- Wauzaji wa nyama ya nyati wamejiimarisha kupitia mitandao ya uhalifu iliyojipanga
- Mnyororo wa uuzaji wa nyama ya nyati, huimarishwa na mapungufu katika ufuatiliaji wa nyama inayouzwa.
- Kupungua kwa nyati kunaathiri mfumo wa ikolojia na kuhatarisha bioanuai.
- Ikiwa wanyamapori watatunzwa ipasavyo, wanaweza kuchangia uchumi wa nchi.
BUJUMBURA, Burundi – Katika lango la kuingia katika Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu, baadhi ya dalili zinadhihirisha ukweli mgumu ambao ni vigumu kupuuza. Picha za mabaki ya mizoga ya nyati zimewekwa wazi katika eneo la ofisi ya hifadhi, huku wawindaji haramu wanaohusika na kuwaua wanyama hao wakiwa bado hawajatambuliwa wala kukamatwa. Nyuma ya kila mzoga imejificha picha kubwa zaidi: biashara haramu ambayo haiishii tu eneo ambalo mnyama huuawa, bali imejiimarisha kupitia mitandao ya uhalifu inayozidi kujipanga kila kukicha.
Ujangili wa nyati katika Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu nchini Burundi, ni changamoto ambayo imeota mizizi. Mongabay kwenye moja ya makala zake, iliwahi kueleza namna biashara ya nyama ya nyati Burundi inavyochangia kutoweka kwa nyati nchini humo.
Kwa mujibu wa tathmini ya Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu iliyofanyika Septemba mwaka 2010, idadi ya nyati ilikadiriwa kupungua kutoka takribani 2,000 mwaka 2000 hadi kufikia mamia kadhaa mwaka 2010. Hata hivyo, tathmini hiyo ilibainisha kuwa hakukuwa na sensa mpya ya kuthibitisha idadi ya wanyama waliobaki.

Tishio hilo liliendelea hata baada ya miaka iliyofuata. Mnamo Novemba mwaka 2017, shirika la habari la Anadolu, lilimnukuu Evariste Buvyiruke, afisa aliyekuwa anasimamia ulinzi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu, akisema kuwa takribani nyati 30 walikuwa wameuawa tangu mwaka 2015.
Hali halisi ya ujangili
Niyonzima Adélaïde, kutoka mji wa Mishika, wilaya ya Kigamba katika mkoa wa Cankuzo, anasema nyati wanaouawa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu, siyo kwa ajili ya kulisha watu wanaoishi karibu na hifadhi hiyo pekee.
“Kuna mtandao mkubwa unaodaiwa kupanga biashara ya nyama ya nyati katika mikoa kadhaa ya mpakani, hususani Cankuzo, Karusi na huenda hadi maeneo ya Muyinga, mpakani mwa Tanzania,” anasema Adélaïde.
Athanasie Mpawenimana ambaye ni mlinzi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu, anasema mtandao huo uko imara na unatumia mbinu mbalimbali kufanikisha malengo yake.
Kwa mujibu wa Adélaïde, hali ya ujangili inaendelea kupanuka kadri miaka inavyopita. Anasema kuanzia mwaka 2008, ujangili huko Cankuzo ulianza kupungua, hasa baada ya mamlaka kuchukua hatua dhidi ya baadhi ya mbinu za uwindaji.
Hata hivyo, anasema kuanzia mwaka 2015, hali ilianza kubadilika. Mitandao iliyokuwa imejipanga, ilianza kujitokeza tena na kujiimarisha katika biashara ya nyama ya nyati.
“Wakati mwingine, hali hiyo ilifikia kiwango cha walinzi wanaolinda hifadhi kufanyiwa vurugu na kujeruhiwa wakati wa operesheni za kupambana na ujangili,” anasema Adélaïde.
“Miezi mitatu iliyopita, walinzi wa wanyamapori waliokuwa doria walikutana na kundi la wawindaji haramu waliokuwa na mapanga na marungu. Mmoja wa wenzetu alijeruhiwa kichwani na akapelekwa hospitalini,’’ anasema Mpawenimana.
Anaongeza kuwa wawindaji hao wana mbwa waliofunzwa vizuri, ambao huwasaidia wakati wa uwindaji. “Mwenzetu mmoja aliumwa na mbwa. Hilo lilimfanya aache kazi yake,” anasema.
Safari ya nyati
Inakuwaje wanyama wanauawa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu? Nyama yao hutokaje katika eneo hilo? Nani huichukua? na je, mamlaka za eneo hilo zinafahamu kinachoendelea ? Hayo ni baadhi ya maswali ya msingi yanayoibuka kuhusu mtandao wa uwindaji na usafirishaji wa nyama ya nyati kutoka ndani ya hifadhi hiyo.

Mongabay ilifanya uchunguzi wa kina kufuatilia safari ya nyati kuanzia hatua ya kwanza wanyama hao wanapofuatiliwa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu hadi nyama yao inapofikishwa sokoni kwa mnunuzi wa mwisho.
Ziara kwenye gereza
Katika uchunguzi wake, Mongabay ilipiga hodi kwenye gereza la Cankuzo, ambako mmoja wa watu wanaokabiliwa na kesi inayohusiana na ujangili wa nyati, anashiliwa. Kutokana na sababu za kiusalama na maadili, katika makala hii jina litakalotumika ni Maxwell Minani ambalo si jina lake halisi.
Ifuatayo ni simulizi ya Minani kuhusu biashara hiyo haramu na mtandao unaotumika kuifanikisha.
Mnyororo wa mtandao
Minani anaanza kwa kuelezea mnyororo unaounganisha makundi mbalimbali ya watu, huku kila kundi likiwa na jukumu lake.
Kuna wawindaji haramu ambao kazi yao ni kuwafuatilia wanyama, kuweka mitego na kuwaua. Wapo wachuuzi ambao husafirisha nyama hiyo kutoka kituo cha kwanza hadi kwa wasafirishaji. Wapo pia wanunuzi ambao wamegawanyika katika makundi mawili; wale wanaonunua nyama katika kituo cha kwanza na kuisafirisha hadi kwa wanunuzi wakubwa na wanunuzi wakubwa ambao husafirishiwa nyama hiyo moja kwa moja, anasema.
Katika mnyororo huo, kila kundi lazima liwe makini kwani uzembe wa kundi moja unaweza kusababisha wakamatwe ama kukwamisha biashara.
Uwindaji na mauaji ya nyati
Uwindaji hauanzii wakati nyati anaposhambuliwa au wakati mitego inapowekwa. Kazi huanza mapema kwa kuwafuatilia nyati ili kubaini mienendo yao, hasa namna wanavyosogea kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Hatua inayofuata ni kuchagua wakati unaofaa kufanya mashambulizi. Hatua ya mwisho ni kufuatilia kwa karibu mienendo ya walinzi katika hifadhi ili kubaini namna wanavyozunguka katika kila eneo, anasimulia Minani.
“Kwa sababu walinzi ni wachache, tunawafuatilia. Wakimaliza kukagua eneo fulani, sisi huhamia katika eneo lililokaguliwa kwa sababu walinzi huendelea kukagua maeneo mengine na huchukua muda mrefu kabla hawajarudi eneo la kwanza. Tukiingia tu hifadhini, haraka haraka tunatayarisha eneo la kuweka mitego yetu,” anasema.
Anasema msimu wa mvua unatoa mazingira muafaka kwa wawindaji haramu, kwa kuwa nyasi ndefu huwasaidia kujificha kwa urahisi zaidi.
“Mitego inaponasa kumuua mnyama , muda huwa adui mkubwa kwetu. Mzoga lazima ukatwe haraka. Nyama igawanywe na kuondolewa kabla walinzi hawajagundua dalili za watu kupita katika eneo hilo,” anasema.
Kumuua nyati ni mwanzo tu
Kwa watu wanaohusika katika biashara hii, kumuua nyati si mwisho, bali ni mwanzo tu. Kuificha nyama, kuisafirisha na kuifikisha kwa wateja wanaoisubiri, ni kibarua kingine, anasema.
“Mara tu nyati anapouawa, kinachohitajika ni kuficha haraka dalili za uwindaji haramu na kuhakikisha nyama inawafikia wale wanaoisubiri bila wahusika kukamatwa,” anasema.
Kwa mujibu wa Minani, wanunuzi si lazima wawe mbali sana na hifadhi. Baadhi ya vituo vya kukusanyia nyama vingine viko maeneo ya jirani. Kabla ya nyama hiyo kusafirishwa kwa njia za siri kuelekea maeneo mengine ya kuuzia, huwekwa kwenye vituo hivyo.
“Kwa nyati, safari yake huishia msituni. Lakini kwa wale wanaofanya biashara ya nyama yake, kwenye vituo vya karibu ndipo hadithi nyingine huanzia: hadithi ya bidhaa ambayo thamani yake sasa hupimwa kwa pesa. Kadri nyama hiyo inavyozidi kusafirishwa kwenda mbali na eneo la Ruvubu, ndivyo thamani yake inavyozidi kuongeza,” anaeleza Minani.
Uchunguzi wa Mongabay unaonyesha pia kwamba nyama hiyo baada ya kuchukuliwa na watu wa kati walio karibu na hifadhi, husafirishwa kwa siri kuelekea maeneo ya kuuzia nyama huko Cankuzo na katika maeneo mengine ya Muyinga na wakati mwingine hutumia njia za biashara zinazovuka mpaka kuelekea nchi jirani.
Maisha ya pili ya nyati
Kutoka Cankuzo hadi Muyinga na Kirundo mtandao huo huvuka mikoa kadhaa kusafirisha nyama. Muyinga inapakana na Tanzania wakati Kirundo ikipakana na Rwanda.
Mnyororo huo wa uuzaji wa nyama ya nyati, hupata nguvu kutokana na mapungufu katika ufuatiliaji wa nyama inayouzwa. Nchini Burundi, kuna mapungufu makubwa katika mfumo mzima wa udhibiti wa nyama, ambapo bidhaa hiyo inaweza kusafirishwa na kuuzwa bila kukaguliwa.
Usafirishaji haramu wa nyama ya nyati pia unakuwa rahisi pale wafanyabiashara wanapotumia njia zisizo rasmi za biashara.
“Mara nyama ya nyati inapokatwa vipande na kuchanganywa na vipande vingine vya nyama, inakuwa vigumu zaidi kutambua asili yake kwa kuangalia tu. Kwa mlaji, inaweza kuwa vigumu kabisa kujua ikiwa nyama anayoinunua imetokana na mnyama wa kufugwa aliyechinjwa kihalali au nyati aliyeuawa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu,” anasema Minani.

Mafuvu ya nyati yaliyowekwa kwenye lango la ofisi za Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu, zilizoko Cankuzo, katika wilaya ya Kigamba. Kwa mujibu wa Mhifadhi wa wanyamapori katika hifadhi hiyo, Athanasie Mpawenimana, baadhi ya mafuvu hayo ni ya hivi karibuni, jambo linaloashiria kuwa ujangili bado unaendelea ndani ya hifadhi hiyo. Picha na Lionel Mugisha.
Kufuatia ushuhuda wa Minani, Mongabay ilitaka kufahamu mamlaka zinachukua hatua gani ili kudhibiti uhalifu huo.
Mamlaka zinafanya nini?
Marc Bakundintwari, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu, alikiri kuwepo kwa mtandao huo wa ujangili. Hata hivyo alisema upungufu wa vifaa na wafanyakazi unafanya juhudi za Serikali na wadau wengine kukabiliana na makundi hayo kuwa ngumu.
Makundi hayo yanatumia mbwa na vifaa ambavyo wakati mwingine vina uwezo mkubwa wa kuwadhuru walinzi kuliko vifaa wanavyotumia wao.
Katika kukabiliana na hali hiyo, uongozi wa hifadhi umekuwa ukifanya uhamasishaji na kuwashirikisha wanajamii wanaoishi pembezoni mwa hifadhi katika juhudi za uhifadhi.
“Tunawaelimisha wakazi wa maeneo yanayozunguka hifadhi kuhusu wajibu wao wa kushiriki katika kulinda na kuhifadhi mfumo wa ikolojia wa hifadhi,” anaeleza Bakundintwari.
Licha ya jitihada zinazofanywa na mamlaka za kupambana na ujangili na kulinda wanyamapori, mauaji ya nyati bado yanaendelea katika maeneo mbalimbali. Zifuatazo ni miongoni mwa sababu zilizotajwa kuchangia kuendelea kwa vitendo hivyo.
Udhaifu katika ulinzi
Kwa mujibu wa Bakundintwari, idadi ya walinzi katika Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu ni ndogo ukilinganisha na ukubwa wa hifadhi hiyo ambao ni zaidi ya hekta 50,000.
“Licha ya idadi ndogo ya walinzi, lakini pia kuna changamoto ya raslimali hasa vitendea kazi na vyombo vya usafiri. Changamoto hizi zinatoa mwanya kwa mitandao ya ujangili kufanya shughuli zao,” anasema Bakundintwari.
Anafafanua kuwa kwenye karatasi, Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu ni eneo salama lililolindwa. Lakini katika uhalisia, ni eneo kubwa
“Udhibiti huu dhaifu wa kijiografia umewezesha kuibuka kwa mitandao ya uhalifu inayozidi kujipanga,” anasema Bakundintwari.
Mkoa wa Cankuzo una nafasi ya kipekee katika kufanikisha biashara hiyo na kuongeza changamoto katika kuidhibiti. “Kwa muda mrefu, eneo hili limekuwa na uhusiano wa kibiashara na nchi jirani. Ukaribu wake na mpaka unawezesha usafirishaji wa watu na bidhaa kwa urahisi zaidi,” anasema Bakundintwari.
Mtandao imara wa ujangili
Biashara ya nyama ya nyati inadaiwa kuwa inafanywa na makundi ya watu ambayo yamejiimarisha na yanatumia mbinu za kisasa. Mnamo Machi 2026, chombo cha habari cha Iwacu kilichapisha ushuhuda wa walinzi waliodai kuwepo kwa makundi yaliyopangwa ya wawindaji haramu, wakati mwingine yakiwa na watu kadhaa.
Kwa mujibu wa ushuhuda huo baadhi ya wawindaji haramu hufanya kazi katika makundi. Katika baadhi ya matukio ya uwindaji, makundi yenye watu kati ya 20 na 30 yalidaiwa kuonekana.
“Aina hii ya mpangilio inabadilisha kabisa ukubwa wa tatizo. Wakati kundi linaweza kufuatilia mienendo ya wanyama, kumuua nyati, kukata mzoga na kusafirisha nyama, uwindaji hauwi tena shughuli ya mtu mmoja mmoja, bali operesheni ya pamoja,” ilisema taarifa ya Iwacu.
Walinzi wa wanyamapori waliohojiwa na Uwacu walieleza pia matukio ambayo wawindaji haramu walidaiwa kufanya ikiwa ni pamoja na kwenda kumchukua mwenzao baada ya kukamatwa. Walinzi walidai kuwa walikabiliana na kundi kubwa lakini wakashindwa nguvu na likafanikiwa kumchukua mwindaji haramu pamoja na nyama iliyokuwa imekamatwa.
Athari za mauaji ya nyati kwa uhifadhi
Mauaji ya nyati kwa njia ya ujangili nchini Burundi yana athari hasi kwa uhifadhi wa wanyamapori, hasa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu, ambayo ni eneo muhimu la hifadhi ya savana na mojawapo ya maeneo makubwa yaliyohifadhiwa nchini humo. Taarifa za UNESCO zinaeleza kuwa hifadhi hiyo ina makazi mbalimbali ya wanyamapori, yakiwamo savana, misitu na maeneo oevu, huku nyati wakiwa miongoni mwa mamalia wakubwa wanaopatikana humo
Kitabu kinachojulikana kama Ecology and Management of the African Buffalo kinaeleza kuwa ongezeko la mahitaji ya nyama ya wanyamapori, pamoja na upotevu wa makazi na uwindaji usiodhibitiwa, vimechangia kupungua kwa idadi ya nyati katika maeneo mbalimbali ya Afrika.
Kwa mujibu wa kitabu hicho , katika baadhi ya maeneo vifo vya nyati vilizidi kiwango cha kuzaliwa na kuwalazimisha kubaki katika maeneo machache yenye ulinzi. Kwa muktadha wa Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu nchini Burundi, hali hii inaibua umuhimu wa kudhibiti ujangili na kufuatilia mnyororo wa biashara ya nyama ili kuzuia kupungua zaidi kwa idadi ya nyati.
Kitabu hicho kinaeleza kuwa nyati ni sehemu muhimu ya mifumo ya ikolojia ya Afrika na kwamba ujangili na upotevu wa makazi ni miongoni mwa vitisho vinavyohatarisha uhai wao.
Kupungua kwao kunaweza pia kuathiri uwiano wa mfumo wa ikolojia na kuhatarisha uendelevu wa bayoanuai katika eneo hilo, inasema sehemu ya kitabu hicho.
Suala hili lina umuhimu mkubwa hasa nchini Burundi, ambako, kwa mujibu wa Jukwaa la Kitaifa la Bioanuwai la Burundi, Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu ni kimbilio la baadhi ya spishi ambazo zimetoweka katika maeneo mengine ya nchi. Hivyo, mauaji ya mara kwa mara yanatishia si tu uhai wa nyati, bali pia uhifadhi wa sehemu ya urithi wa asili wa nchi.

Nini kifanyike
Bakundintwari anapendekeza kuongeza idadi ya wafanyakazi na bajeti, kutoa vifaa vinavyofaa, pamoja na kuimarisha ushiriki wa mamlaka za kiutawala na mahakama.
Hata hivyo, mapendekezo mengine yanakwenda zaidi ya ulinzi na ufuatiliaji wa hifadhi pekee.
Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) linapendekeza kuchukua hatua katika mnyororo mzima wa biashara haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyamapori. Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha utekelezaji wa sheria, kudhibiti njia zinazotumika kusafirisha bidhaa hizo kwa njia haramu na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wadau.
WFP pia inasisitizwa kuwa mapambano dhidi ya ujangili hayapaswi kulenga wawindaji haramu pekee, bali pia yawabaini na kuwachukulia hatua wale wanaoratibu usafirishaji na uuzaji wa bidhaa hizo.
Hatua nyingine ni kuzishirikisha jamii zinazoishi pembezoni mwa hifadhi katika juhudi za uhifadhi. Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Asili (UICN) unapendekeza kutafuta na kuandaa suluhisho kwa kushirikiana na jamii husika, hasa katika maeneo yenye upungufu wa walinzi wanyamapori.
Kulingana na mazingira ya eneo husika, hatua hizo zinaweza kujumuisha kufuatilia mashamba ili kuzuia uharibifu unaosababishwa na wanyamapori, kuweka mifumo ya kutoa tahadhari mapema na kuanzisha utaratibu wa kufidia hasara zinazotokana na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Kulingana na mazingira ya eneo husika, hatua hizo zinaweza kujumuisha kufuatilia mashamba ili kuzuia uharibifu unaosababishwa na wanyamapori, kuweka mifumo ya kutoa tahadhari mapema na kuanzisha utaratibu wa kufidia hasara zinazotokana na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
“Iwapo mitandao hii ya kusafirisha na kuuza nyama haitavunjwa kuanzia kwenye chanzo chake, ujangili utaendelea kugeuza utajiri wa asili wa Burundi kuwa bidhaa ya biashara ya magendo,” anasema Bakundintwari.
Kwa mtazamo wake, umefika wakati serikali ichukue hatua madhubuti za kulinda hifadhi hii na wanyama wake. Anaamini kwamba ikiwa rasilimali hizi za wanyamapori zitatunzwa na kuthaminiwa ipasavyo, zinaweza kuwa hazina yenye mchango kwa uchumi wa nchi.
Picha ya bango: Mhifadhi wa wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Ruvubu, Jerome Nduwayo, akionyesha fuvu la nyati wakati akielezea historia ya hifadhi hiyo. Picha na Lionel Mugisha.
Aliyekutwa na vipande vya nyama ya nyati afutiwa adhabu ya miaka 20 jela