- Polisi wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini na kuwakamata waliohusika.
- Wahifadhi hao walikuwa kwenye operesheni ya kukamata mifugo iliyodaiwa kuingizwa hifadhini.
- Uchunguzi wa awali unaonyesha uwezekano wa wanyama hao kufa kutokana na sumu.
- NCAA imeanzisha uchunguzi wa kitaalamu kubaini chanzo cha vifo hivyo.
TABORA, Tanzania – Watu sita wakiwemo wanaojihusisha na uhifadhi wameuawa na wengine watano kujeruhiwa baada ya kambi ya operesheni kuvamiwa na kundi linalodaiwa kuwa la wafugaji katika kijiji cha Ipole, Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.
Katika tukio hilo, silaha moja aina ya AK-47 na gari aina ya Toyota Land Cruiser, lenye namba za usajili T 623 EAV, vilichomwa.
Kamanda wa Polisi katika mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Twaha Juma Lulengelule, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo mwishoni mwa wiki na kusema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini na kuwakamata waliohusika.

Waliouawa ni askari wa wanyamapori wa vijiji (VGS) na askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA). Wametajwa kuwa ni VGS Daniel Mshama, mkazi wa Itimile; VGS Robert Charles Msabaha (36), mkazi wa Ipole; Gift Eliyaika (24), mkazi wa Inyonga; Ofisa wa Wanyamapori aitwaye Praygod Lyalo (38), mkazi wa Majengo; James Maganga (35), mkazi wa Ipole; na dereva Mathew Damas (35), mkazi wa Ipole.
Waliojeruhiwa ni VGS Andrew Charles (35), mkazi wa Ipole; VGS Edison Kafupa (33), mkazi wa Ipole; VGS Victor Mengo (26), mkazi wa Ipole; na askari wa TAWA Joseph Mwaipola (43), mkazi wa Inyonga. Mjeruhi mwingine jina lake halikuwekwa wazi katika taarifa iliyopo.
Kwa mujibu wa maelezo ya awali, tukio hilo lilitokea wakati askari wa TAWA na walinzi wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Ipole (JUHIWAI) wakiendesha operesheni ya kukamata na kuweka kwenye uzio mifugo iliyodaiwa kuingizwa hifadhini.
Inadaiwa kuwa kundi la wafugaji lilifika kambini usiku wa manane likitaka kuchukua mifugo iliyokamatwa, kabla ya kuzuka kwa mashambulizi yaliyotumia silaha za jadi.
“Jeshi la Polisi mkoa wa Tabora linaendesha uchunguzi ili kuhakikisha waliohusika wanakamatwa ili hatua nyingine za kisheria zichukuliwe,” Lulengelule alisema. Kamanda huyo amewataka wafugaji kutochukua sheria mikononi na kufuata taratibu zinazowekwa na sheria katika kushughulikia migogoro ya mifugo na maeneo ya uhifadhi.
Simba 10 wauawa Ndutu, Ngorongoro
Wakati uchunguzi wa tukio la Ipole ukiendelea, upande mwingine wa Tanzania, eneo la Ndutu, ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kumeibuka athari za uhusiano kati ya binadamu na wanyamapori.

Simba 10 wameuawa katika eneo la Ndutu, Kata ya Endulen. NCAA imeanzisha uchunguzi wa kitaalamu kubaini chanzo cha vifo hivyo.
Kaimu Meneja wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma wa NCAA, Hamis Dambaya, amesema simba hao waliuawa Septemba 18, 2026, na uchunguzi wa awali unaonyesha uwezekano wa wanyama hao kufa kutokana na sumu.
Dambaya amesema mamlaka hiyo imeanzisha uchunguzi wa kisayansi ili kubaini chanzo vifo hivo, na kama sumu ilitumika katika tukio hilo. Hadi sasa, NCAA haijataja aina ya sumu iliyohusika, wala haijamtaja mtu au kundi lolote lililohusika na vifo hivyo.

Matukio ya Ipole na Ndutu ni tofauti, lakini yote yanaonyesha changamoto zinazoweza kujitokeza katika uhusiano kati ya uhifadhi, jamii na wanyamapori. Tukio la Ipole limehusisha mauaji ya wahifadhi na madai ya wafugaji kuvamia kambi ya operesheni baada ya mifugo yao kukamatwa.
Kwingineko Ndutu, mamlaka inachunguza vifo vya simba 10 katika mazingira yanayodhaniwa kuhusisha sumu.
Picha ya Bango: Mabaki ya simba waliokufa yakiwa yamechomwa na askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro. Picha na Dotto Kadoshi.
Washukiwa wanne wakamatwa kuhusiana na vifo vya tembo 18 katika mfumo wa ikolojia wa Amboseli