- Hukumu ya hatia iliungwa mkono na ushahidi wa kuaminika wa mashahidi na nyaraka.
- Adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela haikupingwa kwa hoja yoyote mahsusi ya kisheria.
- Rufaa hiyo inakataliwa na hukumu ya hatia itaendelea kusimama.
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga imebariki Evarist Alfred kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kwa kukutwa na vipande saba vya nyama ya nyati, bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Hukumu hiyo imetolewa mbele ya Jaji Thadeo Mwenempazi katika rufani namba 000005245 ya mwaka 2026, iliyotokana na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Mlele katika kesi namba 000035443 of 2024.
Jaji Mwenempanzi alitupilia mbali rufani iliyowasilishwa na Alfred akipinga kutiwa hatiani na adhabu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Mlele dhidi yake baada ya kuona haina mashiko.
Alikutwa na nyama za nyati
Upande wa mashitaka ulidai kuwa Desemba 5, 2024, katika Kituo cha Kijiji cha Kanoge, Wilaya ya Mlele, Mkoa wa Katavi, Evarist alikutwa akiwa na vipande saba vya nyama ya nyati vilivyokuwa na thamani ya Dola za Marekani 2,500, sawa na takribani Sh milioni 6.6.
Nyama hiyo ilidaiwa kuwa mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba Evarist hakuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kumruhusu kuwa nayo.
Alikana shtaka hilo. Upande wa mashtaka uliita mashahidi saba na kuwasilisha vielelezo vitano, huku Evarist akitoa ushahidi wa kiapo na kuita mashahidi wawili wa utetezi waliopinga kuhusika kufanya makosa hayo.
Mahakama ya Wilaya ya Mlele iliridhika kuwa kosa lilikuwa limethibitishwa pasipo shaka na kumtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 20 jela.
Alikata rufaa kupinga hukumu
Baada ya kutoridhishwa na hukumu hiyo, Evarist aliamua kukata rufaa Mahakama Kuu akipinga hatia pamoja na adhabu.
Mrufani aliwakilishwa na Wakili Laurence Mwalabila na aliweka hoja nne, akidai kwamba mahakama ya chini ilikosea kumtia hatiani wakati kosa halikuwa limethibitishwa pasipo shaka.
Alidai kuwa upekuzi uliofanyika ulikuwa kinyume cha sheria, vielelezo viliharibiwa bila kufuata utaratibu wa kisheria na
vielelezo vya maandishi vilipokelewa na mahakama bila kufuata utaratibu unaotakiwa.
Mrufani aliomba Mahakama Kuu itupilie mbali vielelezo vilivyolalamikiwa, ifute hukumu na hatia, itengue adhabu na iamuru aachiwe huru.
Akifafanua Wakili Mwalabila, alidai kuwa upekuzi ulifanyika bila hati ya upekuzi na kwamba hakukuwa na mazingira ya dharura yaliyoweza kuhalalisha upekuzi huo.
Pia alidai kuwa Evarist hakupatiwa risiti ya vipande saba vya nyama vilivyokamatwa, jambo alilosema lilikiuka taratibu za upekuzi na ukamataji wa mali.
Kuhusu uharibifu wa nyama hiyo, Wakili Mwalabila alidai kuwa Evarist hakushirikishwa wala kupewa nafasi ya kusikilizwa kabla ya vielelezo hivyo kuharibiwa.
Jamhuri yapinga rufaa
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Juma Sisa alipinga rufaa hiyo na kusema upekuzi ulikuwa halali.
Alidai kuwa taarifa kuhusu Evarist zilipatikana jioni ya Desemba 5, 2024 wakati mahakama zikiwa zimefungwa. Kwa mujibu wa Serikali, polisi waliomba na kupata idhini kutoka kwa Ofisa Mkuu wa Kituo cha Polisi Inyonga, ambaye alisaini hati ya upekuzi.
Serikali ilitegemea kifungu cha 39(1)(a), (b) na (c) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai , kifungu cha 20, kuonyeshah kwamba mazingira hayo yalihalalisha upekuzi wa dharura.
Kuhusu kutokupatiwa risiti tofauti ya mali iliyokamatwa, Wakili Sisa alidai Evarist alisaini cheti cha ukamataji eneo la tukio, hivyo alitambua ukamataji huo.
Kuhusu uharibifu wa nyama, Serikali ilisema Evarist alifikishwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo akiwa pamoja na nyama hiyo na kwamba alipewa nafasi ya kutoa maoni na akasaini fomu ya orodha ya vielelezo.
Uamuzi wa mahakama
Katika kuchambua hoja hizo, Jaji Mwenempazi alisema Mahakama Kuu, ikiwa ni mahakama ya kwanza ya rufaa, ilikuwa na wajibu wa kuchunguza upya ushahidi wote na kufikia hitimisho lake yenyewe.
Alisema Mahakama ilipaswa kuhakikisha kuwa ushahidi ulipatikana kwa njia halali, ulipokelewa ipasavyo na ulikuwa wa kuaminika kiasi cha kuthibitisha kila kipengele muhimu cha kosa pasipo shaka.
Jaji Mwenempanzi alisema Mahakama ilibaini kuwepo kwa tofauti katika namba ya jalada la polisi na kosa la kiuchapaji lililoonyesha mwaka 2026 badala ya 2024 katika sehemu moja ya kumbukumbu. Hata hivyo, alisema tofauti hizo hazikuonyesha kuwa nyama ilibadilishwa au kuchanganywa na vielelezo vingine.
Mahakama ilihitimisha kuwa mnyororo wa utunzaji wa vielelezo haukuvunjika kwa kiwango cha kuathiri kesi.
Mahakama ilisema kuwa hukumu ya hatia iliungwa mkono na ushahidi wa kuaminika wa mashahidi pamoja na ushahidi wa nyaraka.
Jaji alisema Mahakama ilibaini kuwa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela haikupingwa kwa hoja yoyote mahsusi ya kisheria na kwamba adhabu hiyo ilitolewa kwa kuzingatia kifungu cha sheria kinachotumika katika kosa hilo.
“Kwa sababu hiyo, Mahakama inaamuru kuwa rufaa hiyo inakataliwa kwa ujumla wake, hukumu ya hatia dhidi ya mwombaji kwa kosa la kumiliki nyara ya Serikali kinyume cha sheria imeendelea kusimama, huku adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela ikithibitishwa,”alisema Jaji Mwenempanzi.
Picha ya bango: Usafirishaji, umiliki au biashara haramu ya viungo vya wanyamapori unaweza kusababisha kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria. Picha kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.
Washukiwa wanne wakamatwa kuhusiana na vifo vya tembo 18 katika mfumo wa ikolojia wa Amboseli