- Ugavi wa maji kwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi, unategemea Mto Tana wenye mkondo ulio na urefu wa takribani kilomita 1,000 kutoka milima ya Aberdare hadi Bahari ya Hindi.
- Kwa miongo kadhaa sasa, wakulima wamekuwa wakiharibu misitu ili kupanda mazao kwenye miteremko, hasa kwenye maeneo ya juu ya bonde la mto, hali ambayo imesababisha uharibifu wa ubora wa maji.
- Ili kukabiliana na hali hii, Upper Tana-Nairobi Water Fund ilianzishwa mwaka 2015, ikiwa na lengo la kukusanya fedha kutoka kwa mashirika binafsi, taasisi za serikali na mashirika ya uhifadhi ili kurejesha vyanzo vya maji na kupanda miti upya.
- Ingawa jitihada hizi zimepata mafanikio fulani, kumekuwa na changamoto, hasa katika kujenga uelewa na utaalamu wa kutosha miongoni mwa maafisa wa sekta ya maji kuhusu suluhu zinazotegemea asili.
Ugavi wa maji kwa wakazi zaidi ya milioni tano wa mji wa Nairobi na wengine milioni nne pembezoni mwa mji unategemea Mto Tana. Kwa miongo mingi sasa, upanuzi wa kilimo kwenye maeneo ya juu ya bonde la Tana umechochea ukataji wa miti na hivyo kusababisha mmomonyoko wa udongo ambao umeharibu mashamba na kushusha ubora wa maji ambayo wakaaji wa jiji hilo wanategemea. Kila mara udongo unaposombwa kwa kasi kipindi cha mvua kubwa, mchanga huingia mtoni na kusababisha kupungua kwa rutuba ya mashamba, huku ukiziba mabwawa ya kuzalisha umeme na miundombinu ya kusambaza maji.
Mto huu unasafiri kutoka magharibi kuelekea mashariki, kupitia eneo la tambarare na milima ya Kaunti ya Garissa, ambako wafugaji wanafuga mifugo katika mazingira ya ukame ambayo pia hutegemewa na wanyamapori walio hatarini kama swala wa gerenuk na twiga wa Rothschild. Baadaye mto huo hupitia kwenye maeneo yenye misitu kabla ya kuishia kwenye delta kubwa katika Ghuba ya Ungwana.
Shida zinazosababishwa na ukosefu wa misitu zimeenea na kuathiri watu wengi kwenye bonde la Tana na kwingineko. Wakazi wengi wa Nairobi hulazimika kununua maji kwa madumu ili kupata ya kunywa, kupikia na kuoga, huku viwanda na biashara vikilazimika kuwa na mipango ya dharura. Kadri idadi ya watu inavyoongezeka na mabadiliko ya tabianchi kuathiri upatikanaji wa mvua, usalama wa maji unazidi kuwa changamoto kubwa.
Naabia Ofosu-Amaah, mshauri mwandamizi wa shirika la The Nature Conservancy, anasema iwapo mifumo ya maji safi haina afya, haiwezi kuwa na msingi unaohitajika na binadamu, mimea, wanyama, miji na hata uchumi. Wanyama kama swala wa gerenuk, pundamilia wa Grévy, twiga wa Rothschild, tembo, simba na faru hupatikana katika eneo la bonde la Tana.

Mnamo mwaka 2015, TNC ilizindua Upper Tana-Nairobi Water Fund (UTNWF) ili kufadhili miradi ya kuhifadhi maji katika maeneo ya juu, ikiwemo urejeshaji wa vyanzo vya maji na upandaji miti. Fedha zilitoka kwa mashirika makubwa kama East African Breweries, Coca-Cola, Nairobi City Water and Sewerage Company na hata kampuni ya kuzalisha umeme ya KenGen. Iwapo uharibifu wa bonde la mto huo hautakabiliwa, mashirika haya yatapoteza mengi.
Ofosu-Amaah, akiongea kwenye hafla iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) hivi karibuni, alisema kuwa mradi huo una lengo la kuimarisha uhusiano wa usawa kati ya maji na udongo katika bonde la Mto Tana, ukiwaangazia wakulima wadogo wapatao 3,000 wanaolima mazao kama chai, kahawa na ndizi.
Huku ikishirikiana na wakulima na mamlaka za eneo husika, jitihada hizi zimeanzisha maeneo ya kinga kando ya mito, kuendeleza kilimo cha miti na mazao (agroforestry), kutengeneza matuta kwenye mashamba yenye mteremko mkali ili kupunguza mmomonyoko, kupanda nyasi kama Napier ili kuzuia udongo kusombwa, na kurejesha maeneo ya misitu yaliyoharibika.
Pia umeunga mkono uundaji wa mistari ya nyasi kando ya mashamba na kupunguza mmomonyoko kwenye barabara za udongo.
Uboreshaji wa ubora na wingi wa maji
Edith Alusa, mkurugenzi mtendaji wa UTNWF, aliieleza Mongabay kwamba maeneo matatu ya kipaumbele katika bonde la juu la Mto Tana — mito ya Sagana-Gura, Maragua na Thika-Chania — yana jukumu muhimu katika kuboresha ubora na wingi wa maji katika bonde hilo.
Mradi huo umehusisha wakulima pamoja na mamlaka za mitaa katika maeneo hayo, ili kuunda maeneo ya kinga kando ya mito, kuendeleza kilimo mseto cha miti na mazao (agroforestry), na kutengeneza matuta kwenye mashamba yenye miteremko mikali ili kupunguza mmomonyoko wa udongo.
Pia umeunga mkono urejeshaji wa misitu iliyoharibika pembezoni mwa misitu, kuanzishwa kwa mistari ya nyasi kando ya mashamba, na kupunguza mmomonyoko kwenye barabara za udongo. Wakulima wamekuwa wakipanda nyasi aina ya Napier ili kuzuia mmomonyoko wa udongo katika Bonde la Mto Tana.

Alusa alisema: “Mikakati hii imethibitisha kuwepo kwa manufaa makubwa ya kuanzishwa kwa mfuko wa maji, kwa kuwa kumekuwa na zaidi ya asilimia 50 ya upunguzaji wa matope kwenye mito na hadi asilimia 15 ya ongezeko la upatikanaji wa maji kila mwaka katika maeneo ya vyanzo vya maji vilivyopewa kipaumbele msimu wa kiangazi.”
“Kwa ujumla, uwekezaji wa dola za Marekani milioni 10 katika miradi ya mfuko wa maji unatarajiwa kuleta faida za kiuchumi zenye thamani ya dola za Marekani milioni 21.5 katika kipindi cha miaka 30.” Aliongeza kuwa ingawa UTNWF ilianza kama mpango wa shirika la TNC, tangu mwaka 2021 imekuwa taasisi huru iliyosajiliwa kisheria.
Ofosu-Amaah aliambia Mongabay kuwa mfano huu umeonyesha mafanikio, lakini pia umekumbwa na changamoto. Baadhi ya maafisa wa sekta ya maji wamezoea mbinu za uhandisi wa moja kwa moja, hivyo kuwapa mafunzo kuhusu thamani ya suluhu zinazotegemea asili ni jambo muhimu ambalo pia linahitaji muda na rasilimali zaidi. Anatumaini kuwa katika miaka mitano ijayo, uwekezaji mkubwa zaidi utaelekezwa katika suluhu za asili na kwamba spishi nyingi zaidi za wanyamapori zitarudi katika makazi yake yaliyorejeshwa huku watumiaji wa maji nyumbani na viwandani wakifaidika na maji bora na ya uhakika.
Paul Gacheru, meneja wa spishi na maeneo wa shirika la Nature Kenya, ambalo ni shirika la uhifadhi za muda mrefu barani Afrika, anasema UTNWF ni njia mbadala na muhimu ya kufadhili uhifadhi kwa kutoa rasilimali kwa jamii zinazoishi katika maeneo ya juu ya bonde la Tana. “Inaweza kuendeleza usimamizi endelevu wa ardhi na urejeshaji wa mandhari. Hii itaboresha ubora na kiasi cha maji, na kuhakikisha kuwa mfumo wa ikolojia unatunzwa na kulindwa,” aliiambia Mongabay.

Hata hivyo, aliongeza kuwa anaona mfuko huo kama nyenzo inayosaidia kazi zinazoongozwa na Wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu katika kulinda bonde hilo. “Kwa maoni yangu, UTNWF haipaswi kuchukua nafasi ya jukumu la serikali lililoainishwa kwenye katiba katika kusimamia ardhi, bali iunge mkono juhudi hizo,” aliongeza.
Ofosu-Amaah anasema kuwa bila mifumo imara ya maji safi, hakutakuwa na maji ya kutosheleza mahitaji ya binadamu au mazingira. “Ni muhimu sana mifumo ya kiasili iwe msingi wa usalama wa maji. Ndiyo maana ulinzi na urejeshaji wa mazingira ni nguzo kuu ya kuhakikisha tunakuwa na maji ya kutosha sasa na siku zijazo,” anasema.
Picha ya bango: Mkulima Rachael Njeri ameanzisha mistari ya malisho shambani kwake, hatua inayosaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo huku ikiwapa ng’ombe wake chakula. Picha na Georgina Smith/CIAT kupitia Flickr (CC BY-NC-SA 2.0).
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 29/10/2024.