- Watu saba wakiwemo wavuvi watatu, wanadaiwa kuuawa ndani ya mwezi mmoja.
- Uharibifu wa makazi ya asili ya wanyama huongeza hatari ya mashambulizi.
- Uhifadhi wa mamba uende sambamba na ulinzi wa maisha ya binadamu.
- Licha ya matukio ya vifo kuripotiwa, mamlaka hazijachukua hatua madhubuti kwa wakati.
BURUNGA, Burundi – Watu saba wakiwemo wavuvi watatu katika wilaya ya Nyanza, mkoani Burunga, nchini Burundi, wamepoteza maisha katika kipindi cha mwezi mmoja kutokana na mashambulizi ya mamba yaliyotokea katika mwambao wa Ziwa Tanganyika. Vifo hivyo vilitokea katika kipindi cha kuanzia mwanzoni mwa Septemba na Oktoba 9, 2026.
Taarifa hiyo ilitolewa na Kamishna wa Polisi wa jimbo la Burunga ambaye pia ndiye mkuu wa usalama katika jimbo hilo, Aloys Nduwayo, wakati wa hitimisho la mkutano wa usalama ulifanyika katika jimboni humo, ukiongozwa na Gavana wa jimbo hilo, Parfait Mboninyibuka.
Mkutano huo uliowashirikisha pia viongozi wa utawala na usalama pamoja na wananchi, ulilenga kujadili masuala ya kiusalama katika jimbo hilo hususan matukio ya mamba kushambuliwa wananchi.

Akiongea katika mkutano huo, Kamishna Nduwayo, alisema mashambulizi hayo saba yalitokea katika vilima vya Rubindi na Rimbo, kando ya ziwa Tanganyika. Alisema licha ya kusababisha vifo, yaliwaacha wananchi wengine wakiwa majeruhi.
Mtoto aliuawa wakati akioga ziwani
Pascal Bucumi, mkazi wa Rubindi, anakumbuka kifo cha mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka tisa, aliyeshambuliwa na mamba Septemba 3, 2026, alipokuwa amekwenda kuoga katika ufukwe wa Ziwa Tanganyika kabla ya kwenda kusali.
“Watu waliokuwa karibu walikimbilia eneo la tukio na kupiga kelele ili kumfukuza mnyama huyo, lakini hawakufanikiwa kumwokoa mtoto kwani mnyama alikuwa tayari amemshambulia hadi kumuua,” anasema Bucumi.
Kwa mujibu wa Bucumi, tukio lingine linalohusisha mamba, lililiripotiwa kutokea kwenye kilima hicho, mnamo Oktoba 5, alasiri wakati, mwanamume mmoja alipouawa.
“Wananchi walipoona tukio hilo, walianza kupiga kelele. Mamba alirudi ziwani na kuuacha mwili wa mtu huyo ufukweni,” anasema Bucumi.
Mkutano wa usalama
Akiongea katika mkutano huo, Gavana Mboninyibuka alikiri kuwa hali hiyo ni ya dharura na kwamba inahitaji kutafutiwa suluhisho la haraka.
Kamishna Nduwayo, yeye alisisitiza ukubwa wa athari za mashambulizi hayo kwa maisha ya watu na umuhimu wa watu kuchukua tahadhari.
Ingawa viongozi hao wawili wa jimbo, hawakubainisha hatua madhubuti zitakazochukuliwa kuzuia matukio kama hayo yasijirudie, lakini walieleza nia ya wadau kuendelea kufanya mashauriano ili kupata haraka suluhisho la kukabiliana na tishio hilo.
Katika mkutano huo, hoja ya msingi iliyovuta hisia za wengi ilikuwa kutafuta suluhisho la haraka dhidi ya mashambulizi ya mara kwa mara ya mamba.
Baadhi ya wakazi wa maeneo yaliyoathiriwa na matukio hayo, walieleza wasiwasi wao kuhusu usalama wao. “Tunategemea ziwa katika maisha yetu ya kila siku, hasa kwa shughuli za uvuvi. Pia tunahitaji maeneo salama ya kuchota maji. Tunataka kujua viongozi wetu wanachukua hatua gani kupunguza vitendo vya kushambuliwa,” alihoji Agnès Bayubahe, mmoja wa wananchi walioshiriki kikao hicho.
Vichocheo vya hatari
Akizungumza na Mongabay kuhusiana na suala hilo, Blaise Nduwarugira, ambaye ni mtaalamu wa mazingira alisema matukio hayo yanachochewa na sababu mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa shughuli za binadamu karibu na ziwa, tabia za wanyama na mabadiliko ya makazi yao.
“Mamba wanaweza kuwashambulia binadamu wanapowachukulia kama mawindo. Vilevile, wanaweza kuwa wakali wanapohisi kwamba mayai yao au watoto wao wako hatarini,” alisema.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, uharibifu wa makazi ya asili na kuongezeka kwa shughuli za binadamu karibu na maeneo wanayoishi wanyama wa majini, huchangia kuongezeka kwa mafarakano kati ya wanyama na binadamu.
“Viboko wanahitaji mito na maeneo ya malisho ili kuishi. Kwa upande mwingine, mamba hutegemea mazingira ya majini ili kupata chakula, kuzaliana na kujilinda. Binadamu wanapoharibu uoto wa asili, kuchukua maeneo ya kandokando ya maji au kuvuruga mazingira hayo, migogoro kati ya wanyama hawa na wanadamu huongezeka na inaweza kuleta madhara makubwa zaidi,” alisema Nduwarugira.
Israël Derrick Gelengi, mwanafunzi wa shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Burundi, ambaye ni mtaalamu wa usimamizi wa mifumo ya ikolojia ya misitu na uhifadhi wa bioanuwai, alisema uharibifu wa makazi ya asili unaweza kuongeza mwingiliano kati ya binadamu na wanyama hawa.
Viboko nao ni tishio
Mamba si wanyama pekee wa majini wanaotishia maisha ya watu wanaoishi kando ya ziwa Tanganyika, katika mkoa wa Burunga. Viboko pia wanahusishwa na matukio yanayosababisha vifo.
Béatrice Bucumi, mkazi wa eneo la Mukungu alisema kijana mmoja mwenye umri wa takribani miaka 20 alipoteza maisha baada ya kujeruhiwa vibaya na kiboko alipokuwa akijaribu kuogelea ili kuwafikia wenzake waliokuwa wamekwenda kuvua samaki ziwani. Tukio hilo lilitokea Oktoba 12, 2026.

“Kijana huyo alikuwa anachimba mchanga kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika, lakini baadaye aliamua kuwafuata wenzake waliokuwa wakivua samaki ziwani. Kabla ya kufika kwenye chombo chao cha uvuvi, alikutana na kiboko aliyemjeruhi vibaya tumboni. Hatimaye, alifariki kutokana na majeraha hayo,” alisema Bucumi.
Ili kupata suluhisho la kudumu la changamoto hiyo, wataalamu mbalimbali pamoja na wananchi wanatoa mapendekezo kadhaa.
Ulinzi wa makazi ya asili
Ili kuwezesha binadamu na mamba kuishi pamoja kwa amani, Nduwarugira, anasema hatua ya kwanza ni kulinda makazi ya asili ya wanyama hao. Anasema makazi hayo yanapovamiwa au kuharibiwa, mamba hulazimika kujilinda.
“Mamba hutegemea mazingira ya majini ili kupata chakula, kuzaliana na kujilinda. Uharibifu wa mazingira hayo na shughuli nyingi za binadamu kwenye mwambao wa ziwa vinaweza kuongeza mawasiliano kati ya binadamu na mamba, na hivyo kuongeza hatari ya mashambulizi,” anaeleza Nduwarugira.
Anaongeza kuwa kuzuia uvamizi wa maeneo hayo, kuhifadhi uoto wa asili na kulinda makazi ya wanyama ni miongoni mwa hatua muhimu za kupunguza migogoro kati ya wanadamu na wanyama.
Hata hivyo, Gelengi anasema licha ya umuhimu wao katika mifumo ya ikolojia ya majini, uhifadhi wa mamba unapaswa kwenda sambamba na ulinzi wa maisha ya binadamu.
“Uhifadhi wa wanyama hawa unapaswa kwenda sambamba na ulinzi wa maisha ya binadamu, kupitia usimamizi unaofaa wa maeneo hatarishi na ushiriki wa jamii zinazoishi kando ya ziwa,” alisisitiza.
Amani itategemea wajibu wa pamoja
Kwa mujibu wa Nduwarugira, binadamu na wanyama hao kuishi pamoja kwa amani kutategemea wajibu wa pamoja. Alisema: “Hatua ya kwanza ni mamlaka husika kutambua maeneo hatari yaliyo karibu na ziwa na kuweka mabango ya tahadhari. Sambamba na hayo, wanapaswa kuweka mazingira salama katika maeneo yanayotumiwa na watu na wanyama hawa ili kuhakikisha hakuna mwingiliano”.
Hatua nyingine, Nduwarugira anasema ni kuwaelimisha wananchi kuhusu hatari zinazotokana na wanyama wa majini.
“Wananchi wanapaswa kuelewa kwanza ili waepuke kuogelea au kuvua samaki katika maeneo ambayo wanapatikana wanyama hawa,” anaeleza.
Kwa upande wa Gelengi, licha ya kuelimisha jamii, ni muhimu kuanzisha mfumo wa tahadhari ya haraka, kufuatilia maeneo hatari na kuwashirikisha wataalamu katika mikakati ya kutafuta namna ya kutatua changamoto hiyo.
Kwa upande wa wananchi, Nduwarugira anasema wanapaswa kuepuka maeneo hatari na kuzingatia tahadhari zinazotolewa.
Joséphine Ndayisenga, mkazi wa kilima cha Rimbo anawashauri wananchi kuacha kufanya shughuli katika maeneo yanayozunguka ziwa hasa yale yanayosemekana kuwa na wanyama hao.
“Ni muhimu pia kwa watu kutowachokoza wanyama hawa wala kuharibu makazi yao ya asili kupitia uchafuzi wa mazingira. Uharibifu wa makazi yao unaweza kuwafanya kuhamia kimyakimya katika maeneo ambayo wakazi hawadhanii kuwa wanyama hao wapo, na hivyo kuongeza hatari ya mashambulizi,” anaonya Joséphine.
Wavuvi wanategemea ziwa Tanganyika
Ingawa wataalamu wanaona kuelimisha wananchi na kuandaa maeneo salama kunaweza kutasaidia kupunguza matukio haya, watu wengine, akiwemo Gelengi, wanasema kwamba ufanisi wa hatua hizo utategemea ufuatiliaji wa karibu na ushirikiano wa dhati kati ya mamlaka, jamii na wataalamu wa masuala hayo.
Anasema ni vema wananchi wakiwemo wavuvi wakashirikishwa ili kutoa maoni yao na namna bora ya kuamliza changamoto hiyo. “Itakuwa vigumu kuwazuia kwenda ziwani, kwa kuwa wanalitegemea ili kupata chakula na kukidhi mahitaji ya familia zao,” alisema.
Licha ya wavuvi kuelewa hatari inayowakabili kutokana na wanyama hao, lakini wanasema riziki zao zinapatikana kupitia uvuvi katika ziwa Tanganyika.
Jean Claude Tuhabonye, mvuvi na mkazi wa kilima cha Rimbo anasema: “Tunafahamu kwamba wanyama wa majini kama mamba na viboko wanaweza kutoka majini na kutushambulia, lakini hatuna namna kwa kuwa tunalihitaji ziwa Tanganyika kwa ajili ya maisha yetu ya kila siku”.
Kwa upande Gahungu Balthazar, mvuvi kutoka eneo la Mukungu, ziwa hilo ndio mtaji wao lakini kila wanapolikaribia, wanajiweka kwenye hatari ya kukutana na mamba au viboko.
“Kuzuia mashambulizi kunahitaji ushirikiano kati ya viongozi, vyombo vya usalama, wataalamu wa wanyamapori na jamii zinazoishi kando ya ziwa wakiwemo wavuvi,” alisema Gelengi.
Wakati wavuvi hawaelewi la kufanya kutokana na hali hii, Jean de Dieu Ndereyimana, mtaalamu wa masuala ya mazingira, anashauri wadau wote kuungana na kushirikiana katika kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto hiyo.
“Ili shughuli za uvuvi ziendelee kwa usalama, ni muhimu kuwe na ushirikiano wa karibu kati ya wahusika wote, kuweka mipaka ya maeneo salama ya uvuvi, kuepuka kuvua katika nyakati ambazo wanyama hao huwa na shughuli nyingi na kuanzisha mfumo wa tahadhari ya haraka pale mamba au viboko wanapoonekana,” anapendekeza.

Hatua madhubuti zinakosekana
Licha ya matukio ya mashambulizi yaliyoripotiwa katika wilaya ya Nyanza, hatua madhubuti bado hazijachukuliwa kwa wakati. Badala yake, viongozi wa vilima vya Rubindi na Rimbo, ambako matukio hayo yametokea, wameishia kutoa wito kwa wakazi kuwa waangalifu.
“Wananchi wanapaswa kuwa waangalifu kutokana na matukio haya. Wazazi wanapaswa kuwafuatilia watoto wao ili wasiende ziwani bila kuambatana na watu wazima,” alisema Nyandwi Jimmy, Mkuu wa kilima cha Rimbo wakati akilihutubia wananchi katika mkutano uliofanyika kufuatia kifo cha mtu aliyeshambuliwa na mamba.
Aliendelea kuwatahadharisha watu kuepuka kulikaribia ziwa ili kupunguza hatari ya kushambuliwa, kuepuka kuoga katika maeneo hatari na kuongeza umakini wakati wa kuchimba mchanga, kukata nyasi kwa ajili ya mifugo au kufanya shughuli za uvuvi.
Kwa upande wao, wakazi wanashauri mtu yeyote atakayeshuhudia tukio kama hilo kupiga kelele kwa nguvu kwa kuwa wanyama hao hawapendi kelele. “Kupiga kelele tu si hatua ya usalama inayoweza kuhakikishwa,” anaeleza Minani Paul, mkazi wa eneo la Mukungu.
Kama Minani, baadhi ya wataalamu wanaona kwamba ushauri unaotolewa na mamlaka kwa wananchi bado hautoshi na huenda usifuatwe.
“Wakati matukio haya yanapochukua maisha ya watu kwa kasi hii, hatua za ulinzi hazipaswi kuwa ushauri ambao watu wanaweza kuufuata au kuupuuza. Zinapaswa kuwa masharti ya lazima yanayopaswa kufuatwa kikamilifu,” anasema Nduwarugira.