- Athari za mvua hizo haziishii kwenye maeneo ya nchi kavu pekee.
- Changamoto kubwa ni mtiririko wa udongo na uchafu kuelekea pwani.
- Kupotea kwa matumbawe kunaweza kuvuruga mfumo mzima wa ikolojia.
- Wananchi wapewe taarifa sahihi kwa wakati ili kuchukua hatua za tahadhari mapema.
DAR – ES – SALAM, Tanzania – Wakati Tanzania ikijiandaa kukabiliana na athari za mvua nyingi za El Niño zilizotabiriwa kuanza Oktoba, mwaka huu, tahadhari nyingi zimeelekezwa kwenye kilimo na maeneo mengine ya nchi kavu. Hata hivyo, wataalamu wa mazingira wanaonya kuwa maandalizi hayo yanapaswa pia kuzingatia mifumo ya ikolojia ya bahari, ambayo inaweza pia kuathiriwa na mvua kubwa.
Miongoni mwa maeneo yanayoweza kuwa kwenye hatari ni pamoja na matumbawe na mashamba ya mwani.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika utabiri wake ilitoa angalizo kuhusu msimu wa mvua za Vuli (Oktoba – Disemba) 2026, kuathiriwa na kiwango kikubwa cha mvua na hali ya El Nino.
Utabiri ulionyesha kuwa El Niño itasababishwa na joto la bahari kuwa juu ya wastani katika Bahari ya Pasifiki, hali inayotarajiwa kufanya ongezeko la mvua za Vuli 2026 kuwa juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Viktoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
Akizungumza utabiri huo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia Nchi (IPCC), Dkt Ladislaus Chang’a, alisema msimu wa mvua za vuli za mwaka 2026, unatarajiwa kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa, inayotarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba hadi wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba 2026.

Alifanunua kuwa kwa kawaida mvua za msimu wa Vuli huisha mwezi Disemba japo katika msimu wa mwaka 2026, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea hadi mwezi Januari 2027, na ongezeko la mvua likitarajiwa hasa katika kipindi cha mwezi Novemba 2026.
Ili kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo, Dkt Chang’a aliwahimiza wakulima kuandaa mashamba, kupanda na kutumia pembejeo kwa wakati, pamoja na kuchukua hatua za kuzuia maji kutuama, mmomonyoko wa udongo na upotevu wa rutuba.
Athari kwa ikolojia ya bahari
Licha ya tahadhari na ushauri mwingi kuelekezwa kwa wakulima kuhusu namna ya kukabiliana na athari za mvua za El Niño, wataalamu wa mazingira wanaonya kuwa athari za mvua hizo haziishii kwenye maeneo ya nchi kavu pekee. Mvua kubwa zinaweza pia kuathiri mifumo ya ikolojia ya bahari, ikiwemo matumbawe na mashamba ya mwani, kupitia ongezeko la maji baridi na matope yanayoingia baharini kutoka nchi kavu.
Emmanuel Mpina, Kaimu Meneja wa Programu ya Bahari katika shirika la The Nature Conservancy (TNC) Tanzania, anasema mvua kubwa zinazoweza kuambatana na El Niño zinaweza kuongeza mtiririko wa maji kutoka nchi kavu kwenda baharini na kuleta athari kwenye mifumo ya ikolojia ya bahari ikiwemo matumbawe na mashamba ya mwani.
Anasema athari hizo haziishii kwenye mazingira pekee, bali zinaweza pia kugusa maisha ya wavuvi wadogo, wanyakua pweza na biashara zinazotegemea utalii wa pwani.
Yusufu Issa, Meneja wa Mradi wa Sustainable Ocean Alliance (SOA) Tanzania, naye anaelezea namna mvua kubwa zinavyoweza kuathiri moja kwa moja mazingira ya bahari na sekta zinazotegemea uchumi wa bluu, ikiwemo kilimo cha mwani na afya ya matumbawe.
“Sekta ya mazingira ya bahari na uchumi wa bluu, ikiwemo kilimo cha mwani na uhai wa viumbe hai kama matumbawe, viko katika hatari kubwa zaidi ya kuathirika kutokana na mvua hizo kubwa,” alisema Issa katika mahojiano na Mongabay.

Tofauti na athari zinazoweza kuonekana moja kwa moja kwenye mashamba, Issa alisema moja ya changamoto kubwa kwa bahari ni namna maji yanavyosafirisha udongo na uchafu kutoka nchi kavu hadi maeneo ya pwani.
“Mvua nyingi zinaweza kusababisha mmomonyoko wa fukwe na kupeleka kiasi kikubwa cha udongo na tope baharini. Uchafu huo unaweza kupunguza ubora wa maji na kuvuruga mifumo ya ikolojia ya chini ya maji,’’ anasema.
Wakulima wahofia uzalishaji
Kilimo cha mwani ni miongoni mwa shughuli za kiuchumi zinazotegemewa na wananchi wa maeneo ya mwambao wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Issa, mmomonyoko wa fukwe unapoongeza, kiwango cha udongo na tope kinachoingia baharini nacho huongezeka huku huku maji yakichafuliwa na kuathiri mazingira ambayo mwani huhitaji ili kukua.
“Mmomonyoko wa fukwe unapoingiza udongo na tope baharini, maji yanakuwa machafu sana. Hali hii ya uchafuzi inaharibu ustawi wa kilimo cha mwani kwa sababu mwani huhitaji mazingira tulivu na safi ili kukua vizuri,” alisema.
Kwa wakulima wanaotegemea mwani kwa kipato cha kaya, kupungua kwa uzalishaji kunaweza kumaanisha pia kupungua kwa mapato.
Juma Hassan, mkulima wa mwani, anasema wakulima wameanza kujiandaa kufuatilia taarifa za hali ya hewa pamoja na ushauri unaotolewa na wataalamu kuhusu namna ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.
“Tunafahamu mvua kubwa, mawimbi makali na mabadiliko ya joto la bahari vinaweza kuathiri mashamba yetu ya mwani,” anasema.
Hassan anasema taarifa za mapema ni muhimu kwa wakulima kupanga muda wa kupanda na kuvuna, kuchagua maeneo salama ya kilimo na kuchukua hatua za kupunguza hasara.
“Tunaiomba Serikali na wadau wa sekta ya mwani watupatie taarifa sahihi kwa wakati, mafunzo na msaada wa kitaalamu, kwa sababu tukijua mapema kinachoweza kutokea, tutakuwa na nafasi kubwa ya kuchukua hatua za tahadhari,” anasema.
Kuungua kwa matumbawe
Mbali na mwani, matumbawe ni sehemu muhimu ya mifumo ya ikolojia ya bahari. Yanatoa maeneo ya mazalia, chakula na maficho kwa viumbe mbalimbali wa baharini.
Kwa mujibu wa Mpina, joto la maji linapozidi kiwango cha kawaida, matumbawe hupata mfadhaiko na yanaweza kupoteza rangi kupitia mchakato unaojulikana kama kuungua kwa matumbawe, au coral bleaching. Katika hali kali, yanaweza kufa.
“Kupotea kwa matumbawe kunaweza kuvuruga mfumo mzima wa ikolojia kwa sababu viumbe wengi hutegemea miamba hiyo kwa chakula, makazi na kuzaliana,’’ anasema.
Kwa upande wa Issa, mabadiliko ya joto yanaweza pia kusababisha baadhi ya viumbe wa baharini kuhama kutoka maeneo yao ya kawaida, jambo linaloweza kubadilisha usambazaji wa viumbe na mahusiano yao ndani ya mfumo wa ikolojia.
“Matumbawe ndio yanayotajwa kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupotea kabisa kutokana na athari za El Niño,” alisema Issa.
Maandalizi kabla ya mvua
Issa anasema hatua za kudhibiti mmomonyoko wa udongo zinapaswa kuchukuliwa kabla ya mvua kubwa kuanza ili kupunguza kiwango cha udongo na uchafu unaofika baharini.
“Kuna haja ya kuwepo kwa mikakati madhubuti ya kudhibiti mmomonyoko wa udongo kwenye fukwe kabla na wakati wa mvua hizi ili kulinda rasilimali za bahari ambazo ni nguzo muhimu ya utalii na uvuvi nchini,” anasema.
TMA pia imewashauri wakulima kuimarisha miundombinu ya kilimo, kuvuna maji ya mvua na kudhibiti visumbufu vya mimea ili kupunguza athari za mvua nyingi na kuongeza uzalishaji.
Picha ya bango: Wakulima wa mwani wakipakia mwani kwenye mashua huko Pemba, Tanzania. Mwani ni moja ya mazao ambao huenda yakaathiriwa na mvua nyingi zilizotabiriwa kuanza Oktoba 2026.