- Maofisa wa Uhifadhi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na wananchi, washiriki kuudhibiti.
- TANAPA inaendelea na uchunguzi wa chanzo cha moto huo.
- Taarifa ya TANAPA inasema shughuli za utalii katika mlima huo zinaendelea.
Moto umeibuka leo, Jumatatu, Septemba 28 katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, ikiwa ni wiki chache baada ya moto mwingine mkubwa ulioteketeza zaidi ya hekta 1,800 za uoto wa asili katika eneo la Kikelelwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), moto huo umeanza alfajiri, katika eneo la Sangarini, karibu na Kamwanga kuelekea Shira Plateau, upande mwa magharibi wa mlima.
TANAPA imesema timu inayojumuisha maofisa wa uhifadhi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, wadau wa utalii na wananchi imepelekwa katika eneo hilo kwa ajili ya kudhibiti moto.
Chanzo cha moto
Hata hivyo, mamlaka hiyo imesema chanzo cha moto bado hakijajulikana na uchunguzi unaendelea. “Chanzo cha moto bado hakijajulikana,” TANAPA inasema katika taarifa yake kwa umma.
Moto huo umetokea ikiwa ni takribani wiki tatu baada ya moto ulioripotiwa Septemba 3 katika eneo la Kikelelwa, karibu na mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro na Wilaya ya Rombo.
Moto huo uliendelea kwa karibu wiki mbili na, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Serikali, uliathiri zaidi ya hekta 1,800 za uoto.
Katika juhudi za kuudhibiti, TANAPA ilishirikiana na taasisi nyingine za serikali, wadau wa utalii na wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka mlima.
Upepo na hali ya ukavu katika maeneo ya juu ya mlima vilifanya udhibiti wa moto kuwa changamoto.
Shughuli za utalii zinaendelea
TANAPA imesema katika taarifa yake kwa umma kuwa shughuli za utalii katika mlima huo zinaendelea na kwamba usalama wa watalii na wafanyakazi umepewa kipaumbele.

Moto wa mwanzoni mwa Septemba mwaka huu, haukuwa tukio la kwanza la moto katika mlima huo.
Mwaka 2023, moto uliripotiwa katika maeneo ya juu ya mlima na kuathiri uoto wa asili katika eneo la Indonet – Rongai, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TANAPA.
Aidha, mwaka 2022, mlima huo ulikumbwa na mfululizo wa moto katika maeneo kadhaa, yakiwemo Udetu, Samanga, Karanga River, Umbwe, Baranko na sehemu za njia ya Marangu. Taarifa zilizotolewa wakati huo ziliripoti zaidi ya kilomita za mraba 34 za uoto kuathirika.
Lakini miongoni mwa matukio makubwa zaidi ya miaka ya hivi karibuni ni moto wa Oktoba 2020. Moto huo ulianza katika eneo la Whona na kuendelea kwa siku kadhaa. TANAPA ilikadiria baadaye kuwa takribani kilomita za mraba 95.5 za uoto ziliathirika.
Ukubwa kamili wa eneo lililoathiriwa na moto uliotokea Septemba 28, haujatangazwa.
TANAPA imesema kuwa inaendelea na operesheni ya kuudhibiti moto huo, huku uchunguzi wa chanzo ukiendelea.
Picha ya bango: Moto ukiwaka juu ya Mlima Kilimanjaro Septemba 3, 2026 kabla ya kudhibitiwa. Picha kwa Hisani ya TANAPA.
Mbinu za jadi za kutumia moto zaweza kusaidia kuzuia majanga ya moto katika maeneo ya malisho Kenya