- Food Banking Kenya imeokoa tani milioni 1.1 za chakula na kusaidia watu 580,000, huku ikilenga kufikia wanufaika 700,000 kufikia mwisho wa 2026.
- Shule Maalumu ya Waithaka imeongeza kiasi cha mboga kinachopikwa kila siku kutoka kilo 15 hadi kilo 80 kutokana na msaada wa benki ya chakula.
- Upotevu na uharibifu wa chakula huchangia asilimia 8–10 ya uzalishaji wa gesi chafu duniani, huku kupunguza upotevu huo kukisaidia pia kulinda bioanuwai na makazi ya wanyamapori.
NAIROBI, Kenya — Shule Maalumu ya Waithaka jijini Nairobi imekuwa ikipokea mboga ambayo imesaidia kuboresha milo ya wanafunzi wapatao 200 wenye ulemavu. Hali katika shule hiyo inaonyesha kinzani kubwa nchini Kenya: chakula chenye lishe kinapotea au kutupwa, hata wakati watu walio katika mazingira magumu wanashindwa kukipata.
Shule hiyo ni miongoni mwa mamia ya taasisi zinazonufaika na mpango wa Food Banking Kenya, shirika lisilo la faida ambalo huokoa chakula cha ziada kutoka mashambani, masokoni na kwa wauzaji wa rejareja, kisha kukigawanya kwa wanaohitaji. Mfumo huu unasaidia kupunguza njaa na athari za upotevu na uharibifu wa chakula kwa tabianchi na bioanuwai.

Shule Maalumu ya Waithaka, iliyoko Dagoreti jijini Nairobi, ni mojawapo ya taasisi chache za elimu zinazotoa elimu ya msingi na mafunzo kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kiakili na wa ukuaji.
Wanafunzi wengi kati ya takriban 200 wanaosoma katika shule hiyo, wana tawahudi, ugonjwa wa kupooza kwa ubongo (cerebral palsy), au tatizo la upungufu wa umakini na shughuli nyingi (ADHD). Wanahitaji huduma maalumu, ambazo kwa kawaida hazipatikani katika shule za kawaida.
Hata hivyo, kuwalisha kwa lishe bora na kwa njia endelevu kumefanya kazi ya shule hiyo kuwa ngumu zaidi, kutokana na msaada mdogo wa kifedha na matatizo ya ulaji yanayohusiana na ulemavu wanaokabili wanafunzi hao.
UNICEF inasema watoto wenye ulemavu wana uwezekano wa kukabiliwa na utapiamlo ulio mara tatu zaidi, na uwezekano wa kudumaa, kukonda au kufariki kutokana na matatizo ya kiafya yanayohusiana na lishe ulio mara mbili zaidi, ikilinganishwa na watoto wasio na ulemavu.
“Tunapokea wastani wa shilingi milioni 1 za Kenya ($7,708) kwa mwaka kutoka serikalini, na sehemu kubwa ya fedha hizo hutumika kuwalipa wafanyakazi wasaidizi. Serikali pia huajiri na kulipa walimu wa mahitaji maalumu. Kwa chakula, tunategemea ada za bweni zinazolipwa na wazazi na shirika la hisani linalosaidia wanafunzi 25.
“Mpango wa chakula unaofanywa na serikali ya Kaunti ya Nairobi pia hutoa chakula cha mchana mara moja kwa wiki. Wanafunzi wengi wanatoka katika familia maskini,” anasema Jane Kang’ethe, mkuu wa Shule Maalumu ya Waithaka.
Kwa kuwa shule hiyo ina bajeti ndogo, milo ya kawaida hujumuisha ugali au wali pamoja na maharagwe au dengu, na wakati mwingine kabichi. Shule hiyo ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Milo hiyo inayotegemea zaidi vyakula vya wanga inaweza kukosa baadhi ya virutubisho muhimu iwapo haitajumuisha vyanzo vya kutosha vya protini, vitamini na madini.
Hali hiyo imeboreshwa kwa kiasi kikubwa katika miaka miwili iliyopita baada ya shule hiyo kujiandikisha kupata ugavi wa mboga mboga na matunda kutoka kwa mpango wa Food Banking Kenya (FBK), shirika la ndani lisilo la faida linalofanya kazi kupambana na njaa na kupunguza upotevu na uharibifu wa chakula.
“FBK hutuletea mboga, zikiwemo maharagwe ya Kifaransa, brokoli na maboga madogo aina ya courgette, mara moja kila baada ya wiki mbili. Tangu tulipoanza kupokea mboga hizo, kiasi cha mboga tunachopika na kuwapa wanafunzi kimeongezeka kutoka kilo 15 hadi kilo 80 kwa siku,” anasema Kang’ethe.
Utafiti kuhusu lishe na ADHD ulichunguza uhusiano kati ya ulaji wa matunda, mboga, samaki, na vyakula vyenye asidi nyingi ya mafuta yasiyoshiba, pamoja na virutubisho kama vile magnesiamu na zinki, na hatari ya ADHD.
John Gathungu, mwanzilishi na mkurugenzi mtendaji wa FBK, anasema mara kwa mara FBK hupokea marejesho chanya kutoka kwa makundi mengine yanayonufaika na mpango huo. Kati ya makundi 250 yalio kwenye orodha ya wanufaika wa FBK, 150 ni shule na nyumba za watoto.

Gathungu anasema mafanikio ya mpango huo, ingawa bado ni ya kiwango fulani, yanamsogeza karibu na kutimiza ndoto yake ya mda mrefu.
“Nilizaliwa na kukulia Aberdares, moja ya maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa kilimo nchini Kenya. Nilikua nikiona mboga nyingi, kwa mfano, zikipotea na wakati mwingine zikiliwa na ng’ombe kwa sababu ya uzalishaji kupita kiasi na ukosefu wa soko.
“Baadaye, nilipokuja chuoni Nairobi, nilikuwa nikibeba baadhi ya mazao hayo na kuwapa marafiki ambao hawakuwa na uwezo wa kununua chakula. Hapo ndipo nilipopata shauku ya kupambana na njaa. Nilitamani kuwa chakula kisipotezwe wakati watu wanakabiliwa na tatizo la njaa. Niliiona benki ya chakula kama suluhisho la vitendo kwa tatizo la njaa,” anasema Gathungu.
Takriban asilimia 30 hadi 40 ya chakula kinachozalishwa nchini Kenya hupotea au kuharibika kila mwaka kabla halijafika kwa walaji. Wakati huohuo, takriban watu milioni 15, sawa na asilimia 28 ya wakazi wa nchi hiyo, wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula.
Ripoti ya Taasisi ya Rasilimali Duniani (WRI) ilikadiria kwamba Kenya ingeweza kulisha zaidi ya watu milioni saba kwa mwaka kwa kupunguza upotevu na uharibifu wa chakula kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030. Hatua hiyo pia ingeweza kuzuia uzalishaji wa zaidi ya tani milioni saba za gesi chafu, hivyo kusaidia kufikia malengo ya tabianchi ya Kenya na kupunguza shinikizo kwa bioanuai.
FBK inachangia kukabiliana na changamoto tatu zinazohusiana: utapiamlo, mabadiliko ya tabianchi na upotevu wa bioanuwai.
FBK hukusanya chakula cha ziada ambacho bado ni salama na kina lishe kutoka mashambani, kwa wauzaji wa jumla na rejareja, katika viwanda vya kufungasha mazao kwa ajili ya kuuza nje, na katika masoko ya mazao. Badala ya chakula hicho kutupwa, shirika hukisambaza kwa watu na taasisi zinazokihitaji.
Chakula kilichookolewa husambazwa kwa shule, vituo vya kulelea watoto, vituo vya kutoa hifadhi na mashirika yanayohudumia watu walio katika mazingira magumu.
FBK hutumia mfumo wa kidijitali kuunganisha wafadhili wa chakula na taasisi zinazopokea kwa wakati halisi. Mfumo huo huboresha uratibu na kusaidia kupunguza muda wa kuhifadhi chakula na safari zisizo za lazima.

Uzito wa chakula kilichookolewa huingizwa kwenye programu, ambayo hukadiria idadi ya milo iliyotolewa na kiwango cha uzalishaji wa gesi chafu.
Uhifadhi wa chakula kisichosambazwa
Chakula kisichoweza kusambazwa mara moja huhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia chakula kwa ubaridi cha FBK huko Ruaka, takriban kilomita 15 kaskazini-magharibi mwa Nairobi. Chakula kingine huhifadhiwa kwenye makontena katika vituo vya ukusanyaji au kwenye maghala ambayo shirika huendesha katika maeneo ya vijijini.
Chini ya makubaliano ya hivi karibuni na kampuni ya Glovo, inayosafirisha chakula, chakula kutoka kwa maagizo yaliyofutwa huelekezwa kwa jamii zilizo katika mazingira magumu kupitia mtandao wa FBK.
“Madereva wa Glovo wanatakiwa kupeleka chakula kwenye vituo vyetu vidogo vya ukusanyaji ndani ya dakika 30 baada ya agizo kufutwa. Kabla ya ushirikiano huu, chakula hicho kingehifadhiwa kwa muda mrefu, wakati mwingine siku nzima, hadi kikaharibika. Tuna vituo vitano vya aina hiyo jijini Nairobi ambako chakula hicho kinaweza kupelekwa,” anasema Gathungu.
Ushirikiano na Glovo pia umewezesha vituo vya FBK katika miji mbalimbali ya Kenya kupata milo yenye protini nyingi kutoka kwa mikahawa iliyo kwenye mtandao wa kampuni hiyo.
Esther Mwathi, meneja wa Wings of Compassion Rescue Centre, iliyoko Roysambu jijini Nairobi, anasema watoto wanaohudumiwa na kituo hicho walikula kuku kwa mara ya kwanza mwezi Septemba 2026, baada ya kukosa mlo huo kwa miezi tisa kufuatia kampuni kubwa ya ndani inayofuga kuku kusitisha michango yake Januari 2026.
Kituo hicho, ambacho hutoa hifadhi salama kwa akina mama vijana walionusurika katika ubakaji na watoto wao, kilijiunga na mpango wa benki ya chakula wa FBK mwezi Agosti 2026.
Dk. Wanjiru Kamau-Rutenberg, mkurugenzi mtendaji wa kanda ya Afrika katika Alliance of Bioversity International and CIAT, anasema benki za chakula zinaweza kusaidia kujenga mifumo endelevu na ya jumuishi ya chakula.

“Benki za chakula huhakikisha kwamba chakula cha ziada kilicho salama na chenye lishe kinawafikia watu wanaokihitaji, hasa walio katika mazingira magumu, huku zikipunguza upotevu na uharibifu wa chakula. Mbinu hii pia huchangia uendelevu wa mazingira na kuimarisha usalama wa chakula na lishe,” anasema Dk. Kamau-Rutenberg, ambaye ametambuliwa na kutuzwa kama mmoja wa Waanzilishi Bora wa Kilimo-chakula wa 2026 na World Food Prize Foundation.
Alliance of Bioversity and CIAT na FBK wanafanya utafiti wa pamoja ili kutathmini ubora wa lishe wa milo inayookolewa na kusambazwa kupitia mpango wa benki ya chakula.
The Global FoodBanking Network (GFN), mtandao unaojumuisha mashirika ya benki ya chakula kutoka zaidi ya nchi 50 kama wanachama wake, inasema benki za chakula ni muhimu kwa juhudi za kimataifa za kupunguza njaa na kupunguza upotevu na uharibifu wa chakula kwa nusu ifikapo 2030.
Takwimu zilizotolewa na GFN mwezi Julai 2026 zinaonyesha kwamba mwaka 2025, benki wanachama za chakula zilihudumia takriban watu milioni 40.5 waliokuwa wakikabiliwa na njaa katika nchi 47 — ongezeko la watu milioni 2.5 ikilinganishwa na 2024.
Ongezeko hilo linaonyesha kuwa mahitaji yanaedelea kuongezeka, huku jamii zikikabiliwa na misukosuko katika mifumo ya chakula na kupunguzwa kwa ghafla kwa msaada rasmi wa maendeleo.
Ripoti ya GFN inasema kuwa mwaka 2025, benki za chakula ziliokoa takriban tani 534,000 za chakula ambazo zingepotea, na hivyo kuzuia uzalishaji wa takriban tani milioni mbili za gesi chafu.
Upotevu na uharibifu wa chakula huchangia asilimia 8 hadi 10 ya uzalishaji wa gesi chafu duniani. Wasiwasi mkubwa unatokana pia na methane, inayozalishwa chakula kinapooza kwenye madampo. Methane ina uwezo wa kuchangia ongezeko la joto duniani ulio takriban mara 80 hadi 84 zaidi ya ule wa dioksidi kaboni katika kipindi cha miaka 20.
Katika maandalizi ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi wa COP31, utakaofanyika Antalya, Uturuki, kuanzia Novemba 9 hadi 20, 2026, GFN imejiunga na muungano wa mashirika ya kimataifa unaoutaka urais wa COP31 na Mwakilishi Mkuu wa Tabianchi kuchukua hatua za kuharakisha utekelezaji wa lengo la kupunguza taka za chakula duniani kwa nusu ifikapo mwaka 2030.
“Kupunguza taka za chakula ni moja ya njia bora na za ufanisi zaidi za kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kuboresha usalama wa chakula, jambo ambalo limetambuliwa na Urais wa COP31 na Mwakilishi Mkuu wa Tabianchi,” alisema Lisa Moon, Mkurugenzi Mtendaji wa GFN.
“Tukifanya kazi na benki zetu za chakula washirika katika nchi zaidi ya 50, GFN inakusanya na kugawanya chakula cha ziada kwa watu mamilioni, huku ikipunguza uzalishaji wa methane. Tunawasihi viongozi wa kimataifa kutafsiri maono yao kuwa vitendo, kutenga rasilimali na zinazohitajika na kuharakisha hatua zitakazojenga mustakabali wenye afya bora kwa watu na sayari,” alisema katika taarifa ya pamoja.
Upotevu wa chakula pia unahusishwa na uharibifu wa makazi ya mimea na wanyama unaosababishwa na upanuzi wa kilimo, ikiwemo ukataji miti, kilimo cha zao moja na ukaushaji wa maeneo oevu ili kupata ardhi zaidi ya kilimo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) linakadiri kuwa hekta bilioni 1.4 za ardhi ya kilimo duniani, sawa na takriban asilimia 28 ya ardhi hiyo, hutumika kuzalisha chakula ambacho hatimaye hupotea au kuharibika. FAO pia inakadiria kuwa upanuzi wa kilimo unasababisha sehemu kubwa ya ukataji miti.
Dk. Sylvia Nyawira, mtafiti anayejikita katika kaboni ya udongo na uzalishaji wa gesi chafu katika Alliance of Bioversity International and CIAT, anasema kupunguza upotevu na uharibifu wa chakula ni mkakati muhimu wa uhifadhi wa bioanuwai kwa sababu unapunguza shinikizo kwa mifumo ikolojia ya asili.


“Kwa kupunguza upotevu huu, tunaweza kutumia vizuri zaidi ardhi ya kilimo iliyopo na kupunguza haja ya kupanua shughuli za kilimo katika makazi ya asili. Hilo litasaidia kulinda spishi za mimea na wanyama zinazotegemea mifumo hiyo ya ikolojia. Kwa njia hii, kupunguza upotevu na uharibifu wa chakula si tu kuhusu kuboresha usalama wa chakula; ni pia fursa muhimu ya uhifadhi wa bioanuwai,” Dk. Nyawira aliambia Mongabay kwa simu.
“Kupunguza upotevu na uharibifu wa chakula pia kunaweza kusaidia kuhifadhi bioanuwai kwa kupunguza uchafuzi wa mito na maziwa yetu. Kwa mfano, utafiti mmoja ulikadiria kuwa takriban asilimia 46 ya taka katika dampo la Dandora, jijini Nairobi, zilikuwa mabaki ya chakula. Usimamizi duni wa taka hizo huchangia uchafuzi wa mazingira yanayolizunguka dampo hilo, ikiwemo Mto Nairobi,” aliongeza.
Gathungu anasema mwaka 2025 ulikuwa mwaka wenye mafanikio makubwa kwa FBK, ambayo ilirekodi kiwango chake cha juu zaidi cha chakula kilichookolewa na kuwafikia takriban watu 580,000 nchini Kenya. Kulingana na makadirio yaliyotumia fomula ya Wakala wa Ulinzi wa Mazingira wa Marekani (EPA), hatua hiyo ilizuia uzalishaji wa takriban tani 41,000 za methane ambao ungetokea iwapo chakula hicho kingetupwa kwenye dampo.
FBK inalenga kuokoa tani milioni 1.5 za chakula na kuongeza idadi ya watu wanaofikiwa kupitia benki zake za chakula hadi angalau 700,000 kufikia mwisho wa mwaka 2026.

Hata hivyo, FBK inapopanua mtandao wake wa benki za chakula nchini Kenya, ina wasiwasi kuwa uwezo wake wa kusafirisha na kusambaza chakula huenda usitosheleze mahitaji yanayoongezeka, na hivyo kudhoofisha uwezo wake wa kuokoa chakula zaidi cha ziada na kukielekeza kwa wahitaji.
“Ikiwa tunataka kuokoa chakula zaidi na kukisambaza kwa wanufaika wengi zaidi, tunahitaji ufadhili wa kutosha kwa shughuli za usafirishaji. Pia stunakabiliwa na changamoto ya fedha. Ingawa tunapokea chakula bila malipo, bado tunahitaji kulipia gharama za uhifadhi, usalama wa chakula, teknolojia na usambazaji,” Gathungu aliiambia Mongabay.
Picha ya bango: Mfanyakazi wa Benki ya Chakula Kenya akiandaa chakula kitakachosambazwa kwa shule na taasisi nyingine. Picha kwa hisani ya Food Banking Kenya.
Teknolojia inayolenga kubadilisha usimamizi wa taka Kenya, huku ikiibua maswali kuhusu ajira