- Wanawake wa Lamu wanavuka vikwazo vya kitamaduni na kushiriki katika upandaji wa nyasi bahari, usafi wa fukwe na uhifadhi wa kasa.
- Amina Bakari, Mama Nyasi Bahari, anaongoza urejeshaji wa nyasi bahari Pate, akisema juhudi hizo zimechangia kuongezeka kwa samaki.
- Jamila Hassan, Mama Plastiki, anageuza taka za plastiki kuwa bidhaa za kuuzwa, huku akisaidia kusafisha fukwe na kulinda kasa.
- Wanawake hao wanasema uhifadhi umeleta manufaa ya kiuchumi, lakini wanahitaji masoko, utaalamu na ufadhili endelevu.
Hii ni sehemu ya pili ya mfululizo wa makala kuhusua wanawake wanaovunja mila na kurejesha bahari Lamu. Soma Sehemu ya Kwanza hapa.
LAMU, Kenya — Kwa wanawake katika baadhi ya jamii za pwani ya Lamu, kuingia baharini kwa muda mrefu kulionekana kwenda kinyume na mila. Lakini kwa wengine wao, bahari imekuwa mahali pa kuhifadhi mazingira, kuelimisha jamii na kutafuta riziki.
Amina: Samaki wanarudi baada ya wanawake kurejesha nyasi bahari
Amina Bakari, mwanamke kutoka wadi ya Faza, eneo la Shanga Shakani, kisiwani Pate, anajulikana kama Mama Nyasi Bahari, kutokana na kazi ya uhifadhi ambayo amekuwa akifanya baharini.
Mwanamke huyu alisoma hadi darasa la nane. Anatumia elimu yake hiyo kuwafundisha wanajamii kuhusu umuhimu wa kulinda nyasi bahari.
Amina Bakari, mwanamke kutoka wadi ya Faza, eneo la Shanga Shakani, kisiwani Pate, anayejulikana kama Mama Nyasi Bahari. Picha kwa hisani ya Duncan Moore, Flora & Fauna.Amina ni kiongozi wa kikundi cha wanawake cha Shanga Itifaq, kinachofanya kazi ya kuhifadhi ikolojia ya bahari kwa kupanda nyasi bahari na mwani, huku kikilenga kuzuia kuendelea kupungua kwa viumbe wa baharini.
Utafitiunaonyesha kuwa kati ya mwaka 2000 na 2016, eneo la nyasi bahari nchini Kenya lilikuwa likipungua. Kwa wastani, kila eneo la kilomita za mraba 25 lilipoteza kilomita za mraba 1.9 za nyasi bahari. Shanga Itifaq ilianzishwa mwaka 2018 ikiwa na wanawake 13 na wanaume sita.
Siku moja kila wiki, wanachama wake hupanda angalau gunia 17 za kilo 50 za nyasi bahari katika eneo lao la tengefu lililoko Pate Marine Community Conservancy (PMCC), lenye ukubwa wa jumla ya ekari 9,290.
Kwa sasa wamepanda ekari 9 za nyasi bahari aina ya Kambani (Thalassodendron ciliatum), na mtimbi mrefu (Enhalus acoroides). Amina anasema baada ya wiki moja nyasi hizo huwa zimeota na samaki huanza kuonekana katika maeneo hayo, huku akisema asilimia 100 ya nyasi wanazopanda hustawi.
Alianza kwa sababu samaki walipungua
Kwa Amina, msukumo wa kuanza shughuli hizo ulitoka ndani ya familia yake. Mumewe ni mvuvi na alikuwa akilalamika kwamba samaki walikuwa hawapatikani kwa wingi wa kutosha kwa ajili ya kuuza na kwa matumizi ya nyumbani.
Hilo liliwasukuma kujifunza kuhusu umuhimu wa nyasi bahari. “Tulianza kujifunza umuhimu wa kupanda na kutunza nyasi bahari kutoka kwa mashirika kama vile Fauna & Flora International na Northern Rangelands Trust ili kuregesha afya nzuri ya bahari na kurudisha baadhi ya samaki waliokuwa wameanza kupotea,” anasema Amina.
Mbali na upandaji, Amina huongoza mikutano ya uhamasishaji wa jamii. Anasema ametoa elimu kwa takriban watu 65 kuhusu umuhimu wa kupanda na kuhifadhi nyasi bahari. Na sasa, anasema, jamii imeanza kuona matokeo.
Takwimu za Kitengo cha Usimamizi wa Fukwe (BMU) ya eneo lao zinaonyesha kuwa awali wavuvi walikuwa wakirekodi tani mbili za samaki kwa wiki. Kwa sasa, rekodi zinaonyesha tani tano hadi saba kwa wiki.
Wanawake wanadai nafasi yao baharini
Hata hivyo, safari ya Amina haikuwa rahisi. Kwa muda mrefu wanawake katika jamii yake walionekana kutokuwa na nafasi ya kufanya shughuli za baharini. Zaidi ya mila zilizowazuia kwenda baharini, baadhi ya watu waliona hata kazi ya kupanda na kuhifadhi nyasi bahari kuwa jambo la aibu.
Mabadiliko yalianza baada ya jamii kupata mafunzo ya usawa wa kijinsia kutoka Fauna & Flora. Mafunzo hayo, anasema Amina, yaliwasaidia wanawake na jamii kuelewa kwamba wanawake wana haki ya kushiriki katika shughuli za baharini kama wanaume.
“Baada ya kupokea mafunzo hayo, tumefahamu kwamba sisi kina mama tuko na haki sawa na wanaume. Kama wao wanaweza kufanya kazi ya bahari, na sisi pia tunaweza,” anasema.
Mafunzo hayo pia yalibadili mtazamo wa mumewe, Abu Athman. Athman anasema kumuunga mkono mkewe haikuwa rahisi mwanzoni kutokana na mtazamo wa jamii kuhusu nafasi ya mwanamke.
Lakini sasa yeye ni miongoni mwa wanaounga mkono shughuli hizo. “Tumekuwa na mtihani mkubwa sana. Zamani ilionekana mwanamke ni mtu wa kukaa nyumbani, huku kazi za bahari na shughuli za kutafuta kipato zikimlenga zaidi mwanamume. Lakini baada ya watu kuhamasishwa na kupewa mafunzo ya jinsia… watu wengi wameanza kufahamu kwamba mwanamke pia ana nafasi sawa ya kufanya kazi popote,” anasema.
Athman pia anasema amenufaika kutokana na kuongezeka kwa samaki. “Nyasi bahari ni chakula cha samaki na viumbe wengine baharini. Zikiwa zimeimarika, samaki wengi wanakuja na kufanya malisho hapo, na wanakuwa wengi. Binafsi kitambo kwa siku sita nilikuwa naweza kuvua samaki kama tani moja ama moja na nusu, lakini kwa sasa navua tani tatu ama nne,” anasema Athman.
Kwao, uhifadhi wa nyasi bahari umeunganishwa moja kwa moja na riziki ya familia.
Sayansi inatafuta maeneo yanayohitaji kurejeshwa
Juhudi kama hizi zinaungwa mkono na kazi ya watafiti wanaojaribu kuelewa vizuri hali ya nyasi bahari katika ukanda wa magharibi mwa Bahari ya Hindi.
Taasisi ya Utafiti wa Bahari na uvuvi (KMFRI), pamoja na watafiti kutoka Msumbiji Madagaska na visiwa vya Western Indian Ocean, wamekuwa wakitengeneza ramani ya nyasi bahari chini ya mpango wa Large Scale Seagrass Mapping and Management Initiative (LaSMMI). Lengo ni kutambua maeneo ambayo nyasi bahari zinastawi vizuri na kutofautisha maeneo hayo na yale yaliyoathirika.
Charles Muthama, mwanasayansi mtafiti wa nyasi bahari kutoka KMFRI, anasema kama eneo limeharibika kwa zaidi ya asilimia 50, kuna haja ya jamii na wadau wengine kuingilia kati na kulirejesha kwa kupanda nyasi bahari.
Hivyo, kama ilivyo kwa mikoko, uhifadhi wa nyasi bahari unaunganisha maarifa ya jamii, sayansi na mahitaji ya kiuchumi ya watu wanaotegemea bahari. Lakini kwa baadhi ya wanawake wa Lamu, tishio kwa bahari haliko chini ya maji pekee.
Jamila: Vita dhidi ya plastiki kama chanzo cha kipato
Katika hifadhi ya jamii ya Kiunga, Lamu, Jamila Hassan amejikita katika tatizo jingine linaloonekana kila siku kwenye fukwe: plastiki.
Ni takataka zinazoingia baharini kutoka vyanzo mbalimbali na hatimaye kusukumwa na mawimbi hadi ufukweni, zikihatarisha viumbe wa baharini, afya ya jamii na hata uchumi unaotegemea bahari.

Jamila, mama wa watoto watatu, anaongoza kikundi cha Bahari Moja (One Ocean), kinachofanya usafi kwenye fukwe na vijijini, ndani ya hifadhi ya jamii ya Kiunga (Kiunga Community Conservancy), kuondoa plastiki na pia kuhifadhi kasa wa baharini katika hifadhi hiyo.
Juhudi zake zimempa jina la Mama Plastiki. Kikundi hicho kina wanachama 170, wakiwemo wanawake 80, huku wengine wakiwa wanaume na vijana.
Kwa mujibu wa UNEP, kila mwaka tani milioni 19 hadi 23 za taka za plastiki huingia katika mifumo ya ikolojia ya majini, zikichafua maziwa, mito na bahari. Kiasi hicho kinatarajiwa kuongezeka karibu mara tatu ifikapo mwaka 2040 iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.
Jamila anasema alianzisha shughuli hiyo kwa sababu alitaka kuona fukwe na bahari yao zikiwa safi. “Nilichochewa kuanzisha shughuli hii ya kukusanya taka za plastiki kwa lengo la kusafisha fukwe zetu na bahari yenyewe. Bahari ikiwa safi, sisi binadamu pia tunakuwa wenye afya njema,” anasema.
Kwa miaka mitano, mara mbili kila mwezi, Amina huongoza wanawake, vijana na watoto kwenda ufukweni kukusanya plastiki na taka nyingine zinazosukumwa na mawimbi. Baada ya kukusanywa, taka hizo hupangwa na kupimwa kabla ya baadhi yake kubadilishwa kuwa bidhaa.
Taka zinageuka kuwa bidhaa
Baadhi ya plastiki hizo hutumika kutengeneza mapambo kama vipuli, shanga, pazia na vinyago. Huku plastiki nyengine zikitengenezwa kuwa matofali ya ujenzi au kusafirishwa hadi Lamu mjini ambako kikundi hushirikiana na The Flipflopi kuzichakata na kubadilisha vipande vidogo vya plastiki vya viatu vya zamani na kutengeneza viatu vipya.

Bidhaa zao huuza kwa kati ya Shilingi 250 hadi Shilingi 7,000 kwa watalii wanaozuru eneo hilo. Kwa Jamila, mapato hayo yamekuwa muhimu katika maisha ya familia. “Nauza vitu vyangu na napata pesa yangu mwenyewe ambayo inanisaidia kulipia watoto wangu karo shuleni. Kwa sasa sitegemei pesa ya mume wangu,” anasema.
Mwanzoni, baadhi ya watu walikejeli shughuli hiyo. Lakini mtazamo ulibadilika baada ya kuona manufaa yake. Sasa wanawake, wazee na watoto huenda pamoja ufukweni kukusanya plastiki.
Hata mumewe alibadilisha mtazamo. “Mwanzo mwanzo ilikuwa vigumu hata kumshawishi mume wangu kwenda baharini kuokota plastiki, lakini alipoona ninapata pesa, alipendelea na kubadili nia yake. Saa hii tunaenda sote mimi, mzee na watoto,” anasema Jamila.
Soko ni changamoto
Licha ya mafanikio hayo, Jamila anakabiliwa na changamoto ya soko lisilo endelevu. Katika miezi ambayo watalii ni wachache, bidhaa zao hupata wanunuzi wachache. Anasema biashara huimarika zaidi mwezi wa Desemba.
Pia, baadhi ya plastiki iliyoko ndani ya maji ni vigumu kuifikia kwa sababu kikundi hakina boti na wengi wa wanachama hawajui kuogelea. Tatizo jingine ni plastiki inayosukumwa kutoka nje ya eneo hilo. “Utakuta kuwa mnaenda kusafisha bahari leo, mkirudi siku ya pili ni kama hamujafanya kitu,” anasema.
Ili kutafuta soko pana zaidi, kikundi kimeanza kutumia mitandao ya kijamii kama Facebook, TikTok na Instagram kuuza bidhaa zake. Abdull Abuhassan, afisa anayesimamia miradi katika Bahari Moja, anaamini soko bora litawapa wanawake motisha ya kuendelea kusafisha na kutunza bahari.
Plastiki na kasa
Jamila anasema kazi yao pia imeleta mabadiliko kwa kasa wa baharini. Anasema wanawake walipoanza kukusanya plastiki, waliona kasa wakipata shida wakati wa kutaga mayai. Baadhi yao walikuwa wakitaga katika maeneo yenye taka, huku kamba zikinasa na kuwazuia kujinasua.
Sasa, anasema, kasa wanaweza kutaga katika maeneo safi zaidi na kurudi baharini bila matatizo. Kwa Jamila, faida hiyo ya uhifadhi inaenda sambamba na faida ya kiuchumi.
Wanawake wanapopewa nafasi
Jennifer Odero, afisa wa miradi kutoka Fauna & Flora katika kaunti ya Lamu, anasema mafanikio hayo yana uhusiano mkubwa na kubadilika kwa mitazamo kuhusu nafasi ya wanawake.
Fauna & Flora imekuwa ikitoa elimu kuhusu usawa wa kijinsia kupitia mbinu ya Social Analysis and Action, inayolenga pia kuunga mkono Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG 5) kuhusu usawa wa kijinsia, kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu na kupata fursa sawa za uongozi katika maamuzi ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii.
Odero anasema mbinu hiyo imechangia kuondoa baadhi ya vikwazo vya kitamaduni vilivyowazuia wanawake kushiriki katika uongozi na kufanya maamuzi kuhusu rasilimali.
“Kwa muda mrefu kina mama walikuwa wamekosa fursa ya kumiliki na kusimamia rasilimali mbalimbali. Kupitia ushirikiano wetu na shirika la NRT, tumewapatia elimu ya uongozi… Saa hii tunaona ya kwamba kina baba, vijana na kina mama wanafanya kazi kwa pamoja,” anasema.
Kwa mtazamo wake, mwanamke anapopewa elimu na nafasi, manufaa yake huenea hadi familia, jamii na kizazi kijacho. Anasema pia ushirikishwaji wa wanawake katika miradi unaweza kusaidia kutatua migogoro na kufanya miradi iwe endelevu.
Uhifadhi hauwezi kutegemea shauku pekee
Lakini mafanikio ya wanawake hao yanaibua swali kubwa zaidi: je, juhudi za jamii zinaweza kuendelea kwa muda mrefu bila mifumo thabiti ya kitaalamu na kifedha?
Henry Komu, mtafiti kutoka Kenya Forestry Research Institute (KEFRI), anasisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya jamii, serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wengine wanaohifadhi mazingira ya baharini.


Ushirikiano huo, anasema, utawawezesha wanawake na jamii kupata maarifa kuhusu mbinu sahihi za urejeshaji na uhifadhi. “Tukishirikiana kwa pamoja tutaweza kutoa mwelekeo sahihi na kufanya miradi yetu ya uhifadhi wa mazingira ya baharini kwa njia inayostahili,” anasema Komu.
Kwa wanawake kama Amina na Jamila, hata hivyo, matokeo ya juhudi zao tayari yanaonekana katika maeneo wanayoishi: samaki wanaonekana zaidi, fukwe zinasafishwa, kasa wanapata maeneo bora ya kutagia na wanawake wanapata kipato.
Lakini hadithi zao pia zinaonyesha kwamba kulinda bahari si suala la kurejesha mazingira pekee. Ni suala la nani anapewa nafasi ya kuyatumia, nani anashiriki kuyasimamia, na kama watu wanaolinda rasilimali hizo wanaweza kupata maisha bora kutokana na juhudi zao.
Kwa wanawake wa Lamu, safari hiyo inaanza na kuvuka mipaka, ambayo kwa muda mrefu iliwaweka mbali na bahari.
Picha ya bango: Jamila Hassan Shee, anayejulikana kama Mama Plastiki, anaongoza shughuli za usafi wa fukwe, akikusanya taka za plastiki na uchafu wa baharini unaosukumwa na mawimbi hadi ufukweni. Shirika analofanya nalo kazi, Bahari Moja, pia linashiriki katika uhifadhi wa kasa wa baharini kisiwani humo na hutumia plastiki iliyokusanywa kutengeneza bidhaa za mikono. Picha na Duncan Moore, Flora & Fauna.
Teknolojia inayolenga kubadilisha usimamizi wa taka Kenya, huku ikiibua maswali kuhusu ajira
