- Vijana watambuliwe kama wabunifu, watafiti na viongozi wa uchumi wa kijani.
- Serikali, sekta binafsi na taasisi za fedha ziweke mazingira wezeshi kwa vijana.
- Uendelevu wa mazingira haupaswi kuonekana kama jukumu la kutekeleza matakwa ya sheria pekee.
DAR-ES-ALAAM, Tanzania – Vijana wametakiwa kutumia changamoto za mabadiliko ya tabianchi kama fursa ya kujiajiri, kuanzisha biashara na kubuni suluhisho zitakazochochea ukuaji wa uchumi wa kijani nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Tanzania Green Summit 2026, wenye kaulimbiu “Turning Climate Action into Opportunity” (Kugeuza Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Kuwa Fursa).

Masauni amesema vijana hawapaswi kutazamwa kama wanufaika pekee wa programu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, bali wanapaswa kutambuliwa kama wabunifu, wajasiriamali, watafiti na viongozi wa uchumi wa kijani.
“Vijana wanapaswa kutambuliwa kama wabunifu, wajasiriamali, watafiti na viongozi wa uchumi wa kijani, na si wanufaika pekee wa programu za tabianchi,” amesema.
Mhandisi Masauni ametoa wito kwa Serikali, sekta binafsi na taasisi za fedha kuweka mazingira yatakayowawezesha vijana kuanzisha na kukuza biashara zinazozingatia utunzaji wa mazingira.
Hatua katika agenda ya mazingira
Kwa mujibu wa Masauni, Tanzania imeendelea kuchukua hatua katika agenda ya mazingira na tabianchi, ikiwemo kuwa mwenyeji wa Kituo cha Afrika cha Vijana cha Mafunzo ya Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na Ofisi ya Kikanda ya Santiago Network on Loss and Damage, inayolenga kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Richard Muyungi, amesema nchi inaendelea kutumia fursa zinazotokana na mifuko ya kimataifa ya mazingira na tabianchi, huku akitaja pia miradi ya biashara ya kaboni inayoratibiwa kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC).
Muyungi amesema fursa hizo zinapaswa kuendelezwa kwa kuhakikisha mazingira yanalindwa, thamani inaongezwa ndani ya nchi, teknolojia inahamishwa na ajira zinatengenezwa kwa Watanzania.
Amewataka wawekezaji na taasisi za fedha kubuni mifumo ya fedha itakayowezesha biashara za kijani na miradi inayostahimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Uendelevu wa mazingira
Alisema uendelevu wa mazingira haupaswi kuonekana kama jukumu la kutekeleza matakwa ya sheria pekee, bali kama fursa ya kujenga thamani ya kiuchumi ya muda mrefu.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Tanzania Green Summit na Mkurugenzi wa Green Foundation, Redemptus Caesar, amesema jukwaa hilo limeundwa si kuwa sehemu ya kukutana na kubadilishana mawazo tu, bali kuwa kiungo cha kuwawezesha wadau kuona na kutumia fursa zilizopo katika sekta ya mazingira na uchumi wa kijani.
Caesar amesema washiriki watapata fursa ya kufanya mazungumzo ya kibiashara kupitia “Deal Rooms”, zitakazowaunganisha moja kwa moja na wadau wenye fursa mbalimbali za uwekezaji na ubia.
Picha ya bango: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni(katikati) akiwa katika Mkutano wa Tanzania Green Summit ambapo alikuwa mgeni rasmi, unaofanyika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Septemba15, 2026.