- Ilidaiwa eneo ambalo makosa yalitendeka liko Kongo na si Tanzania.
- Utata kuhusu eneo la tukio uliathiri uhalali wa kukiri kwa washtakiwa.
- Upande wa mashtaka haukuonyesha sifa zilizofanya nyavu kuwa haramu.
- Kwa kosa la kuwa Tanzania bila nyaraka, mazingira hayakuonyesha kama walikuwa nchini.
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, imefuta hukumu na adhabu dhidi ya wavuvi watatu raia wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) waliopatikana na hatia ya kuvua bila leseni na kukiuka sheria za uhamiaji, baada ya kubaini utata kuhusu eneo ambalo makosa hayo yalidaiwa kutendeka.
Uamuzi huo umetolewa katika rufaa ya kesi ya jinai namba 62 ya mwaka 2026. Washitakiwa katika kesi hiyo iliyosikilizwa mbele ya Jaji Thadeo Mwenempazi ni Godson Chilambe, Kalunga Kandulwe na Francois Katuta wa Katuta ndhidi ya Jamhuri.
Wavuvi hao walihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Nkasi, Namanyere, baada ya kukiri mashitaka yaliyohusishwa na tukio la Desemba 4, 2025 katika eneo la Kalubamba, Wilaya ya Nkasi mkoni Rukwa.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, mashitaka dhidi yao yalihusisha kuvua bila leseni halali, huku Godson Chilambe akikabiliwa pia na shitaka la kumiliki nyavu kinyume cha sheria. Wote watatu pia walishitakiwa kwa kuwa nchini Tanzania bila nyaraka halali za kuwaruhusu kuingia au kuishi nchini.
Ushahidi wa Jamhuri
Ilidaiwa na upande wa Jamhuri kuwa Polisi wa Tanzania waliokuwa kwenye doria katika Ziwa Tanganyika waliwakuta washitakiwa wakivua samaki bila kuwa na leseni halali za uvuvi.
Baada ya kukamatwa na kupekuliwa, mshtakiwa wa kwanza alidaiwa kukutwa akiwa na nyavu haramu aina ya gill net, ambayo ni miongoni mwa zana za uvuvi zilizopigwa marufuku.
Ilidaiwa kuwa walikutwa wakitumia mtumbwi wa mbao ambao haujasajiliwa, uliokuwa umefungwa injini aina ya Parsun HP 15, pamoja na kuwa na takribani kilo 20 za samaki.
Uchunguzi wa upande wa mashtaka ulidai kubaini kuwa washitakiwa hao walikuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na hawakuwa na nyaraka zinazowaruhusu kuwepo nchini Tanzania.
Washitakiwa walikiri makosa yao, na Mahakama ya Wilaya ya Nkasi iliwatia hatiani. Kila mmoja alitozwa faini ya Sh1.5 milioni kwa kosa la kuvua bila leseni, au kifungo cha miaka mitatu endapo angelishindwa kulipa.
Kwa shtaka la kumiliki gill net, Chilambe alitozwa faini ya Sh2.5 milioni au kifungo cha miaka mitatu, huku kila mmoja wao akitozwa Sh500,000 au kifungo cha miaka mitatu kwa shtaka la kuwa nchini bila nyaraka halali.
Mahakama ya Wilaya pia iliagiza boti ya mbao na injini aina ya Parsun HP 15 vitwaliwe na Serikali kupitia wizara inayohusika na mifugo na uvuvi. Nyavu za gill net ziliagizwa kuharibiwa mbele ya Mahakama.
Hawakuridhishwa na hukumu
Washitakiwa waliwasilisha rufaa wakipinga mamlaka ya Mahakama ya Wilaya ya Nkasi kusikiliza kesi yao, wakidai eneo walilokamatwa, Kalubamba Village, halipo ndani ya Wilaya ya Nkasi wala Tanzania.
Katika rufaa yao waliwakilishwa na Wakili Deogratius Sanga ambaye aliibua hoja mbili kuu, kwanza, kwamba Mahakama ya Wilaya ya Nkasi haikuwa na mamlaka ya kieneo (territorial jurisdiction) kusikiliza shauri hilo na pili, kwamba kukiri kwao kulitokana na mapungufu kwenye vipengele vya makosa waliyoshitakiwa.
Wakili Sanga, aliieleza Mahakama ya Rufani kwamba makosa hayo yalidaiwa kutendeka eneo la Kalubamba, ambalo wadaiwa wanasisitiza halipo Nkasi bali liko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alisema kama eneo hilo halipo ndani ya Nkasi, Mahakama ya Wilaya ya Nkasi haikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo na hivyo mwenendo wote wa kesi ulikuwa batili.
Katika hoja ya pili, Wakili Sanga alidai kukiri hakukuwa kwa wazi kwa sababu kulijengwa juu ya maelezo yenye makosa na yasiyokamilika.
Kwa mujibu wa wakili huyo, katika shitaka la kwanza, upande wa mashtaka haukueleza kwa kiwango kinachohitajika namna au mazingira ambayo uvuvi huo ulifanyika.
Kuhusu shitaka la pili, alidai kuwa haikuelezwa kwa usahihi aina au ukubwa wa nyavu aina ya gill net uliokuwa umepigwa marufuku.
Aidha, kuhusu shitaka la tatu, wakili huyo alisema maelezo ya mashtaka hayakuonyesha kwa kiwango cha kutosha kwamba wadaawa hao walikutwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa sababu hizo, aliiomba Mahakama ya Rufani ibatilishe mwenendo wa kesi, hukumu, adhabu pamoja na amri zilizotolewa na Mahakama ya Wilaya na kuwaachilia huru wadaawa hao. Pia aliomba mali zilizotaifishwa kwa amri ya Mahakama zirudishwe kwa wenyewe.

Kwa upande wa Jamhuri, Wakili wa Serikali, Scholastica Mwacha, alipinga rufaa hiyo na kuitaka Mahakama ya Rufani kuunga mkono uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Nkasi.
Alidai Mahakama ya Nkasi ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa sababu hati ya mashitaka pamoja na maelezo ya mashitaka yaliyosomwa mahakamani yalionyesha kuwa wadaiwa walikutwa Kalubamba Village, ndani ya Ziwa Tanganyika, Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa.
Wakili Mwacha pia ilipinga hoja kwamba kukiri kwa wadaawa hakukuwa kwa wazi, akidai kuwa walielewa mashitaka yaliyokuwa dhidi yao, walikiri ukweli wa maelezo yaliyotolewa na upande wa mashitaka na hawakuweka masharti yoyote kwenye kukiri kwao.
“Kwa kawaida mtu anayekata rufaa baada ya kukiri kosa hawezi kupinga hatia yake isipokuwa katika mazingira maalumu na kwamba rufaa ya aina hiyo kwa ujumla hujikita zaidi katika suala la adhabu,’’ alisema Wakili Mwacha.
“Upande wa Serikali tunawasilisha hoja mbadala kwamba endapo Mahakama ya Rufani ingeona kulikuwa na kasoro katika makiri ya wadaawa, hatua inayofaa haikuwa kuwaachilia huru moja kwa moja, bali kuamuru kesi isikilizwe upya (retrial),”alidai Wakili Mwacha.
Hata hivyo, katika majibu yake ya nyongeza Wakili Sanga alisisitiza kuwa suala la mamlaka ya mahakama ni suala la kisheria ambalo linaweza kuibuliwa wakati wowote, hata katika hatua ya rufaa.
Alidai kosa lililopo kwenye hati ya mashtaka au maelezo ya upande wa mashtaka haliwezi kuipa mahakama mamlaka ambayo kisheria haina.
Alisisitiza kuwa ikiwa Mahakama ya Wilaya haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, haingekuwa sahihi kuamuru kesi mpya isikilizwe katika mahakama hiyo.
Uamuzi wa Mahakama
Jaji Mwenempanzi alisema mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kupitia kumbukumbu za rufaa ilibaini kuwa kulikuwa na masuala mawili ya msingi ya kuamua, likiwamo suala la iwapo Mahakama ya Wilaya ya Nkasi ilikuwa na mamlaka ya kieneo kusikiliza kesi hiyo.
Mahakama Kuu ilibaini dosari kubwa katika hati ya mashitaka kuhusu eneo ambalo makosa yalidaiwa kutendeka. Jaji Mwenempanzi alisema mashtaka ya kwanza na ya pili yalitaja Kalubamba Village kuwa ndani ya Wilaya ya Nkasi, wakati shtaka la tatu lililitaja eneo hilo kuwa ndani ya Wilaya ya Namanyere.
“Tofauti hiyo haikuwa kosa dogo kwa sababu eneo la tukio lilikuwa muhimu katika kuamua kama Mahakama ya Wilaya ya Nkasi ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, pamoja na kuamua kama washtakiwa walikuwa wameingia au kuwepo ndani ya Tanzania kinyume cha sheria.
“Washtakiwa walidai pia kwamba Kalubamba Village haipo Tanzania bali iko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
“Mamlaka ya Mahakama hayawezi kuanzishwa kwa kutaja eneo fulani kwenye hati ya mashitaka pekee. Mamlaka ya Mahakama hutokana na sheria na si kwa namna eneo linavyotajwa katika hati ya mashtaka.
“Endapo Kalubamba Village iko nje ya Wilaya ya Nkasi au nje ya Tanzania, basi Mahakama ya Wilaya ya Nkasi isingekuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo,,”alisema Jaji Mwenempanzi.
Kukiri makosa
Mahakama Kuu pia ilichunguza kama kukiri kwa washtakiwa kulikuwa kwa hiari na kwa uelewa kamili wa mashtaka huku ikifafanua kuwa ili mtu atiwe hatiani kwa msingi wa kukiri kosa, maelezo ya mashitaka na ushahidi wa awali unaotolewa na upande wa mashitaka lazima viwe wazi na vionyeshe vipengele vyote muhimu vya kosa.
“Katika kesi hii kulikuwa na utata kuhusu eneo la tukio na kwamba utata huo uliathiri uhalali wa kukiri kwa washtakiwa.
“Mahakama ilibaini pia kuwa katika shtaka la kumiliki gill net, upande wa mashtaka haukuonyesha kwa kina vipimo au sifa zilizofanya nyavu hizo kuwa haramu chini ya sheria husika.
“Kwa upande wa shtaka la kuwa nchini bila nyaraka, mazingira yaliyotolewa hayakutoa msingi wa kutosha wa kuonyesha kwa uwazi kwamba washitakiwa walikuwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa kutokana na utata kuhusu eneo la Kalubamba,”alisema Jaji Mwenempanzi.
Kutokana na kasoro hizo, Mahakama Kuu ilisema kukiri kwa washtakiwa hakukuwa “unequivocal”, yaani hakukuwa kukiri kwa uwazi na bila masharti na hivyo hakukuwa salama kutumika kama msingi wa hukumu.
Jaji Mwenempanzi aliamua kufuta hukumu zote, kuondoa adhabu zilizotolewa na Mahakama ya Wilaya na pia kufuta amri ya kutaifisha boti pamoja na injini.
Mahakama iliamuru washitakiwa hao watatu waachiwe huru mara moja, isipokuwa kama wanashikiliwa kwa sababu nyingine halali.
Picha ya bango: Matumizi ya njia haramu za uvuvi huharibu mazingira ya majini na kuathiri viumbe wa majini kama huyu. Picha kutoka Tovuti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Nguva wanakaribia kutoweka Kenya, jamii za pwani zapambana kuwarejesha kwa kupanda nyasi bahari