- El Niño ambayo imerejea inatarajiwa kufikia kilele chake mwishoni mwa 2026. Barani Afrika, inatarajiwa kusababisha joto kali, ukame na mafuriko makubwa.
- Tukio la mwisho la El Niño, lililotokea mwaka 2023 hadi 2024, lilisababisha makumi ya mamilioni ya watu kukosa mahitaji muhimu, yakiwemo chakula, lishe bora na maji, inaonya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA). Ofisi hiyo inasema kuwa tukio hili linatarajiwa kuwa “kali zaidi.”
- Katika maeneo mbalimbali barani Afrika, serikali na mashirika ya Umoja wa Mataifa wameweka mipango ya kuwaandaa wananchi.
- Nchini Burkina Faso, Zimbabwe na Kenya, wanajamii wamepongeza juhudi hizo, lakini wanasema hazitoshi.
“Mara tu mvua inapoanza kunyesha, eneo la Nairobi Magharibi hufurika maji. Mwaka jana, magari yalisombwa na maji ya mvua na hatukuweza hata kutoka nyumbani. Lakini ninaposikia kwamba mwaka huu tutakabiliwa na El Niño kali zaidi kuwahi kutokea katika historia, ninaogopa, kwa kweli ninaogopa sana. Safari hii hali itakuwa mbaya zaidi,” anasema Abigail Arunga kwa hofu, akizungumza na Mongabay.
Msimu wa mvua jijini Nairobi huanza Oktoba, lakini mwaka huu mvua inaweza kuwa nyingi kuliko kawaida. El Niño ambayo imerejea inatarajiwa kufikia kilele chake mwishoni mwa 2026. Barani Afrika, inatarajiwa kusababisha joto kali, ukame na mafuriko makubwa.
“El Niño iliyopita, iliyotokea mwaka wa 2023 hadi 2024, iliacha makumi ya mamilioni ya watu wakihitaji chakula, lishe, maji, huduma za usafi, huduma za afya, msaada wa kilimo au ulinzi. Utabiri huo unatisha sana : safari hii hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi,” Tom Fletcher, naibu katibu mkuu anayeshughulikia masuala ya kibinadamu katika OCHA, idara ya Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa, alisema katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa X.
El Niño ni nini?
El Niño ni hali ya kawaida inayotokea kwa wastani kila baada ya miaka miwili hadi saba. Kwa mujibu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), hutokana na ongezeko lisilo la kawaida la joto la maji katika Bahari ya Pasifiki. Upepo unapodhoofika, maji ya bahari yenye joto, ambayo kwa kawaida yangesukumwa kuelekea Asia, hukusanyika karibu na pwani za Amerika. Mabadiliko hayo ya mgawanyo wa maji huathiri shinikizo la anga na mvua, na kusababisha ukame na mafuriko makali kuliko kawaida. Kwa kuwa El Niño hutokea mara kwa mara, mashirika ya hali ya hewa yanaweza kuitabiri mapema. Mwaka huu, tahadhari zimekuwa zikiongezeka tangu Mei.
“Tuna taarifa za kisayansi. Tumeonywa mapema. Na bado tuna muda wa kuchukua hatua,” Celeste Saulo, katibu mkuu wa WMO, alisema katika hafla iliyoandaliwa mjini New York mwaka 2026 kama sehemu ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Katika maeneo mbalimbali barani Afrika, serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali tayari wameanza kujiandaa.
Kwa mujibu wa UNICEF, zaidi ya watoto milioni 162, ambao ni zaidi ya theluthi mbili ya watoto wanaoishi Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, wako katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na El Niño. Ethiopia, Kenya, Madagascar, Sudan Kusini na Zimbabwe ni miongoni mwa nchi zilizo katika hatari kubwa zaidi. kwa hiyo, watoto hao wanaweza kukosa chakula na maji safi ya kunywa.
UNICEF iliiambia Mongabay kuwa tayari imeanza kushirikiana na serikali za maeneo husika, WMO na huduma za kitaifa za hali ya hewa katika nchi inazoziona kuwa hatarini ili kukabiliana na hali hiyo. “Utabiri wa hali ya hewa huwa na manufaa ikiwa utasababisha hatua madhubuti kuchukuliwa kabla ya janga kutokea,” Mathilde Lecluse, afisa wa Mpango wa Kimataifa wa Utetezi wa Hali ya Hewa na Lishe katika UNICEF Ufaransa, aliambia Mongabay kupitia barua pepe.
“Leo, utabiri huu unatupa fursa ya kuchukua hatua kabla athari zake hazijasababisha kuongezeka kwa njaa, utapiamlo, magonjwa, kuhama kwa watu kutoka maeneno yao na kukatizwa kwa masomo ya watoto,” aliongeza Lecluse.

Kenya yakabiliwa na hatari ya mafuriko
Nchini Kenya, El Niño ya 2023 na 2024 ilisababisha vifo vya watu 490 na kuwalazimisha wengine 729,000 kuhama makazi yao. Mapema mwezi Septemba, Wizara ya Mambo ya Ndani ilitangaza hatua saba za kuiandaa nchi kukabiliana na mvua kubwa inayotarajiwa. Hatua hizo zilijumuisha kutambua na kuweka kwenye ramani maeneo yaliyo katika hatari ya mafuriko, kujiandaa kwa uhamishaji wa watu kutoka maeneo hatarishi, pamoja na matengenezo ya miundombinu ya kupitisha maji ya mvua.
“Huu ni mwanzo mzuri, lakini Nairobi ina majengo mengi yaliyojengwa kinyume cha sheria. Majengo mazima hujengwa ingawa hayakupaswa kujengwa, wakati mwingine bila vibali, na wakati mwingine kwa vibali vilivyopatikana kwa njia isiyojulikana. Na majengo haya hayajengwi kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa, jambo ambalo linaongeza shinikizo kwenye mifereji. Kwa hivyo, kusafisha mifereji ni jambo zuri, lakini tusiposhughulikia matatizo mengine, nina hofu kwamba hilo halitatosha,” Arunga alisema.
Mongabay iliwasiliana na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ili kupata maelezo zaidi, lakini hakujibu maombi ya maoni.
Zimbabwe yaelekeza nguvu katika sekta ya kilimo
Nchini Zimbabwe, El Niño inatarajiwa kusababisha ukame mkali na joto la juu. Serikali inawahakikishia wananchi kuwa imejiandaa kukabiliana na hali hiyo, na imeweka mpango wenye hatua sita, unaoitwa “mpango wa kukabiliana na ukame” ili kuwasaidia wakulima. “Tunataka kurekebisha mazao yetu yaendane na msimu wa mvua unaotarajiwa kuwa na maji chache na mfupi zaidi; pia tunataka kurekebisha mifumo yetu ya umwagiliaji,” Jiri Obert, katibu mkuu katika Wizara ya Kilimo, Mitambo na Maendeleo ya Rasilimali za Maji, alisema katika mahojiano na kituo cha kitaifa. Mbali na kurekebisha mifumo ya umwagiliaji ili kukabiliana na El Niño, serikali ya Zimbabwe inapanga, miongoni mwa hatua nyingine, kuingia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ili kuagiza nafaka kutoka nje ya nchi. Pia inataka kuhimiza kilimo cha mazao ya asili badala ya mahindi, ambayo hulimwa kwa wingi lakini huhitaji maji mengi.
Ili kutekeleza mpango huo, serikali inasema ilizingatia yaliyotokea mwaka 2023 hadi 2024 kipindi ambacho kilishuhudia ukame mkali zaidi katika kipindi cha miaka 43 iliyopita, kwa mujibu wa Obert. “Tumeandaa ramani za uthabiti wa mazao. Ramani hizi zinajumuisha utabiri wa mvua, na tumeulinganisha na data ya mwaka wa 2024,” alisema. Ramani hiyo inalenga kuboresha mavuno. “Sasa kwa kuwa tuko katika hali inayofanana, au hata mbaya zaidi, tutaweza kuwaambia kwamba ikiwa mko katika eneo hili, haya ndiyo mnayopaswa kufanya. Haya ndiyo mnayopaswa kulima,” aliendelea Obert.
Tendai Ruben Mbofana, mwanaharakati wa kupambana na ufisadi nchini Zimbabwe, alisema hatua hizo zinaonyesha nia njema ya serikali, lakini ni vigumu kuzitekeleza. “Kulazimisha mabadiliko ya mazao, kwa kubadilisha mahindi na nafaka za jadi, kunakwenda kinyume moja kwa moja na mapendeleo ya walaji, ukwasi wa soko na miundombinu ya usindikaji, ambayo karibu yote imeelekezwa kwenye mahindi meupe,” aliiambia Mongabay kwa simu. “Kwa upande wa biashara, kutegemea umwagiliaji kunahitaji gridi ya umeme iliyo thabiti kwa ajili ya kusukuma maji na kujazwa tena vya kutosha kwa maji ya chini ya ardhi, mambo mawili ambayo huzorota haraka wakati wa vipindi virefu vya joto kali. Zaidi ya hayo, kutegemea sekta binafsi kuagiza nafaka kutoka nje chini ya SI 87 kunafanya soko la chakula la ndani likabiliwe na kuyumba kwa bei za kimataifa na hatari za viwango vya kubadilisha fedha (za kifedha, maelezo ya mhariri),” aliongeza.
Hali ikoje Afrika Magharibi?
Afrika Magharibi, ukosefu wa mvua unaweza kuibebesha sekta ya kilimo mzigo zaidi. “Kwa sasa kuna maeneo yenye ukame, na hali bado inatia wasiwasi Afrika Magharibi,” Dk. Ulrich Diasso, mtaalamu wa hali ya hewa na mifumo ya tahadhari ya mapema nchini Burkina Faso, ambaye pia anaongoza timu inayotoa usaidizi wa kiufundi kwa Tume ya Umoja wa Afrika, alisema katika mahojiano na Mongabay.
Tahadhari ya hali ya hewa iliyotolewa mwishoni mwa Mei 2026 na Centre régional de formation et d’application en agrométéorologie et en hydrologie opérationnelle (AGRHYMET) inaonyesha kuwa eneo la magharibi mwa Sahel, hasa Senegal, Mauritania na magharibi mwa Mali, linaweza kukumbwa na vipindi vya ukame. Kwa upande mwingine, maeneo ya kati na mashariki mwa Sahel, yakiwemo Niger, Chad, mashariki mwa Mali na sehemu ya kati-mashariki mwa Burkina Faso, yanaweza kupata mvua zinazokaribia au kuzidi kiwango cha kawaida, na hivyo kuongeza hatari ya mafuriko.
AGRHYMET, mojawapo ya vituo vikuu vya utabiri wa hali ya kilimo, maji na hewa, inasema mvua katika eneo la Ghuba ya Guinea zitaambatana na vipindi vya mvua kubwa vinavyoweza kusababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo. Kupishana kwa vipindi virefu vya ukame na mvua kubwa kunaweza kupunguza tija ya kilimo na kuongeza hatari ya mafuriko na upungufu wa maji.
Hata hivyo, Dk. Diasso alisema kufuatilia tahadhari ni hatua ya kwanza tu ya kukabiliana na hali hii ya hewa. “Serikali na wadau wengine wanapaswa kuelekeza upya fedha kwenye miundombinu na huduma zinazowapa wakulima uwezo zaidi wa kukabiliana na hali hiyo,” alisisitiza, akitaja upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa kuwa mojawapo ya nyenzo zinazohitaji kuimarishwa.
Baada ya kutangazwa kwa kurejea kwa El Niño, serikali ya Burkina Faso ilianzisha mipango kadhaa, ukiwemo mpango wa “uchimbaji wa visima kwa bei ya ruzuku.” Mpango huo, ulioanzishwa Septemba 2026, unalenga kuongeza upatikanaji wa maji na kusaidia uzalishaji wa kilimo katika nchi ambayo kilimo chake hutegemea mvua kwa kiasi kikubwa. Kwa mujibu wa serikali, hatua hiyo itasaidia jamii kuongeza mavuno na kukabiliana na uhaba wa chakula. “Changamoto iliyopo sasa [katika Sahel] ni kubwa zaidi kwa sababu wakulima wanaweza kukabiliwa na msimu wenye vipindi vya ukame na vipindi vya mvua kubwa kwa wakati mmoja,” Dk. Diasso alisisitiza.
Kwa mujibu wa UNICEF, takriban watoto milioni 20 katika Afrika Magharibi na Kati wanaweza kuathiriwa na El Niño hii.

Upungufu wa maji unaweza kuzua ukosefu wa usalama katika Sahel
AGRHYMET pia inaonyesha kuwa El Niño itapunguza upatikanaji wa maji katika nchi za Sahel, yaani Burkina Faso, Mali, Mauritania, Niger, Senegal na Chad. Hali tayari inatia wasiwasi katika baadhi ya maeneo ya Niger, Chad, Mali na Burkina Faso, ambako kiwango cha mvua kilichorekodiwa mwaka huu katika baadhi ya maeneo kimekuwa chini ya wastani kwa zaidi ya asilimia 40. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, zaidi ya watu milioni 20 katika nchi hizo wanategemea moja kwa moja ufugaji wa kuhamahama, huku maeneo ambayo wafugaji wanaweza kupeleka mifugo yao malishoni yakizidi kupungua. El Niño inaweza kufanya hali hiyo kuwa mbaya zaidi na kuwalazimisha wafugaji, pamoja na wanyama wa kufugwa na wa porini, kuhama. “Kuhamahama huku kunaweza kuongeza ushindani kwenye vyanzo vya maji na malisho,” Dk. Diasso aliiambia Mongabay.
Utafiti wa Sarah Booghs, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Montréal nchini Kanada, uliochapishwa katika jarida la kisayansi Flux: International Relations Review, unaonyesha kuwa athari zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi zinaweza kuongeza mvutano kati ya wakulima na wafugaji katika maeneo ambako migogoro ya silaha na kuhama kwa watu tayari kunatatiza upatikanaji wa ardhi, masoko na huduma muhimu.
Hata hivyo, hali haitokei kwa namna sawa katika maeneo yote ya Sahel. Hilo linaonekana wazi nchini Niger, ambako baadhi ya maeneo yanakabiliwa na ukame huku mengine yakiwa yamefurika. Kwa mujibu wa OCHA, hadi 14 Septemba 2026, mafuriko hayo yalikuwa yameathiri watu 57,356, hasa katika maeneo ya Maradi, Zinder na Dosso.
“Mabadiliko haya ya kubadilishana kati ya vipindi vya mvua chache na vipindi vya mvua kubwa hufanya iwe vigumu kutoa utabiri sahihi katika maeneo husika,” Boubacar Moumouni Kaougé, mtabiri wa hali ya hewa katika idara ya kitaifa ya hali ya hewa ya Niger, alisema katika mazungumzo ya simu.
Kaougé alisema kuwa, mbali na kufanya utabiri kuwa mgumu, mabadiliko hayo ya hali ya hewa yanaweza kutatiza utoaji wa msaada unaohitajika na watu walioathiriwa. Wakati huohuo, watu wengine wanahama makaazi yao kwa sababu ya ukosefu wa usalama, na vikwazo vya usafiri vinaweza kukwamisha utekelezaji wa sera za kukabiliana na hali hiyo.
“Mchanganyiko huu unaweza kuongeza hatari ya kuadhirika kwa jamii ambazo tayari zinakabiliwa na athari za matukio hatari ya hali ya hewa,” Kaougé alisema.
Picha ya bango: Huu ni ukame mbaya zaidi uliosababishwa na El Niño nchini Ethiopia katika miaka 50. Picha na EU Civil Protection kupitia Flickr (CC BY-NC-ND 2.0).
Citation :
Booghs, S. (2023). Les changements climatiques comme enjeu de sécurité : Le Sahel, une région vulnérable. FLUX: International Relations Review, 14(1). https://doi.org/10.26443/firr.v14i1.149
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kifaransa mnamo tarehe 26/10/2026.