- Makubaliano ya kikanda yaingizwe katika sheria, mipango ya maendeleo na bajeti za kitaifa.
- Ushirikiano unahitaji taasisi zenye uwezo, utaalamu wa kisayansi, teknolojia na fedha.
- Fursa za kiuchumi zitapatikana kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.
- Ushirikiano wa kikanda uambatane na hatua za kitaifa za kutatua changamoto zinazovuka mipaka.
DAR ES SALAAM, Tanzania — Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 6 hadi 9, 2026 umekamilika huku nchi za ukanda wa Bahari ya Hindi Magharibi zikipewa jukumu la kugeuza ahadi za kulinda bahari kuwa vitendo, huku Tanzania ikitaka maamuzi yanayotekelezeka na Afrika Kusini ikisisitiza ushirikiano wa kikanda unaozaa matokeo katika ngazi za kitaifa.
Mkutano huo ambao pia ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 40 ya mkataba unaolenga kulinda mazingira ya Bahari ya Hindi Magharibi, uliwakutanisha nchi wanachama na wadau kujadili utekelezaji wa maamuzi yaliyopita, ufadhili wa uhifadhi na mikakati ya kulinda mazingira ya bahari na pwani pamoja na kutafuta fursa za kukuza uchumi endelevu wa buluu.
Tanzania yataka maamuzi yenye matokeo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, alisisitiza wakati wa ufunguzi wa COP12 Oktoba 6 kuwa maamuzi ya mkutano yanapaswa kuendana na ukubwa wa changamoto zinazokabili mazingira ya bahari na kuwa na uwezo wa kutekelezwa.
“Maamuzi tunayoyafanya hapa lazima yaendane na ukubwa wa changamoto zinazotukabili na yaweze kutekelezwa kwa vitendo,” alisema Masauni.

Alitaja matarajio ya Tanzania kuwa ni kutathmini hali ya Bahari ya Hindi Magharibi, kuhakikisha maamuzi yanatekelezwa, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kushirikisha jamii, wakiwemo vijana.
Msimamo huo ulifafanuliwa zaidi na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, aliyewasilisha vipaumbele sita vya kuimarisha uhifadhi wa mifumo ya ikolojia ya Bahari ya Hindi Magharibi na kukuza uchumi endelevu wa buluu.
Vipaumbele hivyo ni; kuimarisha ushirikiano wa kikanda; kulinda mifumo ya ikolojia ya bahari; kukabiliana na uchafuzi wa bahari; kuwekeza katika ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi; kutumia sayansi na utafiti katika kufanya maamuzi pamoja na kuhakikisha jamii za pwani, wanawake, vijana na sekta binafsi wanashiriki kikamilifu.
Ndejembi alisisitiza umuhimu wa nchi kuvuka hatua ya kutoa ahadi na kuhakikisha makubaliano ya kikanda yanaingizwa katika sheria, mipango ya maendeleo na bajeti za kitaifa.
Mapendekezo hayo yanaweka wazi maeneo ambayo nchi zinapaswa kuyapa kipaumbele baada ya mkutano.
Changamoto zinazovuka mipaka
Msimamo wa Afrika Kusini katika COP12 umeongeza uzito katika hoja kwamba ushirikiano wa kikanda unapaswa kuambatana na hatua za kitaifa zinazolenga kutatua changamoto zinazovuka mipaka.
Katika kauli yake kwenye mkutano huo, Naibu Waziri Narend Singh alisisitiza umuhimu wa kuunganisha ushirikiano wa kikanda na utekelezaji wa sera, matumizi ya sayansi na upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika kulinda mazingira ya bahari.
Nchi hiyo imeeleza kuwa changamoto kama uchafuzi wa bahari, mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa bioanuai na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali, haziishii kwenye mipaka ya nchi moja na kwamba zinahitaji hatua za pamoja.

“Ushirikiano huo hauwezi kufanikiwa kwa matamko pekee. Unahitaji taasisi zenye uwezo wa kutekeleza mipango, utaalamu wa kisayansi, teknolojia na fedha zinazotabirika,’’ alisema.
Afrika Kusini pia imeeleza kuwa zaidi ya watu milioni 65 katika maeneo ya pwani ya ukanda wa Bahari ya Hindi Magharibi hutegemea bidhaa na huduma zinazotolewa na mifumo ya ikolojia ya bahari.
Hali hiyo inaonyesha ukubwa wa athari zinazoweza kutokea iwapo mazingira yataendelea kuharibika, lakini pia fursa zinazoweza kupatikana iwapo rasilimali hizo zitasimamiwa kwa uendelevu.
Kwa mantiki hiyo, msimamo wa Afrika Kusini unaendana na wito wa Tanzania wa kutaka maamuzi yenye matokeo, huku ukisisitiza kuwa mafanikio yanahitaji nchi kufanya kazi kwa pamoja na kutekeleza wajibu wake katika ngazi za kitaifa.
Msimamo wa UNEP
Wito wa kuhamisha ahadi za kimazingira zinakwenda kwenye utekelezaji pia umepewa uzito na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), ambalo limesisitiza umuhimu wa nchi kuhakikisha ahadi zao zinazaa matokeo yanayopimika.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen, ametoa wito kwa nchi kutekeleza ahadi za kulinda mazingira badala ya kuishia katika makubaliano.
Hoja hiyo inagusa moja kwa moja changamoto inayokabili Mkataba wa Nairobi: namna ya kuhakikisha maamuzi ya kikanda yanatafsiriwa kuwa sera, mipango na hatua zinazopunguza uchafuzi, kurejesha mifumo ya ikolojia iliyoharibika na kulinda rasilimali za bahari.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Elizabeth Maruma Mrema, alisisitiza umuhimu wa kutumia sayansi katika kuandaa sera na kufanya maamuzi kuhusu mazingira ya bahari.
Akizungumza katika siku ya ufunguzi, Mrema alisema miaka 40 ya Mkataba wa Nairobi imejenga msingi muhimu wa kutumia sayansi katika maamuzi ya mazingira, huku akisisitiza ushirikiano unaowahusisha vijana, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na jumuiya ya wanasayansi.

Ushirikiano huo ni muhimu katika maeneo yanayohitaji hatua za pamoja, yakiwemo urejeshaji wa mikoko na nyasi bahari, uhifadhi wa bioanuai, kupunguza uchafuzi na kuimarisha ustahimilivu wa maeneo ya pwani.
Fedha ni kikwazo cha utekelezaji
Pamoja na umuhimu wa maamuzi na ushirikiano, upatikanaji wa fedha unabaki kuwa miongoni mwa changamoto zinazoweza kuamua kasi ya utekelezaji wa mipango ya uhifadhi.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Richard Muyungi, alisema Oktoba 7 kuwa changamoto za kimazingira zinazokabili Bahari ya Hindi Magharibi zinahitaji rasilimali zinazozidi uwezo wa vyanzo vya kawaida vya fedha vya kitaifa.
Kauli hiyo inaonyesha kuwa utekelezaji wa ahadi unahitaji zaidi ya utashi wa kisiasa. Nchi zinahitaji pia fedha za kutosha kwa ajili ya mipango ya uhifadhi, kurejesha mazingira yaliyoharibiwa na kuimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Uhifadhi wa bahari ni fursa ya uchumi
Muyungi pia aliangazia fursa za kiuchumi zinazoweza kupatikana kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.
Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na TBC1, alisema COP12 ilitoa nafasi kwa vijana, wanawake na wafanyabiashara kutambua fursa zinazotokana na uchumi wa buluu.
Alitaja uvuvi, utalii wa baharini na kilimo cha mwani kuwa ni miongoni mwa shughuli zinazoweza kukuza kipato na kuchangia maendeleo ya kiuchumi.
Alisisitiza pia umuhimu wa kuwawezesha vijana kupata maarifa ya kutumia fursa hizo, huku wanawake wanaojishughulisha na kilimo cha mwani, hususan katika maeneo ya pwani ya Zanzibar, wakipata nafasi ya kupanua shughuli zao na masoko.
Hoja hiyo inaunganisha ajenda ya uhifadhi na maisha ya wananchi. Bahari yenye afya inaweza kusaidia ajira, chakula, utalii na biashara, lakini manufaa hayo yatadumu tu ikiwa rasilimali zitasimamiwa kwa uendelevu.
Picha ya bango: Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi akiwa na wajumbe wengine kwenye Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12). Picha kwa hisani ya Ofisi ya Makamu wa Rais.
Wadau wanaoshiriki COP12 wataka ahadi za kulinda bahari zigeuzwe kuwa vitendo