- Miezi sita tangu waasi wa M23 waliojihami kwa silaha wachukue udhibiti wa miji mikuu ya majimbo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wanaharakati wa ndani na picha za satelaiti zilizokusanywa na Mongabaywamebainisha maeneo ya upanuzi wa upotevu wa misitu katika Hifadhi ya Taifa ya Kahuzi-Biega.
- Watafiti wanasema hii ni kutokana na kuporomoka kwa juhudi za uhifadhi, ukosefu wa ufuatiliaji wa hifadhi, ukataji miti mikubwa na uzalishaji wa mkaa ndani ya hifadhi ya taifa. Wakati waasi wa M23 na wanamgambo wengine hawazalishi mkaa moja kwa moja, wanafaidika kwa kutoza ushuru wa usafirishaji na biashara yake.
- Wanaharakati ambao wameshutumu unyonyaji huo haramu wamenyanyaswa, kushambuliwa, au hata kuuawa. Baadhi yao, kama Josue Aruna, wamelazimishwa kwenda mafichoni au uhamishoni baada ya kukabiliwa na vitisho vya kuuawa.
- Mnamo Julai 19, serikali ya DRC na waasi wa M23 walitia saini mkataba wa makubaliano ya kusitisha mapigano, huku wahifadhi wakisema wanatumai hali hii itaweka mazingira ya kurejesha usalama katika eneo hilo na kukomesha uharibifu wa msitu wa mvua.
Miezi sita iliyopita, kundi la waasi la M23 liliuteka mji wa Goma, moja ya miji mikubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Baada ya muda huo, wanaharakati wa ndani, na Mongabay, ambayo ilikusanya picha za satelaiti, walitambua maeneo yenye upotevu mkubwa wa misitu katika Hifadhi ya Taifa ya Kahuzi-Biega, kusini magharibi mwa mji wa Goma. Katika eneo hili kubwa la msitu wa msingi, ni nyumbani kwa sokwe wa nyanda za chini za mashariki (Gorilla beringei graueri). Watafiti wanahusisha ongezeko hili la upotevu wa misitu na upanuzi wa uzalishaji haramu wa mkaa, kuporomoka kwa utekelezaji wa uhifadhi, na migogoro ya ardhi.
Mnamo Novemba mwaka 2021, kundi la waasi linaloungwa mkono na Rwanda liliibuka tena katika Jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC baada ya takriban muongo mmoja wa kutokuwepo katika eneo hilo. Matukio yaliongezeka mnamo Januari na Februari mwaka 2025, wakati waasi wa M23 walipoanzisha mashambulizi ya haraka na kutwaa udhibiti wa maeneo muhimu katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini, ikiwa ni pamoja na miji mikuu ya majimbo husika, Goma na Bukavu. Maeneo haya yamesalia chini ya udhibiti wa waasi M23 hadi leo.
Zaidi ya miji hii mikubwa, kundi lililojihami pia linadhibiti ufikiaji wa maeneo muhimu ya uchimbaji madini na maeneo muhimu yaliyolindwa kimataifa, kama vile Hifadhi ya Taifa ya Virunga na Hifadhi ya Taifa ya Kahuzi-Biega, Maeneo ya Urithi wa Dunia wa UNESCO. Hadi sasa, mzozo huo una athari inayoonekana kwa bioanuwai kwa kuzidisha changamoto zilizopo za uhifadhi na ukataji miti, watafiti wanasema.
Katika Kahuzi-Biega, picha za satelaiti kutoka Copernicus, kipengele cha uchunguzi wa Dunia cha mpango wa anga za juu wa Umoja wa Ulaya, zinaonyesha kupungua kwa kasi kwa misitu kati ya Januari na Julai 2025. Maeneo yaliyokuwa ya kijani kibichi miezi sita iliyopita, yakiwa yamefunikwa na msitu mnene, wa msingi, sasa yanaonyesha mabaka ya ardhi tupu. Mongabay ilibaini pia upanuzi wa upotevu wa misitu katika maeneo mengi yanayojulikana, kama vile ncha ya kaskazini ya sekta ya nyanda za juu, upotevu wa miti unaovuja kutoka kwenye mpaka hadi kwenye hifadhi, na maeneo mapya katika eneo la Kabare na karibu na kijiji cha Muhonga, ambapo ukataji miti ulikuwa umesitishwa hapo awali mwaka 2019.


“Mipaka ya msitu huko Kabare imefunguliwa tena kwa ajili ya matumizi mabaya tangu waasi wa M23 walipochukua udhibiti, kwani juhudi za kutekeleza sheria za uhifadhi katika eneo hili zimekoma kwa kiasi kikubwa,” wanasema watafiti Fergus O’Leary Simpson na Lara Collart wote kutoka Taasisi ya Sera ya Maendeleo (IOB) katika Chuo Kikuu cha Antwerp cha Ubelgiji.
“Mkaa na mbao zinazozalishwa katika eneo hili vimekuwa vikiwanufaisha watumiaji wa mijini huko Bukavu,” wanaongeza.
Wanasema hali hiyo haishangazi, huku wakiliita eneo lililoathiriwa kama “eneo wazi lisilo na udhibiti.”
Katika chapisho lililomo kwenye toleo la Jarida la hivi karibuni la Gorilla, watafiti hao wawili wanaonya kwamba waasi wa M23 walitaifisha silaha za walinzi wa eneo hilo walipofika katika makao makuu ya mbuga hiyo huko Tshivanga. Kulingana na watafiti hao, hatua hiyo iliwafanya walinzi kushindwa kuzuia na kuchukua hatua dhidi ya uchomaji haramu wa mkaa ndani ya mbuga hiyo.
“Sehemu kubwa ya nyanda za juu za mbuga hiyo bado lina mzozo mkubwa na mara kwa mara kukabidhiwa mikononi mwa waasi wa M23 au wanamgambo wanaounga mkono Kinshasa (wanaoiunga mkono serikali),” wanaandika. “Kwa hiyo ni vigumu kuhusisha uharibifu wa eneo lolote la bustani kwa mtu yeyote- ikiwa ni pamoja na waasi wa M23. Kutokana na ukweli kwamba mbuga hiyo haijulikani sana kama Virunga, hii inapunguza motisha kwa waasi wa M23 kuipa kipaumbele katika .”
Watu hutengeneza mkaa kutokana na miti mipya iliyokatwa, na kuichoma kwenye matanuru ya kienyeji kwa muda wa wiki moja. Kila kilo ya mkaa inayozalishwa inahitaji kilo 4-10 za kuni. Pamoja na mashambulizi ya waasi wa M23 huko Kivu, mamia kwa maelfu ya wakazi wa DRC wamelazimika kukimbia makazi yao. Mnamo Julai mmwaka 2025, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (UNOCHA) ilikadiria kuwa Kivu Kusini pekee ilipokea wakimbizi wa ndani milioni 1.5. Wengi wao wanategemea mkaa kwa ajili ya kupikia.

Uzalishaji wa mkaa pia ni sehemu ya mtandao wa biashara ambapo baadhi ya machifu wa jamii asili ya Batwa, wanaozidi kuwa na silaha, huwatoza Wabantu ada ya kuwaruhusu kukata miti katika misitu ya mbuga hiyo, kwa mujibu wa watafiti wa eneo hilo waliozungumza na Mongabay kwa masharti ya kutotajwa majina yao kwa sababu za kiusalama. Watu wengi wa jamii za Bantu huingia tu kwenye mbuga wenyewe, wanasema. Kisha mkaa huuzwa katika masoko madogo kando ya mpaka wa mbuga, kama vile Katasomwa, Bugamanda na Buzunga. Kutoka hapo, husafirishwa hadi kwenye masoko makubwa zaidi ya Kabamba na Katana, kabla ya kupakiwa kwenye malori kuuzwa Bukavu, au katika boti kwenye bandari za Ihimbi na Kasheke zinazopelekwa soko la Goma.
“Si waasi wa M23 wala makundi ya Wazalendo” – “wazalendo” kwa Kiswahili, wakimaanisha vikundi mbalimbali vinavyowapinga waasi wa M23 – “kuandaa moja kwa moja uzalishaji,” O’Leary Simpson na Collart wanasema. “Badala yake, wao hutoza ushuru kwenye njia za biashara zinazotoka kwenye mbuga, wakiwa hawafanyi lolote kuzuia shughuli hiyo.”
Mongabay iliwasiliana na Muungano wa Mto Kongo (AFC – Alliance Fleuve Congo), chombo cha kisiasa ambacho kinajumuisha waasi wa M23, kuhusiana na upotevu wa misitu katika mbuga hiyo na juhudi za waasi wa M23 katika uhifadhi lakini hakupata majibu kufikia hadi wakati wa kuchapishwa taarifa hii.
Vitisho vya kifo kwa kuongea
Wanaharakati wa mazingira wahisi maisha yao kuwa hatarini
“Hifadhi ya Taifa ya Kahuzi-Biega inaporwa kimfumo,” anasema Josué Aruna, mwanachama wa Stop Ecocide International na Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Uhifadhi ya Bonde la Kongo (CBCS). “Kuna uvunaji wa miti mikavu aina ya redwood (Pterocarpus tinctorius) na utengenezaji wa mkaa, lakini pia kuna usafirishaji haramu wa wanyamapori – ikiwa ni pamoja na sokwe wanaouzwa. Ikiwa hakuna kitakachofanyika kukomesha hili, mbuga inaweza kutoweka kabisa.”
Aruna amezungumza na jumuiya ya kimataifa, kitendo ambacho anasema sasa kinaweka maisha yake hatarini.
“Siko salama tena huku Bukavu. Walikuja ofisini kwangu mara tatu kujaribu kuniua; walijaribu kuniteka nyara lakini wakashindwa. Simu yangu imedukuliwa; timu yangu inafuatiliwa mara kwa mara… Vyanzo vyangu vilithibitisha kwamba nimewekewa nadhiri kichwani mwangu, kwa hivyo ninaishi mafichoni,” Aruna anasema.


Hajarudi nyumbani kwa miezi kadhaa sasa, anaiambia Mongabay kwa simu, na mara kwa mara huzunguka kwa hofu ya kuuawa. Wale wanaomtishia hawajajitambulisha, kwa hiyo hajui ni nani hasa anayemfuata, Aruna anaongeza.
“Huu ni wakati ambapo watu wanaweza kusuluhisha matokeo haraka, kwa kutumia majambazi wenye silaha wanaozurura mjini. Sauti yangu, na ya watetezi wengine wa mazingira, ndiyo inayosumbua. Wanataka kuinyamazisha,” anasema.
Tangu Bukavu iwe chini ya udhibiti wa waasi wa M23 mnamo Februari 2025, shirika la UNOCHA limeripoti kuenea kwa uhalifu na “matukio kadhaa ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanayohusisha wahusika wenye silaha… ikiwa ni pamoja na kushambuliwa na kupigwa, utekaji nyara, ndoa za kulazimishwa, na ubakaji wa watoto.”
Aruna sio mtetezi pekee wa mazingira na haki za binadamu ambaye amelazimika kukimbia tangu mashambulizi ya waasi wa M23. Wanaharakati wengi wamekimbilia nchi jirani; kwa wale ambao wamechagua kukaa, hali ni hatari sana.
“Wengi walikimbilia Burundi, Uganda, au Uvira,” mji wa Kivu Kusini kwenye mpaka wa DRC na Burundi, “ambako serikali bado inadhibiti eneo hilo,” anasema Espoir Kitumaini Kakoy, mkuu wa UMOJA-AFRICA RDC, shirika la ulinzi wa mazingira. “Wengi wametekwa nyara, wameuawa, au wametoweka. Kwa mfano, wanaharakati watatu kutoka vuguvugu la Lucha” – Lutte pour le Changement, au “Fight for Change,” kikundi cha kutetea haki za binadamu – “waliuawa hivi karibuni.”
Kakoy anaongeza kusema kwamba “wengine sasa wanafanya kazi kwa kificho. Ukitambuliwa, umekwisha – wanatufuata. Tunapokea vitisho.”

Kakoy mwenyewe ni mkimbizi wa ndani na amejificha. Anafuatilia unyanyasaji dhidi ya haki za binadamu na watetezi wa mazingira kwa shirika la Ofisi ya Pamoja ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNJHRO) nchini DRC, hasa katika Kivu Kaskazini. Lakini anasema hali ni mbaya vilevile huko Kivu Kusini.
“Ni vigumu kukadiria ni wanaharakati wangapi wameuawa tangu waasi wa M23 walipochukua udhibiti wa eneo hilo, lakini tunaendelea kufuatilia na kuandika ukiukwaji wote, hata kama sisi wenyewe tunahamishwa na vitisho,” anasema.
Mnamo Julai 19, waasi wa M23 na serikali ya DRC walitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Qatar. Hii ilifuatia makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mjini Washington, D.C, nchini Marekani, mwezi uliopita kati ya DRC na Rwanda, mfadhili mkuu wa waasi wa M23. Makubaliano hayo mapya yanaelezea majadiliano zaidi kwa lengo la kufikia makubaliano ya amani ya kina. Wahifadhi wanasema wanatumaini hii itaweka mazingira ya kurejesha usalama na kukomesha uharibifu wa misitu.
Picha ya bango: Sokwe mchanga wa Grauer akiwa katika Mbuga ya Taifa ya Kahuzi-Biega, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Picha imepigwa na Mike Davison kupitia Flickr (CC BY-ND 2.0)
Nukuu:
Collart, L., & O’Leary Simpson, F. (2025). Armed conflict menaces gorilla habitat in eastern DRC. Gorilla Journal, 70(1). Imetolewa kutoka https://www.berggorilla.org/en/journal/issues/journal-70-1/2025/article-view/armed-conflict-menaces-gorilla-habitat-in-eastern-drc
Urban, J., Berger, J., Botha, Y., Boafo-Mensah, G., Mkwate, A., Bentson, S., & MacCarty, N. (2025). Quantifying conversion factors for the value chain of charcoal production in Malawi and Ghana. (Master’s thesis, Oregon State University). Imetolewa kutoka https://ir.library.oregonstate.edu/concern/technical_reports/2f75rj10q
O’Leary Simpson, F., Titeca, K., Pellegrini, L., Muller, T., & Muliri Dubois, M. (2025). Indigenous forest destroyers or guardians? The Indigenous Batwa and their ancestral forests in Kahuzi-Biega National Park, DRC. World Development, 186, 106818. doi:10.1016/j.worlddev.2024.106818
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 31/05/2025