- Nyangumi alikwama katika ufukwe wa Muanda kwa saa 25 kabla ya kufa.
- Juhudi za kumrudisha baharini zilikwama kutokana na ukubwa na uzito wake.
- Tukio hilo limebainisha changamoto zilizoko katika uhifadhi wa viumbe wa baharini.
- Mamlaka za Kongo zilitangaza mpango wa kufukua mabaki yake ili yatumike katika tafiti.
MUANDA, Kongo-Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo- Miezi miwili iliyopita, bahari ilileta tukio adimu lililovutia watu wengine huko Muanda, katika mkoa wa Kongo-Kati, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baada ya nyangumi mwenye urefu kati ya mita 10 hadi 12, kukwama kwenye pwani ya bahari ya Atlantiki
Nyangumi huyo alikwama ufukweni tarehe 1 Julai 2026, kuanzia majira ya saa 11:00 alfajiri hadi saa 11:30 jioni. Ingawa alikuwa hai, lakini hakuweza kusogea kutoka ufukweni hadi kesho yake, yaani Julai 2, majira ya 1:00 usiku alipokufa. Kwa hesabu za haraka, alikwama kwa saa 25.
Katika kipindi alichokuwa ufukweni, mnyama huyo mkubwa wa baharini aliwavutia mamia ya wakazi, wavuvi na watu wengine waliofika kumtazama. Katika eneo ambalo maisha ya kila siku kwa kiasi kikubwa yanategemea uvuvi na shughuli za baharini, uwepo wa mnyama huyo haukuwa jambo la kawaida.

“Baadhi ya wakazi wamkaribia ili kumtazama, kumpiga picha au kumgusa mnyama huyo wa baharini,” Prisca Lwamba, mkazi wa Muanda, aliiambia Mongabay kwa njia ya simu.
Baada ya nyangumi huyo kufa, mamlaka zilijaribu kuzuia watu wasimkaribie, hasa kwa sababu chanzo cha kifo chake, hakikuwa kimejulikana. Kadhalika, chanzo halisi cha kukwama kwake hakikuwekwa wazi kisayansi.
“Hatujui alikufa kutokana na nini,” alisema De Dieu By’ayombe, mkuu wa mkoa wa Taasisi ya Kongo ya Uhifadhi wa Mazingira (ICCN) huku akiwataka wananchi wasimguse mnyama huyo wala kula nyama yake kabla ya kufanyiwa uchunguzi.
Juhudi za kumuokoa
Kwa mujibu wa Lwamba, juhudi za timu za ICCN kumrudisha nyangumi huyo baharini, zilikwama kutokana na ukubwa na uzito wa mnyama huyo. “Wakati akiwa bado hai, timu za ICCN zilijaribu kumrudisha baharini,” anasema Prisca Lwamba. “Lakini ukubwa na uzito wa mnyama huyo vilifanya operesheni hiyo kuwa ngumu.”
Kwa mujibu wa Lwamba, vifaa mbalimbali vilitumika, lakini ilishindikana kumtoa. “Hatimaye, ilibidi crane yenye nguvu zaidi iletwe kutoka Matadi ili kusaidia kumuondoa mnyama huyo. Licha ya juhudi hizo, nyangumi hakunusurika,” alisema Lwamba.
Tukio la nyangumi huyo linaibua mapendekezo kuhusu namna Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaweza kutumia matukio kama hayo kama fursa ya kufanya tafiti kuhusu viumbe wa baharini.
Profesa Malick Tshibangu, mtaalamu wa mazingira na utawala wa mazingira, anaona kwamba tukio hilo halikupaswa kuishia kwenye kumzika nyangumi huyo tu.
“Yule nyangumi aliyekufa anaweza kuwa kumbukumbu muhimu kwenye sayansi ya bahari. Utafiti kumhusu unaweza kuleta mawazo mapya kuhusu bioanuwai ya baharini, uchafuzi wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi au hata baadhi ya magonjwa yanayojitokeza na kuwaathiri viumbe wa baharini” anaeleza Profesa Tshibangu.
Nyangumi azikwa
Baada ya juhudi za kumuokoa kushindikana, mzoga wa nyangumi huyo ulisafirishwa na kuzikwa huko Makasamba, kwenye barabara ya Muanda-Boma. Operesheni hiyo ilifanyika chini ya uangalizi wa mamlaka, ICCN, huduma za kiufundi na viongozi wa kimila.
Hata hivyo, uamuzi wa kuuzika mzoga huo uliibua maswali miongoni mwa baadhi ya wakazi na wataalamu.
Kwa mujibu wa Lwamba, baadhi watu walitaka mifupa ya mnyama huyo itumike kwenye utafiti wakati wengine walitaka uchunguzi wa kisayansi ufanyike kabla ya mazishi.
“Kabla ya mazishi, hatua kama utambuzi wa aina ya nyangumi, uchunguzi wa mwili baada ya kifo pamoja na kuchukua sampuli za kibaolojia na kijenetiki, vingezingatiwa,’’ alisema Profesa Tshibangu.
Serikali kufukua mabaki
Mwanzoni mwa Septemba, Waziri wa Mazingira, Maendeleo Endelevu na Uchumi Mpya wa Tabianchi, Marie Nyange Ndambo, alitangaza mpango wa kufukua mabaki ya nyangumi huyo.
Timu kutoka katika wizara mbalimbali ilifika eneo hilo, takribani siku 40 baada ya mzoga huo kuzikwa, ujumbe wa wizara mbalimbali ulitembelea eneo alipozikwa nyangumi huyo ili kutathmini hali ilivyokuwa.

Lengo lilikuwa kupata tena mifupa na mabaki mengine ambayo bado yanaweza kutumika katika utafiti. Dieudonné Sidia, mtaalamu wa ICCN, anasema operesheni hiyo ni fursa ya kipekee ya kufanya utafiti. Anasema : “Kumfukua nyangumi huyu ni fursa kwa utafiti wa kisayansi na kuongeza uelewa kuhusu bioanuwai ya wanyama wa baharini Kongo”.
Urithi wa kisayansi
Nyuma ya mpango huo kuna azma ya kugeuza mabaki ya nyangumi huyo kuwa urithi wa kisayansi. “Mifupa yake inaweza kutumika kufundishia biolojia, zoolojia au sayansi za baharini katika vyuo vikuu na vituo vya utafiti vya Kongo, na pia kuwa chombo cha kielimu kinachoweza kufikiwa na umma,’’ anasema Rebecca Mulumba mtaalamu wa bioanuwai.
Kwa mujibu wa Mulumba, tukio hilo linaonyesha pia utajiri wa bioanuwai ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. “Ingawa tukio hili linawakilisha hasara kubwa sana kwa nchi yetu, pia linatuwezesha kutambua utajiri wa maji yetu na kuwafanya viongozi wafikirie zaidi,” anasema Mulumba.
“Mifupa ya nyangumi inaweza kuwa kivutio cha kisayansi na kielimu kwa Muanda, na kuupa urithi wa asili wa jiji hili la pwani sura mpya,” Mulumba alieleza katika barua pepe aliyotuma kwa Mongabay.
Changamoto katika uhifadhi
Eddy Lwamba, mtaalamu wa bioanuwai na mwanafunzi wa shahada ya udaktari (PhD) katika Chuo Kikuu cha Burundi, anasema tukio hilo limeonyesha changamoto katika sekta ya uhifadhi. “Changamoto zilizojitokeza katika jaribio la kumrudisha nyangumi baharini, na baadaye katika kuhamisha mzoga wake, zinaonyesha umuhimu wa kuimarisha rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya dharura za mazingira kwenye pwani ya Kongo,’’ anasema Lwamba.

Kuhusu utafiti zaidi inapendekezwa kuwepo kwa ushirikishwaji wa sekta mbalimbali. “Ili kufanya tafiti zinazofaa na za kina kuhusu nyangumi huyu, wataalamu kadhaa wanapaswa kushirikishwa katika operesheni hiyo,” anaeleza Mulumba.
Anasema kumfukua mnyama mwenye ukubwa huo kunahitaji vifaa vinavyofaa pamoja na utaalamu katika biolojia ya baharini, anatomia, uhifadhi na usimamizi wa sampuli.
Joseph Byamungu, mvuvi wa Muanda, anasema nyangumi huyo atabaki kuwa zaidi ya mnyama aliyekwama kwenye ufukwe. Atakuwa kumbukumbu ya tukio lililoibua hisia kubwa, kuonyesha changamoto katika uwezo wa uhifadhi na sasa kutoa fursa kwa sayansi ya Kongo.
“Mifupa yake inaweza kusimulia hadithi pana zaidi kuliko ile ya kifo chake: hadithi ya nchi inayotafuta kuufahamu vizuri zaidi urithi wake wa baharini, kuimarisha uwezo wake wa kisayansi na kugeuza upotevu wa bioanuwai kuwa chanzo cha maarifa kwa vizazi vijavyo,” anasema Byamungu.
Picha ya bango: Nyangumi aliyekufa baada ya kukwama kwenye pwani ya Bahari ya Atlantiki, eneo la Muanda, mkoani Kongo-Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akizikwa huko Makasamba. Mazishi hayo yaliongozwa na mamlaka za mkoa wa Kongo-Kati kwa kushirikiana na Taasisi ya Kongo ya Uhifadhi wa Asili (ICCN), mamlaka za kimila na timu za kiufundi. Picha na Patrick Mukendi.
Utafiti: Mifumo nyeti ya bahari ya Kenya imo ndani ya maeneo yaliyopangiwa miradi ya mafuta na gesi