- Kuchoshwa namfumo wa uhifadhi unaoongozwa kutoka juu kwenda chini, pamoja na imani kwamba jamii za pwani zinaweza kusimamia rasilimali zao zenyewe, kulimfanya Ali Thani na Lorna Slade kuungana na kuanzisha Mtandao wa Jamii za Pwani wa Mwambao (Mwambao Coastal Community Network).
- Ushirikiano wao ulitokana na uzoefu tofauti. Thani, Mtanzania kutoka maeneo ya pwani ambaye aliwahi kufanya kazi serikalini na mashirika ya kimataifa ya uhifadhi, alileta uelewa wa kina wajamii za pwani. Slade alileta uzoefu wa miongo kadhaa na uelewa wa taasisi za kimataifa zinazofadhili shughuli za uhifadhi.
- Tangu wakati huo, Mwambao imekua na kuwa taasisi yenye bajeti ya kila mwaka ya mamilioni ya dola na imesaidia jamii kujaribu mbinu mbalimbali, ikiwemo kufunga maeneo ya uvuvi kwa muda, usimamizi shirikishi wa rasilimali na programu za kuboresha maisha. Hata hivyo, uzoefu wake haujawa na mafanikio kwa kiwango sawa kila mahali, naimekubaliwa kwa viwango tofauti na jamii.
- Ukuaji huo pia umeibua swali gumu zaidi kwa waanzilishi wake: Je, mfumo unaoongozwa na jamii unaweza kudumishwa kwa mafanikihata taasisi yenyewe inapozidi kuwa kubwa?
UNGUJA, Tanzania — Miongo kadhaa kabla ya kuanzisha pamoja taasisi ya uhifadhi wa bahari, Ali Thani na Lorna Slade walikutana nchini Tanzania.
Miaka kadhaa baadaye, Slade alirejea katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kufanya utafiti kuhusu utalii kwa ajili ya shahada yake ya uzamili, ambapo alishiriki katika mpango uliolenga kuimarisha maarifa na haki za wasimamizi wa rasilimali katika ngazi ya jamii. Mwaka 2008, dunia ilikumbwa na mgogoro mkubwa wa kifedha na shirika lililokuwa likiunga mkono mpango huo lilijiondoa Tanzania. Lilitoa sehemu ndogo tu ya fedha lilizoahidi awali, yaani dola za Marekani 25,000, pamoja na wazo ambalo bado waliona linafaa kuendelezwa.
Walisema, “Sawa, hili ni wazo zuri. Tuna dola 25,000 basi, hizi hapa,” Slade anakumbuka.
Mwanzo huo mdogo hatimaye uligeuka kuwa Mtandao wa Jamii za Pwani wa Mwambao (Mwambao Coastal Community Network), taasisi yenye mizizi katika jamii za eneo husika ambayo sasa inafanya kazi na jamii za pwani za Zanzibar na Tanzania Bara, ikiwa na bajeti ya kila mwaka ya takribani dola milioni 3.5.
Kwa Thani, Mtanzania kutoka maeneo ya pwani ambaye aliwahi kufanya kazi serikalini na katika mashirika makubwa ya uhifadhi, Mwambao ilianzishwa kutokana na imani kwamba uhifadhi hauwezi tu kubuniwa sehemu nyingine na kisha kuletwa kwa jamii. Anasema watu wanaotegemea rasilimali za asili wanapaswa kuwa na maarifa, uwezo na mamlaka ya kushiriki katika kuzisimamia.
Wazo hilo lina umuhimu mpana zaidi wakati ambapo nchi mbalimbali zinafuatilia lengo la kimataifa la kuhifadhi asilimia 30 ya maeneo ya nchi kavu na bahari duniani ifikapo mwaka 2030.
Mashirika ya ndani na jamii yanatarajiwa kubeba sehemu kubwa ya jukumu hilo, licha ya kukabiliwa na changamoto ya kupata ufadhili wa muda mrefu ambao mara nyingi hupatikana kwa mashirika makubwa ya kimataifa na taasisi za kati.
Kazi za Mwambao zinajumuisha kusaidia usimamizi wa uvuvi unaoongozwa na jamii, kufunga maeneo ya uvuvi kwa muda na mipango ya kuboresha maisha.
Hata hivyo, tathmini huru zilizopitiwa na Mongabay pia zimeonyesha kuwa jamii zimekuwa na mitazamo tofauti kuhusu baadhi ya hatua hizo, ikiwa ni pamoja na migogoro na kutokuaminiana kuhusu baadhi ya maeneo yaliyofungwa kwa uvuvi, utekelezaji usio sawa wa sheria na maswali kuhusu kama taasisi za jamii zinaweza kudumisha mafanikio bila msaada wa nje unaoendelea.
Mivutano hiyo sasa inawakabili waanzilishi wa Mwambao.
“Huo ni mjadala wa kimkakati kwetu kwa sasa,” anasema Slade.
Thani na Slade walileta uzoefu tofauti sana katika kuanzisha taasisi hiyo. Thani alileta uelewa wa kina wa jamii za pwani na utamaduni wa eneo hilo, wakati Slade, Mwingereza, alileta uzoefu wa miongo kadhaa wa kufanya kazi Tanzania pamoja na uelewa wa taasisi za kimataifa zinazofadhili shughuli za uhifadhi.
Kilichodumisha ushirikiano wao, wanasema, kilikuwa kitu rahisi.
“Kuheshimiana,” anasema Thani.
Wakati wa safari ya kikazi Zanzibar, David Akana wa Mongabay alikaa na Thani na Slade kujadili Mwambao. Mazungumzo yafuatayo yamehaririwa kwa ajili ya ufupi na mtiririko.

Mongabay: Tuanze mwanzo kabisa. Lorna, hadithi ya Mwambao ilianzaje?
Lorna Slade: Nianze kwa kuangalia miaka takriban 31 iliyopita. Ali alikuwa akifanya kazi na mume wangu katika Idara ya Misitu Zanzibar, mimi wakati huo nilikuwa katika Idara ya Mazingira. Ndivyo tulivyofahamiana.
Tulifanya kazi hapa Tanzania kwa miaka karibu mitano na nusu, kisha kila mmoja akaendelea na njia yake. Baadaye, nilirudi kufanya utafiti wakati wa shahada ya uzamili katika masuala ya utalii. Kupitia utafiti huo, tuliwasiliana na shirika linaloitwa Sand County Foundation, lenye makao yake nchini Marekani.
Walijihusisha zaidi na kutetea haki na maarifa za wamiliki wa ardhi na kuendeleza maarifa kuhusu usimamizi wa rasilimali. Waliniomba niangalie kwa upana kwa ngazi ya kikanda na kuona kama tungeweza kuanzisha aina fulani ya mtandao.
Nilifanya utafiti, na nilipomaliza, nikawaambia, “Nadhani tunapaswa kuzingatia Tanzania. Kuna kazi nyingi za kufanywa.”
Walikubali. Lakini tulipokuwa tunakaribia kuanza, ilikuwa mwaka 2008, kipindi cha mgogoro mkubwa wa kifedha duniani. Waliamua kujiondoa kabisa Tanzania. Kimsingi walisema, “Ni wazo zuri. Tuna dola 25,000 — basi anzeni na hizi.” Ndivyo tulivyoanza.
Wakati huo, Ali alikuwa akifanya kazi na CARE Tanzania na WWF, mimi nilikuwa nikigawanya muda wangu kwa kufanya kazi Uingereza na Tanzania.
Kwa hizo dola 25,000, tuliamua kuanzisha mtandao wa kubadilishana maarifa na kufanya utetezi ili jamii ziweze kubadilishana uzoefu na mbinu zilizofanikiwa.
Tulijifunza kitu kinachojulikana kama uandishi wa habari shirikishi. Unaingia katika jamii, unabuni hadithi pamoja na wanajamii, unawafundisha watu jinsi ya kutumia kamera, kutengeneza na kuhariri hadithi, kuunda filamu, kisha kuisambaza kwa wengine. Nadhani tulitengeneza filamu kama 10 au 12 kwa jumla.
Kisha tuligundua kwamba kupata fedha za maarifa na utetezi ni vigumu sana; unahitaji pia kufanya mambo yenye matokeo yanayoonekana. Tulianza kupata fursa ndogo ndogo, kufanya kazi za ushauri, na hatua kwa hatua kuingia katika utekelezaji.
Kwa muda mrefu, fedha zilikuwa zinaingia taratibu sana. Mwanzoni, tulikuwa tukigharamia shughuli za shirika kwa kutumia mishahara yetu wenyewe. Baada ya miaka miwili hivi, hatimaye tulipata fedha za kutosha kutuajiri wote wawili. Tumepiga hatua kubwa tangu wakati huo.

Mongabay: Ali, ulikuwa umeshafanya kazi serikalini na katika mashirika kama CARE na WWF. Kwa nini uliacha mashirika hayo na kuanzisha kitu chenu wenyewe?
Ali Thani: Kutokana na uzoefu niliokuwa nao, nilihisi kwamba hiyo ingeweza kuwa fursa nzuri ya kuanza kutekeleza usimamizi shirikishi, utawala, na mbinu mengine.
Nilikuwa nimefanya kazi serikalini na WWF. Tuliamini katika kuimarisha uwezo wa usimamizi wa rasilimali. Usimamizi shirikishi ulikuwa mbinu tuliyoamini ingeweza kusaidia kushughulikia matatizo mengi tuliyokuwa tunayaona katika jamii.
Mwanzoni, tulifanya mambo kwa kujitolea. Tuliweka nguvu zetu zote kuhakikisha tunafanya kazi na jamii na kujaribu kutatua matatizo yao.
Kupitia kazi tulizofanya Kenya, Pemba na Tanga, tulikuwa tumeona matatizo mengi. Tuliamini kwamba baadhi yangeweza kushughulikiwa kupitia usimamizi shirikishi na kwa kuimarisha uwezo wa utawala katika jamii.
Mongabay: Lakini nyote wawili mliona jinsi mashirika makubwa ya kimataifa yanavyofanya kazi, huku yakiwa na rasilimali za kutosha. Nini kilikufanya uamini kwamba shirika dogo lenye mizizi ya ndani lingeweza kufanikiwa?
Lorna Slade: Nadhani kulikuwa na mtazamo kwamba kuwa mtu wa eneo husika au, kwa upande wangu, kuwa nimeishi hapa kwa muda mrefu na kufanya kazi na wenyeji, kunakupa uelewa mzuri wa jamii za pwani.
Una watu wanaoheshimika katika jamii za pwani, wanaojua jinsi ya kufanya kazi na watu wa eneo hilo, badala ya shirika la nje kuja na mawazo yake ya jinsi litakavyotatua tatizo. Huo unaweza kuwa mfumo wa kutoka juu kwenda chini.
Mwanzoni, tulifikiri mashirika ya kimataifa yangeweza kuleta mbinu ya kisayansi na ushahidi, ili sisi tubaki tu kuwa wawezeshaji kwa sababu tulikuwa tunaaminiwa na jamii na pia tulikuwa tunafahamu namna ya kutumia mbinu zinazoshirikisha jamii.
Tulifikiri tungeweza kufanya kazi sambamba. Baada ya muda, tuligundua kwamba pia tulihitaji kuimarisha upande wa kisayansi wa kazi zetu wenyewe. Tulianza kutumia takwimu zaidi na kuchukua hatua madhubuti katika kufanya ufuatiliaji.
Mongabay: Ali, umuhimu wa kuwa mwenyeji wa Zanzibar na kuelewa utamaduni wa pwani umekuwa na uzito gani kwa mafanikio ya Mwambao?
Ali Thani: Umekuwa na uzito mkubwa sana. Ili kuelewa uhifadhi, unahitaji kujua utamaduni wa watu. Unahitaji kujua jinsi watu wanavyoona uhifadhi na jinsi ya kuoanisha dhana hizo.
Kama ningekwenda mahali pengine, sidhani kama ningefanikiwa kiasi hicho. Lakini kama Mtanzania wa pwani, ninaweza kufanya kazi hapa. Hata Kenya, ninaweza kufanya kazi huko kwa sababu utamaduni wa jamii za pwani unafanana.
Ukitoka nje, unahitaji kwanza kujifunza na kuelewa jamii. Lorna alikuja kutoka mahali pengine, lakini alijifunza kuelewa jamii. Anajua jamii za pwani. Ameishi na kufanya kazi na jamii za pwani ya Tanzania.

Mongabay: Lorna, bila shaka kuna thamani pia katika maarifa na uzoefu unaotoka nje. Je, aina hizo mbili za maarifa ni kwa namna gani zimefanya kazi pamoja?
Lorna Slade: Tunafanya kazi pamoja kama timu kwa sababu tunaleta ujuzi tofauti mezani. Kuna maeneo ambayo ujuzi wetu unaingiliana, lakini pia ujuzi wetu unatofautiana. Wakati mwingine, ili kuwasiliana na watu watakaotufadhili, unahitaji kuzungumza lugha yao; simaanishi Kijerumani au Kiingereza, ninamaanisha kuelewa matarajio yao, kukidhi vigezo vyao, mambo kama hayo.
Bila shaka, unaweza kujifunza kutoka maeneo mengine. Unaweza kusoma kuhusu kinachoendelea mahali pengine, kuleta watu, kufanya ziara za kubadilishana uzoefu. Lakini tunapozungumza kuhusu utamaduni wa wafadhili na matarajio yao, daima naiambia timu yetu, “Angalieni mnacholeta mezani. Mna thamani kubwa sana.”
Kama timu, kama taasisi na kama watu binafsi, tuna thamani kubwa sana. Watu wanaokuja kutoka nje si lazima waweze kufanya kile tunachofanya. Tuna mitandao hii, tuna ushirikiano huu, tunawafahamu watu hawa, na tunaielewa serikali na mifumo yake. Huwezi tu kuja kutoka nje na kutarajia kwamba utaweza kufanya mambo haya mara moja.
Mongabay: Mlianza na dola 25,000 hivi. Mwambao sasa una bajeti ya kila mwaka ya takriban dola milioni 3.5. Hilo linabadilisha shirika vipi?
Ali Thani: Sasa hivi, tuna timu nzuri sana ya fedha inayohakikisha tunasimamia fedha vizuri. Lakini wafanyakazi walio nje ya timu ya fedha pia wanahitaji kuelewa jinsi ya kuzingatia sera za fedha. Tuna sera za fedha, sera za rasilimali watu, na sera nyingine.
Sidhani kama hilo ni changamoto kubwa sana kwa sasa. Kilicho muhimu zaidi ni kutekeleza sera hizo na kuhakikisha kila mtu anazifuata.
Lorna Slade: Kwangu mimi, moja ya changamoto kubwa zaidi ni kwamba siku moja Ali na mimi tutaondoka. Tunahisi kuwa na umiliki wa taasisi hii kwa sababu tumesimamia ukuaji wa taasisi hii wenyewe; tumeshiriki katika kila sehemu yake, tangu mwanzo kabisa.
Kuleta watu wengine wenye hisia hiyo hiyo ya kuona taasisi kama yao na kudumisha maadili hayo hayo ni changamoto kwa shirika lolote linalokua.
Kupata watu wenye ujuzi wa hali ya juu pia ni vigumu. Wakati mwingine tunacheka kwamba tumekuwa kama chuo cha mafunzo. Unapata vijana wenye shauku, unawafundisha, kisha wanapata kazi nzuri zaidi yenye mshahara mkubwa zaidi na kuondoka.
Hiyo ni vizuri kwao, lakini ni vigumu kwetu. Na unapokua, unahitaji kujiuliza: Je, ni wazo zuri kuendelea kukua, kufikia maeneo mengi zaidi na kuajiri watu zaidi? Unawezaje kuendelea kuboresha kile unachofanya? Huo ndio mjadala wetu wa kimkakati kwa sasa.

Mongabay: Kabla hatujazungumzia mustakabali wa Mwambao, ni mafanikio gani yanakufanya ujisikie fahari hasa?
Lorna Slade: Moja ya mafanikio hayo ni mpango wa eco-credit, kwa sababu nadhani ni jambo jipya na la kipekee. Lakini kwa upana zaidi, ni ushiriki wa jamii katika usimamizi na kuwajengea watu uwezo na kujiamini ili wajue kwamba wanaweza kufanya kazi hiyo wenyewe. Pia tumejenga heshima kutoka serikalini, ili serikali itambue kwamba jamii zinaweza kufanya hivyo.
Kwa kweli, tumewaona watu wakiwezeshwa na kuchochewa kushiriki. Nahisi wameanza kuhisi kwamba wana uwezo wa kuamua kuhusu mustakabali wao. Pia tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika namna ambavyo kamati za usimamizi wa uvuvi katika ngazi ya jamii zinafanya kazi. Kwa mfano, hapo awali hakukuwa na maelekezo mengi yaliyoandikwa kuhusu uwakilishi wa kijinsia au taratibu za uchaguzi. Tumefanya kazi na serikali kuandaa taratibu za kawaida za uendeshaji (SOPs) zinazojumuisha mambo hayo.
Sasa tunakaa meza moja na serikali na kutengeneza taratibu ambazo serikali inazikubali. Hilo pia ni mafanikio.
Eneo lingine ni mipango ya matumizi ya maeneo ya bahari katika ngazi ya jamii. Tuliunganisha mipango ya matumizi ya bahari na usimamizi wa rasilimali katika ngazi ya jamii tukafanikiwa kukutanisha idara mbalimbali za serikali kwenye meza moja. Idara za serikali wakati mwingine hufanya kazi kwa kujitegemea, bila uratibu wa kutosha.
Pia kuna shinikizo kubwa kutoka kwa uwekezaji wa utalii na miradi mingine ya maendeleo. Wakati mwingine jamii hazijui kwamba hoteli imepangwa kujengwa eneo fulani, kuna mradi mwingine unaopangwa sehemu nyingine, au kwamba eneo fulani litapangiwa matumizi maalum.
Ni pale tu unapowakutanisha watu hao wote kwenye meza moja ndipo mambo huanza kuwekwa wazi. Bado tuko mwanzoni, lakini nahisi tumesaidia kuanzisha na kuendeleza mchakato huo.
Mongabay: Tuzungumze kuhusu eco-credit. Kwa nini kuunganisha uhifadhi na namna ya watu kujikimu?
Lorna Slade: Unapofanya kazi katika mazingira ya baharini ambapo watu wanategemea mazingira hayo kwa maisha yao ya kila siku na chakula, huwezi kufanya uhifadhi bila kuzingatia wasiwasi wa watu.
Kujali watu ni jambo sahihi kufanya. Kikwazo kimoja kwa watu wanaotaka kushiriki katika biashara ni kwamba wengi huwa hawajapata mafunzo na hawana uwezo wa kupata fedha taslimu. Programu hii inafanya fedha ndogo zipatikane kwa ajili ya kuwekeza katika biashara, na inatoa mafunzo ya kuchagua biashara, kuiendesha, kupanga bajeti, na kuamua kiasi cha pesa kitakachotumika nyumbani na kiasi kitakachowekezwa tena katika biashara.
Watu wanashukuru sana mpango huo. Hilo linaonyesha kwamba tunawajali, tunajali mazingira, lakini pia tunajali maisha yao. Kuzingatia uhifadhi si jambo rahisi siku zote. Ukisema, “Panda miti mitano,” unaweza kuhesabu miti mitano. Ukisema, “Heshimu eneo hili la bahari lililofungwa,” huwezi daima kujua kama mtu analiheshimu isipokuwa tu kama unafanya doria wakati wote.
Lakini ninashangazwa na jinsi watu wanavyoukubali mpango huo. Changamoto iliyopo ni ukubwa. Tunaweza kuanza na vikundi vitano, vyenye takriban familia 150, lakini tunafanya kazi katika jamii za watu 2,000 hadi 3,000. Kuna vikundi vingine vitakavyolazimika kusubiri. Kwa hiyo, tunaangalia jinsi ya kupanuka.
Ali Thani: Mpango huo wa mikopo unaendana na utamaduni wa jamii. Watu wanavutiwa nao na wanataka zaidi, lakini Mwambao haina uwezo wa kuwafikia na kuhudumia kila mtu.
Moja ya dalili za mafanikio ni kwamba baadhi ya jamii zimeamua kuanzisha mipango kama hiyo. Walichohitaji kutoka kwetu ni maarifa tu. Hiyo ni habari njema.

Mongabay: Kwa mtazamo wako, uhifadhi unaoongozwa na jamii unamaanisha nini kwa vitendo?
Lorna Slade: Lazima kuwe na sheria na miongozo ya kitaifa. Tunaweza kutetea uwepo wa miongozo inayozingatia zaidi mahitaji ya jamii.
Lakini watu wa jamii wanajua kinachofanya kazi katika maeneo yao. Wanawajua watu wao. Wanajua nani ana uhusiano na nani. Wanajua namna wanavyotumia maeneo yao. Wanajua ni mambo gani yana madhara na yapi hayana madhara. Wanajua kwamba rasilimali zimepungua, na mara nyingi wanaelewa sababu ya kupungua huko.
Kuna maarifa mengi sana ndani ya jamii. Watu wanahitaji kuwezeshwa kuyatumia. Hii inamaanisha kuwa na uelewa wa sheria na fursa zilizopo ndani ya sheria hizo. Pia inamaanisha kutoa mafunzo na taarifa ili watu waweze kufanya maamuzi bora zaidi.
Mimi huwa ninaona kwamba utawala bora unahusu kufanya maamuzi mazuri yanayotegemea taarifa sahihi. Serikali nazo hazina rasilimali za kutosha kusimamia maeneo haya makubwa ya pwani na kufanya kila kitu kinachohitajika. Kwa hiyo, usimamizi unaoongozwa na jamii unaweza kuwa na manufaa kwa pande zote.
Mongabay: Ali, tuzungumzie kidogo kuhusu mbinu mbalimbali za utekelezaji wa sheria za uhifadhi. Umesema hukubaliani na mbinu zinazotegemea zaidi matumizi ya nguvu za kijeshi. Kwa nini?
Ali Thani: Sipendezwi na uhifadhi unaotumia mbinu za kijeshi. Ikiwa kuna tatizo, iwe ni uvuvi wa kutumia baruti, ukataji miti au jambo lingine, kwanza unahitaji kuelewa kwa nini walifanya hivyo na ni akina nani walifanya hivyo.
Unahitaji kufanya uchunguzi. Unahitaji kukusanya taarifa. Taarifa hizo zinaweza kukusaidia kushughulikia tatizo. Unapowatambua watu wanaofanya jambo lenye madhara, unaweza kuwaita na kujaribu kuwaeleza kwa nini suala hilo ni muhimu.
Hupaswi kudhani kwamba kila mtu katika jamii anafanya hivyo. Pia unaweza kupata mawazo kutoka kwa watu wenyewe kuhusu nini kifanyike ili kutatua tatizo hilo.
Si lazima kila mara wewe uwe na suluhisho. Mnaweza kutatua tatizo kwa pamoja. Lazima kuwe na sheria, lakini pia unahitaji kuwaelimisha watu kuhusu sheria hizo na kuelewa kwa nini jambo fulani linatokea.
Mongabay: Lorna, bila shaka kuna mazingira ambayo utekelezaji mkali wa sheria ni muhimu?
Lorna Slade: Bila shaka. Ukimkuta mtu akifanya uvuvi wa kutumia baruti, unahitaji kuchukua hatua madhubuti. Anapaswa kuzuiwa kwa sababu kitendo hicho kina madhara makubwa, ni kitendo cha kujinufaisha na si endelevu.
Kuna wakati ambapo unahitaji kuweka mstari na kusema, “Hili haliruhusiwi.” Lakini pia unaweza kufikiria kuhusu njia mbadala: elimu, kujifunza, shughuli za kujipatia kipato na kuongeza thamani ya bidhaa ambazo watu wanazalisha au kuvuna.
Ikiwa watu wanalipwa bei nzuri kwa bidhaa zao, si lazima wachukue rasilimali nyingi kupita kiasi. Na kama rasilimali zitasimamiwa kwa njia endelevu, kutakuwa na upatikanaji endelevu wa rasilimali hizo.

Mongabay: Je, mafanikio yanaweza kumaanisha kwamba Mwambao haitahitajika tena kwa kiwango kikubwa kwa sababu jamii zitakuwa zinasimamia rasilimali hizi zenyewe?
Lorna Slade: Kwa kiwango fulani, ndiyo. Jamii hizi zinaweza kujua kile zinachotaka kufanya. Zinaweza kuwa na mipango mizuri na mifumo mizuri ya utawala. Lakini bado fedha zinahitajika. Kwa uhalisia, sioni jinsi jamii zinaweza kuendelea kuchukua jukumu kubwa zaidi la usimamizi au serikali zitakavyoweza kupata fedha zote zinazohitajika kusimamia maeneo haya kwa ufanisi katika kipindi cha miaka 20 ijayo.
Tumesikia kuhusu mapato yanayorudishwa kwa jamii kutokana na ada za hifadhi za baharini, lakini wakati mwingine kiasi hicho kinaweza kuwa kidogo sana. Huwezi kuendesha doria nyingi au kusaidia mikutano kwa fedha hizo. Kwa hiyo, ndiyo, jamii zinaweza kuendelea kuchukua umiliki zaidi, lakini bado zinahitaji rasilimali.
Mongabay: Je, hilo linazua swali kubwa zaidi kuhusu mfumo wa Mwambao wenyewe? Je, mnapopanuka, mnahamishia rasilimali na majukumu kwa mashirika ya jamii?
Lorna Slade: Ndiyo, kabisa. Huo ndio mjadala wa kimkakati. Tunafanya kazi na mashirika na jamii ambazo tumekuwa tukishirikiana nazo kwa muda mrefu na ambazo sasa zinaweza kupanga shughuli zake zenyewe.
Labda tunapaswa kuanza kuzipatia fedha zaidi moja kwa moja, kwa lengo la kuzisaidia kufanya sehemu kubwa zaidi ya kazi zenyewe. Hapo jukumu letu litabadilika. Tutakuwa tukifuatilia, kusaidia na kuangalia uwajibikaji wa kifedha na upangaji wa bajeti.
Kwa hiyo, swali ni: Je, tunakuwa na timu ndogo yenye ujuzi wa hali ya juu inayosimamia na kugawa tena fedha kwa makundi mengine? Au tunaendelea na mfumo huu wa sasa wa kuongeza ukubwa wa timu na kwenda katika maeneo zaidi? Hilo ni jambo tunalolifikiria.
Ali Thani: Tunapata maombi kutoka maeneo mengine, yakiwemo kutoka kwa viongozi wa kisiasa na serikali, wakituomba twende kufanya kazi huko. Kwa hiyo, pia tunapaswa kuamua kama tutatumia mfumo huu katika maeneo mengine na pia muundo wa taasisi utakavyokuwa hapo baadaye.

Mongabay: Sasa mnafanya kazi kwa karibu na serikali. Mmejifunza nini kuhusu uhusiano huo?
Ali Thani: Kwa sasa, ningesema tunafanya kazi vizuri sana na serikali. Kitu tunachohitaji kuboresha ni namna tunavyoshirikiana; yaani kuwa na makubaliano rasmi, kufanya kazi pamoja na kuwa na mikutano ya mara kwa mara ya kutoa taarifa. Tunafanya kazi na serikali kuu, lakini pia na ofisi za serikali za mitaa na halmashauri za wilaya. Tunahitaji wote waelewe tunachokifanya.
Tunahitaji kuwa na mikutano ya mara kwa mara ambayo tunawasilisha kile tunachokifanya, nao wanatupatia mapendekezo na maoni. Na kwa upande wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), kazi hii si ya shirika moja. Ni ya wote. Kila mmoja anahitaji kuelewa wengine wanafanya nini. Tunahitaji kushirikishana uzoefu na wakati mwingine kugawana majukumu.
Mongabay: Lorna, kwa sasa kuna mashirika mengi zaidi ya uhifadhi yanayofanya kazi katika eneo hili. Je, hilo ni jambo zuri kwa kila hali?
Lorna Slade: Tulipoanza, hakukuwa na mashirika mengi yaliyokuwa yakifanya kile tulichokuwa tunafanya. Katika miaka ya hivi karibuni, yamejitokeza mashirika mengi yanayofanya kazi zinazofanana katika maeneo mbalimbali.
Nadhani hilo ni jambo zuri kwa sababu linaonyesha kwamba huu ni mfumo unaoweza kufanya kazi. Lakini kwa upande mwingine, hilo linaweza kugeuka kuwa ushindani wa rasilimali na ushindani wa maeneo ya kazi. Hilo ni jambo gumu.
Kwa hiyo, tunahitaji kujiuliza kila mara: Je, bado tunaongeza thamani? Tunaweza kufanya nini ili kuongeza thamani zaidi? Na kama hilo linamaanisha kubadilisha mkakati wetu, tunahitaji kuwa tayari kufanya hivyo.
Mongabay: Baada ya yote mliyoyaona, ni nini kinachowapa matumaini kuhusu mustakabali wa bahari?
Lorna Slade: Wakati mwingine ni vigumu kuwa na matumaini, ukizingatia hali ilivyo duniani kwa ujumla. Lakini lazima uwe na matumaini, la sivyo utaacha kabisa, si ndiyo? Tunaona dalili za maboresho. Tunaona dalili za usimamizi bora zaidi wa rasilimali. Kama hayo yanatosha, na kama yanatokea kwa haraka inayohitajika, siwezi kusema. Lakini hiyo haimaanishi kwamba tunapaswa kuacha kufanya chochote.
Lazima uwe na matumaini kwa watu. Lazima uwe na matumaini kuhusu mazingira na uwezo wake wa kujirekebisha na kustahimili changamoto. Lakini huwezi kuyaacha tu mambo yaende yenyewe. Lazima ufanye juhudi kadiri uwezavyo ili kujenga uwezo wa watu na mazingira kustahimili changamoto.
Ali Thani: Sina uhakika wa asilimia 100 kuhusu mustakabali wa bahari. Lakini nina matumaini kwamba uwezo wa jamii na mifumo ya ikolojia kustahimili changamoto utaendelea kuimarika kupitia juhudi za jamii zenyewe. Hapo ndipo ninapoona mustakabali unapaswa kuwa.
Picha ya bango: Waanzilishi wa Mwambao wanasema kuelewa utamaduni wa eneo husika ni muhimu katika uhifadhi. Picha kwa hisani ya Mwambao.
Mahojiano haya yalichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 2/10/2026.
Teknolojia ya kisasa yabadilisha ukulima wa mwani na kuongeza kipato cha wakulima Kenya