiografia na teknolojia za uchunguzi wa mbali ambazo zinasaidiwa na washirika wa maendeleo kama vile FAO.
Ukaguzi wa awali ulionyesha matokeo ya kushangaza ambayo yaliweka msingi wa juhudi za muda mrefu.
“Tuligundua kwamba kulikuwa na tofauti kati ya maeneo mbalimbali: Baadhi ya maeneo yalikuwa na miti yenye afya, wakati mengine hayakuwa na miti kabisa,” alisema Daniel.
Kwa kutumia seti ya data za awali, Kampala ilitengeneza mkakati wa miaka 20 iliyouita Urban Forest Management Plan (Kiswahili, Mpango wa Usimamizi wa Misitu ya Mijini). Hati inayobainisha mradi huo, ambayo haikuwekwa hadharani lakini Mongabay imepata nakala yake na kuipitia, inaeleza jinsi jiji linavyopanga kuongeza utofauti wa aina za miti asilia, kuunda mfumo uliopangwa wa kusimamia msitu wa mijini, kuongeza uelewa kwa wananchi, na kuongeza idadi ya miti kutoka13 hadi 30 kwa kila ekari (3274 kwa kila hekta) katika jiji lote.
“Ulinzi ambao miti hutoa uko dhahiri,” alisema Bogere wakati akizungumzia athari za joto kali maeneo ya mijini, dhana inayoelezea jinsi joto linavyojikusanya katika maeneo yenye majengo mengi, kama vitongoji vya biashara vya kati. “Kama tutaweza kufuata viwango vifanavyoelezwa katika mkakati, tunaweza kupunguza athari ya joto katika mtaa wa biashara wa kati.”
Kwa mujibu wa Daniel, kutekeleza Mpango wa Usimamizi wa Misitu ya Mijini hakutatatua athari za joto kali maeneo ya mijini pekee, bali itasaidia pia kwenye kuzuia mafuriko na ubora wa hewa. “Ubora wa hewa yetu uko juu zaidi ya viwango vilivyopendekezwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO),” alisema.
Kama ilivyo kwa miji mingine mingi duniani, jiji la Kampala limekuwa likikumbwa na matukio ya hali mbaya ya hewa kwa kiwango kikubwa zaidi katika miaka ya hivi karibuni — ikiwemo kuongezeka kwa joto, mvua kubwa, na mafuriko makubwa zaidi. Katika kukabiliana na changamoto hizi, wapangaji wa jiji na wanaikolojia wameanza kuangalia miti kama njia bora na ya gharama nafuu ya kupunguza athari hizo.
Hata hivyo, Daniel na Bogere wanasema kuwa ili kuwe na mabadiliko ya kweli, matunzo ya muda mrefu ni jambo la msingi.
“Misitu ya mijini hapa Kampala siyo tu ya kupanda miti, bali ni kukuza miti,” alisema Daniel, na kisha kuongeza, “Tunahitaji miti hiyo iendelee kustawi hadi kwenye msimu wa kiangazi wa kwanza na wa pili.”
Daniel alifafanua kuwa maono yao si tu kuhesabu miche, bali kuhakikisha inastawi na kuweza kuunganishwa vyema na mfumo wa ikolojia wa jiji.

Mti uliooteshwa kando ya barabara ya waenda kwa miguu na kufa ndani ya mwaka mmoja hautimizi kusudi lake. Kwa sababu hiyo, Kampala ilianzisha kile ambacho wataalamu wanakiita “Dashibodi ya Ufuatiliaji wa Afya ya Miji”, ambayo ni nyenzo ya kidijitali iliyotengenezwa kwa ushirikiano na FAO inayofuatilia afya na uhai wa kila mti. Dashibodi hii husaidia kuchukua hatua za haraka, kufuatilia hatari na kusaidia kufanya maamuzi endelevu.
Kutokana na kuongezeka kwa hofu kuhusu upotevu wa bioanuai, Kampala kwa sasa inajiandaa kuchukua hatua itakayoiwezesha kuwa mji unaostahimili mabadiliko ya tabianchi na ulio rafiki kwa wanyamapori: ukiboresha “miundombinu ya bluu” kwa kuunganisha mifumo ya maji iliyosanifiwa na maeneo asilia ya mabwawa na mito. Hatimaye, wapangaji wa jiji wanakusudia kuandaa mpango kabambe wa miundombinu ya kijani na bluu.
“Hatukuishia tu kwenye mimea, bali tuliuliza: Je, vipi kuhusu wanyama na bioanuai? Je, tunahakikisha kuwa wanyamapori wanatunzwa?” alisema Daniel.
Kampala ni makazi ya aina mbalimbali za wanyamapori, baadhi yao wakiwa kwenye orodha ya spishi zinazohitaji ulinzi wa uhifadhi. Katika utafiti uliofanyika mwaka 2023 ambao Mongabay imeupitia, lakini haujachapishwa mtandaoni, kabla ya kuandaliwa kwa mpango kabambe wa jiji la Kampala, mamlaka ilitambua njia za bioanuai zitakazosaidia kuunganisha makazi ya wanyamapori yaliyokatwakatwa na miji inayokua kwa kasi. Lengo ni kuruhusu ndege, vipepeo na wanyama wengine kuzunguka katikati ya maeneo ya kijani.
Kwa Daniel, changamoto kubwa bado ni kwamba halmashauri zilizo nje ya jiji haziungwi mkono na wananchi lakini pia hakuna utashi wa kisiasa wa kutosha kuweza kuweka mipango vizuri.
“Bila matumizi ya ardhi yaliyo na mpangilio, maeneo ya mabonde ya mafuriko yanajengwa, vilima vinamomonyoka, na joto linaongezeka,” alisema, akiongeza kuwa sehemu muhimu ya kufanya mambo yawe sahihi ni kushirikisha jamii. “Kama watu wataelewa kwa nini tunapanda miti na faida yake kwao ni nini, basi wataona mradi ni wao. Na hapo ndipo mabadiliko ya kweli hutokea.”
“Tuna hali ya hewa, na tuna watu,” alisema Bogere. “Hali ya hewa inataka miti ikue, na watu pia wanaitaka.”
Picha ya bango: Mwonekano wa katikati ya Jiji la Kampala. Picha na Padde Daniel.
Nukuu:
Ettinger, A. K., Bratman, G. N., Carey, M., Hebert, R., Hill, O., Kett, H., … Wyse, L. (2024). Street trees provide an opportunity to mitigate urban heat and reduce risk of high heat exposure. Scientific Reports, 14(1). doi:10.1038/s41598-024-51921-y
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya kiingereza mnamo tarehe 15/08/2025.