- Kati ya asilimia 60 hadi 80 ya watu Tanzania wanatumia mimea dawa kutibu magonjwa mbalimbali.
- Uvunaji usio endelevu wa mimea dawa ni tishio kubwa kwa mifumo ya ikolojia.
- Mimea dawa mingi inayouzwa kwenye masoko makuu inavunwa bila mpango wa upandaji endelevu.
- TFS wafanye utafiti wa kuorodhesha miti dawa yote inayotumika sana na adimu na kuiotesha kwenye vitalu vyao.
Matumizi ya mimea na miti kama dawa yanaendelea kuongezeka kwa kasi, hali inayotishia uhai wa baadhi ya spishi, bioanuwai na afya ya misitu. Hali hii inazua swali muhimu: Je, jamii nchini Tanzania zinawezaje kuendelea kunufaika na mimea ya dawa huku spishi zilizo hatarini na misitu vikiendelea kulindwa?
Matumizi ya mimea dawa: Hali halisi
Taarifa zilizopo zinaonyesha nchi nyingi duniani sasa zinatumia mimea kama dawa. Kwa mfano, Ripoti ya mwaka 2019 ya Shirika la Afya Duniani, (WHO) kuhusu mimea na tiba asili ilionyesha kuwa nchi wanachama (nchi ambazo WHO inafanya kazi) 170 kati ya 194, sawa na asilimia 88, zilikuwa zinatumia mimea kutibu maradhi mbalimbali.

Barani Afrika, ambapo kuna upatikanaji wa mimea na misitu mingi asilia, hali ya matumizi ya mimea dawa ni kubwa zaidi. Kwa mujibu wa ripoti ya Kanda ya Afrika ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2010 kuhusu matumizi ya dawa asili barani Afrika, kati ya asilimia 70 hadi 80 ya Waafrika wanategemea mimea kwa ajili ya afya zao.
Nchini Tanzania, Chapisho la WHO linaonyesha kuwa kati ya asilimia 60 hadi 80 ya wananchi wanatumia mimea dawa kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu na wanyama wa kufugwa.
Kwa mujibu wa chapisho hilo, matumizi hayo yanakwenda sambamba na uwepo wa mtandao mpana wa waganga wa jadi, wanaokadiriwa kufikia 75,000 ambao kwa kiasi kikubwa hutegemea mimea hiyo kama chanzo cha dawa.
Machapisho mbalimbali pia yanaonyesha ongezeko la matumizi ya mimea kama dawa. Kwa mfano, utafiti uliofanywa na mtafiti Hilonga na wenzake mwaka 2019 katika mikoa mbalimbali nchini, pia ulithibitisha kuwepo kwa uhitaji na matumizi makubwa ya mimea dawa sehemu nyingi nchini Tanzania.
Chapisho la Chrispin Shangali na wenzake (2008) lililoangalia Hifadhi za Milima ya Tao la Mashariki nchini Tanzania (Eastern Arc Mountains) na kabila la Wahehe mkoani Iringa, pia lilionyesha namna wananchi wanavyotegemea miti dawa. Kwa mujibu wa chapisho hilo, zaidi ya asilimia 80 ya jamii zinazozunguka safu hizo za milima, zinategemea mimea dawa inayopatikana ndani ya misitu ya Tao la Mashariki.
Matokeo ya utafiti wa Nahashon Michael wa mwaka 2013 yanaonyesha kwamba mnyororo wa biashara ya spishi za mimea dawa unaanzia msituni na kisha unasambazwa kwa wadau mbalimbali, kama vile wakusanyaji, wauzaji, waganga wa jadi, watumiaji na wauzaji wanaopeleka nje ya nchi.
Kwa mujibu wa utafiti huo, kuna mahitaji makubwa ya mimea dawa maeneo ya mijini hasa Dar es salaam ambako utafiti huu ulifanyika. Aidha kupitia utafiti huu Nahashon Michael alibaini uwepo wa mahitaji makubwa ya mimea dawa kwenye masoko ya kimataifa ya nchi za nje, jambo ambalo ni tishio kwa mimea hii ambayo kwa kiasi kikubwa inavunwa bila kuzingatia uhifadhi wake wa baadaye.
Wakati taarifa zilizopo zinabainisha wazi kiwango kikubwa cha matumizi ya mimea kama dawa, swali muhimu ni: Je, matumizi haya yanawezaje kuendelezwa bila kusababisha uharibifu wa misitu asilia na kuhatarisha uhai wa mimea inayotumika kama dawa? Je, jamii nchini Tanzania zinawezaje kuendelea kunufaika na mimea ya dawa huku spishi zilizo hatarini na misitu vikiendelea kulindwa?
Katika mahojiano na watalaamu mbalimbali, ilibainika kuwa iwapo uvunaji wa mimea ya dawa utafanyika kwa njia endeleavu, matumizi ya mimea hiyo kwa ajili ya tiba yanaweza kuendelea bila kusababisha athari kwa mazingira au kupunguza upatikanaji wake.
Uvunaji salama wa mimea dawa
Elibariki Akyoo, Mhifadhi Mwandamizi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), anayesimamia uhifadhi wa misitu Nyanda za Juu Kusini, anasema kuwa ili kuhakikisha uvunaji wa mimea ya dawa unafanyika kwa njia endelevu, wameweka udhibiti dhidi ya uvunaji holela. TFS haitoi kibali au leseni kwa ajili ya uvunaji wa mimea ya dawa katitka maeneo yenye misitu asilia (Forest nature reserves).

Anasema kuwa katika misitu mingine ya akiba pamoja na ile iliyopandwa kwa ajili ya uzalishaji kama mbao, TFS hutoa vibali au leseni kwa watu kuvuna mimea ya dawa kwa kuzingatia taratibu za uhifadhi. Uvunaji huo unatakiwa kufanyika bila kukata, kuondoa au kuua mti mzima. Pia wanaruhusiwa kuchuma majani, maua au matunda kwa njia inayozingatia uendelevu wa raslimali hizo.
Mbaapa Lengaswa, mvunaji, mtengenezaji na muuzaji wa mimea ya dawa kutoka Kiteto, Manyara, anaeleza namna uzingatiaji wa taratibu zilizowekwa, pamoja na mawasiliano mazuri kati ya wavunaji na uongozi wa kijiji yanavyosaidia katika utekelezaji wa uvunaji endelevu na unaozingatia sheria.
“Wakati wa kuingia msituni kwa ajili ya kutafuta mimea dawa huwa tunawasiliana na uongozi wa kijiji kupitia kamati za maliasili. Pia tunazingatia sheria ndogo za vijiji zilizoweka kuhakikisha tunavuna salama na kuacha mimea hiyo iendelee kusitawi na kukua,’’ anasema Lengaswa.
Hata hivyo anasema wapo watu wengine ambao wanaingia msituni kuvuna bila kibali na mara nyingi watu wa aina hiyo ndio huvuna kwa kuharibu au kuua mmea hiyo. Hawa hutoka vijiji vingine ambavyo sio vilivyo karibu na msitu huo na wanaingia bila vibali.
Neema Ernest, Afisa Uhifadhi Mistu wa Hifadhi ya Chome, anasema kwa kushirikiana na jamii zinazozunguka hifadhi ya misitu, wamejiwekea taratibu ambazo husaidia katika kuimarisha ulinzi wa mazao ya misitu kwenye maeneo yao. Miongoni mwa taratibu hizo ni kama kutoruhusu mtu kuingia msituni akiwa na silaha yoyote kama panga, jembe na mkuki pamoja na kufanya ulinzi na ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini wanaovunja sheria hizo.
Uvunaji usio endelevu
Ili matumizi ya mimea ya dawa yasilete madhara, tafiti mbalimbali zimeainisha mambo yanayopaswa kuepukwa wakati wa uvunaji.
Tafiti zilizofanywa kuhusu matumizi ya mimea ya dawa na athari zake katika uhifadhi katika Milima ya Tao la Mashariki, zinaonyesha kuwa uvunaji usio endelevu wa mimea dawa ni tishio kubwa kwa mifumo ya ikolojia, hasa pale mahitaji yanaongezeka na mimea hiyo huvunwa moja kwa moja kutoka katika mazingira yake ya asili.
Licha ya uvunaji wa aina hiyo kusabababisha kutoweka kwa aina za uoto wa spishi muhimu za mimea asilia, tafiti nyingine zinasema hali hiyo inatishia maeneo yenye bayoanuai ya kipekee ikiwemo Hifadhi za Milima ya Tao la Mashariki nchini Tanzania (Eastern Arc Mountains) kama vile Uluguru, Udzungwa, na Usambara. Milima hii inahifadhi vyanzo vikuu vya maji na viumbe hai adimu.
Kuvunwa kwa spishi za mimea dawa hadi kupitilizaitu huku kukiwa hakuna mkakati wowote wa kupanda nyingine, ni changamoto nyingine kubwa inayoikabili mimea dawa.
Dkt Frank Mbago ambaye ni mtafiti wa mimea na mkutubi mstaafu wa maktaba ya kuhifadhi sampuli za mimea, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema: “Kuna baadhi ya mimea dawa imeingia kwenye soko la kimataifa hivyo wafanyabiashara huivuna kwa wingi kwa kipindi kifupi na kuhatarisha kutoweka kwenye sura ya dunia”.
Kwa mujibu wa Dkt Mbago, mmea wowote wa asili unaovunwa kibiashara unapaswa kufanyika sambamba na juhudi za kuotesha mwingine ili kutimiza ile kauli mbiu ya uhifadhi ya kata mti panda miti.

Ushahidi mwingine wa kisayansi uliofanyika katika mikoa mbali mbali hapa Tanzania umebaini kuwa asilimia 69 ya mimea dawa yote iliyoko sokoni imevunwa kutoka katika misitu asilia bila mpango wowote wa uvunaji endelevu, kama aliyotaja Sambayi na wenzake kwenye utafiti uliofanyika mwaka 2026.
Wataalam wa ikolojia; Akyoo, Dkt Mbado na Ernest wote wanaonya kuwa mbinu kama vile kuchuna magome yote ya mti kwa mzunguko au kung’oa mizizi mikuu kunazuia miti hiyo kujizalisha na kusababisha ikauke na kufa kwa kasi kuliko uwezo wake wa asili wa kukua tena.
Ripoti ya pamoja ya Mashirika ya Uhifadhi wa Misitu na Kilimo-Miti (CIFOR-ICRAF) pia ilionya kuwa spishi nyingi za mimea tiba zipo hatarini kutoweka kutokana na uvunaji uliopitiliza, ambao kwa kiasi kikubwa unafanyika bila kibali.
Mimea dawa katika soko la nje
Taarifa nyingine zinaonyesha kuwa uharibifu wa misitu asilia nchini, unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mahitaji makubwa ya kibiashara ya mimea dawa kwenye masoko ya kikanda na kimataifa.
Ripoti ya TRAFFIC ya mwaka 2023 iliyoandikwa na Martin Andimile na Camilla Floros kuhusu ongezeko kubwa la matumizi ya mimea dawa, inaonyesha kushamiri kwa biashara hii licha ya kutopewa uzito mkubwa katika udhibiti na uhifadhi.
Spishi zilizo hatarini kutoweka
Kwa mujibu wa DktMbago, kutokana na uvunaji haramu na ujangili wa mazao ya misitu, idadi kubwa ya mimea asili inaendelea kutumiwa kama dawa na mapambo sehemu mbalimbali duniani kwa namna ambayo si endelevu.
Dkt Mbago anataja spishi kadhaa alizosema zinazokabiliwa na hatari kubwa ya kutoweka nchini iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Spishi hizo ni pamoja na Mkunungu (Zanthoxylum chalybeum); Mjafari au Oloisuki kwa Kimasai, mti unaopatikana maeneo ya ukame na nusu-ukame kama Arusha, Manyara (Simanjiro), Kilimanjaro, Dodoma, na Singida. Unavunwa sana kutibu matatizo ya upumuaji, malaria, na maumivu ya tumbo.
Spishi nyingine ni Mvumo wa Milimani (Warburgia ugandensis), mti adimu unaopatikana kwenye misitu ya miinuko yenye unyevu ya Tao la Mashariki (Tanga na Iringa). Dkt Mbago anasema mti huo unapungua kwa kasi kwa sababu ya magome yake inasemekana yanatibu fangasi na bakteria.
Kwa mujibu wa Dkt Mbango, Mpingo (Dalbergia melanoxylon), Mninga (Pterocarpus angolensis), na Mvule (Milicia excelsa), miti inayopatikana kanda za miombo na savanna (Lindi, Mtwara, Pwani, Morogoro, na Tabora) inakabiliwa na ukatwaji kwa ajili ya mbao za thamani lakini pia inashambuliwa sana kwa ajili ya dawa za asili za kutibu magonjwa ya ngozi na kuhara.
Spishi nyingine ni Mchaichai mwitu au Murihani (Ocimum suave), mmea ambao majani yake hutumika kama kinga na tiba ya magonjwa ya koo, kikohozi, na kusaidia kushusha homa na kutibu malaria. Mti mwingine ni Fula (Artemisia afra), moja ya spishi maarufu za mwituni zinazotumika kwenye tiba ya mvuke (kujifukiza) kutibu mafua, matatizo ya mfumo wa upumuaji, na minyoo ya tumboni.

Kitucha (Euphorbia hirta), mmea mdogo unaotumiwa kwa katika kutibu pumu (asthma), matatizo ya kuhara damu (dysentery), na kikohozi sugu; Msandali (Osyris lanceolata), mti ambao mizizi yake na vigogo vyake hutumiwa kukamua mafuta ya uturi na bidhaa nyinyine. Mti huu hupatikana kwenye Misitu ya nyanda za juu Mbulu Babati Iringa na Milima ya Usambara na Kilimanjaro umbande ule Mkavu.
Mti mwingine ulioko hatarini ni Mkakatika (Senna abbreviata), mti ambao mizizi yake hutumiwa na katika makabila mengi Tanzania kama kama antibiotic. Unaota maeneo ya ukame kuanzia nyanda za chini hadi nyanda za juu.
Nini kifanyike kuokoa spishi zilizo hatarini?
Dkt Mbago anatoa mapendekezo kadhaa ikiwa ni pamoja na kushauri Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuotesha mbegu za miti dawa ambayo inatumika sana hasa kwa biashara ili miche hiyo igawiwe kwa watumiaji kwa ajili ya kuipanda mashambani.
Iddi Rajabu, aliyekuwa mtaalamu wa maabara kutoka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), anapendekeza kuhamasisha waganga wa jadi na jamii kuanzisha mashamba na bustani maalum za mitishamba majumbani badala ya kutegemea misitu ya asili pekee.
Pia, anapendekeza kuimarishwa kwa utekelezaji wa Sheria ya Misitu ya Mwaka 2002, pamoja na kudhibiti biashara ya magendo ya mimea ya dawa katika masoko ya mijini, kama hatua muhimu ya kulinda na kuokoa mimea hiyo.
Mikakati ya TFS
Kwa mujibu wa Akyoo, TFS ina mpango wa usimamizi wa spishi maalumu zilizo katika hatari ya kutoweka katika maeneo inayosimamia. Ili kufanikisha hilo, wamezitambua na kuziweka katika mpango maalumu spishi hizo. Pia wanatambua aina za mimea ya dawa yenye mahitaji makubwa na inayotumika kwa kiwango kikubwa, kwa lengo la kuimarisha usimamizi na ulinzi wa maeneo ambayo mimea hiyo inapatikana.
Ili kudhibiti ujangili na biashara haramu ya mazao ya misitu, ikiwemo mimea dawa, changamoto ambayo Akyoo amekiri kuwepo, TFS imeimarisha doria na kuongeza usimamizi katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto hizo.
TFS pia wana mpango endelevu wa kuzalisha mbegu na miche ya mimea ya dawa inayotumiwa sana na jamii kwa ajili ya kuwapa watu kuipanda kwenye maeneo yao ili kupunguza uvunaji uliokithiri wa mimea hii ndani ya maeneo ya hifadhi za misitu, alisema Akyoo.
Picha ya bango: Mizizi ya aina mbalimbali za mimea ya dawa ikichemshwa kwa ajili ya kuandaa dawa ya kutibu magonjwa mbalimbali. Dawa hii hutumiwa zaidi na jamii ya Wamasai wa wilaya ya Kiteto Manyara: Picha na Hillary Mrosso.