- Kikundi cha Yungi Mwenjeni Conservation Group kina zaidi ya mizinga 100 ya nyuki na kinaendesha ufugaji nyuki katika misitu ya mikoko ya Kwale ili kupunguza ukataji wa miti hiyo.
- Wanawake hao wanasema ukataji wa mikoko umepungua tangu waanze kuweka mizinga ya nyuki msituni, huku ufugaji huo ukiwapatia kipato kupitia uuzaji wa asali.
- Kikundi hicho kimepanda zaidi ya miche 500,000 ya mikoko na kina miche zaidi ya 38,000 iliyo tayari kuuzwa na kupandwa katika maeneo yaliyoharibiwa.
- Ufugaji nyuki unakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo mvua nyingi zinazodondosha maua ya mikoko na ukame unaokausha masega na kupunguza uzalishaji wa asali.
KWALE, Kenya – Kwa kipindi cha miaka mitatu, Khadija Khamisi alikuwa mwalimu wa shule ya msingi katika kijiji anachoishi cha Mwenjeni, eneo bunge la Lunga Lunga. Baadaye aliamua kuacha kazi hiyo na kujikita katika shughuli za ufugaji wa nyuki katika maeneo ya msitu wa mikoko kama njia moja ya kulinda miti hiyo dhidi ya ukataji holela. Pia alilenga kujipatia riziki.
Khadija anasema kipato chake kama mwalimu kilikuwa duni, kwani alikuwa ameandikwa chini ya mpango maalum wa kulipwa na wazazi.
Fatuma Saidi pia alijikuta katika hali hiyo, na alihitaji suluhisho.

Wawili hawa walishirikiana na wanawake wengine mwaka wa 2022 na kuunda kikundi cha wanawake wanaolinda mazingira. Waliita kikundi hicho Yungi Mwenjeni Conservation Group, wakianza na wanachama 36, kumi kati yao wakiwa wanaume.
Lengo kuu la kikundi hiki kilikiwa ni kulinda mazingira ya baharini kwa kupanda mikoko, kufuga nyuki kwenye mikoko ili kuilinda, kupanda mwani baharini na uokotaji wa taka kwenye ufuo wa bahari.
Khadija anasema walianza kwa kutengeneza mizinga 12 ya nyuki. Baada ya miezi minne, tisa kati yao zilikuwa tayari kuvunwa. Hata hivyo hawakuwa na ujuzi wa kuvuna asali. Walitafuta mhisani aliyewasaidia kuvuna asali hiyo.
“Tulitafuta jirani hapa, ambaye ni mtaalamu, akaja akatuvunia. Alituvunia kidogo akasema imeisha na kwamba iliyobaki ni chakula cha nyuki. Tulikubali kwa sababu hatukuelewa chochote. Huyo huyo aliyetuvunia akarudi akavuna tena na akachukua akaenda nayo,” Khadija alielezea.
Lakini kwa sasa Khadija anasema hakuna mtu anaweza kuwaibia tena, kwani baada ya kisa hicho walipata mafunzo kutoka kwa shirika la uhifadhi wa mazingira la Coastal and Marine Resource Development (COMRED), ya jinsi ya kutega mizinga kwenye mikoko na kutengeneza asali.

Sasa Khadija na Fatuma ni miongoni wakufunzi wa wakufunzi sita katika kikundi hicho cha uhifadhi wa mazingira cha Yungi Mwenjeni.
Kazi yao kubwa ni kusafisha mizinga, kisha kuangalia sehemu za kutega mizinga hiyo kwenye msitu wa mikoko.
Miongoni mwa mambo wanayoyazingatia sana wakati wa kuweka mizinga ni eneo ambalo lina mikoko iliyokomaa vizuri. Hii hutoa mazingira mazuri ya nyuki kufanya uchavushaji, na iko kwenye hatari ya kukatwa.
Mikoko ni aina ya miti au vichaka vinavyokua katika maji ya chumvi, hasa kwenye fukwe za bahari za kanda za tropiki.
Mikoko ni mifumo muhimu ya ikolojia ya pwani inayosaidia kupunguza mmomonyoko wa ardhi, kuzuia nguvu za mawimbi makubwa ya bahari, na kutoa mazalia mazuri ya samaki pamoja na viumbe wengine wa baharini.

Kulingana na FAO, nyuki pia huchangia ustawishaji wa mikoko. Nyuki hula nekta kutoka kwenye maua ya mikoko. Kitendo hicho ni muhimu kwa sababu huongeza uchavushaji, na hivyo kusaidia mikoko kuzaliana na kukua vizuri zaidi, na kuboresha ikolojia ya bahari na mazalia ya samaki.
Takwimu kutoka shirika la huduma ya misitu nchini zinaonyesha kuwa asilimia 40 ya misitu ya mikoko imeharibiwa, watu wakiikata na kutumia kama kuni, makaa na kujengea, jambo linalosababisha kudhohofika kwa ikolojia ya bahari na kuharibu mazalia ya samaki.
Fatuma Saidi, ambaye ni mwandishi wa kikundi hicho cha Yungi Mwenjeni, na pia mkufunzi wa wakufunzi kwa masuala ya ufugaji na utengenezaji wa asali, anasema tangu waanze harakati hizo za ufugaji nyuki, kiwango cha watu wanaoingia msituni humo kimepungua.
“Kabla tuanze ufugaji wa nyuki kwenye mikoko, hungekosa kuona watu wawili, au hata watano kwa mwezi, wakikata mikoko. Lakini tangu tuweke mizinga ya nyuki, tunaweza kukaa hata mwezi bila kuona mtu akikata mikoko. Hii ni kwa sababu wanaogopa kushambuliwa na nyuki,” anasema Fatuma.
Kwa sasa, Fatuma anasema kikundi hicho kina zaidi ya mizinga 100 ya nyuki ambayo wameiweka katika maeneo mbalimbali ndani ya misitu ya mikoko.
Fatuma pamoja na wakufunzi wenzake hupanga zamu ya kuangalia mizinga hiyo kila siku kwa siku 14, ili kuona kama nyuki wameingia na kujenga. Baadaye huhamisha mizinga hiyo na kuipeleka kwenye eneo lililotengwa kwa ufugaji nyuki, ambalo wamejenga ndani ya msitu, na kuendelea kuiangalia kwa umakini kabla ya kuvuna asali yake.
Kwa mujibu wa Fatuma, mzinga mmoja hutengeneza kilo 15 za asali, ambazo huuzwa kwa KSh650 ($5.01) kila moja. Wao huvuna mara tatu ama nne kwa mwaka, kulingana na hali ya hewa na upatikanaji wa maua.
Hata hivyo, Khadija anasema kazi hiyo haikosi changamoto zake. Anasema wakati wanaposhuhudia mvua nyingi, maua ya mikoko huanguka, hivyo nyuki hukosa pa ya kutengenezea asali.
Pia kunaposhuhudiwa kipindi kirefu cha kiangazi, masega hukauka, na kuifanya vigumu kwa nyuki kutengeneza asali. “Mabadiliko ya tabianchi mara nyingi huathiri shughuli zetu. Kwa mfano, nilikuwa na mizinga, ambayo nilitarajia kuvuna asali yake Septemba. Lakini kwa sasa haina asali kwa sababu mvua ilikuwa nyingi ikaangusha maua mengi,” anasema Khadija.
Dk. Judy Okello, mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Bahari na Uvuvi (KMFRI) na mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mikoko, anasema ingawa bado hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha uhusiano huo moja kwa moja, shughuli mbadala za kijamii za kujipatia kipato, kama vile ufugaji wa nyuki kwenye misitu ya mikoko, zinaweza kuwa na mchango mkubwa katika uhifadhi wa mikoko na rasilimali nyingine za asili.
“Tunajua watu wengi wanategemea rasilimali za asili kupata riziki kwa sababu ya umaskini. Ukiweza kuwapatia njia nyingine za kujipatia kipato kupitia rasilimali hizo, basi unapunguza utegemezi huo na kuwapa sababu zaidi za kuhifadhi mazingira,” Dk. Okello aliiambia Mongabay.
Aliongeza kuwa miradi ya kiuchumi, ikiwemo ufugaji nyuki, inaweza pia kusaidia kuimarisha ulinzi wa misitu ya mikoko kwa njia nyingi. “Unapokuwa na mradi wako karibu na msitu, unalazimika kuutembelea mara kwa mara ili kuuangalia na kuhakikisha shughuli zako zinaendelea vizuri. Kwa namna hiyo, unakuwa kama mlinzi wa eneo hilo, kwa sababu uwepo wako unasaidia kufuatilia kinachoendelea.
“Zaidi, nyuki si wadudu wa kuchezea. Watu wakijua kuna mizinga ya nyuki eneo fulani, baadhi yao wataepuka kuingia humo. Kwa njia hiyo, ufugaji nyuki unaweza kusaidia kuzuia watu kuingia msituni kiholela na hivyo kuchangia katika uhifadhi wa mikoko,” anaeleza Dk. Okello.
Mbali na ufugaji wa nyuki kwenye msitu huo, kina mama hao wa Majoreni pia hupanda mikoko kwenye maeneo ambayo yameharibiwa kabisa ili kuregesha msitu huo.
Misitu ya mikoko katika Kaunti ya Kwale inakadiriwa kuwa eneo la takribani ekari 8,354, ikijumuisha maeneo ya Msambweni-Vanga, Gazi na Ukunda.
Eneo la bahari la Msambweni-Vanga lina ukubwa wa ekari 7,638, na linajumuisha misitu ya mikoko ya Ramisi, Majoreni na Kisiwa cha Sii. Mfumo huu ni miongoni mwa maeneo muhimu ya mikoko katika kaunti hiyo.

Tafiti zinaonyesha kuwa takribani ekari 3,725, sawa na asilimia 45 ya misitu yote ya mikoko katika Kaunti ya Kwale, zinahitaji kurejeshwa na kuimarishwa ili kukabiliana na uharibifu na kuhakikisha mikoko inaendelea kutekeleza jukumu lake la kulinda mazingira ya pwani.
Fatuma anasema kama kikundi, hadi kufikia sasa wamepanda zaidi ya miche 500,000 ya mikoko kwa kujitolea katika msitu huo. Miongoni mwa mikoko ambayo wao hupanda ni pamoja na Mchu (Avicennia marina), Mdiago (Rhizophora mucronata), Mkandaa (Ceriops tagal) na Mkoko mweupe (Avicennia marina), huku wakilenga maeneo ambayo yameharibiwa kabisa.
Wao pia huuza miche ya mikoko kwa wanunuzi wa kibinafsi na mashirika kwa kati ya KSh50 ($0.39) na KSh70 ($0.54). Pesa hizo huingia kwenye mfuko wa kikundi na mwishoni mwa mwaka wao hugawanya.
Kwa sasa, wana zaidi ya miche 38,000 ya mikoko ambayo iko tayari kuuzwa na kupandwa. Juhudi hizo zinaanza kuzaa matunda, kwani kulingana na >COMRED, vikundi mbalimbali vya kulinda mazingira, vikiwemo Mwandamu na Majoreni katika Kaunti ya Kwale, hadi kufikia sasa vimepanda na kuhifadhi mikoko katika eneo lililoharibika lenye ukubwa wa takriban ekari 1.77.
Juhudi hizo za wanawake za kuhifadhi msitu wa mikoko katika eneo la Majoreni zinaendana na ripoti mpya ya mwaka 2026 kuhusu hali ya mikoko duniani, iliyotolewa na Global Mangrove Alliance.
Ripoti hiyo imeonyesha kupungua kwa kasi ya ukataji wa mikoko, huku jamii ikiongeza uelewa wao kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa misiu hiyo.
Kwa sasa, zaidi ya asilimia 42 ya mikoko iliyosalia duniani iko chini ya ulinzi rasmi kwa ajili ya uhifadhi, huku juhudi za kurejesha maeneo yaliyoharibiwa zikiongezeka pamoja na matumizi ya mbinu bunifu za uhifadhi.
Ripoti hiyo inasisitiza umuhimu wa kushirikisha jamii ya maeneo husika katika kusimamia miradi ya uhifadhi wa mikoko, kwani jamii zinaposhirikishwa huwa na nafasi kubwa ya kukidhi mahitaji yao, kukabiliana na sababu za uharibifu wa mikoko na kupata uungwaji mkono wa kudumu.
Fatuma anasema mbali na kulinda ikolojia ya mikoko na kuimarisha mazalia ya samaki kwa wavuvi kupata mavuno mazuri, ufugaji wa nyuki na uuzaji wa asali umeinua maisha ya jamii ya eneo hilo kiuchumi.
Anasema fedha wanazopata zimesaidia sana wanawake hao kujitegemea, kuwa na uhuru wa kufanya maamuzi, kulipia watoto wao karo ya shule, kuboresha nyumba zao, na kujenga mtaji wa kuanzisha biashara ndogondogo.
“Mimi pia nilikuwa mkulima wa nchi kavu. Siku moja nyani walishambulia shamba langu na kuharibu mahindi na kunde zangu zote. Nilikoma kulima. Tangu nianze ufugaji wa nyuki na upandaji wa mikoko, nimeshuhudia uzuri wa kipato chake. Hata mume wangu sasa tunasaidiana naye kujikimu kimaisha,” anasema Fatuma.
Mohammed Bakari, mkaazi wa kijiji hicho cha Mwenjeni, anasema japo yeye si mmoja wa wanachama, amemruhusu mkewe kujiunga na kikundi hicho cha uhifadhi.
“Mimi niliacha mke wangu ajiunge na kikundi hiki na mimi nishike njia nyengine za kuleta mapato nyumbani. Yaani yeye alete, na mimi niende kuleta. Hata saa hii mke wangu yuko kwa mikoko. Kupitia kikundi hiki, mke wangu amenunua viti viwili nyumbani. Nashkuru,” anasema Bakari.

Kwa wanawake wa Yungi Mwenjeni Conservation Group, ufugaji wa nyuki na upandaji wa mikoko umekuwa zaidi ya njia ya kujipatia kipato. Shughuli hizo zimewapa nafasi ya kujitegemea kiuchumi huku zikichangia kulinda misitu ya mikoko inayotegemewa na jamii za pwani kwa maisha na riziki zao.
Kadiri wanavyoendelea kurejesha maeneo yaliyoharibiwa na kutunza mizinga yao, wanawake hao wanatumai kuwa juhudi zao zitaendeleza uhifadhi wa mikoko na kuimarisha maisha ya vizazi vijavyo.
Picha ya bango: Khadija Khamisi na Fatuma Saidi kwenye msitu wa mikoko wa Majoreni wakionyesha baadhi ya mizinga ya nyuki ambayo wametega kwenye mikoko ili kuilinda dhidi ya ukataji kiholela. Picha na Ruth Keah, Mongabay.
Wanawake wanarejesha bioanuwai, lakini hawana umiliki wa ardhi wanayotunza