- Kongamano lakutanisha zaidi ya wajumbe 5,000 kutoka zaidi ya nchi 50.
- Serikali za Afrika zinapaswa kujiandaa kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
- Uwekezaji endelevu katika kilimo unahitaji wataalamu wenye ujuzi na sera madhubuti.
- Hatua za Serikali kupunguza hatari kwa vijana wanaokopa benki zinaweza kuleta matokeo chanya.
Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha mifumo ya uzalishaji wa chakula ni miongoni mwa masuala yaliyopewa kipaumbele katika Kongamano la Mifumo ya Chakula Afrika (AFSF 2026), lilinalofanyika Kigali, Rwanda.
Washiriki zaidi ya 5,000
Kongamano hilo lenye kaulimbiu, “Kuwekeza katika Mifumo ya Klimo na Chakula Barani Afrika,’’ liliwakutanisha zaidi ya wajumbe 5,000 kutoka zaidi ya nchi 50. Miongoni mwa mambo muhimu yaliyojadiliwa ni uwekezaji katika kilimo, miundombinu ya kilimo, ajira kwa vijana, usalama wa chakula na namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Dk. Robin Arani Buruchara, mtaalamu wa utafiti na maendeleo ya kilimo kutoka Kenya, amesema Serikali za Afrika zinapaswa kujiandaa mapema kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwemo uwezekano wa El Niño.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuwekeza katika umwagiliaji, hifadhi ya maji, mbegu zinazostahimili ukame na mafuriko, pamoja na mifumo ya utabiri na tahadhari za mapema, ili kulinda uzalishaji wa chakula.

Prof Jean Jacques Muhinda, Mkurugenzi wa Masuala ya Kilimo wa AGRA, katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, amesema kongamano hilo limejikita katika maeneo matatu muhimu: ‘’kuunda ajira kwa vijana, kuwekeza katika miundombinu ya kilimo na kuongeza uwekezaji wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi’’.
Mifumo ya umwagiliaji
Akizungumzia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Muhinda amepongeza Serikali ya Rwanda kwa kuendeleza mifumo ya umwagiliaji katika Wilaya za Nyagatare, Bugesera na maeneo mengine. Amesema mifumo hiyo inawawezesha wakulima kuendelea kuzalisha hata wakati wa kiangazi na uhaba wa mvua.
Kwa mujibu wa Muhinda, mpango mkakati wa miaka 10 wa AGRA unalenga kuhamasisha uwekezaji wa takribani dola bilioni 100 za Marekani katika sekta ya kilimo barani Afrika, huku AGRA ikipanga kuchangia angalau dola milioni 10.
Epaphras Milambwe, mtaalamu wa kilimo kutoka Tanzania anayewakilisha East-West Seed katika ukanda wa Afrika Mashariki na Magharibi, amesema uwekezaji salama na endelevu katika kilimo unahitaji wataalamu wenye ujuzi pamoja na sera madhubuti.

Sera madhubuti
“Tunahitaji Serikali kuwekeza na kutunga sera zitakazoweka miongozo sahihi katika kuwekeza kwenye kilimo. Bila kuwa na sera madhubuti zinazoongoza masuala ya uwekezaji wa kilimo na uwekezaji bora, hatuwezi kufanikiwa,” amesema Milambwe.
Donal Brown, Makamu wa Rais Msaidizi wa IFAD, amesema mifumo ya chakula barani Afrika inahitaji suluhisho pana za kifedha zinazozingatia mahitaji ya biashara za kilimo katika hatua mbalimbali za ukuaji.
Rais wa Rwanda, Paul Kagame, amesema hatua za Serikali za kupunguza hatari kwa vijana wanaochukua mikopo benki zinaweza kuleta matokeo chanya, kwa kuwa vijana wanaonufaika huanzisha shughuli zinazozalisha kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi.
Naye Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia na Mwenyekiti wa Bodi ya CGIAR, Hailemariam Desalegn, amesema ‘’Kilimo kinapaswa kutazamwa kama msingi wa maendeleo ya uchumi, viwanda, biashara ndogo na ustawi wa taifa.
Uwekezaji zaidi katika kilimo
Kongamano la AFSF 2026 limeendelea kuimarisha wito wa kuongeza uwekezaji katika kilimo, kuunda ajira kwa vijana, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kujenga mifumo endelevu ya chakula barani Afrika’’.
Katika kongamano hilo, IFAD na AgDevCo zimesaini mkataba wa mkopo wa dola milioni 10 za Marekani kwa ajili ya uwekezaji katika biashara za kilimo barani Afrika.
Fedha hizo zinalenga kusaidia biashara changa za kilimo katika maeneo ambayo hayajahudumiwa vya kutosha, ili ziweze kupanua shughuli, kuongeza tija na kufikia masoko mapya.
Picha ya bango: Baadhi ya viongozi walioshiriki kongamano la Afrika (AFSF 2026), lilinalofanyika Kigali, Rwanda. Picha na Christopher Karenzi.