- Utafiti wa Mongabay umebaini kuwa upotevu wa haraka wa mikoko katika Mkoa wa Zambezia nchini Msumbiji unahusishwa na shughuli za kampuni yaMozambique Heavy Sand Company VIII, ambayo inamilikiwa kwa sehemu na kundi kubwa na lenye ushawishi la uchimbaji madini kutoka China.
- Upotevu huo wa mikoko ulitokea katika eneo linalochukuliwa kuwa “mojawapo ya mifumo ya midomo ya mito yenye bayoanuwaina tija ya kibayolojia kubwa zaidi duniani.”
- Picha za satelaiti zinaashiria kuwa uharibifu huo ulisababishwa na kile kinachoonekanakuwa kuziba kwa njia za maji, ambapo shughuli za uchimbaji wa mchanga zilionekana kufanyika kati ya 2022 na 2026.
- Wanamazingira wanazidi kutoa tahadhari kuhusu athari za kimazingira zinazotokana na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini mazito katika maeneo mapana ya ukanda wa pwani ya Msumbiji.
ZAMBEZI, Msumbiji – Uchunguzi wa Mongabay umebaini kuwa shughuli za uchimbaji wa mchanga kando ya pwani ya Mkoa wa Zambezia, katikati mwa Msumbiji, imeharibu mamia ya hekta za misitu ya mikoko katika miaka michache tu.
Eneo hilo liko chini ya leseni ya kampuni ya Mozambique Heavy Sand Company VIII, ambayo inamilikiwa kwa sehemu na Jinan Yuxiao Group, kampuni ya uchimbaji madini ya China yenye ushawishi mkubwa, inayodai kumiliki zaidi ya hekta 500,000 (ekari milioni 1.24) za ardhi kwa ajili ya shughuli za uchimbaji nchini Msumbiji. Maeneo hayo ya uchimbaji hulenga zaidi mchanga wenye madini mazito, ambayo huwa na madini yenye titani, hasa ilmeniti na rutaili, yanayotumika katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali, kuanzia rangi na plastiki hadi krimu za kujikinga dhidi ya jua.
Wanaharakati wa mazingira wanatoa tahadhari kuhusu hatari zinazotokana na uchimbaji wa madini mazito kando ya pwani ya Msumbiji, na vyombo vya habari vya ndani vimeandika kuhusu tishio linaloongezeka kutokana na shughuli hiyo. “Maeneo yetu yote ya pwani yana miradi hii ya mchanga wenye madini mazito,” alisema Fatima Mimbire, mtetezi wa uwazi katika sekta ya madini nchini Msumbiji katika mahojiano na Mongabay. Aliongeza kwamba kampuni nyingi zinazochimba mchanga huo wenye madini nchini Msumbiji ni za Kichina. “Kampuni hizi zinasababisha uharibifu bila kujali mazingira wala watu wanaoathiriwa.”
Global Mangrove Watch (GMW) ni jukwaa lililoundwa kufuatilia maeneo ambayo mikoko inarejea na yale ambayo inapotea, ndilo lililotoa tahadhari ya kwanza kuhusu upotevu wa mikoko katika wilaya ya Chinde mkoani Zambezia. Lammert Hilarides, mtaalamu wa uchunguzi wa Dunia kwa kutumia picha za setlaiti kutoka shirika la Wetlands International (WI), aliiambia Mongabay jinsi alivyoanza kuona ongezeko la ishara za uharibifu wa mikoko katika eneo hilo mwishoni mwa mwaka 2023. Shirika la WI ni mojawapo ya mashirika yaliyobuni na sasa yanasaidia kuendesha jukwaa la GMW.
Katika miaka iliyofuata, Hilarides, ambaye ni afisa mkuu wa kiufundi katika shirika la WI, alifuatilia taarifa za tahadhari kutoka eneo hilo. Kwa kuchunguza kwa kina mwenendo wa tahadhari hizo, alihitimisha kuwa shughuli za binadamu huenda ndizo zilizosababisha upotevu huo.

Utajiri wa pwani
Msumbiji, nchi iliyo kusini mwa Afrika yenye ukanda wa pwani wa kilomita 2,700 (maili 1,680) kando ya Bahari ya Hindi, ina eneo kubwa zaidi la misitu ya mikoko barani Afrika Mashariki, likiwa na ukubwa wa hekta 304,263 (ekari 751,850).
Miti na vichaka vya mikoko vina uwezo wa kustahimili maji ya chumvi na maji baridi ambayo yanaweza kuua mimea myanayochanganyika. Kiwango kikubwa cha chumvi kwenye maji huifanya iwe vigumu kwa mimea isiyostahimili chumvi kufyonza maji, hali inayoweza kusababisha mimea hiyo kukauka. Spishi mbalimbali za mikoko zimebadilika na kuwa na uwezo wa kuchuja au kutoa chumvi, jambo linaloziwezesha kustawi kando ya pwani, katika maeneo ambayo mito hukutana na bahari (midomo ya mito), na katika maeneo yanayoathiriwa na kupwa na kujaa kwa maji ya bahari.
Eneo la misitu ya mikoko nchini humo lilikuwa likipungua kwa kasi kati ya mwaka 2015 na 2022, kulingana na takwimu za jukwaa la GMW. Katika miaka ya hivi karibuni, Msumbiji imeonyesha ongezeko la jumla la eneo la mikoko, ingawa haijulikani ni kiasi gani cha ongezeko hilo kinatokana na juhudi za kupanda upya mikoko. Misitu ya mikoko inaendelea kupotea nchini humo kutokana na majanga ya asili pamoja na shughuli za binadamu.
Miti hii hulinda makazi ya viumbe wa maeneo ya pwani, ikifanya kazi kama kinga dhidi ya mawimbi yanayoongezeka na nguvu za vimbunga vinavyoikumba nchi hiyo mara kwa mara. Mikoko pia hupotea kutokana na majanga haya ya asili. Uchimbaji wa mchanga usiodhibitiwa kando ya pwani ya Msumbiji si tu kwamba unaleta tishio linaloongezeka kwa mifumo hii ya ikolojia ya baharini na mito, bali pia huharibu ulinzi muhimu dhidi ya majanga ya hali ya hewa.
“Eneo hili katika mdomo wa Mto Zambezi lilijitokeza kwa sababu lilikuwa tofauti sana na maeneo mengine,” Hilarides alisema. “[Kawaida], tunaona tahadhari nyingi katika eneo hili lakini nyingi hutokana na mmomonyoko wa asili wa pwani au dhoruba.” Hii ilimfanya mtaalamu wa Mifumo ya Habari za Kijiografia (GIS) wa jukwaa la GMW kukagua picha za setilaiti tangu wakati tahadhari zilipoonekana. “Picha za setilaiti zilionyesha moja ya midomo ya mto ikifungwa na shughuli za uchimbaji holela wa mchanga,” alisema.

“Msumbiji ni nchi tajiri kwa mchanga wenye madini mazito, hasa ilmeniti,” alisema José Mendes, mwenyekiti wa Chama cha Jiolojia na Uchimbaji Madini cha Msumbiji, shirika la kisayansi linalowakilisha wanajiolojia na wataalamu wa sekta ya madini.
Mara nyingi mdomo wa mto huwa na mkusanyiko mkubwa wa mchanga wenye madini mazito kwa sababu mito mbalimbali huwa na mashapo mengi, kama ilivyo katika mdomo wa Mto Zambezi, Mendes alisema. Mchanga wenye madini hayo hupatikana kando ya mito, kwenye fukwe za mchanga, na kwenye matuta ya mchanga kando ya pwani.
Kuchimba madini mazito kutoka kwenye pwani za mchanga huwa kunabadilisha umbo la pwani na kuondoa mashapo. Picha za setilaiti zilizoonekana na Mongabay zinaonyesha kwamba kuanzia mapema 2022 hadi 2026, shughuli hizi zilifunga njia za maji katika mdomo wa Mto Zambezi, na kukata muunganisho kati ya mdomo wa mto na bahari.
Kubadilisha haidrolojia ya mifumo kama hii, kwa mfano kwa kuzuia mtiririko wa maji ya bahari, kunaweza kubadilisha kemia ya udongo wenye maji mengi na kuhatarisha mikoko.
“Kinachonitia wasiwasi zaidi ni ukweli kwamba baadhi ya miradi hii inatekelezwa bila kuwa na tathmini yoyote ya athari za mazingira,” alisema Mimbire, ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya uongozi ya Mpango wa Uwazi wa Viwanda vya Uchimbaji (Extractive Industries Transparency Initiative, EITI), kikundi chenye makao yake makuu nchini Norway kinachofanya kazi katika kuboresha utawala wa maliasili. Msumbiji ilijiunga na EITI mwaka 2009.
Alielezea alichokiona wakati wa ziara zake katika maeneo ambako uchimbaji mkubwa wa mchanga wenye madini mazito hufanyika, ikiwemo uharibifu wa pwani, matuta ya mchanga na visiwa.

Wawekezaji wa kigeni wanavutiwa na mchanga wenye madini
Maeneo ya pwani ya Msumbiji yamekuwa yakilengwa kwa muda mrefu kwa ajili ya uchimbaji wa mchanga, ambao hutumiwa zaidi katika ujenzi, na kwa kawaida hufanywa na waendeshaji wa ndani. Hata hivyo, katika miongo miwili iliyopita, mchanga wenye madini mazito nchini humo umeanza kuvutia zaidi wawekezaji wa kigeni kutokana na uwepo wa madini muhimu kama vile ilmeniti, zirikoni na rutaili. Zirconium ni elementi ya kemikali inayopatikana hasa katika madini ya zircon, ambayo kwa kawaida hupatikana pamoja na ilmeniti. Rutaili na ilmeniti ni malighafi zinazotumika kutengeneza dioksidi ya titani, ambayo hutumika kama rangi. Msumbiji ni muuzaji mkuu wa malighafi ya titani katika masoko ya kimataifa.
Uchambuzi wa leseni za uchimbaji madini uliofanywa na Mongabay umebaini kuwa ukanda wa pwani wa Msumbiji, hasa katika mikoa ya Inhambane, Zambezia na Nampula, na kwa kiasi fulani Cabo Delgado, kaskazini, umejaa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini. Sehemu kubwa ya maeneo haya imetengwa kwa ajili ya uchimbaji wa mchanga wenye madini mazito, kama vile eneo linalomilikiwa na kampuni ya Mozambique Heavy Sand Co. VIII huko Chinde.
Eneo hilo la uchimbaji huko Chinde, ambapo Hilarides alibaini kupotea kwa mikoko, lina ukubwa wa hekta 3,281 (ekari 8,108) na liko ndani ya eneo pana la mdomo wa Mto Zambezi. Mdomo huo wa mto ni eneo la Ramsar, yaani ardhi oevu yenye umuhimu wa kimataifa kwa sababu inachukuliwa kuwa “mojawapo ya mifumo ya midomo ya mito yenye viumbe hai vingi na tija kubwa zaidi duniani.”
Kwa kuunganisha picha za satelaiti, Hilarides aliandika kumbukumbu za mchakato wa upotevu wa mikoko kwa kipindi cha miaka minne. Katika kipindi hicho, barabara mpya zilijengwa katika eneo hilo la mdomo wa mto na meli kubwa zikaanza kuonekana kwenye njia nyembamba za maji. Kufikia mwanzoni mwa mwaka wa 2026, eneo ambalo awali lilikuwa limejaa mikoko minene na yenye afya lilikuwa limebaki na mfereji wa maji pekee, uliozungukwa na ardhi kavu.
“Ni janga,” alisema Hilarides. “Kama kungekuwa na mpango madhubuti zaidi, hali hiyo ingeweza kuzuilika. Muunganisho kati ya mdomo wa mto na bahari ungeweza kudumishwa, na kuna uwezekano mkubwa kwamba mikoko hiyo ingeweza kuokolewa.”

Wizara ya Rasilimali za Madini na Nishati ya Msumbiji haikujibu maswali ya Mongabay kuhusu upotevu wa mikoko, wala ombi la Mongabay la kupata taarifa za leseni za uchimbaji madini. Taarifa za leseni za uchimbaji ambazo Mongabay ilizipata zinatoka katika wizara hiyo; hata hivyo, serikali ilisema hairuhusu matumizi ya taarifa hizo kwa kuwa kesi hiyo bado inaendelea mahakamani.
Rekodi za umma zilizopatikana na Mongabay zinaonyesha kuwa kampuni ya Mozambique Heavy Sand Co. VIII ni kampuni tanzu inayomilikiwa, kwa kiasi, na Jinan Yuxiao Group. Jinan Yuxiao ndiyo mwekezaji mkuu katika kundi la makampuni yanayofanya kazi chini ya jina la Mozambique Heavy Sand. Makampuni kadhaa yanayohusiana kama vile Mozambique Heavy Sand V, Mozambique Heavy Sand VII, VIII na IX yameanzishwa katika muongo uliopita. Kwa pamoja, makampuni haya yalikuwa na angalau leseni sita halali, ambazo zilikuwa halali mwanzoni mwa mwaka 2026, huku maombi mengine manne yakiwa katika hatua ya tathmini.
Katika tovuti yake, kundi la Jinan Yuxiao linadai kuwa “kampuni kubwa zaidi ya uchimbaji madini ya China nchini Msumbiji.” Kulingana na kampuni hiyo, maeneo yake ya uchimbaji yanakadiriwa kuwa na akiba ya madini ya ziricon na titani inayozidi tani milioni 100.
Kundi hilo limekuwa likifanya kazi katika Mkoa wa Zambezia tangu mwaka wa 2015, wakati kampuni ya Mozambique Heavy Sands ilipopata leseni katika eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 8,613 (ekari 21,283). Mnamo mwaka wa 2022, kampuni hiyo ilikuwa na maeneo mawili yenye leseni za uchimbaji yenye ukubwa wa angalau hekta 8,786 (ekari 21,711) katika wilaya ya Chinde pekee. Rekodi rasmi za mwaka wa 2023 zinaonyesha kuwa kampuni ya Mozambique Heavy Sands ilikuwa ikisafirisha nje maelfu ya tani za madini ghafi ya ilmenaiti kutoka migodini mkoani Zambezia.
Kampuni ya Mozambique Heavy Sand VIII iliomba leseni ya uchimbaji madini mwaka wa 2022 kwa ajili ya eneo ambalo baadaye lilikumbwa na uharibifu wa mikoko. Katika eneo hili, inaonekana kuwa mikoko ilianza kunyauka wakati wa hatua ya utafiti katika eneo ambalo kwa sasa liko chini ya leseni ya uchimbaji Na. 11015.
Kampuni nyingine zinazojulikana kuhusishwa na kundi la Jinan Yuxiao nchini Msumbiji ni pamoja na Africa Great Wall Mining Development Company na Cronus Minerals. Kundi hilo linaendelea na juhudi za kupanua shughuli zake na kwa sasa ina zaidi ya leseni 60 za utafiti wa madini, kulingana na tovuti yake.

Kupunguza madhara
Uharibifu wa mazingira ni suala linalojitokeza mara kwa mara katika sekta hii, kama ilivyoainishwa na mashirika ya kiraia. Mnamo mwaka wa 2024, ripoti iliyotolewa na Centro de Integridade Pública (CIP), ambayo ni tawi la shirika la Transparency International nchini Msumbiji, iliweka wazi uharibifu wa mazingira uliosababishwa na kampuni tatu: Dingsheng Minerals katika Mkoa wa Gaza, Haiyu (Mozambique) Mining Co. Lda katika Mkoa wa Nampula, na kampuni ya Jinan Yuxiao inayojulikana kama Africa Great Wall Mining Development Company katika Mkoa wa Zambezia.
“Takwimu zilizokusanywa kutoka nyanjani zinaonyesha kuwa kampuni hizo zimesababisha madhara makubwa ya kimazingira na kijamii, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa makazi ya viumbe vilivyo hatarini, uchafuzi wa mazingira, pamoja na kuhamishwa isivyofaa kwa wakazi na/au kutolewa kwa fidia isiyo ya haki,” ilisema ripoti hiyo.
“Kila mradi unahitaji hatua fulani za kupunguza athari, kulingana na kiasi cha mchanga kinachochimbwa na eneo ambako uchimbaji unafanyika,” alisema Mendes kutoka Chama cha Jiolojia na Uchimbaji Madini. “Hilo ni jukumu la mwenye leseni ya uchimbaji.”
Kampuni ya Mozambique Heavy Sand Company VIII na Jinan Yuxiao Group hazikujibu maswali ya Mongabay kufikia wakati wa kuchapishwa kwa habari hii.
Mendes alisema kuwa madini yanayochimbwa na kampuni hizi, kama vile titani, huwa na thamani ya sokoni inayokaribia mara 10 ya thamani ya madini ghafi kabla ya kusindika. Lakini sehemu kubwa ya ongezeko la thamani hufanyika nje ya nchi huku Msumbiji ikinufaika kwa kiwango kidogo. China ndiyo mnunuzi mkuu wa malighafi ya titani inayotoka Msumbiji.
“Kwa sasa, Msumbiji haina miundombinu wala nishati ya kutosha kuwezesha usindikaji wa madini kufanyika nchini humo,” alisema. “Wamiliki wa leseni za uchimbaji wanatumia fursa ya hali hiyo kuchukua rasilimali za ndani na kwenda kuzisindikia nje ya nchi.”
Serikali ya Msumbiji inatambua kuwa inapoteza mapato stahiki kutokana na hali hiyo. Mwaka huu, srikali ilifanya marekebisho makubwa ya kanuni za sekta ya madini, ikiwemo kuweka vikwazo dhidi ya usafirishaji wa madini ambayo hayajasindikwa kwenda nje ya nchi.
Hata hivyo, kulingana na Mimbire, sheria hiyo mpya haitumiki kwa leseni za uchimbaji zilizopo, kama vile ile inayomilikiwa na kampuni ya Mozambique Heavy Sand Co. Ltd VIII mkoani Zambezia.
Hilarides aliiambia Mongabay kuwa ana matumaini serikali ya Msumbiji itazingatia matokeo ya utafiti wake na kuchukua hatua za kupunguza uharibifu huo wakati bado kuna muda. “Kurejesha muunganisho kati ya mto na bahari kungeiwezesha mikoko kustawi tena kiasili,” alisema. “Ni hatua inayohitaji juhudi ndogo lakini inaleta matokeo makubwa.”
Matumaini haya yanatokana na uwezo wa miti hiyo kustahimili mazingira magumu: Ikiwa viwango vinavyofaa vya chumvi na mashapo vitarejeshwa, miti iliyosalia inaweza kustawi na kufufua eneo hilo la mikoko. Hata hivyo, muda wa kuchukua hatua unazidi kupungua; Hilarides alisema, “Kadiri unavyochelewa, ndivyo inavyozidi kuwa vigumu.”
Picha ya bango: Mfano wa picha ya eneo la uchimbaji mkubwa wa mchanga nje ya pwani ya Msumbiji. Picha kwa hisani ya Estacio Valoi.
(José Jaco alichangia taarifa kutoka Msumbiji).
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo 27/08/2026