- Mabadiliko ya tabianchi yasitazamwe kama suala la mazingira pekee.
- Changamoto za mabadiliko ya tabianchi zigeuzwe fursa za uwekezaji katika uchumi wa kijani.
- Biashara ya kaboni ni kiungo kati ya uhifadhi wa mazingira na uchumi.
Tanzania imepanga kutumia hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama kichocheo cha uwekezaji, biashara na ajira, huku ikisisitiza ushiriki wa vijana katika uchumi unaozingatia utunzajii wa mazingira.
Mtazamo huo umeibuliwa katika Tanzania Green Summit 2026, inayofanyika jijini Dar es Salaam ikiwakutanisha zaidi ya washiriki 900 kutoka mataifa mbalimbali, wakiwemo viongozi wa Serikali, wawekezaji, taasisi za fedha, sekta binafsi, wataalamu, washirika wa maendeleo na vijana.
Mkutano huo wenye kaulimbiu “Turning Climate Action into Opportunity” kwa Kiswahili ikimaanisha, “Kugeuza Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kuwa Fursa’’, unalenga kuangalia namna hatua za ulinzi wa mazingira zinavyoweza kwenda zaidi ya kupunguza athari za tabianchi na kuwa chanzo cha fursa za kiuchumi.
Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Yusuf amesema mabadiliko ya tabianchi hayawezi tena kutazamwa kama suala la mazingira pekee, kwa kuwa yana uhusiano wa moja kwa moja na maendeleo ya uchumi.

Mabadiliko ya tabianchi
“Mabadiliko ya tabianchi si changamoto ya kimazingira pekee; ni pamoja na masuala ya maendeleo ya kiuchumi,” amesema Waziri Masauni.
Ameongeza kuwa changamoto hiyo inapaswa kugeuzwa kuwa fursa za uwekezaji katika uchumi wa kijani, ajira, ubunifu, nishati safi, kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, utalii endelevu, usimamizi wa taka na suluhisho zinazotegemea mifumo ya asili.
Badala ya mijadala ya sera pekee, Tanzania Green Summit, inaunganisha majadiliano kuhusu fedha za kijani, uwekezaji, biashara , ubunifu wa vijana, nishati jadidifu, masoko ya kaboni, usafiri wa umeme, uchumi wa mzunguko, kilimo endelevu na ajira za kijani.
Sehemu ya mkutano huo, inayojulikana kama Deals Room, inawakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji katika majadiliano kuhusu masoko ya kaboni, biashara za kijani na usafiri wa umeme.
Kikao kingine kinajadili namna Tanzania inavyoweza kubadili mipango yake ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuwa miradi inayoweza kufadhiliwa na kuvutia mitaji kutoka taasisi za fedha na wawekezaji binafsi.
Vijana kama injini ya uchumi wa kijani
Kuhusu vijana, Masauni amesema vijana hawapaswi kuonekana kama wanufaika wa programu za tabianchi pekee, bali kama wabunifu, wajasiriamali, watafiti na viongozi wa uchumi wa kijani.
Amesema wanahitaji kuunganishwa na ujuzi, teknolojia, mitaji, ushauri wa kitaalamu na masoko ili hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ziweze kuwapatia ajira na fursa za biashara.
Biashara ya kaboni ni eneo jingine ambalo Serikali inaliona kama kiungo kati ya uhifadhi wa mazingira na uchumi.
Masauni amesema Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) tayari kimesajili miradi 117 ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Amesema fursa hizi zinaweza kusaidia kuunganisha juhudi za kupunguza hewa ukaa na uwekezaji katika miradi ya mazingira.
“Lakini kadiri soko hilo linavyokua, umuhimu wa usimamizi wa miradi hiyo unakuwa mkubwa ili kuhakikisha shughuli zinazolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinaendana na ulinzi wa mazingira na maslahi ya jamii,’’ amesema.
Nishati safi ya kupikia
Katika sekta ya nishati, Tanzania imeweka lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Masauni amesema Tanzania pia imeongeza uwezo wake wa kuzalisha umeme baada ya kuanza kufanya kazi kwa mradi wa Julius Nyerere Hydropower wenye uwezo wa megawati 2,115.
Kwa mujibu wa Waziri, mradi huo umeongeza zaidi ya mara mbili uwezo wa Tanzania wa kuzalisha umeme, na hivyo kutoa msingi wa nishati kwa maendeleo ya viwanda.
Kwa upande wake Mkururenzi wa benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, taasisi hiyo inaendesha programu kubwa ya ugharamiaji endelevu na kijani (Green Financing) inayogharimu Sh bilioni 600 kupitia mkakati wake wa miaka mitano wa ukusanyaji mitaji.
Programu hii inajumuisha Mpango wa Dhamana za Kijani, Kijamii na Endelevu wenye thamani ya Sh bilioni 780 ($300 milioni) uliopitishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).
Kitovu cha majadiliano
Tanzania Green Summit imeweka fedha za kijani katika kitovu cha majadiliano yake, huku wadau wakitafuta namna ya kufanya miradi ya mazingira iweze kufikia vigezo vya ufadhili na kuvutia wawekezaji.
Masauni amezitaka taasisi za fedha na sekta binafsi kuchukua nafasi kubwa zaidi katika mageuzi ya uchumi wa kijani kwa kubuni mifumo ya fedha inayoweza kusaidia biashara za kijani na miradi inayostahimili mabadiliko ya tabianchi.
“Hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinahitaji mitaji, na maendeleo endelevu yanahitaji uwekezaji,” amesema.
Mwenyekiti, Tanzania Green Summit, Redemptus Caesar, amewashukuru wadau wa sekta ya mazingira na biashara kwa kujitokeza kushiriki katika mkutano.

Amesema mkutano huo unalenga kuangazia fursa za kibiashara zinazopatikana katika sekta ya mazingira, akisisitiza kuwa mazingira ni sekta yenye uwezo mkubwa kiuchumi na inayobeba fursa nyingi za biashara.
“Bado baadhi ya watu wamekuwa wakitazama mazingira zaidi kama eneo la uhifadhi na si kama sekta yenye fursa za kibiashara na faida,”amesema.
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Susan Ngongi Namondo, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa, amesema Tanzania ipo katika wakati muhimu wa safari yake ya maendeleo, huku ikitengeneza na kutekeleza mikakati ya kuhakikisha maendeleo yanakuwa shirikishi na yanawanufaisha wananchi wengi.
Amesisitiza umuhimu wa kuwa na majukwaa yanayowakutanisha wadau mbalimbali ili kujadili fursa, kujenga ushirikiano na kuhakikisha mazingira yanakuwa sehemu ya juhudi za kukuza maendeleo endelevu.
Picha ya bango: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Tanzania Green Summit unaofanyika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Picha na Chimba Jerry.