- Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi imeadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwake, huku wanamazingira wakipinga miradi ya maendeleo wanayosema inaweza kuathiri ardhi na mazingira ya hifadhi.
- Mzozo unahusu mipango ya kuhamisha na kupanua Nairobi Animal Orphanage pamoja na eneo la maegesho linalohusishwa na ujenzi mpya wa Bomas of Kenya.
- KWS inasema miradi hiyo imefuata taratibu za mazingira na kwamba hakuna ardhi ya hifadhi inayopotezwa, huku wapinzani wakiendelea na kampeni za umma na hatua za kisheria kupinga maendeleo hayo.
NAIROBI, Kenya — Jumapili ni siku ambayo barabara za Nairobi huwa na shughuli nyingi za kijamii, lakini Agosti 30, kando ya barabara ya Lang’ata yenye shughuli nyingi, mkabala wa Bomas of Kenya, kundi la watu lilikuwa na ujumbe tofauti.
Wakiwa wamevalia mavazi ya kijani, wakibeba mabango na kuimba nyimbo za kuitaka Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi ilindwe, watoto na watu wazima walikusanyika kuunga mkono kampeni dhidi ya mipango ya maendeleo ambayo waandamanaji wanasema inaweza kuathiri sehemu ya hifadhi hiyo.
Ilikuwa pia siku ambayo Nairobi National Park iliadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwake.
Miongoni mwa washiriki wachanga zaidi walikuwa mapacha wenye umri wa miaka 10, Tumaini Mwangi na Malikia Mwangi, walioandamana na mama yao Wanjiru Mwangi. Tumaini alisema alishiriki katika maandamano hayo kwa sababu alitaka hifadhi hiyo ilindwe kwa ajili ya watoto na vizazi vijavyo. “Nataka kuokoa hifadhi ili watoto wangu wa baadaye waweze kuwaona wanyama,” alisema.

Alisema angependa serikali, pamoja na Rais William Ruto, ifahamu kwamba watoto na wananchi wanajali kuhusu mustakabali wa hifadhi hiyo.
Pacha wake, Malikia, alisema pia aliamua kujiunga na wanaharakati wengine siku hiyo kwa sababu hakutaka kufikia wakati ambapo kizazi chake kitawajua wanyama wa Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi kupitia picha pekee.
Mama yao alisema uhusiano wake na hifadhi hiyo ulianza miaka mingi iliyopita, alipokuwa na umri wa miaka 20. Wakati huo aliwahi kulala katika nyumba ya wageni ndani ya hifadhi pamoja na mama yake, ambaye sasa ana miaka 88.
Sasa, miaka kadhaa baadaye, aliwaleta mabinti zake kushiriki katika juhudi za kuitetea hifadhi hiyo.
Wazee na vijana wakutana kuitetea hifadhi
Maandamano hayo yaliwaleta pamoja watu kutoka makundi mbalimbali, wakiwemo wanachama wa Friends of Nairobi National Park, washiriki wa Save Nairobi National Park campaign, pamoja na Just Act.
Miongoni mwao alikuwa Sham Patel, mtengenezaji wa filamu na mshiriki wa Friends of Nairobi National Park. Patel alisema kampeni hiyo imekuwa ikiendelea kwa miezi kadhaa kupitia hatua za kisheria, uhamasishaji wa umma na maandamano.
Kundi hilo pia limeanzisha kampeni ya kimataifa mtandaoni, likiwataka watu kutoka Kenya na nchi nyingine kuunga mkono juhudi za kuilinda hifadhi. Kwa Leslie Hannah, mwanachama wa Friends of Nairobi National Park, uhusiano wake na hifadhi hiyo ulianza alipokuwa mtoto.
Hannah alisema alifika Kenya akiwa na umri wa miaka minane mwaka 1972. Wazazi wake walikuwa wakimpeleka Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi mara kwa mara.
Alisema uzoefu huo ulimjengea mapenzi kwa wanyamapori na baadaye akawa mtengenezaji wa filamu za wanyamapori. “Hifadhi ilinipa upendo wangu kwa wanyamapori. Ilinipa riziki yangu na shauku yangu,” alisema.
Siku ya Jumapili, Hannah alifika katika eneo la maandamano kwa boda boda akiwa amebeba mitungi miwili ya maji.
Maji hayo yalikuwa ya kumwagilia miti ya asili iliyopandwa katika eneo lililo karibu na eneo linalohusishwa na mipango ya kujenga maegesho ya magari, mkabala na jengo kubwa la Bomas of Kenya linaloendelea kujengwa. Ujenzi huo ni miongoni mwa miradi inayopingwa na waandamanaji.
Hannah alisema miche 16 ya miti ilipandwa wakati wa maandamano yaliyotangulia, ingawa baadhi haikustawi. Yeye na mshiriki mwingine wamekuwa wakigawana jukumu la kuitunza.
Mpango unaozua mvutano
Mzozo huo unahusu, miongoni mwa mambo mengine, mpango wa kuhamisha na kupanua Nairobi Animal Orphanage, yaani kituo cha watoto yatima cha wanyama waliokosa wazazi au walezi na wanaohitaji kuokolewa, kutibiwa na kutunzwa.
Shirika la Huduma kwa Wanyamapori Kenya (KWS) pia limehusisha mpango huo na kuboresha huduma za uokoaji, ukarabati na ustawi wa wanyama.
Kwa mujibu wa KWS, kituo cha sasa, kilichoanzishwa mwaka 1964, hakikidhi tena mahitaji ya kisasa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanyama wanaohitaji huduma, ongezeko la wageni na mahitaji ya viwango bora vya ustawi wa wanyama.
KWS imesema eneo jipya limechaguliwa baada ya kutathminiwa kwa chaguzi mbalimbali na kwamba linafaa kwa kituo cha kisasa cha uokoaji na ukarabati wa wanyama. KWS pia inasema mradi ulifanyiwa tathmini ya athari kwa mazingira na kupata leseni kutoka kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) mnamo Desemba 2025.
KWS pia inasema hakuna ardhi ya hifadhi inayopotezwa kwa sababu eneo jipya litaendelea kuwa chini ya usimamizi wa Nairobi National Park. Lakini makundi ya mazingira yanapinga matumizi ya sehemu zaidi ya hifadhi kwa maendeleo hayo.
Akshay Vishwanath, Mkurugenzi Mtendaji wa Just Act na mshiriki wa kampeni ya Save Nairobi National Park, alisema kundi hilo haliwezi kupinga haja ya kuboresha huduma za wanyama, lakini linapinga kupotea kwa ardhi ya hifadhi kwa ajili ya maendeleo.

Vishwanath aliambia Mongabay kuwa Nairobi National Park tayari imekabiliwa na shinikizo la miradi ya miundombinu, ikiwemo barabara maarufu ya Southern Bypass na reli ya kisasa ya Standard Gauge, iliyopita katikati ya mbuga hiyo.
Kampeni hiyo pia inapinga eneo kubwa la maegesho linalohusishwa na maendeleo ya Bomas of Kenya, ikisema linaweza kuongeza shinikizo na changamoto kwa mazingira ys wsnyama kwa hifadhi.
Kesi mahakamani
Mzozo huo umeendelea hadi mahakamani. Zaidi ya wananchi 4,600 wamejiunga na hatua za kisheria zinazopinga mpango huo, huku kesi ikiendelea katika Mahakama ya Mazingira (Environment and Land Court).
Pande zinazopinga mradi zimekuwa zikisema kuna masuala kuhusu matumizi ya ardhi ya hifadhi, athari kwa mazingira na namna mchakato wa ushirikishwaji wa umma ulivyofanyika.
KWS, kwa upande wake, inasema mradi ulifuata taratibu zinazohitajika za mazingira na sheria za uhifadhi.
Kikao kingine cha kesi kinatarajiwa kufanyika mwezi Septemba, huku kampeni hiyo ikisema itaendelea kutumia mahakama na njia nyingine za ushawishi pamoja na maandamano.
Maandamano yaendelea bila fujo
Mnamo Agosti 30, waandamanaji waliendelea kuimba na kuinua mabango yenye ujumbe kama “Save Nairobi National Park” na “Save Our Lions”, huku magari yaliyokuwa yakipita Lang’ata Road yakipiga honi.

Polisi walifika katika eneo hilo na kuwauliza waandaaji kuhusu kibali cha maandamano. Waandamanaji waliwasilisha nyaraka walizosema zinawaruhusu kufanya shughuli hiyo.
Polisi waliendelea kuwepo wakati maandamano yakiendelea, lakini hakukuwa na fujo na shughuli ziliendelea kwa amani hadi waandamanaji walipoondoka.
Kwa Tumaini na Malikia, hata hivyo, ujumbe wao haukuwa kuhusu kesi pekee. Walitaka hifadhi hiyo iendelee kuwepo wakati watakapokuwa watu wazima. Wanataka wao na vizazi vijavyo waweze kutembelea Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi na kuona wanyamapori, badala ya kuambiwa kwamba wanyama hao waliwahi kuwepo.
Picha ya bango: Baadhi ya wanaharakati walioshiriki katika maandamano ya kuadhimisha miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi na kupinga shughuli za ujenzi ndani ya hifadhi hiyo pamoja na mpango wa kuhamisha Nairobi Animal Orphanage. Picha na Anne Ngugi, Mongabay.
Bioanuwai hatarini: Uhamisho wa kituo cha wanyama yatima wazua wasiwasi miongoni mwa wahifadhi