- Wastani wa umri wa wakulima nchini Kenya umefikia miaka 60, huku vijana wakichangia asilimia 29 tu ya nguvu kazi ya kilimo, ikilinganishwa na asilimia 47 mwanzoni mwa miaka ya 2000.
- Mabadiliko ya tabianchi, yakiwemo ukame na mvua zisizotabirika, yanapunguza faida ya kilimo na kuwafanya vijana wengi kutafuta njia nyingine za kujipatia kipato.
- Kisa cha Lucky Kazungu kinaonyesha jinsi vijana wanavyoweza kuunganisha maarifa ya jadi na mbinu mpya, kama kilimo mseto cha miti, uvunaji wa maji ya mvua na umwagiliaji wa matone.
- Wakati serikali ikitumia mipango kama 4K Club na NAVCDP Agripreneur kuwahamasisha vijana kuingia katika kilimo, kuondoka kwao kunatishia upotevu wa maarifa muhimu ya kilimo na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Alipokuwa mtoto, Lucky Kazungu alijifunza kilimo kutoka kwa babu yake. “Alipanda mazao mengi katika shamba moja: mahindi, kunde, choroko, mbaazi na maboga. Alinifundisha pia kilimo cha miti na ufugaji wa mbuzi,” anakumbuka.
Mbinu nyingi alizofundishwa na babu yake zinaendana na misingi ya kilimo-ikolojia (agroecology) inayotumika leo.
Kwa mujibu wa FAO, mkabala huo hutumia kanuni za ikolojia katika kilimo na kuunganisha sayansi na maarifa ya jadi ya wakulima.

“Kulima aina mbalimbali za mazao kulisaidia kuhifadhi rutuba ya udongo. Zao moja liliposhindwa kustawi, mengine yaliweza kuendelea kukua. Ufugaji wa mbuzi pia ulimsaidia kukabiliana na ukame. Mbuzi walipata malisho ya nyasi wakati wa mvua na kula vichaka wakati wa kiangazi,” anafafanua Kazungu.
Mwaka 2017, Kazungu alirejea Kaunti ya Kilifi, alikotoka familia yake, akiwa na maarifa aliyorithi kutoka kwa babu yake pamoja na shahada ya kwanza katika ikolojia ya mimea na sayansi ya mazingira. Huko alianzisha Lukanza Farm, shamba analotumia mbinu za kilimo rejeshi (regenerative farming).
Kwa sasa, shamba hilo lina ukubwa wa ekari nane. Kazungu alianza kwa kufuga mbuzi, ambao bado wanachungwa katika sehemu ya ekari sita.
Baadaye alipanua shughuli zake kwa kuanzisha kilimo mseto cha miti na mazao (agroforestry) katika sehemu iliyobaki. Ili kutumia vyema mvua chache zinazonyesha Kilifi, alijenga mfumo wa kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua wenye uwezo wa kuhifadhi lita 10,000. Pia anatumia matuta ya kilimo yaliyochimbwa chini ya usawa wa ardhi pamoja na mfumo wa umwagiliaji wa matone. Pia amebadilisha vyombo vya plastiki na magunia ya saruji yaliyotupwa na kuvitumia kutengeneza bustani za wima, ambamo analima mchicha na mrunge.

Akiwa na umri wa miaka 30, Kazungu ni miongoni mwa vijana wachache walioamua kujikita katika kilimo. ‘Haikuwa rahisi,’ anasema. “Hata sasa, watu wengi wananidharau. Wanasema: umesoma, kwa nini hutafuti kazi ya kweli?”
Kwa vijana wengi, kilimo si shughuli wanayoichagua kwa hiari.
Hadithi ya Kazungu inaonyesha nafasi mbili muhimu ambazo vijana wa Kenya wanaweza kuchukua katika kilimo: kuhifadhi maarifa ya vizazi vilivyowatangulia na kuleta mbinu na mawazo mapya mashambani. Vijana wanapoachana na kilimo, maarifa ya jadi yaliyohifadhiwa na vizazi vilivyowatangulia yako hatarini kupotea. Wakati huohuo, jamii zinakosa fursa ya kunufaika na ubunifu na mawazo mapya ya kizazi kipya.
“Nilipokuwa mtoto, sikutaka kuwa mkulima. Nilitaka kuwa daktari,” anasema Kazungu huku akicheka. “Lakini yale aliyonifundisha babu yangu yangekwenda wapi?”
Hali hii inatokea wakati ambapo kilimo nchini kinakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na mvua zisizotabirika na uharibifu wa udongo. Hata hivyo, vijana wanaopaswa kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na changamoto hizi wanazidi kuondoka katika sekta hiyo.
Idadi ya vijana wanaojihusisha na kilimo nchini Kenya inapungua, huku idadi ya wanaoingia katika sekta hiyo ikiwa haitoshi kuziba pengo linaloachwa na wanaoondoka. Hali hii imechangia kuongezeka kwa wastani wa umri wa wakulima nchini Kenya hadi miaka 60. Kwa sasa, vijana wanaunda asilimia 29 tu ya nguvu kazi katika sekta ya kilimo, ikilinganishwa na asilimia 47 mwanzoni mwa miaka ya 2000. Hali hii inajitokeza licha ya takriban robo tatu ya wananchi wa Kenya kuwa na umri wa chini ya miaka 35.

Kwa kuwa wakulima wadogo huzalisha zaidi ya robo tatu ya chakula nchini, kupungua kwa idadi ya vijana wanaojihusisha na kilimo kunaweza kuhatarisha usalama wa chakula na maendeleo ya sekta hiyo. “Idadi ya watu inaongezeka kwa kasi kuliko uzalishaji wa chakula. Tunahitaji kuwavutia vijana zaidi katika kilimo, la sivyo tutaendelea kutegemea chakula kinachoagizwa kutoka nje,” anasema Timothy Njagi, mchumi katika African Network of Agricultural Policy Research Institutes, mtandao unaofanya utafiti na kutoa ushauri kuhusu sera za kilimo barani Afrika.
Kuondoka kwa vijana katika kilimo kunatokea wakati ambapo ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana nchini bado ni mkubwa. Njagi anahoji kwamba viwanda na huduma haviwezi kuwapokea vijana wote wa Kenya.
Mabadiliko ya tabianchi ni mojawapo ya sababu kuu zinazowafanya vijana waondoke. Nchini Kenya, hali ya hewa isiyotabirika na kali imepunguza faida ya kilimo, na kwa wengine, imekifanya karibu kutowezekana. Jacinta, mwenye umri wa miaka 31, anatoka katika familia ya wakulima huko Mtito Andei, eneo kame kusini mashariki mwa Kenya.
Kwa kukatishwa tamaa na kipato kidogo na kisicho na uhakika kinachotokana na kilimo, aliamua kutofuata nyayo za wazazi wake. “Wazazi wangu walikuwa wakilima mboga. Lakini katika miaka 10 iliyopita, mito imekauka, nao wakahamia mazao yenye thamani ndogo yanayohitaji maji kidogo, kama mahindi, maharagwe na kunde. Hata hivyo, bado hakuna uhakika: ukame unaweza kuharibu mavuno ya msimu mzima,” anaeleza. “Baada ya kuona jinsi mabadiliko ya tabianchi yalivyoathiri kilimo, nilihitimisha kuwa sikuwa na uhakika wa kuendelea kujikimu kupitia kilimo.”
Katika eneo lake, vijana wachache sana huingia kwenye kilimo. Sasa anajipatia riziki kupitia kazi za mtandaoni, akifanya kazi za usaidizi wa kiutawala kwa kampuni za Kenya na za kimataifa. “Nilihitaji kitu kilicho thabiti zaidi,” anasema.
Mabadiliko ya tabianchi pia yanapunguza maeneo yenye mazingira yanayofaa kwa kilimo, hali inayofanya iwe vigumu zaidi kwa vijana kuingia katika sekta hiyo. “Sehemu ndogo tu ya ardhi ya Kenya ndiyo inayochukuliwa kuwa ya kilimo, na inapungua kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi. Ilikuwa asilimia 20 miaka michache iliyopita; sasa ni takriban asilimia 15 hadi 16,” anasema Njagi.

Ardhi pia inazidi kugawanywa katika vipande vidogo kadiri inavyorithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mashamba yanapogawanywa na kuwa madogo zaidi, uwezo wake wa kuzalisha hupungua. Hali hii inawasukuma baadhi ya vijana kuuza ardhi wanayorithi na kuhamia mijini. Hata hivyo, kwa wanaobaki, jibu huenda liko katika yale ambayo vizazi vilivyotangulia vilikwisha yajua.
Kuanzia mwaka 2016, jamii anayotoka Kazungu ilikumbwa na ukame uliodumu kwa karibu miaka mitatu, hali iliyosababisha watu wengi kupoteza vyanzo vyao vya kujipatia kipato. Ndipo alipoanza kutathmini upya mbinu za kilimo zilizokuwa zikitumiwa katika jamii yake. “Nilitambua kuwa mbinu tulizokuwa tukitumia hazikuwa tena na matokeo mazuri. Kilimo cha kisasa, ambacho trekta hutumika kusafisha shamba lote, kilikuwa kikizidisha hali hiyo,” anasema. “Matumizi ya viuatilifu yalikuwa yakichangia kuharibu udongo. Zaidi ya hayo, wakulima wengi walikuwa wakilima mahindi pekee mwaka baada ya mwaka, hali iliyozidi kudhoofisha udongo. Hapo ndipo nilipotambua kuwa mbinu za kilimo alizonifundisha babu yangu zilikuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kustahimili changamoto tunazokabiliana nazo sasa.”
Tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, serikali na wafadhili wa kimataifa wamekuwa wakihimiza matumizi ya mbinu za kilimo cha kisasa na kibiashara katika sehemu mbalimbali za Afrika. Programu kama Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA), iliyozinduliwa mwaka 2006 kwa ufadhili wa mamilioni ya dola kutoka Bill & Melinda Gates na Rockefeller Foundation, zilihimiza wakulima kutumia mbegu zilizoboreshwa au chotara, mbolea za viwandani na viuatilifu, pamoja na kuimarisha mbinu za kilimo cha kibiashara. Lengo lilikuwa kuongeza mavuno na kulisha watu wengi zaidi.
Mbegu zinaonyesha kile kilicho hatarini. Mabadiliko hayo yalipa kipaumbele mbegu za kibiashara badala ya mifumo ya jadi ya kuhifadhi na kubadilishana mbegu iliyokuwa ikitumiwa na wakulima kwa muda mrefu. Kutokana na hali hiyo, maarifa yaliyohusiana na mifumo hiyo yalianza kupotea.

Huko Gilgil, Kaunti ya Nakuru, Beatrice Nyambura mwenye umri wa miaka 44 anasimamia benki ya mbegu ya jamii, ambako rafu zimejaa mitungi yenye mbegu za maharagwe, mtama na mnavu. Alianza kuhifadhi mbegu miaka michache tu iliyopita, baada ya shirika la Seed Savers Network kuwatambulisha wakulima wa eneo hilo kwa mbegu za asili. Hapo ndipo alipogundua kuwa wazazi wake pia walikuwa wakihifadhi mbegu hizo tangu zamani.
Kwa miaka mingi, utaratibu huo wa wakulima kuhifadhi na kubadilishana mbegu za asili ulikuwa umekumbwa na vikwazo vya kisheria. Mwaka 2022, Beatrice alikuwa miongoni mwa wakulima 15 waliofungua kesi dhidi ya serikali kupinga vifungu vya Sheria ya Mbegu na Aina za Mimea (Seeds and Plant Varieties Act), vilivyoweka adhabu za jinai kwa shughuli zinazohusisha mbegu ambazo hazijaidhinishwa. Mnamo Novemba 2025, Mahakama Kuu ilitangaza vifungu hivyo kuwa batili. “Sasa naweza kubadilishana mbegu zangu bila hofu ya kutozwa faini,” anasema.
Tafiti kuhusu aina za asili za mazao (landraces) barani Afrika zinaonyesha kuwa mbegu zilizochaguliwa na kuhifadhiwa na wakulima kwa vizazi vingi zina sifa zinazozisaidia kustawi katika mazingira ya maeneo husika. Faida hii ni muhimu zaidi katika mashamba yanayotumia pembejeo chache za kilimo. Lakini ujuzi wa jinsi ya kuzichagua na kuzihifadhi unashikiliwa zaidi na wakulima wazee. “Ni nadra sana kuwaona vijana wakijihusisha na kilimo katika eneo hili,” anasema Beatrice. “Lakini wanapokuja, huwa na hamu kubwa ya kujifunza.”
Taasisi za kimataifa zinazidi kuonyesha umuhimu wa mbinu mbadala za kilimo zinazoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Mwaka 2022, Jopo la Kiserikali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) liliorodhesha kilimo mseto cha miti na mazao, hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinazoongozwa na jamii, utofautishaji wa mazao na matumizi ya ardhi, pamoja na mbinu endelevu za usimamizi wa ardhi na kilimo-ikolojia, kuwa miongoni mwa njia madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mwaka 2024, FAO ilieleza kuwa mifumo imara ya chakula na kilimo, pamoja na mbinu endelevu za uzalishaji, inaweza kusaidia kutatua changamoto zinazohusiana na chakula, maji, ardhi na bioanuwai.

Vijana wanaojihusisha na kilimo si warithi wa maarifa ya vizazi vilivyowatangulia pekee, bali pia wana nafasi ya kuendeleza maarifa hayo kwa kutumia mbinu na teknolojia mpya. Vijana wanapoondoka katika kilimo, mchakato wa kurithishana maarifa ya jadi na kuendeleza ubunifu mpya pia unakatizwa. Hata Jacinta, ambaye anajiandaa kuachana kabisa na kilimo, amewafundisha wazazi wake mbinu mpya za kukabiliana na changamoto za uzalishaji.
“Nilimfundisha mama yangu mbinu za kuendelea kuzalisha mazao licha ya ukame, ikiwemo kuchimba mashimo shambani ili kukusanya na kuhifadhi maji ya mvua yatakayosaidia mboga kuendelea kustawi. Ingawa kuchimba na kutunza mashimo hayo kunagharimu fedha nyingi, mama yangu ameyatekeleza katika sehemu ya shamba lake na mbinu hiyo imeanza kuleta matokeo,” anasema.
Katika shamba lake, Kazungu anachanganya mbinu za jadi alizorithi kutoka kwa babu yake na mbinu mpya za kilimo. “Nilianzisha kilimo mseto cha miti. Pia nilianza kujifunza zaidi kuhusu mimea ya dawa,” anasema. “Kuna maarifa mengi mapya yanayopatikana kupitia mtandao. Vijana wanaweza kuyatumia kujifunza na kubuni mbinu mpya za kilimo.”
Serikali pia inajaribu kubadili hali hii kwa kuhamasisha vijana zaidi kujihusisha na kilimo. Mojawapo ya mipango yake muhimu ni 4K Club, ambayo ilizinduliwa upya na kupanuliwa mwaka 2025. Kupitia klabu hizo, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari hujifunza kuhusu kilimo na mbinu mbalimbali, zikiwemo umwagiliaji wa matone, bustani za wima na uhifadhi wa udongo. Tayari kuna klabu 2,700 kote nchini. Kupitia mpango wa NAVCDP Agripreneur, serikali pia huwawezesha wahitimu wa masomo ya kilimo kutoa ushauri kwa wakulima.
Hata hivyo, mipango hiyo italazimika pia kukabiliana na mtazamo hasi kuhusu kilimo miongoni mwa vijana. “Kilimo kinaonekana kama kazi isiyohitaji ujuzi mkubwa kwa watu wasio na elimu,” anasema Njagi. “Tunahitaji kukipa kilimo taswira mpya kwa vijana. Kilimo hakihusu uzalishaji wa mazao pekee, bali pia huduma za ugani, usambazaji wa pembejeo, ununuzi wa mazao na shughuli nyingine zinazohusiana na sekta hiyo. Hizo pia ni fursa za ubunifu.”
Habiba, mwenye umri wa miaka 17, ni mwanachama wa 4K Club katika shule yake huko Kiboro, Eastleigh. Akiupapasa udongo kuangalia kiwango cha unyevu, anaonyesha sehemu mbalimbali za bustani na kutaja mazao yanayolimwa hapo: “Kuna maboga, spinachi, sukuma wiki na maharagwe.”
Anasema hakuna hata mmoja wa marafiki zake anayetaka kuwa mkulima, na yeye mwenyewe hana mpango wa kuingia katika kilimo. Badala yake, anatamani kuwa mtaalamu wa mazingira. “Nataka kuwafundisha wakulima kuheshimu udongo zaidi na kutumia viuatilifu kidogo,” anaeleza.
Kazungu anatumaini kuwa shamba lake litawatia moyo vijana wengine kujihusisha na kilimo. Huandaa ziara za shambani kwa vijana wanaotaka kujifunza kuhusu kilimo-ikolojia, ambapo kila mshiriki hulipa Sh1,000 (takriban dola 8). Pia hutoa mafunzo kwa mashirika mbalimbali, jambo linalompatia kipato cha ziada mbali na mapato ya kilimo. “Baadhi yao wameamua kuanza kujihusisha na kilimo baada ya kuona simulizi langu mtandaoni. Tunaendelea kuwasiliana na kubadilishana maarifa,” anasema.
Picha ya bango: Leah Tembi George, mwenye umri wa miaka 58, akionyesha mavuno yake ya kunde katika shamba lake eneo la Tharaka Kaskazini, Kenya. Leah hupeleka mavuno yake katika Kituo cha Ukusanyaji wa Nafaka cha Mukothima, kilichoanzishwa kwa msaada wa AGRA. Shukrani kwa bei ya juu anayolipwa kwa kila kilo ya mazao yake, Leah ameweza kusomesha watoto wake wote sita. Picha na Karel Prinsloo, kwa hisani ya The Rockefeller Foundation.
Benki za chakula zageuza upotevu wa chakula kuwa milo na kupambana na mabadiliko ya tabianchi