- Wakazi wa Lamu wameandamana wakitaka serikali kuweka wazi suala la fidia na kuwashirikisha katika mradi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote.
- Salim Tima Swale na walalamikaji wengine 132 wamewasilisha kesi kuhusu ardhi yenye nambari L.R. 13061, wakipinga shughuli katika eneo hilo wakati shauri lao likisubiri kusikilizwa na kuamuliwa.
- Mahakama imeagiza hali ilivyo sasa katika L.R. No. 13061 idumishwe hadi Oktoba 14, 2026, lakini amri hiyo haikusitisha hafla ya kuanza ujenzi wa kiwanda hicho.
- Kiwanda hicho kinapangwa kuwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku na, kwa mujibu wa taarifa za awali za mradi, kinatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu.
LAMU, Kenya – Wakazi wa Lamu wameandamana wakitaka serikali isimamishe shughuli katika ardhi inayotengewa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote hadi suala la fidia na ushirikishwaji wao katika mradi huo lishughulikiwe. Haya yalijiri siku moja kabla ya Rais William Ruto kuongoza hafla ya kuanza ujenzi wa mradi huo unaokadiriwa kugharimu takriban Sh2.2 trilioni (karibu dola bilioni 16), kulingana na ripoti za hivi karibuni.
Waandamanaji walikuwa na mabango wakitaka serikali kuweka wazi suala la fidia ya ardhi zao na kuhusishwa kikamilifu katika mradi huo. Walitawanywa na maafisa wa polisi waliotumia vitoa machozi.
Mkurugenzi wa Shirika la Muhuri, Khalefu Khalifa, aliiambia Mongabay kuwa lengo lao halikuwa kupinga mradi huo, ila waliitaka serikali kuweka wazi suala la fidia za ardhi ya walioathirika na mradi huo.
Seneta Shakila Abdalla, akijumuika na waandamanaji, alisema kuwa baadhi ya viongozi ambao si wa kuchaguliwa hawakuhusishwa katika mradi huo.

“Hata sisi kama viongozi hatuna ufahamu. Huo mkutano uliowekwa ulihusisha viongozi waliochaguliwa pekee. Twasikia tu kuna hafla ya kuanza ujenzi. Hafla hiyo pekee si muhimu, maana mradi unaweza kuanzishwa lakini usiendelee. Serikali ilifaa kuhusisha kila mmoja. Na ikiwa utakuwa unafanyika tuna haki ya kulilia haki zetu,” alisema Shakila.
Mwanaharakati Mohammed Skandi alisisitiza kuwa ni sharti kuwe na ushirikishwaji. “Serikali na wawekezaji hawajahusisha wakazi wa eneo hilo. Hawajaambiwa ni wapi watakwenda, watalipwaje fidia, na ni wazi ardhi hizo ni za wakulima na wafugaji ambao hawana jawabu katika suala hilo,” alisema Mohammed.
Kesi yafunguliwa mahakamani
Maandamano hayo yalijiri siku moja baada Salim Tima Swale na walalamikaji wengine 132 kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Malindi wakitaka shughuli katika kipande hicho cha ardhi yenye mgogoro zisimamishwe wakati ombi lao likisubiri kusikilizwa na kuamuliwa.
Wakazi hao wa eeneo la Hindi, Manda na Magogoni wanadai kuwa ingawa hawana hatimiliki za ardhi hiyo, wamekuwa wakiitumia kwa kilimo na ufugaji kwa miongo kadhaa, huku pia wakijenga misikiti na makazi katika eneo hilo.
Mahakama haikusitisha mradi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote. Badala yake,Jaji Jane Onyango alliamuru wahusika kudumisha hali ilivyo sasa katika ardhi yenye nambari L.R. 13061 hadi Oktoba 14, 2026, wakati shauri hilo litakaposikilizwa. Amri hiyo haikusitisha hafla iliyopangwa ya kuanza ujenzi, ingawa shughuli katika eneo la mradi zinaweza kuathiriwa wakati mahakama ikiendelea kusikiliza shauri hilo.
Kampuni ya Dangote, inayohusishwa na bilionea wa Afrika Aliko Dangote, katika taarifa yake, imesema kuwa mahakama haikusitisha uzinduzi wa ujenzi, ila shughuli katika eneo la ujenzi huenda zikaathirika na uamuzi wa Mahakama hadi kesi itakaposikilizwa.
Akinukuliwa na Reuters akiwa katika mkutano wa wawekezaji jijini Nairobi (Septemba 28), Dangote alionesha imani kuwa kiwanda hicho kitajengwa licha ya upinzani, akisema kuwa hayo ni mambo ya kawaida.
Meli iliyobeba vifaa vya ujenzi yawasili
Septemba 26, meli MV Da Yang Bai He ya vifaa vya ujenzi wa kiwanda hicho ilitia nanga katika bandari ya Lamu. Meli hiyo ilitoka Uchina.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KAA) William Ruto, alipokea meli hiyo ambayo ilibeba shehena ya vifaa vya uzito wa tani 2,930.29. Alisema ujenzi wa kiwanda hicho ni hatua kubwa katika kuonesha uwezo wake wa kupokea meli kubwa na pia ukanda wa LAPSSET.
Kiwanda hicho kitasafisha mafuta ghafi kutoka Lokichar, Kaunti ya Turkana, pamoja na mafuta ghafi kutoka mataifa mengine ya Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika na kwingineko, kabla ya kusambaza bidhaa za mafuta zilizosafishwa katika masoko ya kanda hiyo.
Rais aonya wanaopinga ujenzi wa kiwanda
Akiwa katika ziara ya Ukanda wa Pwani, Rais Ruto alionya wanaopanga kuvuruga mafanikio ya ujenzi wa kiwanda hicho cha kusafisha mafuta cha Dangote, akisisitiza kuwa kiwanda hicho kitaimarisha uchumi, pamoja na kuzalisha kawi ya umeme na pia kutoa nafasi za ajira kwa zaidi ya vijana elfu 60.
“Nawasikia hapo wakisema wanaunga mkono Dangote, lakin ni wao ndio wanafadhili kesi za mahakamani kwa sababu hamjapata mnachotaka. Sitakubali mudhoofishe uwekezaji katika nchi hii. Imetosha,” alisema Ruto akiwa mjini Kilifi.
Rais Ruto ataongoza viongozi wengine 14 wa mataifa ya Afrika katika hafla hiyo ya uzinduzi wa ujenzi wa kiwanda hicho kesho mnamo Septemba 30.
Kuhusu kiwanda
Katika ripoti iliyochapishwa na Reuters, Makamu Rais wa Kitengo cha Mafuta na Gesi wa Dangote Industries Limited Edwin Devakumar alithibitisha kuwa kiwanda hicho chenye uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku kitajengwa katika Kisiwa cha Lamu na kinatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu.
Iwapo mradi huo utakamilika, utafuata mfano wa kiwanda cha Dangote kilichopo karibu na Lagos, Nigeria, chenye uwezo wa kusafisha mapipa 650,000 kwa siku, na ambacho kilianza uzalishaji mwaka 2024 na ndicho kikubwa zaidi barani Afrika.
Picha ya bango: Wakazi wa lamu waandamana kupinga mradi wa usafishaji wa mafuta katika Kaunti ya Lamu, Kenya. Picha na Amina Chombo, Mongabay.
Uwekezaji zaidi wa Dangote Tanzania: Watalaamu wataka matumizi endelevu ya raslimali yazingatiwe