- Kwa mujibu wa utafiti mpya, spishi mpya ya samaki wa killifish au kwa jina la kisayansi Nothobranchius sylvaticus, imegunduliwa katika mabwawa ya msimu kwenye maeneo ya kinamasi yanayokauka ya msitu wa kihistoria wa Gongoni uliopo pwani ya Kenya.
- Wanasayansi kutoka Canada, Ufaransa, Kenya na Afrika Kusini wameripoti kuwa makazi ya samaki hao, ambayo ni ya msimu na yapo kwenye Mto Mkurumudzi katika pwani ya kusini-mashariki mwa Kenya, yako hatarini na yanatishia uwepo wa spishi hiyo.
- Samaki huyo wa killifish, ambaye ni wa kipekee kwa kuwa na magamba ya bluu yenye mng’ao, alama nyekundu na mapezi yenye rangi angavu, ametunzwa katika Makumbusho ya Taifa ya Kenya na pia katika Makumbusho ya Kifalme ya Afrika ya Kati.
- Mtaalamu mmoja ametoa wito kwa Msitu wa Gongoni kutangazwa rasmi kuwa eneo muhimu la bioanuwai, pamoja na kushirikisha jamii za eneo hilo katika kuwalinda samaki hao wa maji baridi, ili kuhakikisha wanaendelea kuishi na kuepuka hatari za kutoweka.
NAIROBI – Spishi mpya ya samaki wa killifish, inayojulikana kisayansi kama Nothobranchius sylvaticus, imeonekana katika mabwawa ya msimu ya Msitu wa kale wa Gongoni nchini Kenya, kwa mujibu wa utafiti mpya.
Katika utafiti uliochapishwa mwezi huu kwenye jarida la Zootaxa, wanasayansi kutoka Canada, Ufaransa, Kenya na Afrika Kusini wanasema kuwa uhai wa spishi hiyo ya samaki uko hatarini kutokana na eneo lake la kuishi kuwa dogo na kupungua kwa kasi. Makazi hayo ni sehemu ya Mto wa msimu wa Mkurumudzi, ulioko pwani ya kusini-mashariki mwa Kenya.
N. sylvaticus, jina la Kilatini lenye maana ya “anayehusiana na msitu,” ni samaki wa kwanza wa aina ya killifish anayestahilimi kuishi msituni, na sampuli yake ilichukuliwa kutoka Msitu wa Gongoni mwaka 2017 na 2018.
Magamba yake ya bluu yanayomeremeta, alama nyekundu zilizo wazi kichwani, na mapezi yenye rangi angavu ndiyo yanayomtofautisha na spishi nyingine za Nothobranchius. Sampuli ya samaki huyo imehifadhiwa katika Makumbusho ya Taifa ya Kenya jijini Nairobi, na sampuli za kulinganisha zimehifadhiwa katika Makumbusho ya Kifalme ya Afrika ya Kati huko Tervuren, Ubelgiji.
Kwa mujibu wa kiongozi wa utafiti huo, Profesa Dirk Bellstedt, mtaalamu mstaafu wa biokemia kutoka Chuo Kikuu cha Stellenbosch, Afrika Kusini, mwaka 2017 aliitwa na Quentin Luke, mtaalamu wa mimea kutoka Makumbusho ya Taifa ya Kenya na mshiriki mwenza wa utafiti, kusaidia kufuatilia mazingira karibu na mgodi wa Base Titanium ulioko Kaunti ya Kwale, karibu na mji wa Diani Beach, pwani ya Kenya.
“Nimewahi kufanya utafiti kuhusu mimea ya misitu katika maeneo ya pwani ya Afrika Mashariki hadi Afrika Kusini, na ndiyo maana nilivutiwa sana. Nilipofika pale, niliona kuna madimbwi ndani na nje ya msitu. Kwa kuwa pia nilikuwa nafanya kazi kwenye mradi wa bara zima la Afrika kuhusu jenasi ya samaki wa Nothobranchius, niliamua kuwa hili ni eneo muhimu kuchunguza,” Bellstedt aliambia Mongabay.

Kwa bahati, alikuwa tayari ana taarifa kuhusu spishi za Nothobranchius wa pwani ya Kenya, alizopewa na mwenzake, Béla Nagy, mtaalamu wa wanyamapori wa Hungary aliyeishi Ufaransa, ambaye amebobea kwenye masuala ya samaki wa killifish wa Afrika, hasa wa jenasi ya Nothobranchius. Mtalaamu huyu ambaye alishirikiana naye katika andiko, amegundua pia spishi za Nothobranchius, samaki wanaojulikana kwa ukakamavu na ameeleza spishi nyingi mpya za Nothobranchius kote Afrika.
“Nilijua kuwa baadhi ya (Nothobranchius) zinaweza kupatikana katika eneo hilo. Mgodi wa (Base Titanium) uliomba nitathmini samaki katika eneo la Msitu wa Gongoni chini ya mgodi kusaidia katika ufuatiliaji wao wa mazingira,” anasema Bellstedt.
Akiwa na viatu vya kuingia majini, neti na makopo, yeye na wafanyakazi wake walianza kukusanya sampuli za samaki. “Nilipata viumbe wadogo wenye ukubwa wa kama sentimita ,moja hadi mbili wa spishi hiyo, ambao walionekana kuwa Nothobranchius, lakini hawakuweza kutambuliwa hadi ngazi ya spishi.
Uchambuzi unaohusiana na masuala ya kinasaba wa spishi hiyo ya Kenya ulionyesha kuwa siyo tu spishi mpya bali pia ni mfuatano wa asili wa spishi mpya kabisa kwa Kenya, kwa maneno mengine, ugunduzi wa kipekee unaoangaliwa kwa mtazamo wa Kenya,” Bellstedt aliiambia Mongabay.
Mnamo mwaka 2018, walikusanya tena mifano ya samaki waliokomaa na kutathmini muundo wao na wakagundua tofauti za wazi za muundo kutoka kwa spishi nyingine za Nothobranchius zinazopatikana karibu, kama ushahidi wa pili kuthibitisha kuwa ni spishi mpya.
“Ili kuhifadhi spishi, lazima ujue kuwa zipo katika eneo fulani na utafiti huu umebaini kuwa msitu huu una spishi ya samaki wa asili wa eneo hilo, na kuufanya kuwa wa kipekee kabisa Kenya. Spishi hii ni sehemu muhimu ya utofauti wa viumbe wa eneo hilo na inaongeza maarifa kuhusu spishi za asili za eneo hilo,” anasema Bellstedt.

Watafiti wanasema Msitu wa Gongoni, unaojumuisha takriban kilomita za mraba 8.2 (takriban maili za mraba 3.2), una zaidi ya miaka milioni 7.1 na unaonyesha mfano wa mchoro wa Afrika Mashariki, ambao ni mchanganyiko wa savana na sehemu za misitu zinazotambaa kutoka Pondoland Afrika Kusini hadi pwani ya kusini ya Somalia.
“Sehemu ya msitu ilikuwa na unyevunyevu zaidi muda wote, na katika nyakati za ukame, spishi za savanna huenda zilikauka, lakini spishi hii haikufa. Pwani ya Mashariki ya Afrika ina sehemu za misitu zinazojirudia kutoka Somalia hadi Afrika Kusini, ambazo zina spishi nyingi za mimea, wanyama na ndege zinazojitokeza katika kila sehemu ya msitu, na huyu ni samaki wa kwanza kuonekana kuwa wa kipekee katika sehemu ya msitu. Umri wa samaki, uliobainishwa kwenye uhakiki wa phylogenetic, unaonyesha umri wa sehemu ya msitu. Hivyo, umri wa sehemu ya msitu, sifa maalum ya mimea, unahesabiwa kulingana na samaki wanaoishi humo,” anasema Bellstedt.
Kwa mujibu wa Luke, ugunduzi huu unaonyesha hitaji la haraka la kuhifadhi sehemu hii ya msitu na kulinda spishi hiyo.
“Kuvutwa kwa maji na mgodi ilikuwa tishio, lakini mgodi umemaliza shughuli zake mwishoni mwa mwaka 2024, hivyo tishio hili limekwisha,” anasema Bellstedt, akiongeza kwamba kuna haja ya kuzuia uvamizi wa binadamu na kilimo katika sehemu ya msitu, ikiwemo kuvutwa kwa maji kwenye mpaka wa kusini kwa ajili ya kilimo cha mazao.
Dario Valenzano, mwanabiolojia anayefanya utafiti wa killifish wa Afrika na ambaye hakuhusika katika utafiti huu, anakubaliana kwamba vitendo vya binadamu kama kilimo na uchimbaji madini vinaweza kuharibu sana makazi madogo ya killifish.
“Wanaishi katika maeneo madogo ambapo chanzo cha maji pia huwa hakidumu kutokana na ukame na hii tayari ni tishio kwao. Kenya na Tanzania zina aina nyingi na ueneaji mkubwa wa samaki spishi za killifish, na kuna haja ya kuwalinda wasitoweke. Tunahitaji kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wao, na upekee wao ili waweze kuona umuhimu wa kuwalinda,” anasema Valenzano, ambaye ni mkuu wa Kundi la Utafiti la Valenzano linaloshirikiana na Taasisi ya Leibniz ya Uzee – Fritz Lipmann Institute nchini Ujerumani.

Kwa mujibu wa Ashley Simkins, mwanafunzi wa shahada ya uzamivu (Ph.D.) katika taaluma ya zoolojia katika Chuo Kikuu cha Cambridge anayevutiwa na tafiti kuhusu spishi zilizo hatarini kutoweka, ulinzi wa spishi hiyo katika makazi yake ya asili ni jambo la msingi, kwa kuwa inategemea sana makazi hayo, hasa katika hatua muhimu za maisha kama ukuaji wa mayai.
“Iwapo eneo hili litaathiriwa vibaya au kupotea kabisa, spishi hii huenda ikatoweka. Baadhi ya spishi ni vigumu sana kuzalishwa zikiwa maeneo mapya, hasa pale ikolojia yake inapokuwa haieleweki vizuri; na kwa kuwa hii ni spishi mpya, huenda hali hiyo ikajitokeza. Kutokana na hili, au mabadiliko yoyote ya kitabia yanayotokea zikiwa maeneo mapya, ni bora zaidi kusaidia uzalishaji na ukuaji wa idadi yake katika mazingira yake ya asili badala ya kutegemea ufugaji katika maeneo mapya,” Simkins anaiambia Mongabay.
Anatoa wito wa kutambuliwa rasmi kwa Msitu wa Gongoni kama eneo muhimu la bioanuwai, na kuhusisha jamii za wenyeji katika kutafuta njia za kulilinda eneo hilo ili kuilinda spishi hiyo na makazi yake.
“Kwa kuwa huyu ni samaki mdogo wa maji baridi, na tukikadiria kuwa ana uwezo mkubwa wa kuzaliana kwa wingi, kulinda makazi yake – kupitia kutangazwa eneo lake kuwa la hifadhi au njia nyingine – kunatosha kumsaidia arejee katika hali ya asili na kuepuka hatari.”
Picha ya bango: Watafiti wametambua spishi mpya ya samaki wa aina ya killifish, Nothobranchius sylvaticus, katika bwawa la muda mfupi kwenye Hifadhi ya Msitu ya Gongoni nchini Kenya. Picha na Dirk Bellstedt.
Nukuu:
Bellstedt, D.U., Nagy, B., Merwe, P.D., Cotterill, F.P., Luke, Q., & Watters, B.R. (2025). The description of a critically endangered new species of seasonal killifish, Nothobranchius sylvaticus (Cyprinodontiformes: Nothobranchiidae), a relict species from an East African forest refugium in south-eastern Kenya. Zootaxa, 5601(1), 86-108. doi:10.11646/zootaxa.5601.1.4
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 27/03/2025