- Upungufu wa samaki unahusishwa na uvuvi wa jadi pamoja na uchafuzi wa ziwa.
- Ufugaji wa samaki kwa vizimba utaongeza uzalishaji wa samaki na kulinda mazingira.
- Uvuvi wa kienyeji katika maeneo oevu utapungua au kutoweka.
Katika alfajiri yenye upepo baridi kutoka Ziwa Victoria, mwalo wa Kabindi, ulioko kata ya Kashenye, wilaya ya Missenyi, John John, mvuvi anayetegemea nyavu za asili pekee, anarejea nyumbani akiwa amebeba mtungo mmoja wenye samaki wanne aina ya sangara, mbali na wale aliowauza mwaloni, na kuweka kibindoni shilingi 50,000 tu. Anasonya, akikumbuka huko nyuma alikuwa akijipatia burungutu la fedha na kitoweo cha kutosha, kabla ya samaki kuadimika ziwani.
Kupungua kwa samaki katika Ziwa Victoria kunahusishwa na mambo mbalimbali, ikiwemo uvuvi wa jadi usiokuwa na zana bora na uchafuzi wa ziwa. Hali hiyo imeathiri mapato ya wavuvi na kuwafanya watafute njia mbadala za uzalishaji wa samaki.
Uvugaji kwa vizimba kama fursa
Katika mazingira hayo, ufugaji wa samaki kwa vizimba umeibuliwa kama fursa ya kuongeza uzalishaji wa samaki, huku maandalizi ya eneo na utunzaji wa mazingira ya ziwa yakiwa sehemu muhimu kabla ya mradi kuanza.
Florent Kyombo, Mbunge wa Jimbo la Missenyi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tanzania (TAMISEMI), anazungumzia umuhimu wa maandalizi kabla ya kuanza kwa mradi, na pia umuhimu wa utunzaji mazingira ya ziwa Victoria.

“Ni muhimu kuchagua eneo lenye maji safi yenye oksijeni ya kutosha, yasiyo na uchafu, yenye kina cha kutosha na ambako hakuna mawimbi makali. Pia eneo linapaswa kuwa salama dhidi ya wavuvi haramu na lisilotumiwa sana nan vyombo vya majini,’’ anasema Kyombo.
Akiongea na Mongabay wakati alipotembelea eneo linaloandaliwa kwa ajili ya mradi huo wa samaki kwa vizimba, Kyombo alisema kuwa utunzaji wa mazingira ya ziwa Victoria ni jambo muhimu kwa uvuvi endelevu, na akawahimiza wenye vizimba vilivyo tayari, na wale wanaoendelea kuviandaa kuhakikisha wanazingatia utunzaji wa mazingira.
“Kwa kuwa ufugaji huu wa vizimba unaendeshwa na watu binafsi na vikundi vya vijana, haitakuwa rahisi kwa wavuvi haramu wanaotumia sumu au nyavu zisizoruhusiwa, kwani kila mmoja atakuwa mlinzi wa ziwa, na hivyo kuiongezea nguvu kamati ya ulinzi wa ziwa (BMU),’’ alisema Kyombo.
Vizimba kupunguza ufugaji wa kienyeji
Amesema kuwa iwapo ufugaji wa samaki kwa vizimba utaongezeka, uvuvi wa kienyeji katika maeneo oevu au matingatinga, ambayo ni machujio ya maji,utapungua au kutoweka, na hivyo kusaidia kulinda maeneo hayo.

Aidha, amewahimiza wafugaji kutonunua kiholela chakula cha samaki kisicho na ithibati, kwani kinaweza kuathiri ukuaji wa samaki, na mabaki ya chakula yanayoanguka majini yakichangia uchafuzi wa ziwa.
Kwa mujibu wa Kyombo, eneo lililobainishwa na kupimwa linaanzia mwalo wa Kabindi, ulioko mpakani mwa Tanzania na Uganda, katika kata ya Kashenye, likielekea Bushago, Kigarama katika kata ya Kanyigo na kuambaa kuelekea kata ya Ishozi. Eneo hilo lina kina cha maji kinachozidi mita tano na linakidhi vigezo vilivyowekwa.
Diwani wa kata ya Kashenye, Domitian Nshekanabo, ambaye pia ni mfugaji mwenye vizimba, amesema amekuwa akiwahimiza wavuvi, hasa wale wanaovua kandokando ya ziwa na kuchoropoa ardhi ili kuweka mitego yao, akiwaasa kujiunga na vikundi vya uvuvi wa vizimba, ili kulinda mazingira ya ziwa.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa Nshekanabo, inaweza kusaidia kupunguza shughuli za uvuvi zinazohusisha kuchoropoa ardhi kandokando ya ziwa kwa ajili ya kuweka mitego, na hivyo kupunguza uharibifu wa maeneo hayo. Kujiunga na vikundi vya ufugaji wa samaki kwa vizimba pia kunaweza kuwapa wavuvi njia mbadala ya kupata kipato bila kutegemea shughuli zinazoweza kuathiri maeneo ya kandokando ya ziwa.
Vyakula vyenye kemikali
Primitiva Pastory, Afisa Mazingira wa Mkoa wa Kagera, anasema wafugaji wa samaki kwa vizimba wana wajibu wa kutunza usafi wa ziwa kwa kuhakikisha hawaingizi ziwani vyakula vyenye kemikali. Amesema suala hilo limekuwa likizingatiwa, huku vikundi vya ulinzi wa ziwa (BMU) vikipatiwa mafunzo na kufuatilia suala hilo.
Kwa mujibu wa Pastory, takriban asilimia 70 ya ufugaji wa samaki unategemea vyakula vinavyotengenezwa na binadamu. Amesema endapo vyakula hivyo si salama, vinaweza kuhatarisha si samaki wanaofugwa pekee, bali pia samaki wasiofugwa na viumbe wengine wa majini.Pastory pia amezungumzia usafi wa ziwa akisisitiza wajibu wa wadau mbalimbali katika hilo.

”Usafi wa ziwa si jukumu la wavuvi pekee, bali watu wengine wakiwemo wakulima ambao wanapaswa kuhakikisha hawalimi kwenye vyanzo vya maji wala kutiririsha kemikali kuelekea ziwani wanapotumia mbolea na dawa za kuua wadudu,’’ amesema Pastory.
Pia amesisitiza kuendelea kupiga vita uvuvi haramu wa kutumia sumu ili kudumisha uvuvi endelevu.
Ripoti ya Utafiti wa wataalamu katika Ziwa Victoria, “Environment Impact of Cage Culture in Lake Victoria (Shirati Bay)’’ ilibainisha kuwa ufugaji wa samaki kwa vizimba unaweza kuwa na athari hasi kwa mazingira iwapo usafi wa ziwa hautazingatiwa na wafugaji.
Matumaini mapya
Kwa wavuvi kama John, kupungua kwa samaki katika ziwa kumeathiri maisha na kipato. Hata hivyo, fursa ya ufugaji wa samaki kwa vizimba imeanza kuleta matumaini ya kupata njia nyingine ya kujipatia kipato.
Renatha Jovan, anayemiliki mtumbwi wa uvuvi mwalo wa Kabindi, amesema angependa kujiunga na mradi huo, lakini ana wasiwasi kuhusu usalama wa vizimba kutokana na taarifa za samaki kuibwa katika maeneo mengine.
Godfrey Nzimara, mvuvi na mwekezaji katika ufugaji wa samaki kwa vizimba, amesema uzoefu wake umempa matumaini na yuko tayari kutoa elimu kwa wavuvi wa mwalo wa Kabindi.
Kwa John na wavuvi wengine, ule mtungo mmoja wa samaki, anaona siyo tu samaki, bali njia mpya ya kuishi; kwa mara ya kwanza tangu samaki walipoanza kupungua, anaona vizimba kama njia itakayoweza kumkomboa mvuvi.
Picha ya bango: Mbunge wa Jimbo la Missenyi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tanzania (TAMISEMI), Florent Kyombo, na wataalam wakikagua kizimba ambacho tayari kimeanza ufugaji wa samaki. Picha kwa hisani ya ofisi ya mbunge.