- Serikali iendelee kutoa elimu nchi nzima, na si Ngorongoro pekee.
- Ngorongoro inazidi kuharibika kwa sababu ya ongezeko kubwa la makazi ya binadamu.
- Bila wanyama na bila utunzaji wa mazingira Ngorongoro itapoteza utambulisho wake.
- Dhana ya kusema eneo fulani ni la kabila moja pekee, inakwenda kinyume cha sheria za nchi.
Ni vigumu kuzungumzia uhifadhi katika maeneo ya Ngorongoro bila kugusia mvutano wa muda mrefu unaohusu uwiano kati ya uhifadhi wa mazingira na wanyamapori, shughuli za utalii, pamoja na haki na maisha ya jamii zinazooishi katika eneo hilo, hususan jamii ya Wamaasai.
Uwiano kati ya uhifadhi na haki za jamii
Msingi wa mvutano huo ni namna ya kusawazisha mahitaji ya uhifadhi na haki za jamii kuendelea kuishi na kunufaika na ardhi ambayo imekuwa sehemu ya maisha yao kwa muda mrefu.
Serikali kwa upande wake inataka baadhi ya wakazi wahame kutoka eneo la hifadhi kwenda maeneo yaliyotengwa kama Msomera, ikieleza kuwa ongezeko la watu na mifugo limeongeza shinikizo kwa ardhi, malisho, mazingira na uhifadhi wa wanyamapori.

Kwa upande wa jamii zinazoishi eneo hilo, baadhi wanapinga kuondoka wakidai kuwa Ngorongoro ni ardhi yao ya asili, ambako wameishi na kuendesha shughuli za ufugaji kwa vizazi, huku maeneo hayo yakiwa na umuhimu wa kiutamaduni na kiimani.Mjadala ulichukua sura mpya mwaka 2022 wakati Serikali ilipoanza kutekeleza mpango wa kuwahamisha kwa hiari baadhi ya wakazi kutoka eneo la Ngorongoro kwenda maeneo mengine, ikieleza kuwa ongezeko la watu na mifugo lilikuwa linaongeza shinikizo kwenye ardhi na rasilimali za hifadhi. Hata hivyo, zoezi hilo lilikumbwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakazi na wadau, waliodai kuwa uhamaji huo haukuwa wa hiari na kwamba wananchi hawakushirikishwa ipasavyo katika zoezi hilo.
Tume za rais
Kutokana na mvutano huo, Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume mbili mwezi Desemba 2024,moja kuchunguza utekelezaji wa zoezi la uhamaji wa hiari kutoka Ngorongoro na nyingine kuchunguza migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro. Tume hizo ziliwasilisha ripoti zao Machi 12, 2026, baada ya kufanya uchunguzi na kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali.
Miongoni mwa mambo yaliyobainishwa na tume ya uhamaji ni kwamba wananchi hawakushirikishwa ipasavyo katika kufanya maamuzi na kwamba zoezi lilitumia zaidi ushawishi wa Serikali kuliko ridhaa ya wananchi. Tume pia ilibaini kuwa zoezi hilo halikufikia malengo yaliyokusudiwa, kwani wakati wa kuwasilishwa kwa ripoti, ni takribani asilimia 7 tu ya kaya zilizokuwa zimehama tangu mpango huo uanze mwaka 2022.
Kwa upande wa uhifadhi, tume ya kuchunguza migogoro ya ardhi ilisema ongezeko la watu na mifugo limeongeza ushindani wa matumizi ya ardhi kati ya makazi, malisho, uhifadhi na utalii. Ripoti hiyo ilieleza kuwa idadi ya watu katika eneo la Ngorongoro imeongezeka kwa kiasi kikubwa tangu hifadhi ilipoanzishwa, sambamba na ongezeko la mifugo na makazi, hali ambayo tume ilisema imeongeza shinikizo kwa mazingira na maeneo ya malisho.
Tume ya kuchunguza zoezi la uhamaji wa hiari iliyoongozwa na Musa Iyombe ambaye ni Katibu Mkuu Mstaafu ilipendekeza zoezi la uhamaji liendelee lakini kwa ushirikishwaji na utoaji wa elimu kwa wananchi, pamoja na kuundwa kwa chombo huru kitakachoratibu mchakato huo, huku huduma za kijamii zikiendelea kutolewa kwa wakazi watakaobaki Ngorongoro.
Tume ya kuchunguza migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo iliyoongozwa na Dk. Gerald Ndika ilipendekeza kufanyiwa marekebisho au kuondolewa kwa mfumo wa matumizi mseto ya ardhi, ambao iliona haukuwa endelevu, na kufanyiwa mapitio kwa sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro ili iendane na hali ya sasa, sambamba na kuwatambua na kuwaorodhesha rasmi wakazi, makazi na mifugo katika eneo hilo.
Mwenyekiti wa Jamii ya Wamaasai, Alaigwanani Isack ole Kisongo (wa pili kulia walioketi) pamoja na baadhi ya wazee wa Maarya baada ya kikao ambacho pamoja na mambo mengine kilikuwa cha kuwalaani vijana wa kabila hilo wanaomshambulia Mwenyekiti huyo kutokana na msimamo wake wa kutaka Ngorongoro ilindwe. Picha na Lekoko Lepilal.
Kauli ya serikali
Akipokea ripoti hizo Machi 2026, Rais Samia alikiri kwamba Serikali ilifanya zoezi hilo kwa nia njema lakini ilikosea katika baadhi ya maeneo, na akaahidi kufanyia kazi changamoto zilizobainishwa na tume. Miongoni mwa mapendekezo ambayo Serikali inapaswa kuyafanyia kazi ni kuboresha ushirikishwaji wa wananchi, kuhakikisha huduma za kijamii zinaendelea kwa wakazi waliobaki, kupata takwimu sahihi za watu na mifugo, na kuanzisha chombo huru cha kuratibu uhamaji wa hiari
Suala hilo limeendelea kuvuta hisia na mijadala kutoka kwa watu mbalimbali huku kila mmoja akieleza msimamo wake kuhusu suala hilo. Miongoni mwao ni Mwenyekiti wa Jamii ya Wamaasai nchini Tanzania, ambaye ana historia ndefu kuhusu eneo hilo.
Kaika mahojiano maalum na Mwandishi wa Mongabay, anaweka wazi utetezi wake wa uhifadhi na masuala kadhaa ambayo yamekuwa kitovu cha mjadala kuhusu mustakabali wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA).
Mongabay: Naomba nianze kwa kukupa nafasi ya kujitambulisha.
Kisongo: Naitwa Isaac ole Kisongo Maijo. Mimi ni Mkristo niliyeamini Biblia, na jina langu la ubatizo ni Isaac.
Mongabay: Ni kwa namna gani Ukristo na uongozi wa jadi vinaendana?
Kisongo: Ukristo na uongozi wa mila havipingani; vyote vinasimamia haki na ukweli. Hili baraza letu la kimila ni kubwa na lina historia ndefu. Wajumbe wanatoka Loliondo, Simanjiro, Tanga, na kila mahali kuja hapa. Mimi nina umri wa miaka 71. Ingawa sikubahatika kwenda shule rasmi enzi za Nyerere, nimejifunza kusoma na kuandika (elimu ya watu wazima). Nimesomesha watoto wangu vizuri; mmoja ni daktari katika hospitali ya KCMC (Moshi).
Mimi ni mhifadhi wa mazingira tangu asili yangu, na nasimamia ukweli kwa misingi ya neno la Mungu kuwa binadamu alipewa bustani ya Eden ili aitunze. Ngorongoro ni kama bustani yetu ya Eden, na lazima tuilinde kwa gharama yoyote kwa faida ya vizazi vijavyo na dunia nzima.
Msukumo katika uhifadhi
Mongabay: Mara kadhaa umesikika ukizungumzia suala la uhifadhi na ulinzi wa maeneo ya hifadhi, huku ukisisitiza haki za wafugaji kama raia halali. Nini kiini cha msimamo wako?
Kisongo: Nilisema kuwa Ngorongoro, kwa asili yake, itapoteza sifa isipokuwa na Wamasai. Vilevile, Ngorongoro bila wanyama na bila utunzaji wa mazingira itapoteza utambulisho wake.
Ngorongoro ni daraja linalounganisha dunia kwa sababu hapo ndipo lilipopatikana fuvu la binadamu wa kwanza na nyayo za kale duniani. Hivyo, ni lazima ilindwe kimataifa kwa sababu ya historia yake kubwa.
Nimezungumza kama kiongozi anayeelewa umuhimu wa mazingira hayo. Nimeshauri serikali iendelee kutoa elimu kwa Wamasai. Kama kiongozi, wajibu wangu ni kusema ukweli daima. Ngorongoro lazima ilindwe na uwepo wa Wamasai utambulike. Nilitumia mfano wa ndege inayopaa ikiwa na mizigo iliyozidi uwezo na marubani wengi mno. Swali ni: Je, tupunguze nini? Je, wabaki wanyama, mizigo, au binadamu? Ni lazima tukae chini na kutathmini jinsi ya kutoa elimu.
Kisheria, Watanzania wote wana haki ya kutembea na kuishi popote ndani ya Jamhuri ya Muungano. Ngorongoro haikaliwi na Wamasai pekee, bali kuna makabila mengine kama Wairaqw na Wasonjo, ingawa inajulikana zaidi kwa jina la Wamasai.
Kila Mtanzania ana haki ya kuishi, lakini lazima tufuate katiba. Hakuna eneo lililotengwa kwa ajili ya kabila moja pekee nchini Tanzania. Wamasai sasa hivi wako kila mahali; Ruvuma, Morogoro, na hata Zanzibar na hakuna anayewazuia kwa sababu ni haki yao kama Watanzania. Hivyo, dhana ya kwamba kuna ardhi ya kabila moja pekee si sahihi.
Mabadiliko Ngorongoro
Mongabay: Kutokana na umri na wadhifa wako, unaonaje tofauti kati ya Ngorongoro ya miaka ya 1960 na 1970 na hii ya sasa?
Kisongo: Ngorongoro ya leo imebadilika sana; inazidi kuharibika kwa sababu ya ongezeko kubwa la makazi ya binadamu. Ikiwa hatutaisimamia vizuri kitaifa na kimataifa, itatoweka. Na si Ngorongoro pekee, bali hata maeneo kama Mlima Kilimanjaro, Ziwa Victoria, bahari, na mito yetu lazima vilindwe. Binadamu ndiye kiumbe mharibifu zaidi wa mazingira duniani ikiwa hataongozwa kwa akili.
Mongabay: Je, ungependekeza nini kifanyike sasa, hususan kuhusu suala la kuwahamisha watu kutoka Ngorongoro kwenda maeneo Msomera na kwingine?
Kisongo: Jambo la kwanza ni elimu kwa Wamasai wenyewe. Lazima wafundishwe kuwa rasilimali zina ukomo. Nashukuru serikali kwa kutenga maeneo mbadala ambako wananchi wanaweza kuishi vizuri bila kuteseka.
Serikali haiwezi kuendelea kujenga shule na hospitali katika eneo ambalo tayari linaangamia. Elimu inapaswa kutolewa kwa miaka kadhaa; labda mitano au kumi, hadi watu waelewe na kuhamia maeneo salama kwa hiari yao. Elimu hii isihusu watu wa Ngorongoro pekee, bali Watanzania wote na Wamasai wa mikoa mingine yote.
Mongabay: Kuna hoja kuwa wakati wananchi wakitakiwa kupungua ndani ya Ngorongoro, idadi ya hoteli za kitalii inazidi kuongezeka. Je, unalionaje hili?
Kisongo: Hayo yote ni mambo yanayopaswa kuangaliwa ili kulinda mazingira. Ikiwa majengo yanajengwa ovyo, ni lazima yadhibitiwe kwani nayo ni sehemu ya ongezeko linaloathiri hifadhi. Nchi yetu ina katiba na sheria zake, na uhuru wetu lazima uheshimiwe.
Tume kuhusu Ngorongoro
Mongabay: Kwa upande wa Serikali, kuna jambo gani ambalo unadhani halijakaa sawa?
Kisongo: Nimeishauri Serikali isitumie nguvu kubwa, bali itoe elimu zaidi. Rais aliunda tume mbili ambazo zilileta majibu sahihi kuwa Ngorongoro lazima ilindwe. Wamasai hawajafukuzwa kikatili, bali wamepewa maeneo mbadala yenye tija. Ngorongoro ni kubwa, inaenea mpaka Loliondo. Serikali imefanya mambo makubwa. Si busara kuendelea kuweka miundombinu ya kudumu ndani ya hifadhi ikiwa eneo hilo limepangiwa matumizi mengine.
Mongabay: Wewe kama mhifadhi, umezungumzia Ngorongoro na Loliondo. Lakini vipi kuhusu maeneo mengine nchini ambako shoroba za wanyama zimevamiwa, kama kule Manyara na Mswakini?
Kisongo: Idadi ya watu imeongezeka na makazi yameingia kwenye shoroba. Serikali ikiona kuna madhara, ina uwezo wa kurekebisha mipango hiyo ili kulinda asili. Huwezi kuishi kwa amani ikiwa umeingilia maeneo ya hatari.
Mongabay: Nini kauli yako kwa Watanzania kuhusu Ngorongoro na uhifadhi?
Kisongo: Kwanza, naiomba jamii iipe serikali nafasi ya kupanga. Bunge lipo kwa ajili ya kusema kero za wananchi. Lazima tuwe na mipango ya maendeleo ili tusonge mbele. Tanzania bado tuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi tukifuata mipango.
Elimu iendelee kutolewa
Mongabay: Una jambo jingine la kueleza?
Kisongo: Naishauri Serikali kuendelea kutoa elimu nchi nzima, na si Ngorongoro pekee. Ngorongoro si mali ya Wamasai pekee, ni mali ya Watanzania. Sitaki Wamasai waonekane wakorofi; nataka waonekane kama raia wanaoheshimu katiba na sheria. Tutumie ardhi kitaalamu. Wakati utafika ambako hatutafuga kienyeji; tutafuga ng’ombe wachache wenye tija kubwa badala ya mamia wasio na faida.
Dhana ya kusema eneo fulani ni la kabila moja pekee ni hatari na inakwenda kinyume na utaratibu wa nchi. Ikiwa tutaruhusu hilo, basi kila kabila litadai eneo lake na kuzuia wengine.
Bomba la mafuta kutoka Hoima kwenda Tanga limepita kwenye maeneo ya watu na wamepisha kwa faida ya taifa. Hivyo ndivyo nchi inavyojengwa. Nchi ni mipango, na maendeleo yanahitaji ushirikiano. Mimi namshukuru Mungu kwa kunijalia kuona maendeleo ya nchi nyingine; nimesafiri kwa ndege na treni za kisasa na nimeona jinsi dunia inavyobadilika.
Mongabay: Nakushukuru sana, Olaiguanani ole Kisongo.
Kisongo: Nami nakushukuru pia. Karibu sana.
Picha ya Bango: Mwenyekiti wa Jamii ya Wamaasai, Alaigwanani ole Kisongo akihutubia Baraza la Mila la Maarya jijini Arusha. Picha na Lekoko Lepilal.
