- Mahakama Kuu yatupilia mbali rufani waliyokata kupinga kutiwa hatiani.
- Jaji asema upande wa Jamhuri walithibitisha mashitaka, bila kuacha shaka yenye msingi.
- Ushahidi uliwaunganisha washtakiwa na nyara hizo moja kwa moja.
- Hakuna madhara yaliyowapata washtakiwa kutokana na mabadiliko ya mahakimu.
DAR-ES-SALAAM, Tanzania – Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyoketi Morogoro, imetupilia mbali rufaa ya Aclay Mda na Ramadhani Pangala waliohukumiwa kwa kukutwa na vipande vitatu vya meno ya tembo chini ya kitanda, katika nyumba ya kulala wageni, huko Ruvuma baada ya kubaini mashtaka dhidi yao yalithibitishwa pasina kuacha shaka.
Hukumu hiyo ilitolewa mbele ya Jaji Stephen Magoiga baada ya kusikiliza rufani iliyowasilishwa kupinga hatia na adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela ama faini ya TSh217,600,000 ($82,346) iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro. Oktoba 7, 2025.

Warufani Aclay Mda na Ramadhani Pangala, ambao katika kesi hiyo walikuwa pamoja na washitakiwa wengine watatu ambao hawakukata rufaa, walishitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro kwa shtaka moja la kumiliki nyara za Serikali kinyume cha Sheria.
Washitakiwa hao walifunguliwa mashitaka chini ya kifungu cha 86(1), (2)(b) na (3) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, (Sura ya 283 Toleo la 2022) kama ilivyorekebishwa, kikisomwa pamoja na aya ya 14 ya Jedwali la Kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Udhibiti wa Uhalifu wa Kiuchumi na Uhalifu wa Kupangwa, (Sura ya 200 Toleo la 2022).
Ilidaiwa katika maelezo ya shitaka kwamba, Oktoba18, 2024 ndani ya Ruvuma Guest House, eneo la Uhindini katika wilaya ya Kilosa, mkoa wa Morogoro, waombaji hao wawili walikutwa wakiwa na nyara za Serikali, ambazo ni vipande vitatu vya meno ya tembo, vyenye thamani ya $40,000 (TSh108,800,000), mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Waombaji hao walikana shtaka lililokuwa linawakabili, hivyo upande wa mashtaka ulipewa jukumu la kuwasilisha ushahidi dhidi yao na wakati wa usikilizwajj upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 10.
Ushahidi upande wa mashtaka
Mashahidi 10 walioitwa ni shahidi wa kwanza (PW1), askari mwenye namba H340 CPL Justine kutoka Kituo cha Polisi Kilosa na mtunzaji wa vielelezo; PW2, Laurent Lubinsha, Afisa wa Wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na mtunzaji wa vielelezo; PW3, F.24987 A/Insp. Estoni Mwasinyanga, askari aliyewakamata washtakiwa; PW4, John Rashid Mtimbanjayo, afisa aliyefanya tathmini ya thamani ya nyara, PW5 Shida Hija Kiputiputi, mhudumu wa nyumba ya wageni na shahidi huru wa upekuzi na ukamataji.
Mashahidi wengine ni (PW6), Hosea Mgunda, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlimani Boma na shahidi huru wa upekuzi na ukamataji, PW7, G.7468 D/SGT Joram, mpelelezi wa polisi na aliyechora ramani ya eneo la tukio, PW8 Juma Raisi, mlinzi katika Ruvuma Guest House na shahidi wa upekuzi na ukamataji, PW9 Tiberius Kimbusu, afisa wa wanyamapori aliyekuwa akisaidia polisi katika doria na ukamataji pamoja na PW10, A/Insp. Pagekuwa, askari wa polisi aliyeshiriki kuwakamata washukiwa wengine katika kijiji cha Madizini.
Upande wa mashtaka pia uliwasilisha vielelezo 10 ikiwemo simu ya Tecno (P1), simu ya Itel (P2), kitabu cha rejesta cha Ruvuma Guest House (P3), meno matatu ya tembo pamoja na mfuko wa sulphate (P4), rejesta ya vielelezo ya mahakama (PF No.16) Na.1 ya mwaka 2024 (P5), daftari la vielelezo la Hifadhi ya Taifa ya Mikumi (P6), hati ya upekuzi (PF 91) na ramani ya eneo la tukio katika Tuhuma Guest House ya Oktoba 19, 2024 (P10).
Waombaji hao walikuwa miongoni mwa washtakiwa watano waliokuwa wamefikishwa mahakamani awali. Washtakiwa watatu baadaye waliachiliwa baada ya mahakama kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuwa umeonyesha kesi ya kujibu dhidi yao kwa mujibu wa sheria.
Ushahidi wa Jamhuri
Ilidaiwa kuwa Oktoba 18 mwaka 2024, watu watatu walidaiwa kufika Ruvuma Guest House na kukodi chumba kilichoitwa “Zambia” na kwamba Polisi na maafisa wa uhifadhi walipokea taarifa kutoka kwa mtoa taarifa na kwenda kufanya upekuzi wa chumba hicho, wakiongozana na mwenyekiti wa mtaa pamoja na mhudumu na mlinzi wa nyumba hiyo ya wageni.
Katika upekuzi huo, walidaiwa kukutwa na nyara za Serikali ambazo ni meno ya tembo yaliyokuwa yamefichwa ndani ya mifuko ya sulphate chini ya kitanda.

Aclay na Ramadhani walikamatwa eneo hilo. Washukiwa wengine watatu walikamatwa baadaye katika kijiji cha Madizini. Wote walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi namba 32336 ya mwaka 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
Utetezi wa warufani
Katika utetezi wao, warufani walikana shitaka na kutoa ushahidi wao wenyewe bila kuita mashahidi wengine. Walidai kwamba hawakukamatwa ndani ya chumba cha “Zambia” katika Ruvuma Guest House wala hawakuwa na meno ya tembo. Walidai walikamatwa sehemu tofauti, barabarani.
Ramadhani alisisitiza pia kwamba jina lake halikuonekana katika rejesta ya wageni ya Ruvuma Guest House (P3) na kwamba wao walisingiziwa na maofisa waliowakamata.
Hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Baada ya kusikiliza kesi kwa ukamilifu, Oktoba 7,2025 Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro ilibaini kuwa upande wa mashtaka ulikuwa umethibitisha kesi kwa kiwango kinachotakiwa katika kesi za jinai.
Mahakama hiyo iliwatia hatiani na kuwahukumu kila mmoja kulipa faini ya TSh217,600,000 ($82,346), au kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.
Kwa kutoridhishwa na hukumu ya kutiwa hatiani pamoja na adhabu, waombaji hao wawili walikata rufaa Mahakama Kuu wakipinga kuhumiwa.
Hoja za rufani
Awali kila mmoja alikuwa na rufaa yake. Ramadhani alikuwa na rufaa ya jinai namba 6441/2026, huku Aclay akiwa na rufaa ya jinai namba 4236/2026. Hata hivyo, kwa ushauri wa wakili wao, Mkilya Daudi, waliamua kuziunganisha rufaa hizo.
Warufani kwa pamoja waliwasilisha hoja 16 za rufaa, zikiwemo madai kwamba,mahakama ya chini ilikosea kisheria kwa kutozingatia masharti ya kifungu cha 29(1) cha EOCCA kuhusu muda wa kumfikisha mtuhumiwa mahakamani. Mahakama haikueleza sababu za kubadilishwa kwa mahakimu watatu waliokuwa wakiongoza shauri hilo.
Wakili Daudi akiwakilisha wateja wake alidai utetezi wao haukuzingatiwa ipasavyo au ulikataliwa bila sababu za msingi na kwamba Mahakama ilitegemea ushahidi usio na uthibitisho wa kutosha au usioaminika.
Alidai upande wa mashtaka haukuthibitisha shtaka bila kuacha shaka yenye mantiki, hakukuwa na hati ya kuwakamata na hakukuwa na maelezo ya kuridhisha kuhusu kutokuwepo kwake.
“Kulikuwa na ukinzani katika ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, hakukuwa na ripoti ya kitaalamu ya kuthibitisha utambulisho wa meno hayo kuwa ni meno ya tembo,”alidai Wakili Daudi.
Alidai kuwa, kwa vile walikuwa watu wasio na uwakilishi wa kisheria, hawakupewa maelezo ya haki zao ipasavyo wakati shtaka liliporekebishwa.
Wakili Daudi alidai pia kuwa mahakama ilitegemea kitabu cha rejesta cha Ruvuma Guest House (P3), licha ya jina la Ramadhani kutokuwamo na kwamba hakukuwa na ushahidi wa maandishi kuthibitisha kwamba PW8 alikuwa mfanyakazi wa Ruvuma Guest House.
“Kulikuwa na kasoro na kutokubaliana katika ushahidi kuhusu meno ya tembo na mifuko ya sulphate, mahakama ilishindwa kutathmini ushahidi wote, ukiwemo ushahidi wenye migongano, kulikuwa na kasoro katika mwenendo wa shauri ambazo zilifikia mzizi wa kesi na mahakama ilishindwa kuzingatia ipasavyo ushahidi wao wa utetezi,” alidai Wakili Daudi.
Majibu ya upande wa Jamhuri
Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Ephraim Ngaki ambaye alipinga hoja hizo na kueleza kuwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka uliwaunganisha washtakiwa na chumba ambako meno ya tembo yalipatikana.
Wakili Ngaki alikiri kwamba kulikuwa na ucheleweshaji wa siku 26 kati ya kukamatwa kwa waombaji na kufikishwa kwao mahakamani. Hata hivyo, alipinga kwa nguvu hoja kwamba kuchelewa kumfikisha mtuhumiwa mahakamani, kwa upande wake pekee, kunaweza kufanya hukumu ya kutiwa hatiani kuwa batili iwapo mshtakiwa alipata nafasi kamili ya kushiriki katika kesi na kujitetea kwa msingi wa ushahidi uliowasilishwa.
Kwa mujibu wa wakili huyo, dawa sahihi ya kisheria kwa kucheleweshwa kwa kumweka mtuhumiwa kizuizini kabla ya kesi kuanza ni kufungua madai ya fidia katika shauri la madai, kutokana na kunyimwa uhuru wake na si kumuachia huru kwa kuifuta hukumu ya hatia.
Aliongeza kwamba, kwa kuzingatia ushahidi wa PW7, ucheleweshaji huo ulikuwa na sababu za msingi kwa sababu uchunguzi ulikuwa mgumu na ulihitaji kufuatilia na kuwatafuta washtakiwa wengine watatu.
Kuhusu kubadilishwa kwa mahakimu alieleza kwamba kizuizi kilichowekwa na kifungu cha 230(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 Toleo la 2023, kinahusu hasa kesi ambazo usikilizwaji wake ulikuwa umeanza lakini haujakamilika, ambapo hakimu mwingine anachukua kesi na kuendelea na ushahidi uliokuwa tayari umerekodiwa na hakimu aliyemtangulia.
Alieleza kwamba kumbukumbu za kesi zinaonyesha kuwa katika hatua za awali kesi hiyo ilikuwa ikitajwa tu mara kwa mara mahakamani, na kwamba usikilizwaji halisi wa kesi ulianza tarehe 4 Machi, 2025 mbele Hakimu Mkazi Mwandamizi aliyepewa mamlaka ya kusikiliza.
Alidai hakimu wa kesi ya awali alifanya uchambuzi wa kina wa utetezi wa mshtakiwa wa kwanza (DW1) na DW2 katika kurasa za 8 hadi 11 za hukumu. “Mahakama ilifanya uamuzi sahihi kwamba madai ya waombaji kwamba walishambuliwa na kuporwa wakiwa barabarani yalipingwa kikamilifu na mlolongo wa ushahidi wa upande wa mashtaka.
Tembo ni miongoni mwa wanyamapori ambao viungo vyao, kama vile meno, hukutwa mikononi mwa watuhumiwa wanaokamatwa.

“Shitaka la kumiliki meno matatu ya tembo kulithibitishwa bila kuacha shaka yenye mantiki kupitia ushahidi wa mashahidi walioshuhudia tukio hilo,”alidai Wakili wa Serikali.
Uamuzi wa Mahakama Kuu
Jaji Magoiga alisema Mahakama ilizingatia ushahidi wa askari, mhudumu wa guest house, mwenyekiti wa eneo na mlinzi wa guest house.
Alisema Mahakama Kuu pia ilikubaliana kwamba mtaalamu wa wanyamapori, John Mtimbanjayo, alitambua meno hayo kuwa ya tembo na kuyathamini kwa TSh108,800,000 ($41,173).
“Ushahidi wa kitaalamu kuhusu utambulisho na thamani ya nyara hizo haukutikiswa na upande wa warufani. “Kuhusu kucheleweshwa kufikishwa mahakamani ni kwamba washtakiwa walifikishwa mahakamani baada ya zaidi ya muda wa saa 48 uliotajwa kisheria lakini hawakuonyesha namna ucheleweshaji huo ulivyowasababishia madhara au kuathiri kesi yao.
“Mahakama inaikataa hoja ya kucheleweshwa kufikishwa mahakamani. Pia inakataa hoja kuhusu mabadiliko ya mahakimu kwa sababu mahakama iliyoendesha usikilizwaji wa ushahidi na kutoa hukumu ndiyo iliyosikiliza kesi kuanzia mwanzo hadi mwisho, hakuna madhara yaliyowapata washtakiwa kutokana na mabadiliko hayo ya awali,” alisema Jaji Magoiga.
Katika suala la upekuzi na kukamatwa bila hati ya kukamata, Mahakama ilisema mazingira ya tukio yaliwaruhusu maafisa kuchukua hatua za haraka kwa kuwa walikuwa wakifuatilia taarifa kuhusu nyara zilizokuwa zimefichwa.
Jaji Magoiga alisema uwepo wa mashahidi huru wakati wa upekuzi uliunga mkono uhalali wa mchakato huo. Baada ya kuchambua hoja zote za rufaa, Mahakama Kuu ilihitimisha kuwa ushahidi uliowasilishwa uliunganisha washtakiwa na nyara hizo na kwamba upande wa mashtaka ulithibitisha kosa bila kuacha shaka yenye msingi.
Mahakama Kuu ilitupilia mbali rufaa hiyo kwa ukamilifu na kuacha hukumu pamoja na adhabu iliyotolewa na Mahakama ya chini ikiwa imesimama.
Picha ya bango: Kutumia mkondo wa sheria ni njia mojawapo inayotumika kulinda wanyamapori, ambapo wanaokamatwa wakiwa na viongo vya wanyama hao hushitakiwa chini ya kifungu cha 86(1), (2)(b) na (3) cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, (Sura ya 283 Toleo la 2022) kama ilivyorekebishwa, kikisomwa pamoja na aya ya 14 ya Jedwali la Kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Udhibiti wa Uhalifu wa Kiuchumi na Uhalifu wa Kupangwa, (Sura ya 200 Toleo la 2022). Picha kutoka Mtandaoni.
Aliyekutwa na nyama ya nyati kusota jela miaka 20, rufani yake yatupwa