- Maendeleo ya viwanda Dongo Kundu yanaibua maswali kuhusu hatima ya misitu ya kaya, mimea ya dawa na bioanuai inayotegemea maeneo hayo.
- Awamu ya kwanza ya shughuli ya kuhamisha mizimu, iliyoanza karibu na eneo la mradi wa kiwanda cha gesi cha Taifa Gas, ilihusisha mizimu minne kati ya 46 iliyotambuliwa katika eneo la takriban ekari 3,000 lililotengwa kwa ajili ya maendeleo.
- Mizimu hiyo ilikuwa ikihifadhiwa katika vichaka vidogo ambavyo jamii za wenyeji zililinda kwa mujibu wa mila na desturi zao, kabla ya baadhi ya wakazi kuhamishiwa upande wa pili wa barabara ya Dongo Kundu.
MOMBASA, Kenya – Waganga wa kienyeji katika eneo la Dongo Kundu, Mombasa, wameanza kuhamisha mizimu kutoka katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya miradi ya viwanda. Hatua hiyo imeibua wasiwasi kuhusu hatima ya misitu ya kaya, ambayo imekuwa ikihifadhi mimea ya dawa na kuwa makazi ya viumbe wa porini.
Wakati Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA) ikiendeleza miradi ya uwekezaji katika eneo hilo, waganga hao wanataka kutengewa ardhi mbadala ambako wataendeleza mila na tamaduni zao na kushiriki katika kurejesha miti na uoto wa asili ulioharibiwa na shughuli za ujenzi.

Wakiongozwa na mzee Nyundo Bedzitso Mwero, waganga hao wanasema kuhifadhi mizimu hiyo kwa muda katika boma la mtu binafsi si suluhu ya kudumu. Wameipa KPA siku 21 kutenga ardhi mbadala ya ekari 16 yenye mibuyu na vichaka vya asili, ambako wataweza kufanya tambiko zao, kupata mimea ya dawa na kusaidia kurejesha makazi ya viumbe wa porini.
Wakati huohuo, tathmini ya athari za kimazingira na kijamii ya mradi huo inaeleza kuwa Dongo Kundu ni sehemu ya mfumo wa ikolojia wa misitu ya pwani ya Afrika Mashariki, na kusisitiza umuhimu wa mabaki ya misitu yaliyosalia katika eneo hilo.
Shughuli hiyo, ikiongozwa na waganga, ilianza karibu na eneo la mradi wa kiwanda cha gesi cha Taifa Gas. Awamu ya kwanza ya shughuli hiyo imeshuhudia kuhamishwa kwa mizimu minne kati ya 46, ambayo ilitambuliwa katika eneo hilo la ekari 3,000, ambayo ilihifadhiwa katika vichaka vidogo vya jamii zilizoishi humo kabla ya kuhamia upande wa pili wa barabara ya Dongo Kundu.

Nyundo, ambaye pia ni mratibu wa muungano wa waganga wa kienyeji katika Kaunti ya Mombasa, anadai kuwa kutoondolewa kwa mizimu hiyo ilikuwa imeanza kuleta madhara kwa wale wanaofanya kazi katika maeneo ya viwanda na kwamba ilikuwa sharti watoe kwa kufanya tambiko na kutoa sadaka.
“Tuliondoa ili kuhakikisha usalama wa binadamu wanaotumia eneo hilo. Kwa sasa tumeweka hapa nyumbani kwa muda, ila tunataka serikali, kupitia KPA, kutupimia ekari 16 ya sehemu iliyo na mibuyu na kichaka mbali na maeneo ya makazi. Tayari tumepata sehemu hiyo, na tunasubiri tu watugawie,” Nyundo aliiambia Mongabay.
Waganga hao wamekuwa wakihifadhi vichaka vidogo kando na makazi ya watu ambapo walitumia kama maeneo matakatifu. Kwa mujibu wa viongozi hao, vilikuwa na miti asili, miti ya matunda na pia makazi ya ndege, nyoka na nyuki.
Kwa maelezo ya Mohammed Ali Cheusi, matibabu yao yanategemea sana miti, na walikuwa wakiipata kutoka kwa vichaka walivyovihifadhi na kulinda.

“Mbali na kuhifadhi mila na tamaduni, katika kichaka kilichokuwa na mzimu palikuwa na mwembe ambao nilikuwa nikichuma maembe na kugawia watu, ndege na nyoka,” anaelezea mganga Cheusi. “KPA wana mradi wa kupanda miti na hivyo tunawaomba pia sisi watupe hiyo miche, ikiwemo ya matunda, ili tupande upande huu tuliohamia ili kulinda mazingira na kurejesha makazi ya viumbe wa msituni,” aliongezea.
Dongo Kundu na umuhimu wa misitu ya pwani
Wazee hao wanasema hawapingi miradi ya maendeleo, lakini wanataka hatua zichukuliwe kulinda misitu ya kaya na bioanuai. Wasiwasi wao unaibua maswali kuhusu athari za ukataji wa miti ya nchi kavu na mikoko, pamoja na uchimbaji wa mchanga unaofanyika ili kutoa nafasi kwa ujenzi wa viwanda na miundombinu ya biashara.
Tathmini ya athari za kimazingira na kijamii (ESIA) ya mradi wa miundombinu katika eneo lililotengwa kwa ajili ya viwanda na uwekezaji inaeleza kuwa Dongo Kundu ni sehemu ya misitu ya pwani ya Afrika Mashariki yenye bioanuai muhimu.
Kwa mujibu wa tathmini hiyo, uoto wa asili katika eneo hilo umepungua kwa miaka mingi kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo shughuli za kibinadamu. Mabaki ya misitu yanapatikana katika maeneo machache, baadhi yake yakiwa misitu ya kaya ambayo jamii za wenyeji huyalinda kwa mujibu wa mila na desturi zao.
Baada ya mizimu minne kuhamishwa Oktoba 12, mingine 42 imesalia katika eneo lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji. Hali hiyo inaibua maswali kuhusu hatua zinazochukuliwa kulinda misitu iliyosalia na viumbe wanaotegemea makazi hayo, wakati shughuli za maendeleo ya viwanda zikiendelea.
KPA yaanzisha juhudi za kurejesha uoto wa asili
KPA inaendeleza juhudi za kurejesha misitu iliyoharibiwa na shughuli za kibinadamu na viwanda.
Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa KPA, Kapteni William Ruto, mamlaka hiyo inapanga kupanda miche 270,000 kwa kushirikiana na jamii zinazoishi kando ya pwani. Mpango huo unalenga kurejesha misitu na kuchangia katika kupunguza athari za uzalishaji wa gesi chafuzi unaohusishwa na shughuli za viwanda.
Kapteni Ruto alisema upandaji wa mikoko ni sehemu ya juhudi za KPA za kuendeleza bandari endelevu, kwa kushirikiana na jamii na kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi.
Akizungumza na wanahabari baada ya shughuli ya kuhamisha mizimu Dongo Kundu, Mgandi Kalinga, msimamizi wa kamati inayoshughulikia migogoro inayohusiana na miradi ya maendeleo ya bandari, alisema kuwa suala la kupata ardhi mbadala kwa ajili ya mizimu na vigango vya waganga bado linajadiliwa.
“Tunajadili iwapo watapewa fedha za kununua shamba mbadala au kutengewa ardhi katika eneo la mradi wa kiuchumi. Eneo hilo lingewekwa uzio na kutumiwa kwa shughuli zao za kimila na tiba asili,” alisema Mgandi.

Alisema mizimu minne iliyohamishwa ilikuwa katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya miradi ya Taifa Gas, na Afri Exim Bank. Kwa mujibu wake, mizimu mingine pia inadaiwa kuwepo katika eneo la mradi wa Milly Gas.
Alisema kuwa, kupitia mpango wa KPA wa kupanda miti, waganga na wazee wa kaya watahusishwa katika kutafuta mbegu na miche ya aina za miti ya asili zilizokuwa zikimea katika maeneo yao ya awali, ili zipandwe katika maeneo mapya wanayoishi.
Kuhusu upandaji wa miti katika maeneo mapya, Mgandi alisema baadhi ya wakazi wenye hati miliki za ardhi tayari wameanza kupokea miche, huku wengine wakisubiri ardhi zao kupimwa na mipaka yake kuthibitishwa.
Katika eneo lililotengwa kwa ajili ya viwanda na uwekezaji kulikuwa na kaya mbili, Vikadini na Vibuyuni. Wakazi wa kaya hizo walihamishiwa eneo la Kaya Mtongwe, lililo kwenye ardhi inayomilikiwa na KPA lakini nje ya eneo la mradi.
Baada ya wakazi wa eneo la mradi kuhamishiwa karibu na Kaya Mtongwe, wazee wa kaya wanasema msitu huo unakabiliwa na shinikizo linaloongezeka kutokana na shughuli za kibinadamu. Wanaomba kuwekwa kwa uzio ili kulinda msitu dhidi ya shughuli zinazoweza kuuharibu.
Aula Juma Ndago, mwenyekiti wa kaya 14 katika eneo maalumu la kiuchumi na uwekezaji la Dongo Kundu, aliiambia Mongabay kuwa changamoto zinazowakabili ni pamoja na mifugo kuingia msituni, ukataji wa miti na uwindaji wa wanyama, wakiwemo swala. Pia wanasema manyani na mbega wanaosalia katika eneo hilo wanasumbuliwa na shughuli za kibinadamu.
“Ninachokililia ni hati miliki. Kaya zote hazina hati miliki, na baadhi ya maeneo yamechukuliwa na kupewa watu wengine kwa sababu hayajapimwa na mipaka yake haijalindwa kwa nyaraka. Tunaomba, watakapoweka uzio, pia watuletee miche tupande ili kurejesha hadhi ya msitu wetu,” alisema Aula.
Tobias Ndau Mwakio, mganga anayetumia dawa za miti shamba, anasema uharibifu wa miti unaohusishwa na miradi ya maendeleo umewalazimisha waganga kutafuta baadhi ya mimea ya dawa katika maeneo ya mbali, jambo linaloongeza gharama za kuipata. Anataja mmea wanaouita Malangamia, ambao anasema umekuwa ukipatikana Dongo Kundu lakini sasa unapungua.
Anataja mmea wanaouita Malangamia, ambao anasema umekuwa ukipatikana Dongo Kundu lakini sasa unapungua.
Hatima ya bioanuai
Ripoti ya tathmini ya mazingira ya NEMA inaeleza kuwa eneo hilo lina miti na spishi mbalimbali za wanyama na wadudu. Mtaalamu wa mazingira, Dk. Mohammed Pakia, aliiambia Mongabay kuwa wawekezaji wanapaswa kupanga hatua za kuhifadhi viumbe na mimea iliyopo kabla ya kuanza shughuli zinazoweza kuharibu makazi yao. Alisema hatua hizo zinapaswa kuongozwa na utafiti na mbinu za kitaalamu zinazofaa kwa kila aina ya kiumbe.
“Ni jukumu la wawekezaji kupanga hatua za kuhifadhi mimea na viumbe vilivyopo katika vichaka hivyo kabla ya kuanza shughuli za uharibifu, kwa kutumia mbinu za kitaalamu na matokeo ya tafiti zilizopo,” alisema Dk. Pakia.
Picha ya bango: Vigango vilivyohamishwa katika baadhi ya mizimu minne kati ya 46 iliyotambuliwa katika eneo la takriban ekari 3,000 lililotengwa kwa ajili ya maendeleo. Picha na Amina Chombo, Mongabay.
Jinsi $25,000 zilivyozaa mtandao wa uhifadhi wa jamii: Mahojiano na waanzilishi wa Mwambao Tanzania