KAMPALA, Uganda — Uganda Wildlife Authority (UWA) na Wildlife Conservation Society (WCS) wameingia makubaliano ya miaka 10 ya kusimamia pamoja, sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Queen Elizabeth — hifadhi inayojulikana kwa simba wake wanaopanda miti.
Simon Nampindo, mkurugenzi wa WCS Uganda, amesema WCS itachukua baadhi ya majukumu ya kila siku katika Sekta ya Ishasha, upande wa kusini mwa hifadhi, ikiwemo usimamizi wa bioanuwai, ushirikiano na jamii, na ukuzaji wa biashara za utalii. UWA itabaki na dhamana ya utekelezaji wa sheria na ulinzi wa wanyamapori Ishasha.
Makubaliano haya yanakwenda sambamba na mwelekeo mpana wa ushirikiano kati ya serikali za Afrika na mashirika ya uhifadhi katika usimamizi wa hifadhi.
“Katika nguzo zote, WCS na UWA watafanya kazi kwa karibu katika kuandaa na kutekeleza mipango yote ya shughuli na bajeti,” Nampindo aliambia Mongabay kupitia barua pepe.
Sekta ya Ishasha inaenea takriban kilomita za mraba 500 (500km²) kati ya eneo lote la hifadhi lenye kilomita za mraba 1,978 (1978km²).
Ingawa simba wa Ishasha wamekuwa kivutio kikubwa cha watalii, idadi yao inazidi kupungua. Takwimu za UWA zinaonyesha idadi ya simba katika Queen Elizabeth ilishuka kwa zaidi ya 90% kati ya mwishoni mwa miaka ya sabini na mwaka 2022, ikitoka simba 400 hadi 39.
Nampindo alisema sasa kuna simba chini ya watano Ishasha. Bila kuongeza idadi hiyo — labda kwa kuwaleta simba wengine kutoka maeneo mengine — idadi ya simba haitaweza kujirejesha yenyewe.
Simba wa Queen Elizabeth wamekabiliwa na vitisho vingi, vikiwemo migogoro na wafugaji wa eneo hilo, upotevu wa makazi, na mitego ya wawindaji haramu. Nampindo alisema changamoto hizi zinasosababisha upungufu wa simb, alazima zishughulikiwe kabla ya kuwaongeza simba wengine kwenye hifadhi hilo.
Tangu 2018, simba wameuawa na watu wanaoishi ndani na karibu na hifadhi katika matukio kadhaa. Mwaka 2021, mzoga uliotiwa sumu ulisababisha vifo vya simba angalau sita. Mwishoni mwa 2025, simba wengine watatu walikufa katika hali kama hizo.
Taarifa za Mongabay kutoka Queen Elizabeth zimebaini mvutano kati ya baadhi ya jamii za wafugaji na UWA, ambapo mashambulizi ya simba kwa mifugo yamechochea malalamiko ya muda mrefu kuhusu sheria kali za malisho.
Nampindo alisema WCS inanuia kuajiri “walinzi wa simba” na wapelelezi kutoka miji inayozunguka Ishasha ili kujenga msaada wa uhifadhi. Shirika hilo pia limefadhili ujenzi wa mazizi na visima vya mifugo.
“[Hatua za migogoro kati ya binadamu na wanyamapori] zitaimarishwa zaidi chini ya [ushirikiano huu wa usimamizi] na kuzinduliwa kupitia mashauriano ya kina na jamii katika miezi sita ya kwanza,” Nampindo alisema.
Uchunguzi wa Mongabay wa 2024 uligundua madai ya kuaminika ya mauaji ya nje ya sheria na ukatili mwingine uliofanywa na walinzi wa UWA hifadhini humo. Nampindo alisema makubaliano hayo yanajumuisha ulinzi wa haki za binadamu, ikiwemo mfumo wa malalamiko na kanuni za mwenendo.
“WCS inafahamu madai hayo na imeyajadili moja kwa moja na [UWA], huku mashirika yote mawili yakikubaliana na hatua kadhaa za dhahiri za kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu, uwajibikaji, na ushirikiano na jamii,” alisema.
Picha ya jalada: Kundi la simba ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Queen Elizabeth. Picha na Ashoka Mukpo kwa Mongabay.