- Huko Shimoni, Kenya, bandari mpya ya uvuvi inatarajiwa kufunguliwa baada ya kukamilishwa mwezi wa Saba.
- Wakati serikali inawaahidi wenyeji fursa za kazi na biashara pindi shughuli zikianza, baadhi ya wakazi wanaona madhara zaidi ya bandari kuliko manufaa.
- Baadhi ya shughuli za uhifadhi – ikiwa ni pamoja na miradi ya kurejesha nyasi za baharini, matumbawe na mikoko pamoja na uvuvi, kilimo cha mwani na shughuli za utalii – tayari vimeathirika wakati wa awamu ya ujenzi wa bandari, iliyoanza mwaka wa 2022, wenyeji wa eneo hilo wanasema. Wanahofia kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi wakati bandari itakapofunguliwa, hasa iwapo mchakato wa uchimbaji utaendelea.
- Afisa wa serikali ya kaunti alisema kaunti ya Kwale inafuatilia hali hiyo na aliahidi kupunguza athari zozote na kulinda shughuli za uvuvi na juhudi za uhifadhi.
SHIMONI, Kenya — Nyuma ya lango la shamba dogo lenye msitu kando ya bahari huko Shimoni, mji mdogo ulioko pwani ya kusini mwa Kenya, maandalizi ya kurejesha matumbawe yalikuwa yakiendelea alasiri moja mwezi Machi. Sehemu moja ya kiwanja ilikuwa imetapakaa kwa sinki za zege, ngome za chuma na plastiki na vizuizi vya kupachika. Vijana wa kiume na wa kike walitumia fursa ya kivuli kufanya kazi wakiwa wamekingwa na jua kali la pwani. Walikuwa wakijenga miundo ya miamba ya kushikilia matumbawe machanga ambayo hivi karibuni wangepanda karibu sana na baharini, sehemu ya mradi unaoongozwa na tawi dogo la Shirika lisilokuwa la kiserikali la Uholanzi, REEFlution. Tangu mwaka 2018, mradi huo umeweka miundo 3,600 ya miamba bandia ili kurejesha miamba ya matumbawe kwenye zaidi ya mita za mraba 5,000 (futi za mraba 54,000) za Mkondo wa Wasini.
Kwa mbali kidogo magharibi mwa kiwanja cha REEFolution, pia kwenye Chaneli ya Wasini, bandari mpya ya uvuvi inakuja. Majengo yake makubwa ya rangi ya samawati na nyeupe yametawala mandhari. Jeti mpya imefunika ile ya awali iliyokuwa inatumiwa na wavuvi wa ndani. Hivi karibuni, wenyeji wataanza kuona meli kubwa za kimataifa za uvuvi zikitia nanga kwenye bandari hiyo. Mradi huo wa bandari, ambao umeungwa mkono na Rais wa Kenya, William Ruto, uliigharimu serikali shilingi bilioni 2.6 za Kenya (sawa na dola za Marekani milioni 20) na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni.
Huku serikali ikiwaahidi wenyeji fursa za ajira na biashara pindi shughuli zikianza, wakazi wengine wanaona madhara zaidi kuliko faida kutokana bandari hiyo. Shughuli za uhifadhi na watu kujipatia riziki tayari zimeathirika wakati wa awamu ya ujenzi, iliyoanza mwaka wa 2022, na inahofiwa kuwa huenda zikaathiriwa zaidi baada ya bandari kufunguliwa.


Kulikuwa na “uharibifu wa moja kwa moja wa makundi ya matumbawe na nyasi za bahari kwenye eneo la ujenzi,” Ewout Knoester, mwanasayansi mkuu katika REEFolution, aliiambia Mongabay katika barua pepe. Lakini hadi sasa, matumbawe katika eneo pana zaidi, ikiwa ni pamoja na kwenye sehemu ya urejeshaji ya REEFolution, mwaka 2024, yalionekana kuathiriwa zaidi na wimbi la joto la baharini kuliko ilivyokuwa. Athari hizo zilichangiwa na ubora duni wa maji yaliyotumika wakati wa ujenzi wa bandari.
“Nina wasiwasi kama kweli wataanza kuchimba … matumbawe yaliyosalia katika eneo pana yataathiriwa zaidi,” Knoester alisema, akimaanisha mpango wa kuchimba njia ya meli kwa bandari ambayo bado haijafanyika. Aliongeza kuwa “inategemea ukubwa na muda wa kuchimba, na tahadhari zinazochukuliwa (kama vile uchunguzi wa vibofu) – ikiwa zipo.”
Kwenye taarifa iliyotumwa kwa Mongabay, Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA) ilisema mradi huo wa bandari unajumuisha gati la kisasa, eneo la kutua kwa wavuvi, kituo cha kuhifadhia samaki, kiwanda cha kutengeneza barafu, ghala la kuhifadhia kiwanda cha kusindika samaki na kiwanda cha kutengeneza chakula cha samaki na vifaa vingine vya msaada. “Hakujawa na changamoto kubwa kwa wenyeji kwani kumekuwa na ushiriki wa jamii kabla na wakati wa utekelezaji wa mradi,” ilisema taarifa hiyo. KPA haikujibu maswali ya ufuatiliaji ya Mongabay kuhusu wasiwasi ulioonyeshwa na wanajamii.
Roman Sherah, Waziri wa Kilimo, Mifugo na uUvuvi katika kaunti ya Kwale, ambako ndiko liliko eneo la Shimoni , alisema anakubaliana na KPA kuhusu manufaa ya bandari. “Bandari itaboresha upatikanaji wa wavuvi wa jamii kwenye masoko ya kikanda na kimataifa ya bidhaa za samaki,” Sherah aliiambia Mongabay kupitia barua pepe. “Kituo cha kuhifadhia samaki na cha usindikaji vitapunguza hasara baada ya kuvuna na kuongeza mapato ya wavuvi na ajira katika shughuli za bandari, usafiri, na usindikaji wa samaki utaongeza njia mbadala za watu kujipatia riziki.”
Hata hivyo, Sherah pia alikubali kuwepo kwa uwezekano wa athari mbaya za bandari ambazo zingejitokeza wakati inaanza kazi. Aliiambia Mongabay kupitia barua pepe kwamba uchafuzi wa mazingira kutoka melini na shughuli za bandari “unaweza kusababisha kupungua kwa idadi ya samaki,” na kwamba “ujenzi, uchimbaji unaweza kuharibu miamba ya matumbawe na wavuvi wa wadogo wanaweza kuhangaika kushindana na meli za kibiashara zenye vifaa bora.”


Malalamiko ya Ujenzi
Baadhi ya wenyeji huona mapungufu tu. Said Ahmed, Nibu Mwenyekiti mpya wa Kitengo cha Usimamizi wa Ufukwe (BMU) katika Kisiwa cha Wasini, ng’ambo ya pili ya Wasini kutoka bandarini, ni mmoja. Nchini Kenya, vitengo vya usimamizi wa Fukwe (BMUs), ni mashirika ya kijamii yanayotambulika kisheria ambayo huwaleta pamoja wenyeji wanaotegemea shughuli za uvuvi ili kujiingizia kipato. Wengi, ikiwa ni pamoja na Kitengo cha Usimamizi wa Ufukwe cha Wasini, husimamia maeneo ya uhifadhi ya jamii, yanayojulikana kwa jina la kienyeji kama tengefu, la lugha ya Kiswahili linalomaanisha “kuweka kando.” Tengefu la Wasini lina matumbawe na majani bahari ambayo jamii imekuwa ikijitahidi kuyarejesha kwa miaka mingi kama kitalu cha mazalia ya samaki na kivutio cha watalii.
Licha ya kuwa Naibu Mwenyekiti wa Kitengo cha Usimamizi wa Ufukwe BMU, Ahmed pia ni mkusanyaji data wa Wasini tengefu, ambapo hufuatilia eneo hilo mara mbili kwa mwezi. Mnamo Februari, yeye na wenzake walibaini kuwepo kwa majani bahari kwenye tengefu yasiyo na afya na matumbawe yaliyokuwa yamepauka. Alihusisha yote mawili na mchanganyiko wa udongo kutoka kwa ujenzi wa gati la bandari, mmomonyoko wa udongo kutokana na msimu wa mvua pamoja na joto la juu la maji.
“Nilipotazama majani bahari, hayakuwa na afya njema na yalikuwa yamemebadilika rangi,” Ahmed alisema. “Yalifunikwa kwa udongo na hayakuonekana kuchangamka kama yalivyokuwa kabla ya ujenzi kuanza.”
Mara ya mwisho jamii ilipopanda matumbawe na majani bahari kwenye tengefu ilikuwa Julai 2024. Tangu wakati huo, wamekuwa wakifuatilia hali hiyo. Tangu uongozi mpya wa Kitengo cha Usimamizi wa Ufukwe (BMU) uchukue madaraka mwezi Machi, bado hawajaamua kama wataendelea na urejeshaji kutokana na hali mbaya ya mazingira iliyopo.
Kupiga nyundo kwa sauti kubwa wakati wa ujenzi wa gati, pamoja na udongo, viliwatisha samaki, hii ni kwa mujibu wa wavuvi wa jamii. Wavuvi wengi wa Wasini hutumia mitego ya vikapu na nyavu kuvua samaki, ama kutoka kwenye mitumbwi ya kitamaduni au boti zinazoendeshwa kwa injini au kwa kupiga mbizi kuweka zana zao. Kwa ujenzi huo, iliwabidi wasogee mbali zaidi ili kuvua samaki, jambo ambalo lilikuwa ni kero. Kulingana na Ahmed, sasa wamerejea kwenye uvuvi maeneo ya karibu, lakini upatikanaji wa samaki ni mdogo kuliko ilivyokuwa kabla ya ujenzi kuanza.
Kabla ya ujenzi wa bandari hiyo kuanza, Rashid Mohamed Rashid, mvuvi kutoka Wasini, aliiambia Mongabay kuwa angevua kilo 6 hadi 8 (sawa na pauni 13-18) za samaki kwa siku, ila hali haikuwa hivyo. “Sasa ninavua kati ya kilo 2 hadi 3 za samaki na hii inaniingizia kati ya shilingi za Kenya 600 na 1,200,” Rashid alisema. (Hiyo ni pauni 2.2-6.6 za samaki kwa $4.60-$9.30.) Rashid ni mmoja wa wavuvi 155 katika Kitengo cha Usimamizi wa Ufukwe (BMU) Wasini; wanachama wengine 109 ni wauza samaki na waendesha boti.


Feisal Abdalla na mkewe Amina Sabel wanaendesha biashara ya nyumba za kulala wageni Kisiwani Wasini, ambapo kwa miaka mitatu iliyopita wameshuhudia maendeleo ya bandari ya wavuvi.
Kulingana na wanandoa hao, kabla ya ujenzi kuanza, serikali iliahidi ujenzi kufanywa wakati wa mchana tu. Hata hivyo wanasema, kazi hiyo ilifanyika mchana na usiku. Sehemu ya Wasini inajulikana sana kwa utazamaji wa pomboo, na pomboo maarufu ni ile inayojulikana kwa jina la kitaalam la (Jenasi Tursiops) na nyingine ijulikanayo kama Indo-Pacific, kwa jina la kitaalam la (Sousa chinensis), ambao wanaogelea karibu, nje kidogo ya vyumba vya kulala vya Abdalla na hoteli ya Sabel.
Ujenzi wa gati ambayo iliwatisha samaki iliwaogopesha pomboo pia. “Walipokuwa wakigonga vifaa na kupiga nyundo kwenye ujenzi, pomboo hao walikuwa hawaji kabisa hapa,” Abdalla alisema. “Na wakati mtu alipokuwa akipiga mbizi, ungeweza kusikia kelele ukiwa chini.”
Kuwakaribisha watalii wanaokuja kujionea vivutio vya Kisiwa cha Wasini, ikiwa ni pamoja na pomboo na kuwapeleka kwenye matembezi ya karibu ya hifadhi ya kitaifa ya Kisite Mpunguti, ndio chanzo cha mapato cha Abdalla. Kwa hiyo, kutoweka kwa pomboo hao kulidhuru biashara yake.
Gati sasa imekamilika, na ujenzi uliobaki unafanyika kwenye ardhi. Hata hivyo, mwanga kutoka kwenye nguzo tatu kubwa zilizosimamishwa kwenye tovuti ni mkali sana kiasi kwamba unaathiri biashara ya Abdalla na Sabel, maisha yao ya kibinafsi, na hata wanyamapori wa kisiwa hicho. Kulingana na Abdalla, ndege aina ya popo bawa walikuwa wakitua kwenye miti kando ya nyumba ya kulala wageni ili kula matunda. “Hatuna mwanga wa asili jioni tena,” Sable alisema. “Huwezi hata kulala na mwanga huo wote.”
Ng’ambo ya pili upande wa bara, kusini mwa Shimoni, ni kijiji cha Kibuyuni. Huko, Fatuma Mohamed amekuwa akilima mwani kwa miaka mingi na ni mwanachama mwanzilishi wa Ushirika wa Wakulima wa Mwani Kibuyuni. Alizitaja changamoto za hali ya hewa kuwa ni pamoja na kunyesha mvua kubwa na joto kali ambazo zimesababisha upotevu wa mwani. Na tangu ujenzi wa bandari hiyo uanze, alisema wanachama wa ushirikiano wamepoteza zao la mwani, kutokana na udongo unaoletwa na mawimbi kutoka Shimoni hadi kwenye mashamba yao huko Kibuyuni.
“Wakati gati lilipokuwa likijengwa, udongo ulisombwa hadi Kijiweni ambako uliharibu mwani wote,” alisema. Matope hayo pia yaliua samaki ambao kikundi cha jamii kiliwaweka kwenye vizimba kama sehemu ya mradi wa ufugaji wa samaki, na walilazimika kuanza upya.

Wasiwasi wa siku za usoni
Wasiwasi mkubwa wa wakazi sasa ni kwamba uchimbaji utaanza kwenye mkondo ili kuruhusu meli kubwa kutia nanga bandarini. Tathmini ya Athari kwa Mazingira ya mradi inaonyesha kuwa hilo litatokea wakati wa awamu ya pili ya mradi. “Ujenzi wa bandari ya viwandani utahusisha shughuli za uchimbaji na utupaji ili kufikia rasimu inayotarajiwa ya -8m [-26 ft] ili kuruhusu meli kubwa za uvuvi zinazolengwa kutia nanga bandarini,” Tathmini ya Athari kwa Mazingira ya mradi inasema.
Mohamed alisema anahofia kuwa uchimbaji ukitokea, samaki waliofungiwa, mwani na uvuvi vitavurugwa tena. Wakazi wa Wasini, Shimoni na Kibuyuni walisema wamesikia uchimbaji unaweza kufanywa katika sehemu ya kusini ya bandari – kutoka tengefu ya Wasini Kitengo cha Usimamizi wa Ufukwe hadi karibu na mashamba ya mwani ya Kibuyuni, na hivyo kuharibu miaka mingi ya juhudi za jamii. Hili bado halijatimia, lakini serikali haijatoa kauli kwamba halitatimia.
Tathmini ya Athari kwa Mazingira ya mradi iliona changamoto, ikiwa ni pamoja na “athari za uchimbaji na utupaji kwenye mfumo ikolojia wa baharini, umwagikaji wa mafuta na usimamizi wake, kupoteza maisha na uchafuzi wa mazingira,” na ilipendekeza hatua za kupunguza athari hizo ikiwa ni pamoja na mrundiko wa udongo ambao unaweza kupunguza athari za uchimbaji. Lakini kwa vile mirundiko hiyo haikutumika wakati wa ujenzi wa gati katika awamu ya kwanza, wakazi wa eneo hilo hawana imani kwamba tahadhari zozote zitachukuliwa katika awamu ya pili.
Zaidi ya hayo, kadri ujenzi wa bandari unavyokaribia kukamilika, wakazi walisema wanaamini changamoto zaidi zitakuja, ikiwa ni pamoja na wingi wa samaki watakaoletwa bandarini kuua soko la samaki wao na pia kuvutia wanyama wasiohitajika. “Kwa sababu ya meli hizi kubwa kwenda kwenye kina kirefu cha bahari na kuja kutia nanga hapa bandarini, tunaamini kuwa papa wanaweza kuwafuata hapa … ambayo itakuwa hatari kwetu,” Rashid alisema.
Pia walionyesha wasiwasi wao kwamba juhudi zao za uhifadhi – tengefu, urejeshaji wa matumbawe ya REEFlution, miradi ya kurejesha mikoko na majani bahari – vinaweza kusimamishwa kabisa. “Bila shaka, huwezi kuziambia meli kuepuka baadhi ya maeneo ambayo tumetenga kwa ajili ya kuhifadhi, au kutomwaga mafuta,” Ali Issa, mjumbe wa kamati ya muda ya Shimoni Kitengo cha Usimamizi wa Ufukwe, aliiambia Mongabay. “Watamwaga mafuta na hakutakuwa na samaki. Maeneo ya hifadhi yataharibiwa.”
Wakati huo huo, Abdalla na Sable walisema mustakabali wao Wasini haujulikani kutokana na athari za bandari katika biashara zao. “Giza sana, giza tororo,” ndivyo Sable alivyoiweka. “Tunafikiria sana tunaweza kufanya nini na maisha yetu ya kibiashara, kwa sababu hatuwezi kutegemea hapa. Hujui kinachoendelea, hujui jinsi hali itakavyokuwa, mbaya zaidi. Hakika hatuwekezi tena kwa sasa kwa sababu hatujui kuna manufaa, na kwa kweli tunakuna vichwa vyetu,” Sable alisema.
Kulingana na Sherah, serikali ya kaunti ya Kwale ina taarifa kuhusu athari za ujenzi wa bandari hiyo lakini bado haijafanya tathmini kuthibitisha ukubwa wake. Alisema serikali ya kaunti inafuatilia hali hiyo na ipo tayari kujadiliana na washikadau walioathirika.
“Iwapo athari mbaya zitathibitishwa, tutafanya kazi na mashirika na watengenezaji husika ili kupunguza athari na kuhakikisha kuwa shughuli za uvuvi na juhudi za uhifadhi wa bahari vinalindwa,” alisema.
Picha ya Bango: Baadhi ya wavuvi wanahofia kuwa ujenzi wa bandari mpya utaathiri zaidi upatikanaji wa samaki. Picha na Anthony Langat wa Mongabay.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kingereza mnamo tarehe 23/06/2025