- Mwanasha Mbwana alianza kutegemea rasilimali za bahari akiwa msichana kwa kukusanya makome na kutengeneza mikufu, shughuli iliyomsaidia kujilipia elimu hadi kuwa mwalimu wa chekechea. Sasa anaongoza wanawake 80 wanaoshiriki katika tafiti na urejeshaji wa matumbawe huko Pate.
- Wanawake hao wameingia katika shughuli za baharini licha ya mila za jamii ya Kibajuni zilizowazuia wanawake kwenda baharini au kupanda boti pamoja na wanaume. Kupitia mafunzo ya mashirika ya uhifadhi, wameanza kurejesha matumbawe kwa kutumia miundo bandia.
- Zulfa Hassan Mote, anayejulikana kama Mama Mangroves, ameongoza juhudi za wanawake kurejesha mikoko Mtangawanda, Pate. Kikundi chake, kilichoanzishwa mwaka 2018, kimepanda zaidi ya mikoko 500,000 katika zaidi ya hekta 30, huku kikizalisha takriban miche 50,000 kwa mwaka.
- Kwa wanawake kama Mwanasha na Zulfa, uhifadhi umeleta pia mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, na kupanua nafasi ya wanawake katika shughuli zinazohusiana na bahari.
Hii ni sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala kuhusua wanawake wanaovunja mila na kurejesha bahari Lamu. Soma Sehemu ya pili hapa.
LAMU, Kenya — Mwanasha Mbwana, mkazi wa Shangarubu, Kaunti ya Lamu, anakumbuka vizuri jinsi bahari ilivyomsaidia kupata pesa na kujiendeleza kimasomo akiwa na umri mdogo.
Mama Corals: Kutoka kukusanya makome hadi kurejesha matumbawe
Mwanamke huyo, maarufu kama Mama Corals, anasema baada ya kukamilisha shule ya msingi mwaka 1997, alikuwa na hamu ya kuendeleza masomo yake. Lakini kwa sababu ya hali ya umasikini iliyokabili familia yake wakati huo, hakufanikiwa.
Lakini hakukata tamaa. Alijikita baharini kutafuta makome (cowrie shells) na kutengeneza mikufu aliyouzia watalii na wenyeji. Kwa siku, angepata faida ya kati ya KSh70 ($0.54) na KSh100 ($0.77), ambazo aliziweka akiba na baadaye zikamlipia karo ya shule ya upili.

“Nilisoma kupitia shughuli za bahari. Wakati wa likizo, wenzangu wakienda kujivinjari, mimi nilikuwa nikizama baharini kukusanya makome,” anaeleza Mwanasha.
Hatimaye alijisomesha hadi taasisi ya mafunzo ya elimu ya chekechea (Early Childhood Development Education, ECDE) na sasa ni mwalimu wa chekechea. “Sikutaka kuolewa nikiwa na umri mdogo. Sasa, kama mwalimu wa chekechea, maisha yangu yameinuka,” anasema.
Lakini bahari ambayo ilimsaidia Mwanasha kupata elimu pia ilimfunza somo jingine: kwamba rasilimali hizo hazikuwa zisizo na mwisho.
Anasema zamani yeye na wavuvi wengine hawakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu umuhimu wa makazi ya samaki na viumbe wengine baharini. Matokeo yake, shughuli zao zilichangia uharibifu wa mazingira hayo, hasa miamba ya matumbawe ambako makome hupatikana kwa wingi.
“Kitambo tulikuwa hatuna ufahamu na mambo mengi ya baharini, ikiwemo matumbawe. Tulikuwa tukiona ni miamba tu. Tukienda baharini tungezivunja, huku wavuvi wakivua samaki kwa ajili ya kuuza,” anasema.
Mabadiliko yalianza baada ya jamii kupata mafunzo kuhusu mazingira ya baharini na umuhimu wa kuyahifadhi kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali, yakiwemo Northern Rangelands Trust (NRT), The Nature Conservancy (TNC) na Fauna & Flora.
Baada ya mafunzo hayo, Mwanasha aliamua kuingia katika uanaharakati wa uhifadhi. Mwaka 2014, alianzisha kikundi cha wanawake cha Shangarubu Women Fisher. Leo anaongoza wanawake 80 wanaopiga mbizi baharini kufanya tafiti na kurejesha matumbawe yaliyoharibika.
Wanatumia miundo bandia ya matumbawe katika hekta 160 ndani ya eneo la tengefu la Pate Marine Community Conservancy (PMCC), lenye ukubwa wa jumla ya ekari 9,290.

Wanawake dhidi ya mila za kutokaribia bahari
Juhudi hizo zimefanyika licha ya tamaduni zilizowazuia wanawake kuingia baharini.
Katika jamii hiyo, kulikuwa na imani kwamba mwanamke akiingia baharini akiwa katika siku zake za hedhi anaweza kuvutia au kuingiliwa na majini na viumbe vya ajabu vya baharini. Bahari pia ilihusishwa na nguvu za kiroho zisizofahamika na za kutisha, huku wanawake wakionekana kuwa katika hatari kubwa zaidi endapo wangeingia majini bila kufuata kinga za kimila.
Mwanasha anasema katika jamii yake ya Kibajuni, wanawake kwa muda mrefu hawakuwa na nafasi ya kwenda baharini kuvua au kushiriki katika shughuli za uhifadhi sawa na wanaume.
“Kulingana na mila zetu kama jamii ya Kibajuni, na pia Waislamu, hatukuwa tunapewa nafasi ya kwenda baharini. Hasa kuingia kwa boti wanaume na wanawake haikukubalika. Sisi tulikuwa tukienda kandokando ya bahari, maeneo ambayo hayana maji mengi,”anasema.
Jamii haikupokea mara moja uamuzi wake wa kupiga mbizi na kurejesha matumbawe. “Jamii mara ya kwanza haikuchukulia vyema jambo hilo la mimi kupiga mbizi na kupanda matumbawe bandia, lakini niliamua kujistiri na kujilinda. Kama singechukua hatua hiyo, saa hii ningekuwa nimefungiwa ndani ya nyumba. Badala ya hiyo, na kutokana na juhudi zangu, najulikana kimataifa,” anaeleza.
Matumbawe ni wanyama wadogo wa baharini wanaoishi kwa kujenga makoloni na kutengeneza miamba ya baharini. Miamba hiyo ni miongoni mwa mifumo ya ikolojia yenye bioanuwai nyingi na hutoa makazi kwa maelfu ya viumbe vya baharini duniani.
Hata hivyo, shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabianchi vinaendelea kuiweka mifumo hiyo katika hatari. Ripoti ya Global Coral Reef Monitoring Network (GCRMN) inaonyesha kuwa kati ya mwaka 2009 na 2018, dunia ilipoteza takriban asilimia 14 ya matumbawe yake.
Kujenga tena miamba
Mwanasha hukutana na wanachama wa kikundi chake mara mbili kwa mwezi na kuwaongoza katika kutengeneza matumbawe bandia kwa kutumia simiti na waya.
Vipande vya matumbawe hukusanywa kutoka kwenye makoloni yenye afya, kisha hulelewa kwenye meza maalum au vishikiliaji vilivyowekwa chini ya maji kwa miezi kadhaa kabla ya kuunganishwa kwenye miundo bandia.
Wanawake hao hutengeneza aina mbalimbali za miundo, ikiwemo block corals, cake corals na bucket corals, ambayo baadaye hubebwa na kupandwa baharini.

Mwanasha anasema matumbawe hayo huchukua kati ya miezi sita na mwaka mmoja, na wakati mwingine hata zaidi ya mwaka, kukua na kuenea vizuri. Anasema asilimia 100 ya matumbawe bandia wanayopanda humea vizuri.
Mabadiliko hayo, anasema, yameanza kuonekana katika bahari. “Baadhi ya samaki waliokuwa wakipatikana kwenye maeneo ya matumbawe walikuwa wameanza kutoweka. Lakini tangu tuanze harakati hizi, samaki kama tafi (Siganus rivulatus, Siganus canaliculatus na Siganus rivulatus), changu (Lethrinus spp.) na pono (Leptoscarus vaigiensis)wameanza kuonekana,” anasema.
Mwanasha pia hutumia nafasi yake kama mwalimu kuwafundisha wanafunzi kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira ya baharini. Anasema hataki kizazi kijacho kijifunze kuhusu samaki na viumbe wa baharini kupitia vitabu pekee, bali kiweze kuwaona baharini.
Juhudi zake pia zimevuka mipaka ya jamii yake. Amealikwa kushiriki katika makongamano na mikutano ya kimataifa kuhusu bahari na matumbawe, ikiwemo Our Ocean Conference.
Uhifadhi na maisha ya familia
Mwanasha ni mama wa watoto sita. Hufundisha kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, kisha hutumia wikendi na likizo katika shughuli za baharini, isipokuwa anapokuwa na safari za kikazi au mikutano ya uhifadhi.

Wanawake wa kikundi chake pia huokota makome yanayotumika kutengeneza shanga zinazouzwa kwa watalii kuanzia KSh100 ($0.77). Mapato hayo yamewasaidia kuongeza kipato na, kwa baadhi yao, kugharamia elimu ya watoto wao.
Mwanasha anamshukuru mumewe, Ahmed Mohammed, kwa kumuunga mkono katika shughuli zake za uhifadhi.
Mohammed, ambaye ni mvuvi, anasema tamaduni zilizokuwepo hazikumfanya amzuie mkewe kufanya kazi anayopenda. “Mara nyingi mke wangu akiwa baharini mimi humsaidia kuangalia watoto na majukumu ya nyumbani. Nilimruhusu kwenda baharini kupanda matumbawe kwa sababu najua mazingira yakiwa mazuri, samaki watarudi na sisi wavuvi pia tutafaidika,” anasema.
Anaongeza kuwa katika mazingira ambayo maisha yamekuwa magumu, shughuli za baharini zinawasaidia kushirikiana kugharamia mahitaji ya familia.
Mama Mangrove: Mikoko kama fursa kwa wanawake
Hadithi ya Mwanasha inafanana kwa kiasi fulani na ya Zulfa Hassan Mote, mwanamke mwingine wa Lamu aliyejikita katika uhifadhi wa mazingira ya bahari. Zulfa, maarufu kama Mama Mangroves (Mama Mikoko), anatoka Mtangawanda, kisiwani Pate.

Kwa mujibu wa Miongozo ya Kitaifa ya Urejeshaji wa Mfumo wa Ikolojia wa Mikoko ya Mwaka 2025, Kenya ina takriban hekta 61,279 za misitu ya mikoko katika ukanda wa pwani. Lamu inaongoza nchini kwa kuwa na sehemu kubwa ya misitu hiyo, ikikadiriwa kuwa kati ya asilimia 61 na 65.
Mikoko ina mchango mkubwa na hulinda pwani dhidi ya mmomonyoko na mawimbi makubwa, huhifadhi bioanuwai na kusaidia uzalishaji wa samaki. Lakini misitu hiyo imekuwa ikipungua kutokana na shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa Zulfa, kuanza kuhifadhi mikoko kulianza kama fursa isiyotarajiwa. Baada ya kusoma hadi kidato cha nne na kusomea taaluma ya ununuzi, alitafuta kazi bila mafanikio. Hatimaye alijitosa katika uhifadhi, hasa upandaji wa mikoko.
Anakumbuka alivyoshangaa mara ya kwanza kusikia watu wakitaka kupanda mikoko katika eneo lao. Wakati huo, wakazi wa Mtangawanda walitumia mikoko kwa kuni, ujenzi, uzio, kuchoma chokaa na shughuli nyingine.
“Baadhi ya wataalamu walikuja hadi eneo letu la Mtangawanda na wakaona mikoko imekatwa sana kwa ajili ya kutengeneza chokaa na wakataka kuipanda. Nikajiuliza mbona hawa wageni wametoka mbali wamekuja eneo letu kupanda mikoko na wakatulipa? Basi nikasema hapa panaweza kutusaidia sisi kama kina mama ambao tamaduni yetu ilituzuia kuingia baharini kufanya uvuvi,” anaeleza.
Baada ya zoezi hilo, Zulfa aliwakutanisha wanawake walioshiriki na kuwashawishi kuanzisha kikundi. Mwaka 2018, walianzisha rasmi Mtangawanda Mangrove Restoration Initiative wakiwa wanawake 14 na mwanamume mmoja. Leo kikundi hicho kina wanawake 35 na wanaume 10, wakiwemo vijana na wazee.
Kutoka mbegu 10,000 hadi mikoko zaidi ya 500,000
Mwanzo haukuwa rahisi. Siku yao ya kwanza walikusanya mbegu 10,000, lakini baada ya kuzichambua waligundua ni 500 tu zilizokuwa zimekomaa na kufaa kwa upandaji.
Kupitia mafunzo kutoka kwa wataalamu, ikiwemo Huduma ya Misitu Kenya (Kenya Forest Service) na washirika wengine, Zulfa alijifunza kutambua aina mbalimbali za mikoko, mahali pa kupanda na wakati unaofaa wa kupanda.
Leo kikundi hicho kimepanda zaidi ya mikoko 500,000 katika zaidi ya hekta 30 na huzalisha takriban miche 50,000 kwa mwaka katika vitalu. Wanapanda aina mbalimbali, zikiwemo mkandaa (Ceriops tagal), mkoko (Rhizophora mucronata), muia (Bruguiera gymnorrhiza) na mchu (Avicennia marina).
Baadhi ya miche huzalishwa na kupandwa na wanakikundi wenyewe, huku mingine ikipandwa pamoja na wageni wanaotembelea eneo hilo. Mche mmoja huuzwa kwa KSh50 ($0.39).
Lakini kwa Zulfa, uhifadhi hauishii katika kupanda mikoko. Kikundi hicho kimeanza shughuli nyingine zinazowasaidia kupata mapato, zikiwemo ufugaji wa nyuki kwenye mikoko na ufugaji wa kaa. Walipokea mizinga 160 ya nyuki na vizimba 150 vya kufugia kaa kutoka NRT.
Wanavuna asali mara mbili kwa mwaka, huku kilo moja ikiuzwa kwa KSh2,000 ($15.45) na kaa kwa KSh1,900 ($14.68). Pia wamejenga daraja la kutembelea mikoko (boardwalk) ambalo huwatoza wageni kati ya KSh200 ($1.54) na Sh2,000 ($15.45), pamoja na ukumbi wa mikutano unaokodishwa kwa KSh5,000 ($38.62) kwa siku. Mapato hayo hugawanywa kati ya taasisi mbalimbali, kikundi na wanachama wake.

Mwanamke mmoja, jamii inayobadilika
Zulfa anasema mafanikio hayo hayakuja bila upinzani. Katika jamii yao, wanawake kwa muda mrefu walikumbana na vikwazo vya kushiriki katika shughuli zinazohusiana na bahari. Pia, elimu kwa wasichana haikupewa kipaumbele.
“Utapata sisi jamii yetu kielimu iko chini. Kwa sababu kusema mwanamke haruhusiwi kwenda baharini, hiyo si dini. Ni mila na tamaduni… Utapata kitambo ilikuwa msichana pia haruhusiwi kwenda kusoma, akishabalehe tu anaolewa,” anasema.
Anasema baada ya kumaliza masomo alirudi katika jamii yake na kuanza shughuli za upandaji wa mikoko, huku mumewe akimuunga mkono. Uhifadhi umemwezesha kutoka kuishi katika nyumba ya familia na kujenga nyumba yake mwenyewe, ambayo pia ina sehemu anayopangisha.
Sasa anasema hana hamu ya kutafuta kazi ya kuajiriwa. Lengo lake ni kuongeza juhudi za upandaji na uhifadhi wa mikoko ili kunufaika zaidi na fursa ya blue carbon, huku akihifadhi mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa Zulfa, safari hiyo imebadili si maisha yake tu, bali pia mtazamo wa jamii kuhusu wanawake na bahari. Mohammed Bwana, mwanamume pekee aliyejiunga na Zulfa tangu kuanzishwa kwa kikundi mwaka 2018, anakumbuka wakati ambapo wanawake hawakuwa wakiruhusiwa kwenda maeneo ya baharini.
“Nilikuwa mwanamume peke yangu tukianza juhudi za kupanda mikoko na Zulfa kwa sababu wanawake walikuwa hawaruhusiwi baharini. Nilikuwa nikisaidia katika kazi ngumu kama kuchimba vitalu, kukusanya mbegu baharini nikiwaletea wao wazipande kwa mifuko.”
Anasema mafunzo kutoka kwa NRT, Fauna & Flora na mashirika mengine yamechangia kubadilisha mitazamo hiyo, na sasa wanawake wengi wanaingia majini kukusanya mbegu.
Kwa Bwana, mabadiliko hayo yameleta manufaa pia kwa familia yake. Kupitia shughuli za uhifadhi, ameweza kuboresha nyumba yake na kuchimba jabo linalokusanya maji ya mvua katika eneo lenye changamoto ya upatikanaji wa maji.
Si kila eneo linahitaji kupandwa mikoko
Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa kurejesha mikoko si suala la kupanda miche pekee.
Dkt Judy Okello, mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Bahari na Uvuvi (KMFRI) na mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mikoko, anapongeza juhudi za jamii, lakini anasema urejeshaji unapaswa kuanzia kwenye kutambua sababu zilizoharibu eneo.

Jamii pia ina maarifa muhimu kuhusu mazingira yake ambayo wataalamu wanapaswa kuyazingatia. “Ningependa tufikirie kupanda kama suluhisho la mwisho kabisa. Kwanza tuangalie mambo gani yamebadilika na tuyatatue, kama mikoko haiwezi kujirejesha yenyewe kupitia njia asilia, ndipo tufikirie kupanda,” anasema Okello.
Kwa wanawake kama Mwanasha na Zulfa, hata hivyo, kuingia baharini kulianza kwa kuvunja kizuizi kimoja kikubwa: imani kwamba bahari haikuwa mahali pa mwanamke.
Sasa wanaingia humo si kwa ajili ya kujipatia kipato pekee, bali pia kurejesha mazingira ambayo jamii zao zimeyategemea kwa vizazi.
Picha ya bango: Mwanasha Mbwana, anayejulikana kama Mama Coral au Mama Matumbawe, akiwa na pweza aliyemvua hivi karibuni. Ili kuwawezesha kupata njia mbadala za kujipatia kipato katika jamii inayotawaliwa zaidi na wanaume, wanawake hawa wamepatiwa mafunzo kuhusu usimamizi wa uvuvi wa pweza katika Pate Conservancy, eneo la bahari linalosimamiwa na jamii. Mapato yatokanayo na uvuvi wa pweza yameonekana kuboresha maisha ya wakazi wa eneo hilo. Mfano ni Shule ya Awali ya Pweza, iliyopo Kisiwa cha Pate, ambayo sehemu ya ufadhili wake ilitokana na fedha zilizopatikana kutokana na mauzo ya pweza. Picha kwa hisani ya © Duncan Moore / Fauna & Flora.
Wakati Tanzania Ikiandaa COP12, Wadau Washauri Vipaumbele vya Bahari
