- Mahakama imesitisha kwa miezi minne ukataji miti, uchimbaji na ujenzi katika eneo lenye mzozo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Nairobi.
- Kesi hiyo inaungwa mkono na Wakenya 4,642 wanaopinga kuhamishwa kwa Kituo cha Yatima wa Wanyama na ujenzi wa miundombinu saidizi.
- Wahifadhi wanaonya kuwa mradi unaweza kuharibu makazi ya wanyamapori, ardhi oevu na njia za wanyama, huku wakihoji uhalali wa vibali vya mazingira.
- KWS inasema kituo kipya kitaboresha utunzaji wa wanyamapori na kinaweza kuleta ajira 500, lakini mahakama bado haijaamua iwapo mradi ni halali.
NAIROBI, Kenya — Mahakama imeagiza kusitishwa kwa ujenzi na shughuli nyingine kwa miezi minne katika eneo lenye mzozo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Nairobi. Hatua hiyo inawapa wahifadhi na maelfu ya Wakenya muda zaidi wa kupinga mradi wanadai kuwa unaweza kuharibu makazi ya wanyamapori na kuathiri eneo hilo lililolindwa.
Jaji Grace Kemei wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi (Environment and Land Court) alitoa amri hiyo tarehe 27 Oktoba,2026. Amri hiyo inazuia kusafishwa kwa uoto, ukataji wa miti, uchimbaji na ujenzi katika eneo hilo imetolewa wakati kesi inayoungwa mkono na raia 4,642 wa Kenya ikiendelea.
Mahakama iliagiza eneo hilo libaki kama lilivyokuwa wakati maafisa wa mahakama walipolikagua tarehe 21 Julai. Hata hivyo, Kenya Wildlife Service (KWS) inaweza, kwa ruhusa ya mahakama, kufanya kazi zinazohitajika kulinda eneo hilo dhidi ya mmomonyoko wa udongo na uharibifu zaidi. Eneo hilo tayari limechimbwa na kuzungushiwa uzio.

Amri hiyo haizuii KWS kuwatunza wanyama katika Kituo cha Yatima wa Wanyama cha Nairobi (Nairobi Animal Orphanage) kilichopo sasa. Aidha haimzuii pia mshtakiwa wa sita kufanya kazi katika mali yake nje ya hifadhi.
Jaji Kemei aliwaagiza walalamikaji kukamilisha kesi yao ndani ya miezi minne isipokuwa pale mahakama itakapoongeza muda.
Uamuzi huo unasitisha shughuli zilizotajwa kwa muda tu, bila kuamua iwapo mradi unaopendekezwa ni halali ama la. Suala hilo litashughulikiwa wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi.
Raia washangilia ushindi wa muda
Uamuzi huu unafuatia miezi saba ya hatua za kisheria na kampeni za umma dhidi ya mipango ya kuhamisha Kituo cha Yatima wa Wanyama cha Nairobi na kujenga miundombinu saidizi ndani ya hifadhi.
Katika taarifa iliyotolewa baada ya uamuzi wa mahakama, wanaharakati walisema mapambano hayo yaliwachosha na kuwakasirisha, na baadhi yao walihisi kutishwa na kupuuzwa. Walisema msaada wa umma, ukiwemo maandamano, michango, kujipanga na kubadilishana taarifa, uliwasaidia kuendelea wakati ushindi ulipoonekana kuwa mbali.
“Wakenya wa kawaida 4,642 waliipeleka serikali mahakamani,” walisema wanaharakati hao, kwa mujibu wa gazeti la The Standard. Walieleza kuwa uamuzi huo ni ushindi kwa raia wanaotaka kuilinda hifadhi.
Hata hivyo waliwataka wananchi kuendelea kuwa macho katika kipindi cha miezi minne ambacho kesi itakuwa ikiendelea. Waliwaomba watu kurekodi na kuripoti shughuli zozote zilizopigwa marufuku katika eneo hilo, zikiwemo ukataji wa miti, uchimbaji, usafishaji wa ardhi pamoja na ujenzi.
Friends of Nairobi National Park, Just Act Kenya na Green Belt Movement ni miongoni mwa mashirika yanayohusishwa na kampeni hiyo. Ripoti za awali za Mongabay pia ziliandika kuhusu ushiriki wa Save the Nairobi National Park (SaveNNP) na JustAct katika kupinga mradi huo, na jinsi walivyoibua wasiwasi kuhusu upatikanaji wa eneo lililokaguliwa kwa amri ya mahakama.
Katika taarifa aliyotuma kwa Mongabay, Akshay Vishwanath, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Public Interest Litigation and Advocacy for the Environment (PILAE), alisema: “Miezi saba. Miezi saba ya kupigania Hifadhi ya Taifa ya Nairobi. Tumechoka, tumekasirika, tumetishwa na kupuuzwa. Kulikuwa na siku ambapo matumaini yalionekana kuwa mbali sana. Lakini hatukukata tamaa. Katika kipindi hiki chote, jambo la ajabu limekuwa likitokea. Watu ambao hawakuwa wakifahamiana wamekuwa marafiki. Watu wameandamana, kuchangia, kujipanga, kusambaza simulizi zetu na kututia nguvu wakati tulipokuwa hatuna nguvu tena za kuendelea”.

Wanaharakati wanasema lengo lao ni kupata ulinzi wa kudumu kwa hifadhi, si kusitishwa kwa ujenzi kwa muda tu.
Maraga akaribisha uamuzi wa mahakama
Jaji Mkuu wa zamani wa Kenya, David Maraga alikaribisha uamuzi huo wa mahakama, akivipongeza vikundi vya uhifadhi na raia walioiunga mkono kesi hiyo.
“Huu ni ushindi mkubwa wa katiba dhidi ya uvunjaji wa sheria wa serikali,” alisema Maraga, kwa mujibu wa gazeti la The Star.
Alirejelea Ibara ya 42 na 69 za Katiba ya Kenya. Ibara ya 42 inamhakikishia kila mtu haki ya kuishi katika mazingira safi na yenye afya wakati Ibara ya 69 inaeleza wajibu wa serikali wa kulinda mazingira na kusimamia maliasili kwa njia endelevu.
“Utawala wa Ruto unapozichukulia kanuni hizi takatifu kama mapendekezo ya hiari, ni wananchi wanaopaswa kutekeleza sheria,” alisema Maraga katika taarifa iliyoripotiwa na gazeti la The Standard.

Maraga alizitaka bodi na uongozi wa KWS kutimiza majukumu yao na kupinga kuingiliwa kisiasa. Pia alihoji kile alichokiita mgongano kati ya ahadi za kimataifa za serikali kuhusu tabianchi na uungaji wake mkono wa ujenzi wa miundombinu ndani ya hifadhi.
Alisema Hifadhi ya Taifa ya Nairobi inatoa manufaa yanayovuka utalii, ikiwemo kusaidia kusafisha hewa, kudhibiti joto la eneo, kupunguza mafuriko na kulinda rasilimali za maji.
Jaji mkuu huyo wa zamani pia aliwasifu vijana wa Kenya ambao, kwa mujibu wa taarifa yake, walipigwa gesi ya machozi na kukamatwa walipokuwa wakijaribu kuwasilisha ombi kwa KWS na kupanda miti.
Maraga alikamatwa pamoja na waandamanaji wengine wakati wa maandamano dhidi ya mradi huo tarehe 8 Juni. Ushiriki wake umevutia umakini zaidi kwa nafasi ya ushiriki wa umma na maandamano ya amani katika mizozo ya kimazingira.
Nini kimepangwa ndani ya hifadhi?
Kesi hiyo inahusu mipango ya kuhamisha na kuboresha Kituo cha Yatima wa Wanyama cha Nairobi, kituo cha kuegesha magari, barabara ya kuingia na daraja la waenda kwa miguu vinavyohusiana na mpango wa kupanua Bomas of Kenya kuwa kituo cha kimataifa cha mikutano.
Kituo hicho kilianzishwa mwaka 1964 na kwa sasa kiko kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 7.4. KWS inasema vifaa vyake vya sasa vimechakaa na havikidhi tena mahitaji ya kisasa ya utunzaji wa wanyama, uokoaji wa wanyamapori na urekebishaji wao.
Ripoti za awali za Mongabay zilieleza mapendekezo yanayohusisha kati ya ekari 76 na 89 za ardhi ya hifadhi. Mipango hiyo inajumuisha vifaa vya kuokoa na kurekebisha wanyama pamoja na eneo la kuegesha magari 1,300.
Kiasi cha ardhi kinachohusika bado kinabishaniwa. Nyaraka zilizotajwa katika ripoti zinazohusu kesi hiyo zinatoa takwimu tofauti, zikiwemo ekari 26, ekari 64, ekari 76.6 na karibu ekari 90. Walalamikaji wanasema tofauti hizi zinaibua maswali kuhusu ukubwa wa mradi na tathmini ya mazingira iliyotumika kuuidhinisha.
Kituo cha kuegesha magari pekee kinatarajiwa kuchukua takriban ekari nane. Mipango ya muda mrefu pia inajumuisha barabara ya kuingia na daraja la waenda kwa miguu litakalounganisha mradi na Bomas of Kenya kuvuka Barabara ya Lang’ata.
Wahifadhi wanahoji iwapo vifaa vyote hivi vinahitajika kwa kituo cha yatima wa wanyama, au pia vinahudumia mahitaji ya kituo cha mikutano kinachopangwa. Wanasema eneo la kuegesha magari na daraja vinapaswa kutathminiwa kwa athari zake za kimazingira vyenyewe.
KWS inasisitiza kwamba kuhamishwa kwa kituo cha yatima na ujenzi mpya wa Bomas ni miradi tofauti, ingawa iko karibu.
Wasiwasi kuhusu wanyamapori na mazingira
Walalamikaji wanasema mradi huo unaweza kuathiri uoto wa asili, nyika, ardhi oevu za msimu na makazi ya wanyamapori ndani ya hifadhi.
Wanasema tathmini ya mazingira haikuzingatia ipasavyo athari za muda mrefu ambazo eneo kubwa la kuegesha magari na miundombinu mingine zinaweza kuwa nazo kwa mfumo wa ikolojia unaoizunguka.
Kwa mujibu maombi ya kesi yaliyowasilishwa mahakamani, ongezeko la magari linaweza kuleta kelele zaidi, moshi wa magari, mwanga wa bandia na shughuli za binadamu katika makazi ya wanyamapori. Walalamikaji pia wameibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa kumwagika kwa mafuta, kuvuja kwa mafuta ya magari, na maji ya mvua kubeba uchafuzi hadi kwenye ardhi oevu na vijito vinavyoelekea Mto Mokoyiet.
Wanasema nyika na vichaka vya misitu katika eneo hilo ni sehemu za malisho, maeneo ya kuzaliana na njia zinazotumiwa na wanyamapori. Kwa hiyo wanasema eneo hilo linapaswa kutathminiwa kama sehemu ya mfumo mpana wa ikolojia, badala ya kuchukuliwa kama nyika wazi isiyo na thamani kubwa ya uhifadhi.
Hifadhi ya Taifa ya Nairobi ina wanyamapori wakiwemo simba, chui, duma, fisi na kifaru mweusi aliye karibu kutoweka. Ilianzishwa mwaka 1946, inachukua takriban kilomita za mraba 117 na inasifika kwa kuwa kando ya jiji kuu. Makazi yake pia ni sehemu ya mfumo mpana wa ikolojia wa Athi-Kapiti.
Walalamikaji wameuliza iwapo mradi ulipata vibali vyote vinavyohitajika kabla kazi kuanza. Wamehoji kiwango cha ushiriki wa umma, upatikanaji wa nyaraka za tathmini ya mazingira na utiifu wa mahitaji ya mipango, ujenzi na usimamizi wa trafiki.
Wamehoji pia iwapo idhini ya bunge ilihitajika kwa mabadiliko yoyote ya matumizi ya ardhi ndani ya hifadhi ya taifa iliyotangazwa kwenye gazeti rasmi la serikali.
Wasiwasi mwingine ni iwapo mipango hiyo inatii Mpango wa Usimamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Nairobi wa 2020–2030. Walalamikaji wanasema mpango huo unaliweka eneo lililoathirika katika kundi la matumizi ya chini, ambako majengo ya kudumu na barabara mpya zimewekewa vikwazo. Wanasema mpango huo ulitarajia upanuzi wa wastani wa kituo cha yatima kilichopo, si jengo kubwa lenye miundombinu mingi saidizi.
Wasiwasi huu ni sehemu ya hoja za walalamikaji na haujathibitishwa kama matokeo ya uamuzi wa karibuni wa mahakama.
KWS yasema kituo kipya kitaboresha utunzaji wa wanyama
KWS imetetea kuhamishwa kwa kituo, ikisema kituo cha yatima kilichopo kinahitaji vifaa bora zaidi vya kuwatunza wanyama waliookolewa na kusaidia urekebishaji wao.

Shirika hilo linasema kituo kilichoboreshwa kingekuwa na maeneo bora ya kuwahifadhi wanyama, vifaa vya daktari wa mifugo, huduma kwa wageni na hospitali ya wanyamapori. Linasema mradi huo ungeimarisha elimu ya uhifadhi na kutoa nafasi zaidi ya kuwapokea wanyama wanaohitaji uokoaji na matibabu.
KWS pia imesema kituo kipya kingetoa mazingira ya asili zaidi kwa ajili ya kuwarekebisha wanyama waliookolewa, na kuna uwezekano wa kuwaandaa baadhi yao kurudishwa porini.
Shirika hilo limekadiria kuwa mradi unaweza kuzalisha ajira takriban 500. Katika ripoti za awali, Mkurugenzi Mkuu wa KWS Erastus Kanja alisema kituo kilichoboreshwa kingeimarisha hali wanamotunzwa na kurekebishwa wanyama waliookolewa.
KWS inasisitiza kwamba mradi ulifanyiwa tathmini ya mazingira na kwamba Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira (National Environment Management Authority) ilitoa leseni ya mazingira Desemba 2025.
Walalamikaji wanabishana kuhusu iwapo mchakato wa idhini na kazi zilizofanywa katika eneo hilo zilitimiza mahitaji yote ya kisheria. Wanataka mahakama ichunguze leseni na vibali vingine, na kuvifuta iwapo itabainika vilitolewa isivyo halali.
Uamuzi wa karibuni haumalizi mabishano haya bali unasitisha shughuli zilizotajwa wakati mahakama inaendelea kuisikiliza kesi ya msingi.
Mvutano kuhusu ukaguzi wa mahakama
Kesi hii pia imehusisha mzozo kuhusu upatikanaji wa eneo la mradi unaopendekezwa wakati wa ukaguzi wa mahakama.
Tarehe 16 Julai, mahakama ilimwagiza Naibu Msajili Vincent Kiplagat kutembelea eneo hilo pamoja na pande husika na kuandaa ripoti. Ukaguzi ulifanyika tarehe 21 Julai, ukiwahusisha wawakilishi wa KWS na walalamikaji.
Katika ripoti iliyochapishwa tarehe 24 Julai, Mongabay iliandika madai kwamba wahifadhi walipata ugumu kuingia eneo hilo wakati wa ukaguzi.
SaveNNP na JustAct ziliwatuhumu watumishi wa KWS kwa vitisho, na kusema vikwazo hivyo vilipunguza uwezo wao wa kueleza wasiwasi wao mbele ya mahakama na vyombo vya habari. Friends of Nairobi National Park pia iliibua wasiwasi kuhusu upatikanaji wa eneo hilo.
Msemaji wa KWS Duncan Wanyama alikanusha madai hayo, akisema wageni hawakuzuiwa na kwamba walinzi wa wanyamapori walikuwa wakifuata taratibu za kawaida za kusimamia upatikanaji wa hifadhi.
Wanaharakati walisema waliruhusiwa kuingia eneo hilo, baada ya maafisa wa mahakama, wawakilishi wa KWS, wanahabari na wakili aliyeruhusiwa kuingia kukamilisha ukaguzi.
Mzozo huo uliongeza wasiwasi mpana kuhusu uwazi na ushiriki wa umma katika mradi. Hata hivyo, madai kuhusu upatikanaji wa eneo hayathibitishi kwamba mchakato wa idhini ya mazingira ulikiuka sheria.
Maandamano katika mwaka wa maadhimisho ya miaka 80 ya hifadhi
Kesi hiyo imeendelea sambamba na miezi ya upinzani wa umma dhidi ya mradi unaopendekezwa.
Tarehe 8 Juni, Maraga na wanaharakati wengine walikamatwa wakati wa maandamano dhidi ya mradi. Maandamano hayo yalipewa uzito na hofu kwamba miundombinu ya ziada inaweza kuiongezea hifadhi shinikizo zaidi.
Tarehe 30 Agosti, wahifadhi na wananchi walikusanyika karibu na hifadhi kuadhimisha miaka 80 tangu ianzishwe, huku wakipinga kuhamishwa kwa kituo cha yatima na ujenzi unaohusiana nacho.
Wanaharakati wanasema eneo la Hifadhi ya Taifa ya Nairobi kando ya jiji linalokua linafanya ulinzi wake kuwa wa muhimu zaidi, hasa Nairobi inapopanuka na mahitaji ya barabara, maegesho na vifaa vya kibiashara yanapoongezeka.
Kampeni hiyo imewaunganisha raia, mashirika ya mazingira na watetezi wa uhifadhi wanaotaka serikali ieleze jinsi mradi unaopendekezwa utakavyoathiri hifadhi.
Kwa upande wake, KWS inasema kuhamishwa kwa kituo kungeboresha uokoaji wa wanyamapori na ustawi wa wanyama, huku kikisaidia elimu ya uhifadhi na huduma kwa wageni.
Nini kitafuata?
Amri ya miezi minne inawapa walalamikaji muda wa kukamilisha kesi yao, isipokuwa kama mahakama itaongeza muda. Shughuli zilizotajwa lazima zibaki zimesitishwa katika kipindi hicho, isipokuwa katika maeneo machache yaliyopo katika amri hiyo.
Mahakama itahitaji kuzingatia iwapo mradi unatii sheria ya mazingira, kinga za kikatiba zinazoongoza hifadhi, na mahitaji husika ya mipango na uhifadhi wa wanyamapori.
Walalamikaji wanatafuta amri za kusimamisha kabisa kazi zinazobishaniwa, tamko kwamba mradi si halali, na kufutwa kwa idhini wanazosema zilitolewa kinyume na taratibu. Pia wameomba maeneo yaliyoharibiwa yarejeshwe na kuwekewa kinga dhidi ya maendeleo ya baadaye yasiyokidhi mahitaji ya kisheria.

Kwa KWS, kesi hii ni fursa ya kutetea mipango yake ya kuboresha uokoaji na urekebishaji wa wanyamapori, na kujibu maswali kuhusu iwapo mradi unakidhi mahitaji yanayosimamia maeneo yaliyolindwa.
Kwa wahifadhi, kipaumbele cha haraka ni kuzuia kazi zaidi katika eneo lenye mzozo hadi mahakama itakapozingatia masuala ya kisheria na kimazingira.
Uamuzi huo umezipa pande zote mbili muda, lakini haujatatua maswali ya msingi: ni sehemu ngapi ya hifadhi ingeathiriwa, iwapo tathmini ya mazingira ilizingatia ipasavyo athari za pamoja za maendeleo yanayopendekezwa, na iwapo miundombinu hiyo inaweza kujengwa kihalali ndani ya eneo lililolindwa.
Picha ya bango: Mahakama imeagiza kusitishwa kwa ujenzi na shughuli nyingine kwa miezi minne katika eneo lenye mzozo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Nairobi.
Bioanuwai hatarini: Uhamisho wa kituo cha wanyama yatima wazua wasiwasi miongoni mwa wahifadhi
Kenya’s former Chief Justice David Maraga arrested at protest of national park construction