- Mahakama Kuu imewafutia adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela.
- Upande wa Jamhuri haukutokea mahakamani kujibu rufani.
- Ushahidi kuhusu nyama ya swala haukuwa na mnyororo kamili wa utunzaji wa vielelezo.
- Mahakama ilidumisha hukumu ya kumiliki silaha ndani ya hifadhi.
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Katavi, imefuta hukumu na adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kumiliki nyara za Serikali dhidi ya Salvatory Kagoma na Paulo Wales. Aidha imebariki hukumu ya kosa la kumiliki silaha ndani ya Hifadhi iendelee kwa sababu washitakiwa walikiri kosa hilo.
Mahakama hiyo mbele ya Jaji Godfey Isaya ilitoa uamuzi huo baada ya kubaini kuwa upend wa mashtaka wakati katika kesi hiyo, haukuthibitisha kosa la kukutwa na nyara pasina kuacha shaka.
Jaji Isaya alisema mahakama hiyo ilikubali sehemu ya rufaa ya washtakiwa hao ambao waliokuwa wamehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Mlele kwa makosa ya jinai matatu yanayohusiana na wanyamapori na uvuvi ndani ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Ugala.
Washtakiwa hao walikamatwa Machi 14, 2024, katika eneo la Kasandalala, wakiwa na vipande vipatavyo 20 vya nyama vilivyotiliwa shaka kuwa vya wanyamapori, samaki 60, nyavu mbili za uvuvi, ndoano 160, visu viwili, panga, shoka na baiskeli mbili.
Mahakama ya Wilaya iliwahukumu miaka 20
Mahakama ya Wilaya ya Mlele iliwahukumu kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kumiliki nyara za Serikali na miaka 20 kwa kosa la kumiliki silaha ndani ya hifadhi. Adhabu hizo zilitakiwa kutekelezwa kwa wakati mmoja.
Washtakiwa hawakuridhishwa na hukumu hiyo, wakaamua kukata rufaa wakidai kwamba, mahakama ya mwanzo ilikosea kisheria na kimantiki kwa kuwatia hatiani na kuwahukumu kwa makosa ambayo hayakuthibitishwa bila kuacha shaka yoyote yenye msingi wa kisheria.
Walidai mahakama ya mwanzo ilikosea kisheria na kimantiki kwa kushindwa kuzingatia na kutathmini ipasavyo ushahidi uliotolewa na warufani, kama sheria inavyotaka.
Rufaa ilipoitwa kusikilizwa Septemba 22, 2026 warufani walijiwakilisha wenyewe bila kuwa na mawakili wa kuwatetea. Upande wa mjibu rufaa, yaani Serikali ulikuwa unafahamu tarehe ya kusikilizwa kwa rufaa hiyo, lakini haukufika mahakamani.
Jaji Isaya alisema mahakama iliendelea kusikiliza rufaa hiyo bila uwepo wa upande wa mashtaka na ilipowataka warufani kueleza sababu za kukata rufaa, walitoa maelezo mafupi, wakiiomba mahakama izingatie sababu zilizoainishwa katika hati yao ya pamoja ya rufaa na kuitaka itoe uamuzi kwa niaba yao.
Baada ya kuzingatia kwa makini sababu za rufaa, maelezo ya warufani na kumbukumbu za mwenendo mzima wa kesi hiyo katika mahakama ya mwanzo, mahakama hiyo iliamua iwapo makosa waliyoshtakiwa nayo yalithibitishwa bila kuacha shaka yoyote yenye msingi wa kisheria wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya awali.
“Kabla ya kuamua suala hilo, ni muhimu kueleza kuwa katika mfumo wa haki ya jinai, jukumu la kuthibitisha mashtaka ni la upande wa mashtaka. Hivyo, upande huo unatakiwa kuthibitisha kesi yake bila kuacha shaka yoyote yenye msingi wa kisheria. Mshtakiwa anaweza kupatikana na hatia, kutiwa hatiani na kuhukumiwa pale tu upande wa mashtaka utakapothibitisha bila kuacha shaka yoyote yenye msingi wa kisheria kwamba kosa limetendeka na kwamba mshtakiwa ndiye aliyelitenda,’’ alisema Jaji Isaya.
Aidha Mahakama Kuu ilibaini kuwa ushahidi kuhusu nyama iliyodaiwa kuwa ya swala haukuwa na mnyororo kamili wa utunzaji wa vielelezo.
“Kumbukumbu hazikuonyesha nani aliyepeleka nyama hiyo Mahakama ya Mwanzo ya Inyonga kwa ajili ya kuteketezwa, huku hakimu aliyeidhinisha uteketezaji huo akiwa hakuitwa kutoa ushahidi,” alisema Jaji Isaya.
Kutokana na kasoro hiyo, Jaji Isaya alifuta hukumu na adhabu ya kosa la kumiliki nyara za serikali, akisema upande wa mashtaka haukuthibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka.
Kosa la kumiliki silaha
Hata hivyo, mahakama ilidumisha hukumu ya kumiliki silaha ndani ya hifadhi kwa kuwa washtakiwa hawakupinga kuwa walikamatwa wakiwa na visu, panga na shoka ndani ya hifadhi.
Jaji alisema kifungo cha miaka 20 walichopewa kwa kosa hilo kilikuwa kinyume cha sheria, kwa kuwa kifungu cha 17(2) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori kinaweka adhabu ya kifungo kisichozidi miaka mitatu.
Badala yake, mahakama iliwatoza faini ya TSh200,000 kila mmoja, au kutumikia kifungo cha miaka miwili jela kwa atakayeshindwa kulipa, kuanzia tarehe ya kutiwa hatiani.
Kuhusu kosa la tatu la kuvua samaki ndani ya hifadhi bila kibali, mahakama ilidumisha hukumu na adhabu ya awali ya faini ya TSh500,000 au kutumikia kifungo cha miezi sita jela kwa atakayeshindwa kulipa, baada ya kubaini kuwa washtakiwa walikiri kosa hilo.
Mahakama ilihitimisha kuwa rufaa hiyo imekubaliwa kwa sehemu, huku hukumu ya kumiliki silaha na ile ya kuvua samaki ndani ya hifadhi zikiendelea kusimama.
Picha ya bango: Hifadhi ya Wanyamapori ya Ugala ambayo Salvatory Kagoma na Paulo Wales, walidaiwa kukutwa wakiwa na nyara za Serikali. Picha na Tumaini Mgeni, Mongabay.