- Nchini Kenya, mtandao wa vikundi vya wanawake wa jamii za kiasili unarejesha maeneo yaliyoharibiwa ya Msitu wa Mau huku pia ukiwapa wanawake uwezo wa kipato na kufanya maamuzi.
- Kikundi cha Wanawake cha Paran linajumuisha Wamasai, Waogiek na wanajamii wengine wa kiasili wanaojifunza kusimamia biashara kama vile vitalu vya miti, bustani za jikoni, vikundi vya akiba, ufugaji wa nyuki na urejeshaji wa mazingira.
- Utafiti unaonyesha kwamba mipango ya urejeshaji ilioundwa ili kubadilisha majukumu yasiyo sawa ya kijinsiahuongeza nafasi ya wanawake katika kufanya maamzi ya familia, umaarufu zaidi katika makazi na kuboresha matokeo ya uhifadhi.
- Wanachama wa Paran wanasema hapo awali walikuwa wakiwategemea waume zao kwa kila kitu,lakini sasa wana kipato chao na sauti kubwa zaidi katika maamuzi ya kifamilia.
Kabla ya kupambazuka katika kijiji cha Eor Ewaso, kusini-magharibi mwa Kenya, Judy Mukut huwa tayari ameamka. Kufikia saa kumi na mbili na nusu asubuhi, anakuwa ameshateka maji, kukamua ng’ombe wa familia, kuandaa kiamsha kinywa, kusafisha nyumba na kuwasindikiza watoto wake shuleni. Baada ya hapo huondoka nyumbani kuelekea kituo cha rasilimali kinachoendeshwa na shirika la wanawake wa kiasili la Paran, ambako kazi ya uhifadhi ya siku hiyo huanza.
Kwa Mukut, kazi ya uhifadhi wa Msitu wa Mau hufanywa ndani ya saa chache zilizosalia baada ya kutimiza majukumu yake kama mke na mama katika jamii ya Wamaasai. Hata hivyo, juhudi hizi za kusawazisha majukumu zinaakisi mabadiliko ya kimya kimya yanayoendelea katika mojawapo ya mifumo ikolojia muhimu zaidi ya misitu nchini Kenya.
Huku wanawake wa jamii za kiasili wanaporejesha hali ya maeneo yaliyoharibiwa ya Msitu wa Mau, wanajipatia pia mapato ya kujitegemea, kushiriki katika maamuzi ya nyumbani na kufufua maarifa ya kiasili kuhusu mazingira, maarifa ambayo kwa vizazi vingi yamekuwa muhimu kwa maisha ya jamii zao kwa vizazi vingi kabla ya kupotea au kusahaulika.
Baada ya kuanzishwa mwaka wa 2025, kikundi cha Wanawake cha Paran imekuwa na kufikia mtandao wa vikundi 64 vya wanawake wa kiasili vilivyosajiliwa, vingi vikitoka katika jamii za Wamasai na Waogiek katika kaunti ya Narok, pamoja na jamii katika kaunti za West Pokot na Samburu. Kupitia vitalu vya miti vinavyosimamiwa na jamii, bustani za jikoni, vikundi vya akiba vya vijiji, ufugaji wa nyuki na urejeshaji wa mazingira, shirika hilo limeunganisha uhifadhi wa mazingira na uwezeshaji wa wanawake.
Ili kuratibu mtandao wake unaopanuka, Paran ilianzisha vituo saba vya rasilimali za jamii. Badala ya kufanya kazi kama ofisi, vituo hivyo hutumika kama maeneo ya maonyesho ambapo wanawake hupanda miche, hupokea mafunzo ya kiufundi na kubadilishana maarifa ya kitamaduni.
“Kazi hii imetufundisha jinsi ya kujipanga,” alisema Mukut. “Licha ya majukumu yote ya nyumbani, tumejifunza kwamba tukipanga vyema ratiba ya siku yetu, bado tunaweza kuhudhuria mikutano, kutunza familia zetu na kuchangia katika kurejesha hali ya mazingira. Hatungojei tena watu wengine kufanya maamuzi kwa sababu tunajua mchango wetu una umuhimu.”
Utafiti unaendelea kuunga mkono zaidi mbinu kama hizo. Utafiti wa mwaka 2025 uliofanywa na shirika la CIFOR-ICRAF (ambalo sasa linafanya kazi kama Landscape Alliance) ulibaini kuwa programu za urejeshaji wa mazingira zilizoundwa kushughulikia ukosefu wa usawa wa kijinsia huimarisha ushiriki wa wanawake katika kufanya maamuzi ya nyumbani huku zikiboresha matokeo ya muda mrefu ya urejeshaji huo.

Kurejesha misitu, kujenga upya maisha
Kwa Nancy Letina, mwenyekiti wa Kundi la Wanawake la Namaiyana ndani ya mtandao wa Paran, kujiunga na kundi hilo mwaka wa 2021 kulibadilisha si tu mtazamo wake kuhusu uhifadhi bali pia mustakabali wa kiuchumi wa familia yake.
“Awali, tukiwa wanawake wa jamii ya Wamasai, tuliwategemea waume zetu kwa kila kitu, hata mahitaji ya nyumbani kama vile chumvi,” alisema Letina. Lakini hali hiyo ilibadilika mwaka wa 2019 baada ya mumewe kufariki dunia, na kumwacha yeye akiwa ndiye mtafutaji mkuu mwenye jukumu la kugharamia mahitaji ya watoto wake wanne.
Miaka miwili ya kwanza baada ya kufiwa na mumewe ilikuwa migumu. Akiwa na wanawake wengine wachache kutoka kijiji cha Olomaiayana-Iltirben katika kata ya Melelo waliokuwa wakikabiliwa na changamoto kama hizo, Letina alibuni kikundi cha kujisaidia kilichowasaidia wanachama nyakati za uhitaji. Hali yao ilianza kubadilika pale kikundi hicho kilipojiunga na shirika la Paran na kupata mafunzo kuhusu shughuli endelevu za kujipatia kipato.
“Tulipata maarifa yaliyotuonyesha kuwa kila mwanamke anaweza kujikimu kimaisha. Leo, wanawake wana kipato chao wenyewe. Tunaweza kulipa ada za shule zilizochelewa kulipwa pale watoto wetu wanaporudishwa nyumbani kwa kukosa ada, na kushughulikia dharura bila kusubiri msaada.”
Kikundi chake kwa sasa kinasimamia kitalu cha miti chenye ukubwa wa hekta 0.2 (nusu ekari) ambako hupanda spishi za asili kama vile mzeituni wa Kiafrika (Olea europaea subsp. africana). Spishi hizo zina thamani katika urejeshaji wa misitu, kusaidia bioanuwai na kutumika katika dawa za jadi. Kikundi cha Letina kimeuza miche 10,600 kwa shirika hilo tangu kilipojiunga. Mche mmoja unauzwa kwa shilingi 20 ($0.15). Mapato hayo husaidia kugharamia shughuli za wanachama na kikundi.

Wanachama pia huendesha vikundi vya kuweka akiba na kukopa vijijini, ambapo michango ya kila wiki huanzia shilingi 100 ($0.77) tu, na kuwawezesha wanawake kukopa kati ya shilingi 2,000 na 8,000 (takriban $15-$60) wakati wa dharura. Mikopo hiyo huzisaidia familia kulipa ada za shule, kuwekeza katika biashara ndogondogo au kununua mifugo bila kulazimika kukata miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa au kuvuna mbao.
Zaidi ya hayo, Esther Kigen, mwanachama wa kundi la Masi, alisisitiza kwamba mafunzo yanayotolewa na shirika la Paran kuhusu haki za wanawake yamewahimiza kushiriki katika maamuzi ya familia ambayo hapo awali yalikuwa yakifanywa na wanaume pekee.
“Awali, mwanaume angeweza kuuza mifugo bila kumjulisha mtu yeyote kwa sababu kila kitu kilikuwa chake,” alisema Kigen.
“Sasa familia nyingi hukaa pamoja kabla ya kufanya maamuzi muhimu. Wanawake hushirikishwa kwa sababu nao huchangia katika ustawi wa familia.” Kauli hii inaakisi kwa karibu matokeo ya *utafiti* wa mwaka 2021, ambao ulibaini kuwa maamuzi kuhusu kutumia mbinu za kurejesha ardhi mara nyingi huanzishwa na wanawake, lakini hufanikiwa zaidi pale wanachama wa kaya wanapofanya maamuzi kwa pamoja; jambo linaloonyesha namna mahusiano ya kijinsia yanavyoathiri matokeo ya jitihada hizo za urejeshaji ardhi.

Mabadiliko katika mazingira ya eneo
Wanawake hao pia wanaona mabadiliko katka mazingira yao baada ya miaka ya urejeshaji. “Kadri Msitu wa Mau ulivyozidi kuharibika, mvua ilizidi kutotabirika na Mto Ewaso Ng’iro ulikuwa na maji kidogo,” Letina alisema. “Leo, tunaona maji safi na mvua bora. Tunafahamu kuwa watu wengi wamechangia kurejesha msitu, na tunajivunia kwamba kazi yetu ni sehemu ya urejesho huo.”
Lorna Nyaga, mwanasayansi wa kijamii na afisa wa utafiti kutoka shirika la Landscape Alliance, alifafanua kuwa uchunguzi kama huo unapaswa kuungwa mkono na utafiti. Misitu iliyorejeshwa hatimaye inaweza kuboresha muundo wa udongo, kupunguza mmomonyoko na kuongeza upenyaji wa maji kwenye udongo, unaoweza kusaidia kuongeza mtiririko wa maji katika vijito na mito, alisema. Hata hivyo, alionya kwamba ni vigumu kutathmini mradi wa urejesho wa shirika la Paran bila data ya msingi na ufuatiliaji wa muda mrefu.
“Mtazamo wa jamii ni muhimu, lakini swali ni: Je, kuna takwimu za kuuthibitisha? Bila kuwa na takwimu za awali za kulinganishia, ni vigumu kuhusisha mabadiliko hayo na zoezi hilo la urejeshaji kwa uhakika,” alisema.
Nyaga aliongezea kuwa kwamba mtazamo wa jamii na ufuatiliaji wa kisayansi vinapaswa kusaidiana badala ya kushindana.

Uponyaji wa jadi
Kwa Ntoiye Kimorgo wa Kundi la Wanawake la Naretoi, urejeshaji wa mazingira unahusu pia kulinda maarifa ya kiasili.
Yeye ni mtaalamu wa tiba za asili zinazotumia mimea, anawahimiza wanawake wote katika kundi lake kupanda miti ya dawa ya kiasili sambamba na mboga, kwani miti hiyo ni muhimu sana katika utamaduni na mfumo wa jadi wa afya wa jamii ya Wamasai.
“Miti hii imekuwa ikitusaidia kutibu magonjwa mbalimbali,” Kimorgo alieleza. “Ikitoweka, tutapoteza zaidi ya msitu tu; tutapoteza maarifa tuliyorithi kutoka kwa babu na nyanya zetu. Kila mwanamke katika kundi letu amepanda miti ya dawa kwa sababu tunatambua thamani yake.”
Bustani zao ndogo za mboga ya kikundi chao huzalisha sukuma wiki, mrenda, mchicha na mboga nyingine za asili za Kenya ambazo huboresha lishe katika makazi huku zikileta kipato cha ziada kupitia masoko ya ndani.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Paran, Naiyan Kiplagat, alisema kuwa kazi ya shirika hilo imekuwa ikilenga mambo mengi zaidi ya kurejesha misitu iliyoharibiwa. Tangu mwanzo, shirika hilo lililenga kushughulikia changamoto za kimazingira na kijamii zinazowakabili wanawake wa jamii za asili kwa wakati mmoja, likitambua kuwa uhifadhi endelevu ungekuwa mgumu bila kuziimarisha jamii zinazotegemea msitu huo.

Kubuni mipango ya urejeshaaji kulingana na hali halisi ya maisha ya kila siku ya wanawake, Kiplagat alisema, imekuwa mojawapo ya kanuni zinazofafanua shirika hilo. “Wanawake hawa ndiyo walezi wakuu wa familia zao na ndiyo maana tulianzisha bustani za lishe na vitalu vya miti karibu na nyumba zao. Wanaweza kuboresha lishe ya familia zao, kupata kipato na kurejesha mandhari yaliyoharibika bila kuacha majukumu yao nyumbani.”
Tofauti na mipango mingi ya urejesho ambayo inaweka kipaumbele miti ya kigeni inayokua kwa kasi, kikundi cha Paran kinazingatia zaidi spishi za asili ambazo hapo awali zilitawala mfumo ikolojia wa Mau. Vitalu vyake vya mimea huzalisha spishi zikiwemo mzeituni wa Kiafrika pamoja na Warburgia ugandensis, Syzygium guineense, Markhamia lutea, Croton megalocarpus na miti mingine ya kiasili ya dawa ambayo inasaidia bioanuwai huku ikihifadhi mila za kitamaduni.
Kwa Kiplagat, ambaye ni wa jamii ya Ogiek na ameunganishwa na jamii ya Wamasai kupitia ndoa, kulinda spishi hizo pia kunamaanisha kulinda maarifa ya Asili yanayohusiana nayo.
“Tunaamini katika maarifa ya kitamaduni, uvumbuzi na hatua za pamoja,” alisema. “Iwapo wazee wetu wataondoka bila kupitisha maarifa hayo kwa kizazi kipya, basi tunapoteza jambo muhimu sana. Uhifadhi si tu kuhusu kupanda miti. Pia ni kuhusu kuhakikisha watoto wetu wanaelewa kwa nini miti hiyo ni muhimu.”
Kwa hivyo, wanawake wazee huwashauri wanachama wadogo kupitia usimulizi wa hadithi, ukusanyaji wa mbegu, usimamizi wa vitalu vya miche na maonyesho kuhusu matumizi ya mimea ya dawa. Baadhi hubobea katika kutambua mbegu za asili, huku wengine wakifundisha mbinu endelevu za uvunaji au elimu ya mazingira ndani ya jamii zao.
Falsafa hiyo imeendelea kupokea uungwaji mkono wa kimataifa. Kiplagat alisema kuwa mwaka wa 2023, shirika la Paran lilipata dola 100,000 kupitia mfuko wa TerraFund chini ya mpango wa AFR100 Landscapes, mpango unaoungwa mkono na World Resources Institute, kwa ajili ya kurejesh ardhi iliyoharibika katika Msitu wa Mau. Tangu mradi huo uanze, wanawake wanaoshirikiana na shirika hilo wamepanda miche 200,000 ya miti asilia, huku kazi ya kuitunza ikiendelea kadiri miti hiyo inavyostawi na kushika mizizi. Mradi huo wa miaka sita unatarajiwa kukamilika mwaka wa 2029.

Shirika hilo pia linatekeleza mradi tofauti wa urejeshaji wa mazingira unaoungwa mkono kupitia mpango wa ‘Climate Promise’ wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), ambao unachanganya shughuli za kilimo-misitu na zile za kuimarisha ustahimilivu wa jamii. Wanawake hupewa mafunzo ya kuanzisha vitalu vya miche na kupewa vifaa kama vile mirija ya karatasi kwa ajili ya kupanda mbegu na miche, ambayo baadaye huhamishiwa kwenye bustani zao za nyumbani.
Pia, wanawake hufunzwa kutengeneza majiko yanayotumia nishati kwa ufanisi, ambayo huuzwa kwa shilingi 300 (dola 2.30) kila moja, pamoja na mkaa mbadala au briketi za nishati zinazouzwa kwa shilingi 70 (dola 0.50) kwa kila kilo.
Kiplagat alisema miradi hiyo imeonyesha kuwa wanawake wa kiasili wanaweza kuongoza kwa mafanikio urejeshaji mkubwa wanapokuwa na usaidizi wa kifedha na kiufundi. Mafanikio ya Paran pia yamepata kutambuliwa kimataifa, ikiwa ni pamoja na tuzo ya Gender Justice Climate Solutions iliyotolewa wakati wa COP28 huko Dubai mnamo mwaka wa 2023.
Hata hivyo, alisema ufadhili unasalia kuwa changamoto kubwa zaidi ya shirika. Mapato yanayotokana na vitalu vya miti husaidia kuziba mapengo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono mipango ya jamii kama vile makazi ya uokoaji kwa wasichana walio katika hatari ya kukeketwa wakati wa likizo za shule (Ukeketaji ni desturi ya kitamaduni yenye mizizi katika jamii, ambayo ni kinyume cha sheria lakini imeshikiliwa kwa muda mrefu miongoni mwa Wamasai kama desturi ya mpito).
“Changamoto yetu kubwa ni rasilimali, kwani kuna wanawake wengi zaidi wanaotaka kushirikiana na sisi kuliko idadi tunayoweza kuisaidia kwa sasa. Tunapokea ufadhili kwa msingi wa miradi mahususi, lakini mahitaji ya jamii yanaendelea hata baada ya miradi hiyo kukamilika. Hata hivyo, tunaamini kuwa kufanya mambo madogo kwa uthabiti kwa miaka mingi hatimaye huleta mabadiliko makubwa zaidi,” alisema Kiplagat.
Cha kuvutia ni kwamba, wanaume nao wameanza kujiunga na kuanzisha vikundi vinavyoshirikiana na kundi la Paran baada ya kushuhudia athari chanya ambazo mpango huo umekuwa nazo kwa wanawake katika jamii zao. Vincent Leteipa, mkazi wa kijiji cha Eor Ewaso mwenye umri wa miaka 31, alisema alihamasishwa na majirani zake wanawake waliojiunga na mpango huo na kuboresha maisha yao kupitia kilimo cha bustani za mboga na biashara ya vitalu vya miti. “Nilipata hamasa ya kuwa sehemu ya jamii hii baada ya kuona matokeo ya kazi za wanawake hawa,” alisema. Tangu ajiunge mwaka wa 2022, Leteipa ameacha kazi za vibarua vya ujenzi na sasa anaendesha biashara ya boda boda, mabadiliko anayoyahusisha na akiba pamoja na kipato alichopata kupitia shughuli za kikundi hicho. Alisema kuwa kipato hicho cha ziada kimemwezesha pia kujenga nyumba na kumudu gharama za shule za mtoto wake.
Ushirikiano
Shirika la serikali la Huduma ya Misitu ya Kenya (KFS) limekuwa mojawapo ya washirika wa karibu wa kiufundi wa kikundi cha Paran, likitoa mwongozo kuhusu uteuzi wa spishi, uanzishaji wa vitalu, ulinganishaji wa maeneo na mbinu za urejeshaji huku wanawake wakihamasisha jamii na kukuza miche ya spishi ya asili.
Frederick Kibichi, mkulima katika kaunti ndogo ya Narok Kusini, alisema ushirikiano huo umetoa matokeo ya kutia moyo ya kiikolojia licha ya ukame unaozidi kujirudia.
“Wametusaidia sana katika kuhifadhi mazingira,” alibainisha Kibichi, ambaye alisema shirika la KFS hutathmini mafanikio ya urejeshaji hasa kupitia viwango vya uhai wa miche badala ya kuhesabu tu idadi ya miti iliyopandwa.
“Zaidi ya 50% ya miche yao imeendelea kuishi licha ya hali ya ukame kwa sababu inafuata mwongozo wa kiufundi kwa karibu sana.”
Aliongeza kuwa kikundi cha Paran kinaweza kuboresha zaidi maisha ya miti kwa kutekeleza mchakato unaojulikana kama “beating-up” ambapo miche iliyokufa hubadilishwa na ile yenye afya ya spishi zile zile wakati wa msimu ujao wa mvua. Pia alipendekeza kupalilia mara kwa mara ili kupunguza ushindani kutoka kwa magugu, kulinda maeneo ya urejesho kutokana na moto, mifugo na shughuli haramu na kutathmini kiwango cha uhai wa miche baada ya kupandwa tena ili kuhakikisha maeneo hayo yanafikia kiwango kinachohitajika cha uhifadhi.


Zaidi ya kurejesha vitalu vya misitu, kundi la Paran pia limetoa miche ya asili kwa ajili ya shule na shughuli za upandaji miti wa jamii. Humphrey Omollo, kamishna msaidizi wa kaunti katika tarafa ya Ololulunga katika kaunti ndogo ya Narok Kusini, alisema ushiriki wa serikali katika shughuli kama hizo husaidia kuimarisha umiliki wa jamii huku ikitambua wanawake kama viongozi wa mazingira.
“Wakati maafisa wa serikali wanapojiunga na shughuli hizi za urejeshaji, jamii zinaelewa kwamba kazi hii ni ya kila mtu,” Omollo alisema. “Uhifadhi si suala la wanaume au wanawake pekee. Misitu yenye afya hunufaisha jamii nzima, na wanawake hawa wameonyesha kwamba wanaweza kuongoza urejeshaji wa mazingira kwa ufanisi sawa na viongozi wengine.”
Mzee wa kijiji Peter Muya ameshuhudia mabadiliko hayo kwa miaka mingi. “Nilipokuwa mdogo, uongozi ulikuwa umeachiwa kabisa wanaume,” Muya alisema. “Leo, wanawake wanaongoza vikundi vya uhifadhi, wakizungumza katika mikutano ya hadhara na kusaidia familia kufanya maamuzi muhimu. Si kila mtu ameacha mitazamo ya zamani, lakini elimu na mashirika kama Paran yameonyesha jamii yetu kwamba wanawake wana uwezo sawa wa kuongoza.”
Kauli ya Mzee Muya inaungwa mkono na ripoti ya hivi karibuni ya shirika la CIFOR-ICRAF inayosisitiza mijadala ya jamii kama zana bora za kushinda vikwazo vya kijinsia katika urejeshaji kwa sababu husaidia kubadilisha mitazamo ya wenyeji badala ya kuzingatia juhudi za urejeshaji pekee.
Kwa Mukut na mamia ya wanawake wengine wa jamii za kiasili, kuurejesha Msitu wa Mau ni jambo ambalo ni zaidi ya ukarabati wa mfumo wa ikolojia ulioharibika. Ni suala la kuunda njia za kujipatia kipato zinazopunguza shinikizo kwa msitu, kuhifadhi maarifa ya jadi kuhusu mazingira, na kuthibitisha kuwa uhifadhi huwa na nguvu zaidi pale watu wanaoishi katika eneo husika kwa vizazi vingi wanapoaminiwa kuongoza juhudi za kulirejesha katika hali yake ya awali.
Picha ya bango: Ntoiye Kimorgo, mganga wa jadi wa jamii ya Wamasai na mwanachama wa kundi la Naretoi linaloshirikiana na shirika la Paran, anaelezea umuhimu wa kupanda miti asilia kutokana na sifa zake za kimatibabu. Picha na Juliet Ojwang.
Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza hapa kwa lugha ya Kiingereazz mnamo tarehe 11/08/2026
Western Kenya’s most important water-capturing forest is disappearing, satellites show