- Licha ya ongezeko la juhudi za kimataifa za kuhifadhi na kurejesha mikoko, miradi mingi inashindwa; wataalamu wanasema sababu moja ni kwamba juhudi za urejeshaji mara nyingi huongozwa na vikundi vidogo vya jamii vyenye rasilimalichache na utaalamu mdogo.
- Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, shirika lisilo la kiserikali la Seatrees,lenye makao yake makuu huko California, limeunga mkono miradi ya urejeshaji wa mikoko nchini Kenya, Mexico, Marekani na Indonesia kwa kutoa ufadhili wa kupanua upandaji miti, kutoa zana za usimulizi wa hadithi na kujenga uwezo katika sayansi, ufuatiliaji na kipimo cha athari.
- Nchini Kenya, ambapo juhudi zake za urejeshaji zimeendelea zaidi, Seatrees na mshirika wake wa mradi wa ndani wameunga mkono zaidi ya vikundi 30 vya jamii kupanda miche zaidi ya milioni mojaya mikoko, kudumisha vitalu, kuchimba mitaro ili kuboresha haidrolojia na ubora wa maji na kufanya doria katika maeneo ya misitu kwa ajili ya ukataji miti haramu, huku wakiwalipa washiriki kwa kazi hii muhimu.
- Shirika la Seatrees hivi karibuni limefadhili uanzishajina uendeshaji wa kitalu cha miche ya mikoko huko Florida Keys, kinachoendeshwa na CoastLove, shirika lisilo la kiserikali la ndani ambalo linawashirikisha wakazi na watalii katika shughuli za vitendo.
Misitu ya mikoko, inayopatikana kando ya pwani za kitropiki, inazidi kutambuliwa kwa jukumu lake katika kuzuia majanga ya hali ya hewa, kuhifadhi kaboni, kusaidia wanyamapori na maisha ya jamii za pwani. Hata hivyo, hata kama nia ya uhifadhi na urejeshaji wa mikoko imeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, miradi mingi hushindwa, miche hufa, maeneo huharibika zaidi au jamii hujitenga.
Sababu moja, kulingana na Catherine Lovelock, profesa katika Shule ya Mazingira katika Chuo Kikuu cha Queensland nchini Australia na mtaalamu wa ikolojia ya mikoko, ni kwamba juhudi za urejeshaji mara nyingi huongozwa na vikundi vidogo vya jamii vyenye rasilimali na utaalamu finyu. Kwa kweli, tafiti zimeonyesha kuwa karibu 70% ya miradi ya urejeshaji mikoko katika baadhi ya maeneo, hasa Asia ya Kusini-mashariki na Amerika Kusini, huwa na viwango vya chini vya mafanikio.
Ili kuziba pengo hili, mashirika mengi yasiyo ya faida yanatumia uzoefu wao wa kutafuta fedha na uhamasishaji wa rasilimali ili kusaidia jamii za wenyeji kufanya urejeshaji kwa ufanisi zaidi.
Seatrees, shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu huko California (zamani lilijulikana kama Sustainable Surf), ni mojawapo ya mashirika hayo. Badala ya kuendesha miradi yenyewe, shirika hilo linashirikiana na vikundi vya jamii na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali, likitoa ufadhili, utaalamu wa kisayansi na usaidizi wa vyombo vya habari ili kuongeza jitihada za urejeshaji wa pwani na baharini duniani kote, ikiwa ni pamoja na mikoko.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, shirika la Seatrees limeunga mkono miradi ya urejeshaji wa mikoko nchini Kenya, Mexico, Marekani na Indonesia “kwa kutoa fedha zinazohitajika sana ili kuongeza upandaji miti, kutoa zana za usimulizi wa hadithi na kujenga uwezo katika sayansi, ufuatiliaji na kipimo cha athari,” Leah Hays, mkurugenzi wa programu, aliiambia Mongabay.
Shirika la Seatrees ni mojawapo ya mashirika karibu 130 duniani kote yaliyotambuliwa na watafiti katika Chuo Kikuu cha California, Santa Cruz (UCSC), kama mashirika yanayotekeleza jukumu la mpatanishi katika urejeshaji wa mfumo ikolojia. Shirika hilo lilipata alama za juu kwa kufuata mbinu bora na kujitolea kwa uwazi katika utafiti wa UCSC, kama ilivyoandikwa katika Orodha ya Shirika la Urejeshaji Misitu Duniani.

Kuandamana na wimbi la urejeshaji
Seatrees hufuata vigezo thabiti wakati wa kuchagua miradi na washirika wa kuwasaidia. Shirika hilo hupendelea kushirikiana na vikundi vidogo vya kijamii “vyenye uzoefu uliothibitishwa katika kusimamia miradi ya urejeshaji wa mazingira, pamoja na uhusiano imara na mamlaka na taasisi za kitaaluma,” lakini yakiwa na “mapungufu ya uwezo ambayo Seatrees linaweza kusaidia kuziba,” anasema Hays.
Wakati huo huo, huchagua miradi ambayo ina kibali cha kufanya kazi katika eneo husika na kuungwa mkono na jamii ya eneo hilo, jamii za asili na wadau wengine husika, aliongeza.
Kwa mfano nchini Kenya, shirika la Seatrees limeshirikiana na Community Based Environmental Conservation (COBEC), shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi ngazi ya jamii katika maeneo ya pwani kurejesha na kulinda mifumo ya ikolojia ya mikoko. Mpango huo, ulioanza mwaka wa 2020, umesaidia kurejesha zaidi ya hekta 600 (ekari 1,483) katika mfumo wa ikolojia wa mikoko wa Marereni na hekta 153 (ekari 378) katika eneo la Mida Creek, sehemu ya Hifadhi ya Viumbe Hai ya Malindi-Watamu.

Kwa pamoja, washirika wameunga mkono zaidi ya vikundi 30 vya jamii nchini Kenya kupanda miche zaidi ya milioni moja ya mikoko, pamoja na kutunza vitalu, kuchimba mitaro ili kuboresha haidrolojia na ubora wa maji, na kufanya doria katika maeneo ya misitu ili kugundua ukataji miti haramu, huku wakilipwa kwa kazi hiyo muhimu, Hays alisema.
Posho husambazwa kwa viongozi wa vikundi kulingana na idadi ya miche iliyopandwa, huku vikundi vingi vikichagua kukusanya mapato yao ili kuwekeza tena katika njia mbadala za kujipatia riziki, kama vile ufugaji nyuki, utalii wa ikolojia na ufugaji, Hays alisema, akibainisha kuwa vyanzo hivi vya mapato husaidia kutoa utulivu wa kifedha mara tu kazi ya urejeshaji inapopungua au kukamilika.
Shirika la Seatrees huelekeza fedha kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo michango ya makampuni na watu binafsi pamoja na ruzuku kutoka kwa taasisi, ili kusaidia miradi ya urejeshaji wa mazingira ulimwenguni kote. Miradi yake inajumuisha mipango inayoongozwa na jamii huko Papua Magharibi, Indonesia, inayolenga kurejesha maeneo ya msitu wa mikoko ulioharibiwa vibaya katika Kisiwa cha Biak, pamoja na mradi unaoongozwa na wanawake huko Laguna San Ignacio, Mexico, unaolenga mfumo wa ikolojia wa mikoko wa El Dátil; eneo hili ni sehemu ya Urithi wa Dunia na pia ni ghuba ya kuzaliana ya nyangumi wa kijivu (gray whale Eschrichtius robustus).

Hivi karibuni, shirika la Seatrees limefadhili uanzishwaji na uendeshaji wa kiutalu cha miche ya mikoko katika eneo la Florida Keys, mkusanyiko wa visiwa takriban 1,700 vilivyo karibu na pwani ya kusini ya Florida, Marekani. Kitalu hicho kinaendeshwa na CoastLove, shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake Florida, linalowashirikisha wakazi na watalii katika shughuli za upandaji na utunzaji wa maeneo hayo, na hivyo kuwawezesha kujifunza kupitia vitendo.
“Wakazi wa eneo hilo, wageni na mashirika ya ushirikiano hushiriki moja kwa moja katika siku zetu za kujitolea kwenye bustani, hafla za upandaji na shughuli za usafi [wa pwani],” alisema Lanier Whitton, mratibu wa urejeshaji mazingira wa CoastLove, aliongeza: “Tunajitahidi kutoa elimu na kuwashirikisha watu wanaojitolea katika kila hatua ya shughuli zetu.”
Whitton alisema kuwa urejeshaji wa mikoko katika eneo la Florida Keys ni jambo la “muhimu sana,” kwani visiwa hivyo vya chokaa vilivyo katika maeneo ya chini viko hatarini zaidi kuathiriwa na kupanda kwa kina cha bahari, vimbunga na shughuli za maendeleo ya pwani.

Kupata uwiano kamili na kukabiliana na changamoto
Kulingana na Lovelock, ambaye alishiriki katika kuandika ripoti ya “Miongozo ya Mbinu Bora za Kurejesha Misitu ya Mikoko,” hakuna mbinu moja inayofaa kwa hali zote za urejeshaji wa mikoko; badala yake, mafanikio hutegemea kwa kiasi kikubwa hali za kiuchumi na kijamii pamoja na usanifu wa kiikolojia.
“Mikoko hustawi zaidi inapofunikwa na maji ya mawimbi kwa saa chache kwa wakati mmoja,” alisema Lovelock, akibainisha kuwa kufunikwa na maji muda wote au kukosekana kabisa kwa mafuriko ya mawimbi kunaweza kusababisha mikoko kushindwa kukua. Pia alieleza umuhimu wa kuhakikisha eneo la urejeshaji liko katika mazingira mwafaka zaidi kwa ukuaji wa mikoko, ambapo hali ya mazingira inafaa na muktadha mpana zaidi unazingatiwa, ikiwa ni pamoja na taratibu za umiliki wa ardhi, utegemezi wa jamii kwa mikoko, na visababishi vingine vya eneo husika vinavyochangia ukataji miti au uharibifu wa mazingira.
Orion McCarthy, Kiongozi wa masuala ya sayansi katika shirika la Seatrees, alisema kuwa ingawa wanawaamini washirika wa miradi kuongoza shughuli hizo katika maeneo husika kutokana na ujuzi wao wa ndani, shirika hilo huwashauri kuhusu mbinu bora za urejeshaji na ufuatiliaji. Aidha, aliongeza kuwa wanafadhili mikakati ya “usimamizi unaobadilika kulingana na hali”, ili washirika waweze kushughulikia changamoto na fursa zinazojitokeza.

Kwa mfano, nchini Kenya, shirika la Seatrees lilianza kufadhili uchimbaji wa mitaro ili kuboresha haidrolojia pamoja na upandaji miti “wakati ilipobainika kuwa sehemu moja ya eneo lao la mradi ilikuwa inakabiliwa na chumvi nyingi na maji yaliyotuama,” McCarthy aliiambia Mongabay.
Hays alisema shirika hilo pia linawaunga mkono washirika wa mradi katika kufuatilia uhai wa miche ya mikoko katika maeneo yote ya mradi kwa miaka miwili baada ya kupanda na katika kufanya matengenezo ya mara kwa mara ya eneo. Hii ni muhimu kwa sababu maeneo ya urejeshaji yanaweza kuathiriwa na matukio ya hali ya hewa na vitisho vingine.
“Washirika wetu wa mikoko kwa kawaida huripoti viwango vya uhai wa miche vya kati ya asilimia 50 na 80 katika maeneo yenye kiwango cha chini na yale yenye kiwango cha juu cha uhai, mtawalia,” McCarthy alisema.

Katika eneo la Florida Keys, CoastLove ilirekodi kiwango cha uhai cha zaidi ya 80% katika eneo lake jipya la upandaji wa mikoko mwaka wa 2025. Whitton alielezea kwamba timu hiyo hufanya ziara za maeneo mwezi mmoja baada ya kupanda “ili kuhakikisha kila kitu kinaonekana vizuri,” huku ziara za ufuatiliaji zikifanyika miezi 3 hadi 6 baadaye.
Shirika la CoastLove pia hufanya matengenezo ya kivitendo wakati changamoto za msimu, kama vile mwani wa kahawia na nyasi baharini zilizooshwa, zinahitaji kushughulikiwa. “Kulingana na msongamano, tunapaswa kuondoa mwani huo, au nyasi hizo ufukweni wakati mwingine,” Whitton alisema.
Mratibu wa urejeshaji alisema shirika la CoastLove hufuatilia mabadiliko mengine ya mazingira katika maeneo yao, ikiwa ni pamoja na kifuniko cha mimea na uthabiti wa ufuo, huku likifuatilia ushiriki wa wanaojitolea na wa jamii.
“Tumekuwa na mamia ya wanaojitolea na tumeshirikiana na mashirika mengi nchini na nje ya nchi,” Whitton alisema. “Hii imepanua uwezo [wetu] wa urejeshaji huku ikiongeza uelewa wa umma kuhusu mifumo ya ikolojia ya mikoko na umuhimu wake.”

Ufuatiliaji na utoaji taarifa za mafanikio
Ufuatiliaji wa kila mara na kuripoti kwa uwazi matokeo ya mradi ni msingi mwingine wa urejeshaji wenye mafanikio, Lovelock alisema. Ufuatiliaji huwasaidia mameneja kuona ni shughuli zipi zinazohitaji marekebisho, huku utoaji taarifa ukiwaonyesha wadau kwamba mradi unafanya kazi na kuwaweka washiriki katika mradi, mtaalamu wa mikoko alieleza.
Kulingana na McCarthy, miradi ya shirika la Seatrees inalenga zaidi kufuatilia uhai wa miche, lakini nchini Kenya, ambapo juhudi za urejeshaji zimepiga hatua zaidi, wamekuwa wakifuatilia vipimo vya kijamii, kiuchumi na bioanuwai, kama vile maisha bora, msongamano wa mikoko, utofauti wa samaki na wanyama wasio na uti wa mgongo, pamoja na uwepo wa nyani.
Mnamo Desemba mwaka wa 2024, shirika la COBEC lilifanya utafiti wa kijamii huko Marereni ili kutathmini athari za mradi huo kufikia wakati huo na kubaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa. Ingawa matokeo mengi yalikuwa chanya, kwa mfano, asilimia 90 ya washiriki waliopanda mikoko walisema mradi huo uliboresha hali yao ya maisha, utafiti huo pia ulibaini changamoto zinazoendelea, ikiwa ni pamoja na asilimia 88 ya wakazi kuripoti kuwa ukataji haramu wa miti bado ulikuwa tatizo.

Matokeo ya utafiti, ambayo yalitangazwa na shirika la Seatrees, yanaonyesha kujitolea kwa shirika katika kuripoti kwa ushahidi na kwa uwazi, unaotambua mafanikio na mapungufu, McCarthy alisema, akibainisha kuwa matokeo hayo yamefahamisha mipango yao ya baadaye ya mradi huo.
Shirika pia linawekeza katika usimulizi wa hadithi kwa njia ya picha, kwa kutumia upigaji picha na video ili kuongeza uelewa na kuchangisha fedha kwa shughuli ambazo mara nyingi hupuuzwa ikilinganishwa na upandaji miti, lakini ni muhimu kwa athari kubwa zaidi, kama vile doria za misitu, matukio ya ushirikishwaji wa jamii na ufuatiliaji wa muda mrefu.
“Watu wanaelewa kwa urahisi athari na thamani ya kupanda mti,” Hays alisema. “Lakini inaweza kuwa vigumu kuwasilisha umuhimu wa shughuli za ziada za usimamizi … na namna zinavyoongeza faida kubwa kwa jamii na bioanuwai ya ndani.”
Kadiri hamu ya kimataifa ya urejeshaji wa mikoko inavyoongezeka, shirika la Seatrees na washirika wake wanaonyesha kuwa mafanikio hayategemei tu idadi ya miti iliyopandwa, bali pia jinsi sayansi, ushirikishwaji wa jamii na usimulizi wa hadithi vinavyounganishwa.

Picha ya juu: Shirika la Seatrees na mshirika wa mradi, COBEC, pamoja na wanajamii wa eneo hilo huko Marereni, Kenya. Picha kwa hisani ya Seatrees.
Nukuu:
Lovelock, C. E., Barbier, E., & Duarte, C. M. (2022). Tackling the mangrove restoration challenge. PLOS Biology, 20(10), e3001836. doi:10.1371/journal.pbio.3001836
Friess, D. A., Gatt, Y. M., Ahmad, R., Brown, B. M., Sidik, F., & Wodehouse, D. (2022). Achieving ambitious mangrove restoration targets will need a transdisciplinary and evidence-informed approach. One Earth, 5(5), 456-460. doi:10.1016/j.oneear.2022.04.013
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereza mnamo tarehe 06/02/2026
Je, rekodi za upanzi wa mikoko ni suluhu ya urejeshaji wa misitu iliyoangamia?