- Teknolojia ya upangaji taka ya kiotomatiki inaanza kujaribiwa Kenya, kupitia ushirikiano wa TakaTaka Ni Mali na TrashCon, huku Kisii ikiwa eneo la kwanza la utekelezaji.
- TrashBot inalenga kutenganisha taka zilizochanganyika kwa kasi na ufanisi mkubwa, ikitenganisha taka za kikaboni, metali na vifaa vinavyoweza kurejelewa.
- Teknolojia hiyo inaweza kufanya usimamizi wa taka kuwa salama na kuongeza urejeleshaji, lakini inaibua wasiwasi kuhusu ajira za wakusanya taka wasio rasmi.
- Wadau wanasema mashine hazitachukua nafasi ya wafanyakazi, bali zitawasaidia katika ukusanyaji, uendeshaji wa mashine na udhibiti wa ubora. Kazi itakuwa kuona kama ahadi hiyo itatimia.
NAIROBI, Kenya – Asubuhi inapopambazuka juu ya Dandora, moshi wa kijivu hutanda angani. Kabla ya wakazi wengi wa Nairobi kuamka, wakusanya taka tayari wako kwenye kilima, wameinama juu ya taka za asubuhi, wakitenganisha plastiki, vioo, mabaki ya chakula na vifaa vingine kwa mikono mitupu. Miongoni mwao ni Nick Mulwa, ambaye amefanya kazi kwenye dampo hili kwa miaka saba na anaweza kukadiria bei ya kilo ya plastiki kwa jicho tu.
“Nimekulia vijijini Kitui na pia nimeishi hapa Dandora. Nimefanya kazi kwenye dampo hili kwa muda mrefu, lakini hata na uzoefu wangu, si rahisi kujua ni nini kinaweza kukuumiza. Nimenusurika mikato, majeraha ya kuchomwa na vitu vyenye ncha kali, na majeraha mengine yanayohusiana na kazi hii,” Mulwa aliiambia Mongabay kwa lugha ya mtaani ya Sheng, huku akionyesha alama za mikato aliyopata kutokana na kubeba magunia ya taka, kwenye mikono, miguu na shingo yake.
Kazi yake ni kiungo cha kwanza katika mnyororo wa taka nchini Kenya na ni miongoni mwa kazi ngumu zaidi. Utafiti wa mwaka 2025 kuhusu wakusanya taka wa Dandora ulibaini kuwa asilimia 96 walikuwa wamejeruhiwa katika eneo hilo, na asilimia 71 waliripoti matatizo ya kiafya, huku asilimia 15 waliotumia vifaa kamili vya kujikinga. Wengi hupata kati ya KSh300 na KSh500 ($2.23 na $3.86) kwa siku, na karibu saba kati ya kumi wanasema kiasi hicho hakitoshi kukidhi mahitaji yao.
Dampo hili lilitangazwa kuwa limejaa mwaka 2001, robo karne iliyopita, lakini bado hupokea takribani tani 2,000 za taka za jiji kila siku, na kila asubuhi, yeye na maelfu kama yeye wanalisubiri.

Umbali mfupi kutoka hapo, Risper Gachambi anaendesha kituo kidogo cha kukusanya na kununua taka zinazoweza kurejelewa. Huzipima, huzichambua zaidi na kuzikusanya kwa wingi kwa ajili ya wachakataji walioko mbele, naye huona ukosefu wa ufanisi wa mfumo kwa karibu: taka hufika zikiwa zimechanganyika na kuchafuliwa, hivyo kuwa ngumu kushughulikia, jambo linaloshusha bei ya kila kinachopita mikononi mwake.
“Ingawa kupanga taka ngumu hapa ni vigumu sana, uchafu pia hupunguza kiasi tunachowalipa wakusanya taka. Usipopanga taka vizuri, unaweza kufunga biashara kwa sababu ya hasara,” Gachambi alieleza.
Ukosefu huo wa ufanisi ndio hasa unaomkera Geoffrey Mosiria, Afisa Mkuu wa Kaunti ya Nairobi anayehusika na Mazingira na Usimamizi wa Taka, ambaye kwa mwaka uliopita amekuwa akijaribu kuhakikisha utenganishaji wa taka unaotekelezwa kwenye sera unafanyika pia kwa vitendo.

Kaunti ya Nairobi iko katika mchakato wa kukabidhi huduma za usimamizi wa taka kwa kampuni ya kimataifa yenye utaalamu. Kenya ina sheria, anasema. Kile ambacho haijawahi kuwa nacho ni miundombinu ya kufanya utenganishaji uwe na maana kwa watu wanaotakiwa kuufanya.
“Lengo ni kutumia uzoefu wa kampuni hiyo katika nchi nyingine ili kusimamia taka zetu vizuri hapa. Mara tu masuala machache ya kisheria yaliyosalia yatakapotatuliwa, tutatekeleza kikamilifu makubaliano hayo, lakini kwa sasa, kama kaunti, tunabaki na jukumu la usimamizi wa taka,” Mosiria alisema.
Ni katika pengo hili — kati ya matarajio makubwa ya Kenya ya uchumi duara na uhalisia mgumu wa jinsi taka zinavyoshughulikiwa — ndipo ushirikiano mpya umeibuka. TakaTaka Ni Mali, kampuni ya usimamizi wa taka inayoongozwa na wanawake iliyoanzishwa mwaka 2017, imeungana na TrashCon, kampuni ya teknolojia ya taka kutoka Bengaluru, India, ili kuleta upangaji wa kiotomatiki katika mifumo ya taka nchini Kenya.
TakaTaka Ni Mali ilianzishwa na Mary Ngechu, akilenga kugeuza taka kuwa rasilimali ya kiuchumi, kuunda ajira kwa wanawake na vijana. Ndiyo maana kampuni hizi ziliingia katika ubia huu: kuunganisha teknolojia, ujuzi na mitandao ili kuongeza urejelshezaji na thamani ya taka.
Ushirikiano huu unawezeshwa na TRANSFORM, mfuko wa kuharakisha biashara zenye athari chanya unaoongozwa na Unilever, Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza, pamoja na kampuni ya ushauri ya EY.
Hoja kuu ni wazi. “Changamoto ya taka nchini Kenya haiwezi kutatuliwa kwa ukusanyaji pekee. Tunahitaji miundombinu, teknolojia, data, masoko na watu wakifanya kazi pamoja,” alisema Ngechu.
Ukubwa wa tatizo unaeleza uharaka wake. Kenya huzalisha takribani tani 24,000 za taka kwa siku, sawa na tani milioni 8.8 kwa mwaka, na zaidi ya robo tatu ya taka hizo hazishughulikiwi ipasavyo, kwa mujibu wa uchambuzi wa sekta wa mwaka 2024. Ni asilimia 25 tu ya taka zinazozalishwa nchini zinazokusanywa kupitia mfumo rasmi, na ni chini ya moja ya kumi inayochakatwa upya. Taka za kikaboni, ambazo huoza haraka na kuzalisha methani, ni asilimia 70 hadi 80 ya lundo lote.
Teknolojia iliyoko kiini cha makubaliano haya ni “TrashBot” ya TrashCon, ambayo watengenezaji wake wanasema hutenganisha taka za manispaa zilizochanganyika kuwa makundi ya kikaboni na yasiyo ya kikaboni kwa ufanisi wa zaidi ya asilimia 90, katika uwezo wa kushughulikia nusu tani hadi tani 12.5 kwa saa.
TrashBot kwanza huvunja na kusogeza taka zilizochanganyika kwenye mfumo wa mikanda, ambapo sumaku hutenganisha metali, huku mfumo wa hewa ukitumia tofauti za uzito na unyevu kutenganisha taka za kikaboni na zisizo za kikaboni. Taka hizo hutoka katika mikondo tofauti kwa ajili ya mboji, biogas au urejeleshaji.

Hoja ni kwamba teknolojia hiyo inaweza kufanya kwa usafi zaidi na kwa kasi kile ambacho wakusanya taka wa Dandora sasa hufanya kwa mikono katika mazingira hatari. Utekelezaji wake wa kwanza, ushirikiano unkiri, umefungamanishwa na kituo cha urejeleshaji wa malighafi huko Kisii, magharibi mwa Kenya, kilicholenga kuonyesha jinsi upangaji wa kiotomatiki unavyoweza kuimarisha urejeleshaji katika ngazi ya kaunti.
Utekelezaji wa kwanza wa teknolojia hiyo unalenga kituo cha urejeshaji wa malighafi katika Kaunti ya Kisii, ambako kaunti tayari imewekeza katika miundombinu ya upangaji na urejeleshaji wa taka. Kisii imechaguliwa kama eneo la kuonyesha jinsi teknolojia ya kiotomatiki inaweza kuimarisha mifumo ya usimamizi wa taka katika ngazi ya kaunti.
Lakini teknolojia ya kiotomatiki katika sekta inayotegemea makumi ya maelfu ya wafanyakazi wasio rasmi, Chama cha Kitaifa cha Ustawi wa Wakusanya Taka nchini Kenya kikikadiria wanachama wake kuwa 46,000, inazua swali linaloning’inia juu ya kila kituo na dampo: Je, mashine inayopanga taka kwa kasi kuliko binadamu inaweza tu kumfanya binadamu huyo apoteze kazi? Ushirikiano unasisitiza kuwa sivyo.
“Hatuleti teknolojia kuwabadilisha wafanyakazi wa taka wasio rasmi; tunaleta teknolojia kuiboresha sekta,” alisema Ngechu. Wafanyakazi wa taka, kwa mujibu wa hoja hiyo, watahamia kwenye ukusanyaji, uwekaji wa pamoja, ulishaji wa mashine, udhibiti wa ubora, usafirishaji, ukusanyaji wa data na biashara ya malighafi zilizorejeshwa. “Siku zijazo si mashine dhidi ya watu. Ni watu wanaosaidiwa na mashine.”
Ahadi hiyo itapimwa kwa kuzingatia historia ndefu ya miradi iliyolenga kuwashirikisha wakusanya taka, lakini wakati mwingine ikaishia kuwatenga. Wakusanya taka 46,000 waliosajiliwa na chama hicho cha kitaifa cha ustawi wao, na kazi yao ndiyo msingi wa urejeleshaji wowote unaofanyika nchini. Hilo ndilo litakaloonyesha iwapo watu kama Mulwa wataingizwa katika mfumo huo au kuachwa nje yake.
Kuna pia suala la imani, jambo ambalo afisa huyo aliendelea kulirejea. Wakenya, kwa kiasi kikubwa, hawatenganishi taka nyumbani, ushirikiano unakiri, si kwa kutojali bali kwa sababu wameona taka zilizotenganishwa zikimwagwa pamoja tena ndani ya lori la kukusanya. “Watu wakitenganisha lakini lori likachanganya kila kitu tena, wanapoteza imani,” alisema Ngechu.
Angalau, msingi wa kisera sasa upo. Sheria ya Usimamizi Endelevu wa Taka ya mwaka 2022 ilianzisha Uwajibikaji wa Mtengenezaji Uliopanuliwa, ikiwafanya watengenezaji kuwajibika kwa vifungashio vyao baada ya matumizi, na kanuni zilizoambatana zilifuata mwaka 2024. Lakini kaunti bado zinakabiliwa na ukosefu wa fedha.
“Huenda zisimudu iwapo zitatarajiwa kununua kila kitu peke yao,” alikiri Mary, akielekeza badala yake kwenye ufadhili mchanganyiko — mikataba ya ununuzi wa kaunti, ufadhili kupitia mifuko ya uwajibikaji wa wazalishaji, uwekezaji wa sekta binafsi, msaada wa washirika wa maendeleo na ufadhili wa kaboni. “Kaunti hazihitaji kila mara kumiliki mashine; zinaweza kulipia utendaji.”
Kenya si nchi ya kwanza kujaribu teknolojia hii, na mshirika wake anazijua changamoto zake. TrashCon tayari inaendesha mitambo katika miji zaidi ya 20 katika maeneo sita nchini India, huku mifumo yake pia ikiwa imetumika katika Ufilipino. Uzoefu wa TrashCon nchini India pia unaonyesha kwa nini teknolojia pekee haiwezi kutatua tatizo la taka. “Mashine peke yake hazitatui tatizo la taka,” alisema Mary kuhusu uzoefu wa India. “Mifumo ndiyo hutatua tatizo la taka.”

Benki ya Dunia imeonya kuwa taka za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zitaongezeka karibu mara tatu ifikapo 2050, huku nchi za kipato cha chini zikichakata upya asilimia 4 tu ya taka zinazozalishwa. Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa TRANSFORM, Bi Nivedha RM, alisema kampuni hiyo ilisaidia biashara 42 zenye athari chanya katika Afrika Mashariki kupitia ufadhili wa ruzuku na msaada wa kibiashara. Tangu mwaka 2022, biashara hizi zimechangia kuzuia zaidi ya tani 8,600 za taka zisiende kwenye dampo na zimezalisha takribani ajira 3,400 za moja kwa moja. Mabadiliko ya Kenya yenyewe kuelekea uchumi duara yanaweza kuzalisha takribani ajira 46,000 ifikapo 2030 — iwapo miundombinu itafika.
Kwa sasa, swali la iwapo teknolojia hiyo itawanufaisha au kuwaondoa wakusanya taka bado liko wazi Dandora.. Kipimo cha mafanikio, ushirikiano unasema, hakitakuwa idadi ya mashine zilizowekwa, bali kiasi cha taka kilichoelekezwa mbali na dampo, kiasi cha mapato kinachowafikia wafanyakazi, na jinsi kazi yao inavyokuwa salama zaidi. Kwenye kilima, mkusanya taka amesikia ahadi hapo awali.
Jua linapochomoza na kuangaza kikamilifu juu ya dampo, bado yuko pale, bado anapanga taka kwa mikono, akisubiri kuona iwapo, safari hii, mabadiliko yatafika hadi kwake.
Picha ya bango: Clarice Bala Adhiambo anaacha, kwa muda, kazi ya kufungasha chupa zilizotengenezwa kwa plastiki iliyorejelewa ili kupigwa picha katika kiwanda cha urejeleaji taka jijini Nairobi. Picha kwa hisani ya TakaTaka ni Mali.
Ndani ya Kibera, vijana wageuza mapambano dhidi ya taka kuwa kinga dhidi ya mafuriko