- Tanzania itumie COP12 kama fursa ya urejeshaji wa mifumo ya ikolojia ya baharini.
- Umuhimu wa uhifadhi unaoshirikisha jamii upewe kipaumbele.
- Taka za plastiki, zinaendelea kutishia mifumo ya ikolojia ya pwani na bahari.
- Tayari Serikali ya Tanzania imeunda kamati ya maandalizi ya mkutano huo.
Zikiwa zimesalia siku 39 kabla ya kufanyika kwa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), utakaofanyika Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 6–9 Oktoba, na Tanzania kuwa mwenyeji wake, wadau mbalimbali wameeleza matarajio yao kuhusu tukio hilo na fursa ambazo Tanzania inaweza kuzipata kutokana na nafasi yake hiyo.
Wakizungumza na Mongabay kwa nyakati tofauti, wanaharakati wa uhifadhi wa baionuai za bahari wameshauri masuala muhimu ambayo ujumbe wa Tanzania unapaswa kuyasimamia ili kutatua changamoto mbalimbali za uhifadhi nchini.

Laura Rosset, Mwanzilishi na Mshauri wa Kisayansi wa asasi ya utunzaji wa mazingira ya bahari, Under the Wave anashauri Tanzania itumie mkutano huo kukutafuta ushirikiano na fursa zaidi za kuimarisha ulinzi na urejeshaji wa mifumo ya ikolojia ya baharini, hususan miamba ya matumbawe, misitu ya mikoko, nyasi bahari, pamoja na viumbe wa baharini walio katika hatari ya kutoweka.
Laura anasema kuwa Tanzania itakuwa na fursa kubwa kama mwenyej wa mkutano huo kusukuma ajenda zitakazoweza kuchangia kuleta suluhisho kwa changamoto mbalimbali za uhifadhi wa bahari zinazoikabili nchi kwa sasa
“Tanzania inapaswa kusisitiza umuhimu wa uhifadhi unaoshirikisha jamii, utalii endelevu, elimu ya mazingira, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya jamii za wenyeji, mashirika yasiyo ya kiserikali, serikali, wanasayansi, na sekta ya utalii,” Laura ameiambia Mongabay katika mahojiano.
Taka za plastiki ni tishio
Kwa Laura, moja ya maeneo ambayo Tanzania inapaswa kuyapa kipaumbele ni usimamizi wa taka na kupunguza uchafuzi wa bahari. Anasema taka, hasa plastiki, zinaendelea kutishia mifumo ya ikolojia ya pwani na bahari, ikiwamo Zanzibar na maeneo mengine ya ukanda wa pwani wa Tanzania.
Licha ya uchafuzi wa mazingira ya bahari, Laura anaona kuwa ushirikiano kati ya wadau mbalimbali katika kuokoa matumbawe na misitu ya mikoko nchini ni suala linalopaswa kupewa kipaumbele katika mkutano huo.
Aidha anashauri Tanzania kutumia mkutano huo kuendeleza mikakati ya kuweka kipaumbele katika usimamizi endelevu wa uvuvi unaoongozwa na jamii, kwa kuwashirikisha moja kwa moja wavuvi wa pwani katika maamuzi ili kuhakikisha uhifadhi unaendana na mahitaji ya kiuchumi ya wananchi.
Dk. George Lushingisha, Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), anatoa wito kwa Tanzania kutumia uenyeji wake kupata nanufaa katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 mintarafu Uchumi wa Buluu.

Akijibu swali la Mongabay lililotaka kujua mapendekezo yake kuhusu vipaumbele ambavyo Tanzania inapaswa kwenda navyo katika Mkutano wa COP 12, Dk. Lushingisha anasema uenyeji wa Tanzania unaweza kuwa na manufaa makubwa iwapo Watanzania watatumia fursa hiyo kusukuma ajenda zinazotatua changamoto zake katika uhifadhi wa bahari.
“Uchafuzi wa bahari ni tatizo kubwa hivi sasa hasa kutokana na taka ngumu na taka za plastiki kwa hiyo ushirikiano baina ya nchi za Bahari ya Hindi Magharibi ni muhimu kwa kuwa maji ya bahari yanatembea. Bahari ikichafuliwa sehemu moja inaathiri pia sehemu nyingine,” alisema Dk. Lushingisha.
Moja ya maeneo yanayotajwa kuzingatiwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ni uhifadhi bahari na Taifa kunufaika zaidi na rasilimali za bahari ikiwa ni pamoja na jamii ya pembezoni mwa bahari.
Kwa mujibu wa Tanzania Investment and Consultant Group (TICGL), taasisi inayojihusisha zaidi na utafiti wa uchumi, ushauri wa uwekezaji na ushauri wa biashara/sera, bahari hivi sasa inachangia takriban $10.5 bilioni kwenye uchumi wa Tanzania, kwa makadirio ya mwaka 2025.
COP12 iwe fursa ya kuimarisha ushirikiano
Yusuf Issa, Ofisa Programu wa Sustainable Ocean Alliance (SOA), shirika lisilo la kiserikali lililojikita katika masuala yanayohusu uhifadhi wa bahari, ameiambia Mongabay kuwa Tanzania inapaswa kutumia fursa ya mkutano huo kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine wanachama wa Mkataba wa Nairobi ili kuongeza kasi ya urejeshaji wa nyasi-bahari na matumbawe ambayo uhifadhi wake unakabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Masuala kama uimarishaji wa mapambano dhidi ya uchafuzi wa bahari hususan kwa taka za plastiki, usimamizi endelevu wa uvuvi na vita dhidi ya uvuvi haramu, ni baadhi ya mambo yanayohitaji kujadiliwa,” alisema.

“Tanzania inapaswa kutumia COP12 kuonesha jinsi maeneo ya hifadhi za baharini yanayosimamiwa na jamii, na juhudi za urejeshaji zinazoongozwa na jamii zinavyoweza kuchangia kulinda mifumo ikolojia ya bahari na pwani,’’ anasema.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Kitengo cha Maendeleo ya Uchumi wa Buluu na Uratibu, Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Magdalena Ngotolainyo, Tanzania inakwenda kwenye mkutano huo ikiwa imepania kufungua fursa za kiuchumi ikiwemo uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu, kuimarisha sekta za uvuvi na utalii, pamoja na kuanzisha miradi ya kikanda ya hifadhi ya mazingira ya Bahari na ukanda wa pwani.
Ajenda za mkutano
Mhandisi Gregory Mella, Mhadhiri wa chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa kuwa mkutano huo utalenga kutafuta mizania ya vipaumbele vya uhifadhi huku jamii za pwani ya Bahari ya Hindi zikinufaika na rasilimali za bahari.
Tayari Serikali ya Tanzania imeunda Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo wenye Kauli mbiu ‘Bahari Yetu, Urithi Wetu, Mustakabali Wetu’ inayojumuisha wadau kutoka wizara, taasisi na idara za serikali.
Mkutano wa 12 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi unakuja wakati nchi wanachama – Tanzania, Kenya, Msumbiji, Madagascar, Shelisheli, Mauritius, Somali, Comoros, Afrika Kusini na Reunion ya Ufaransa zikikabiliwa na kuongezeka kwa uchafuzi wa mazingira ya bahari kwa taka za kielektroniki na plastiki na hatari kwa viumbe wa baharini kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa nchi za Mkataba wa Nairobi zinaongeza juhudi za kukabiliana na uchafuzi wa plastiki, kulinda baionuai ya hewa ukaa ya baharini (blue carbon ecosystems) kama mikoko na nyasi bahari, na kuhifadhi viumbe walio hatarini kama vile kasa wa bahari.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka UNEP kuhusiana na ajenda za mkutano huo, masuala muhimu yatakayojajdiliwa ni pamoja na uchafuzi wa bahari hasa kwa taka za plastiki, kuboresha mifumo ya usimamizi taka mijini na vijijini, kudhibiti uchafuzi wa bahari kutoka viwandani na kwenye meli na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa mazingira ya bahari.
Mengine ni kuimasharia uhifadhi shirikishi wa bahari na kulinda mimea na viumbe wengine wa baharini.
Picha ya bango: Mzamiaji akichunguza mimea bahari kwa ajili ya urejelezaji. Picha kwa Hisani ya SOA Tanzania.