- Wataalamu wanaonya kuwa kupanda mikoko ni sayansi inayohitaji kuchagua eneo na aina sahihi ya mkoko, kutumia miche yenye afya na kuzingatia muda na mbinu bora za upandaji.
- Kenya ina takribani hekta 61,279 za misitu ya mikoko, huku Lamu ikiwa na asilimia 61 ya eneo hilo; wataalamu wanasisitiza kuwa urejeshaji unapaswa kuhusisha pia ufuatiliaji na ushirikishwaji wa jamii.
- Utafiti wa 2026 katika jarida la Scienceunaonyesha kuwa eneo la mikoko duniani limeanza kuongezeka tangu takribani mwaka 2010, huku upanuzi wa asili ukiwa chanzo kikuu cha ongezeko hilo, ishara kwamba mafanikio ya urejeshaji hayapimwi kwa idadi ya miche iliyopandwa pekee.
Kenya imetambuliwa kimataifa baada ya kupanda miche 4,124 ya mikoko kwa muda wa chini ya sekunde 30, kwa lengo la kuhamasisha juhudi za kurejesha misitu ya mikoko iliyoharibiwa na kuchangia lengo la kitaifa la kuongeza idadi ya miti. Hatua hii iliipa nchi hiyo rekodi ya Guinness World Records.
Rekodi hii iliafikiwa katika eneo la Jomvu Kuu, kaunti ya Mombasa tarehe Julai 26, 2026, ambayo ni Siku ya Mikoko Duniani. Watu 4,124 kati ya 4,196 waliojitokeza walithibitishwa na Guinness World Records kutimiza masharti ya kupanda miti hiyo kwa pamoja.

Shirika la Mpesa Foundation lilifadhili shughuli hiyo kupitia mradi wake wa mazingira, likishirikiana na jamii, huku Kenya Scouts Association ikihamasisha na kuleta maelfu ya vijana na skauti wa eneo la pwani. Bidii Creek Conservancy CBO ilishiriki katika utafutaji wa miche ya mikoko kutoka kwa jamii zinazojishughulisha na uhifadhi wa mikoko, huku serikali, kupitia Shirika la Huduma kwa Misitu (KFS), ikitoa mwongozo wa kitaalamu wa uhifadhi na upandaji wa mikoko.
Rekodi za upanzi wa mikoko 2026
Mwaka 2026 umeshuhudia kuongezeka kwa kampeni za upanzi wa mikoko, huku wadau mbalimbali wakivunja rekodi na kuhamasisha juhudi za urejeshaji wa misitu hiyo.
Mapema mwaka huu, mwanaharakati wa mazingira Antoine Moses alipanda miche 47,460 ya mikoko ndani ya saa 24 katika mkondo wa bahari wa Tudor, Mombasa kabla ya kutwaa taji la mtu aliyepanda miti mingi zaidi ya mikoko ndani ya saa 24.
Wiki chache baadaye, tarehe Mei 23, Kikosi cha Ulinzi cha Kenya (KDF), kwa kushirikiana na jamii na wanafunzi, kilipanda miche 150,000 ya mikoko katika eneo la Tsunza, Kaunti ya Kwale, kama sehemu ya juhudi za kuchangia lengo la taifa la kupanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka 2032.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu, Dkt Deborah Barasa, Kenya imefanikiwa kurejesha mikoko milioni 91.6, sawa na zaidi ya asilimia 65 ya lengo la kurejesha mikoko milioni 140.
Barasa alinukuliwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira akitaja juhudi za jamii pamoja na mashirika ya serikali na yale ya kibinafsi kama yanayochochea ufanisi uliopo.

Lakini je, kupanda maelfu ya miche kwa muda mfupi kunamaanisha misitu ya mikoko imerejeshwa?
Kulingana na Julius Sila, mtaalamu wa urejeshaji wa mikoko nchini Kenya, juhudi za kurejesha mikoko zinapaswa kwenda zaidi ya kupanda miche na pia kushughulikia sababu za kijamii na kiuchumi zinazosababisha uharibifu wa mikoko, ikiwemo umaskini na ukosefu wa njia mbadala za kujipatia kipato.
Sila aliandika hayo katika makala iliyochapishwa na Plant-for-the-Planet mwaka 2025. Anasema kufikia lengo hilo hakutategemea kampeni za upandaji wa siku moja pekee, bali pia utekelezaji wa mbinu za kisayansi, ushiriki wa jamii na ufuatiliaji wa muda mrefu wa maeneo yaliyorejeshwa.
Mwongozo wa Kitaifa wa Urejeshaji wa Mfumo wa Ikolojia wa Mikoko wa mwaka 2025 unasisitiza umuhimu wa kuelewa mazingira ya eneo husika, kuchagua aina sahihi za mikoko, kuondoa vikwazo vya mtiririko wa maji na kufuatilia ukuaji wa miche baada ya kupandwa. Lengo ni kuhakikisha juhudi za urejeshaji zinatoa matokeo ya kudumu kwa mazingira na jamii.
Kwa mujibu wa WWF, mikoko ina mchango mkubwa katika kulinda pwani dhidi ya mmomonyoko na mawimbi makubwa, kuhifadhi bioanuwai, kusaidia mazalia ya samaki, kunasa kaboni na kutoa rasilimali muhimu kwa jamii kama kuni, asali na bidhaa nyingine za misitu. Hata hivyo, misitu hiyo imepungua kufuatia shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa Miongozo ya Kitaifa ya Urejeshaji wa Mfumo wa Ikolojia wa Mikoko ya Mwaka 2025, Kenya ina takribani hekta 61,279 ya misitu ya mikoko katika ukanda wa pwani, katika Kaunti ya Lamu ikiwa na asilimia 61 ya misitu hiyo. Mikoko inawakilisha asilimia 3 ya misitu asili ya Kenya. KWS inakadiria kuwa Kenya inapoteza asilimia 0.7 ya msitu wa mikoko kutokana na shughuli za kibinadamu, uchafuzi, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo, hali inayohimiza hatua za dharura za uhifadhi wa misitu hiyo.
Je, kupanda maelfu ya miche kwa siku ni suluhu?
Kwa mujibu wa Mpango wa Kitaifa wa Usimamizi wa Mfumo wa Ikolojia wa Misitu ya Mikoko (2017–2027), urejeshaji wa misitu ya mikoko unapaswa kuhusisha ushiriki wa jamii pamoja na kufuata mbinu za kisayansi ili kuhakikisha juhudi hizo zinafanikiwa.
Wanasayansi wanasisitiza kuwa wanaorejesha misitu ya mikoko kwa njia ya upandaji wanapaswa kuzingatia miongozo hiyo, ambayo inaelekeza maeneo yanayofaa kwa upandaji wa mikoko na aina zinazopaswa kupandwa.
Upanzi usiozingatia mwongozo wa kisayansi mara nyingi husababisha kiwango cha chini cha uhai wa miche kutokana na kutopandwa kwa aina sahihi katika maeneo yanayofaa.
Kupanda mikoko ni sayansi
Mtafiti mkuu na mwanasayansi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Bahari na Uvuvi Kenya (KMFRI), Dkt James Kairo, anasema mikoko ni tofauti na miti mingine ya misitu na kwamba upanzi wake unahitaji kufanyika kwa kuzingatia misingi ya kisayansi.
Anasema kupanda aina moja ya mikoko katika maeneo yasiyofaa kunaweza kuathiri mfumo wa ikolojia na kupunguza kiwango cha uhai wa miche hiyo.
“Kupanda mikoko ni sayansi ila kinachoendelea sasa ni kwamba tunaona watu wanapanda miti kama miti mengine ile ya misitu. Hatutaki kupanda miti pekee, tunataka kukuza mikoko, na hilo linawezekana tu kwa kufuata miongozo ya kisayansi iliyopo,” anasema Dkt Kairo.

Katika shughuli ya upandaji mikoko iliyogonga vichwa vya habari, naibu mkuu mwandamizi anayehusika na uhifadhi na usimamizi wa misitu KFS, Dr Clement Ng’oriareng’, aliyeongoza shughuli hiyo, anasema wao kama wataalamu walisimamia kitengo cha kiufundi na walichagua sehemu iliyofaa, umbali wa miche, ubora wa miche na namna ya kupanda.
Anaongeza kuwa walifanya utafiti wa eneo la upanzi kabla shughuli hiyo haijafanyika ambapo walipanda mkoko aina ya mchu (Avicennia marina) ambao umekua ukipandwa katika eneo hilo.
Dkt Kairo anasema changamoto ya urejeshaji wa mikoko haipo Kenya pekee, bali ni tatizo linalojitokeza katika mataifa mengi kutokana na uelewa mdogo kuhusu ikolojia ya mikoko.
“Katika taasisi nyingi za elimu, wanafunzi hufundishwa zaidi kuhusu misitu ya nchi kavu kuliko misitu ya mikoko. Hivyo, bado kuna pengo la maarifa kuhusu namna sahihi ya kurejesha na kusimamia mikoko,” anasema.
Kenya ina aina tisa za mikoko zinazopatikana kuanzia Vanga hadi Lamu. Hizi ni Mkoko (Rhizophora mucronata), Mkandaa/Mkoko mwekundu (Ceriops tagal), Mchu (Avicennia marina), Mlilana/mpira (Sonneratia alba), Msinzi /Msisi/Muia (Bruguiera gymnorrhiza), Mkomafi (Xylocarpus granatum), Msikundazi (Heritiera littoralis), Kikandaa/Mkandaa Dume/Kilalamba (Lumnitzera racemosa) na Mkomafi dume (Xylocarpus moluccensis).
Kila aina hustawi katika mazingira tofauti, jambo ambalo wataalamu wanasema linapaswa kuzingatiwa wakati wa kupanga shughuli za urejeshaji wa misitu hiyo.
Hamasa ipo, maarifa ndiyo changamoto
Elena Roddom, mkuu wa kitengo cha ufundi cha urejeshaji wa mikoko kutoka shirika la kimataifa la Wetlands International, amekuwa akifanya utafiti na kuongoza shughuli za kuwajengea uwezo mabalozi wa mikoko katika kaunti za pwani.

Kutokana na kazi yake na jamii pamoja na wanafunzi, anasema wengi wanafahamu umuhimu wa mikoko, lakini bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu aina zinazofaa kupandwa na maeneo yanayofaa kwa kila aina.
“Tumetembelea madrassa, shule na vikundi vya Scouts. Wengi wanatambua umuhimu wa mikoko, lakini kinachokosekana ni maarifa kuhusu mbinu sahihi za kuikuza. Hatutaki washiriki wakate tamaa wanapoona miche waliyoipanda imekufa. Tunataka waelewe hatua zinazopaswa kufuatwa kabla ya kupanda ili kuongeza kiwango cha ustawi wa miche hiyo,” anasema Roddom.
Vigezo gani hutumika wakati wa kupanda mikoko?
Kwa mujibu wa Mwongozo wa Kitaifa wa Urejeshaji wa Mfumo wa Ikolojia wa Mikoko, upandaji wa mikoko unapaswa kuwa hatua ya mwisho baada ya kuangalia uwezekano wa urejeshaji wa kiasili. Kauli mbiu muhimu ni “aina sahihi katika eneo sahihi”, huku kurejesha mtiririko wa maji na mawimbi na kuondoa vikwazo vinavyoweza kuzuia urejeshaji wa asili kukipewa kipaumbele.
Kabla ya kupanda, wataalamu wanapaswa kuangalia hali ya mtiririko wa maji ya mawimbi, mwinuko wa eneo na ukanda ambao aina fulani ya mkoko hustawi. Hali ya udongo na kiwango cha chumvi pia huzingatiwa ili kuhakikisha aina inayochaguliwa inaendana na mazingira husika. Maeneo ambayo mikoko haikuwahi kustawi, kama maeneo yenye chumvi nyingi kupita kiasi, hayafai kulazimishwa kuwa maeneo ya upanzi.
Mwongozo huo pia unasisitiza umuhimu wa kubaini sababu iliyosababisha mikoko kutoweka kabla ya kupanda. Ikiwa, kwa mfano, njia za maji zimezibwa au kuna uchafuzi, changamoto hizo zinapaswa kushughulikiwa kwanza.
Pia, aina ya mkoko inapaswa kuendana na eneo lililochaguliwa. Miche inayopandwa inapaswa kuwa na afya na kuandaliwa katika mazingira yanayofaa. Umbali kati ya miche unapaswa kuzingatia mazingira na aina ya mikoko inayopandwa. Muda wa upandaji pia unapaswa kuzingatia mzunguko wa mawimbi na hali ya eneo ili miche isisombwe na maji.
Roddom aliiambia Mongabay kuwa umaskini unaendelea kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia uharibifu wa misitu ya mikoko, kwani baadhi ya jamii huitegemea kwa kuni, uchomaji wa mkaa na shughuli nyingine za kujipatia kipato.
Anasema changamoto nyingine ni mashirika yasiyo ya serikali yanayojihusisha na urejeshaji wa mikoko kufanya kazi kivyake. “Ingekuwa na manufaa zaidi kama yangeshirikiana, yakabadilishana uzoefu na kuratibu shughuli zao. Ushirikiano huo ungeongeza mafanikio ya urejeshaji wa mikoko,” anasema.
Jamii kama nguzo ya urejeshaji
Kwa zaidi ya miaka 18, wanachama wa Bidii Creek Conservation CBO katika eneo la Jomvu, Kaunti ya Mombasa, wamekuwa wakipanda, kulinda na kufuatilia ukuaji wa mikoko. Kila mwaka, kikundi hicho hujiwekea lengo la kukuza hadi miche 1,000,000 ya mikoko kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Hata hivyo, kiwango hicho hakijawahi kutimia.
Mwenyekiti wa shirika hilo la kijamii, Tima Mwinyi, anasema: “Nilikulia hapa Jomvu. Familia yetu ilitegemea bahari kwa uvuvi, hivyo tulielewa umuhimu wa mikoko katika kuzaliana kwa samaki. Nilianza kupanda mikoko nikiwa shuleni na baadaye tukaanzisha kikundi hiki kinachojihusisha na urejeshaji wa msitu wa mikoko kupitia upanzi, ulinzi na ufuatiliaji wao.”
Tima anasema licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado baadhi ya watu huingia katika misitu ya mikoko na kuikata, jambo linalorudisha nyuma juhudi za uhifadhi.
Katibu wa kikundi hicho, Daniel Chege, anasema alijiunga na harakati za kulinda mikoko baada ya kushuhudia kupungua kwa samaki na kamba pamoja na mabadiliko ya mazingira katika eneo lao.
Anasema kikundi hicho kinaunga mkono kampeni za upandaji wa mikoko kwa wingi na kimekuwa kikishirikiana na mashirika ya serikali na yasiyo ya serikali katika kurejesha maeneo yaliyoharibiwa. “Jamii pia inanufaika kupitia mauzo ya miche ya mikoko. Tunauza miche hiyo kwa mashirika na wadau wanaotekeleza shughuli za urejeshaji wa mikoko,” anasema.

Hata hivyo, anasisitiza kuwa upandaji wa miche pekee hautoshi bila kuwepo kwa mpango wa muda mrefu wa kuitunza. “Sisi kama jamii hatupandi mikoko pekee, bali tunaikuza. Ndiyo maana tunawahimiza wadau wasiishie kupanda na kuondoka. Mikoko inaweza kuchukua zaidi ya miaka 15 kukomaa, hivyo ni muhimu kuwe na mpango endelevu wa kuhakikisha jamii inaendelea kuitunza hadi ikue,” anasema Chege.
Mkurugenzi wa shirika la Big Ship Bosco Juma, ambaye amekuwa akijihusisha na uhifadhi wa mikoko kwa zaidi ya miaka 15 katika eneo la Mikindani, anasema shirika hilo limenawiri kupitia juhudi za muda mrefu za jamii.
Anasema kampeni za kuvunja rekodi ni muhimu katika kujenga hamasa, lakini haziwezi kuchukua nafasi ya uhifadhi endelevu. “Kufanyika kwa jambo lisilo la kawaida kama kuvunja rekodi kunafanya watu wengi wazungumzie uhifadhi wa mikoko. Hiyo ni hatua nzuri, kwa sababu inaongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa mikoko,” anasema.

Anaongeza kuwa wao hufuatilia miche yote inayopandwa kwa kipindi cha kati ya miezi mitatu hadi mitano ili kuhakikisha inastawi.
“Mikoko ikitunzwa vizuri hukua kwa haraka. Baada ya takriban miaka mitatu hadi minne huanza kutoa mbegu na maua, kulingana na aina ya mikoko. Lakini kwa mikoko kukomaa ni miaka 15 na zaidi,” anasema Bosco.
Bosco anadai kwamba mikoko iliyopandwa pwani ya Kenya hivi karibuni, na kutambuliwa kimataifa huenda isifikie kiwango cha asilimia 100 ya uhai. Anatoa makadirio kuwa kiwango cha miche itakayonusurika kinaweza kuwa chini ya asilimia 50, kutokana na kutozingatiwa kwa masuala muhimu ya kiufundi na upangaji kabla ya upanzi katika shughuli za urejeshaji wa mikoko, ikiwemo muda wa upanzi na mtiririko wa maji katika eneo husika, na aina ya udongo.
Bosco anaamini kuwa waliopewa jukumu la kupanga hawakuwashirikisha vya kutosha wataalamu wa uhifadhi, watafiti na jamii zinazoishi katika maeneo jirani ili kupata ushauri wa kiufundi kuhusu urejeshaji wa mikoko.
Pia anasema: “Fedha nyingi hutumika kupanga kampeni za kuvunja rekodi. Kama sehemu ya fedha hizo ingewekezwa kwa vikundi vya jamii vinavyofanya kazi za uhifadhi kila siku, matokeo yangekuwa makubwa zaidi”.
Mongabay haikubaini kiasi cha fedha kilichotumika katika tukio hilo la Julai 26, kwani M-Pesa Foundation haijaweka hadharani bajeti au gharama za tukio hilo. Tukio hilo lililenga zaidi ushiriki mkubwa wa jamii kuliko kuweka wazi gharama za kifedha.
Mikoko ina manufaa zaidi
Mbali na kulinda fukwe dhidi ya mmomonyoko na kuwa mazalia ya samaki na viumbe wengine wa baharini, misitu ya mikoko ina mchango mkubwa katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kunasa na kuhifadhi kaboni. Kwa mujibu wa National Ocean Service, “tafiti za sasa zinaonyesha kuwa mikoko na maeneo oevu ya pwani hunasa na kuhifadhi kaboni kwa kiwango kinachozidi mara 10 kwa mwaka ikilinganishwa na misitu ya kitropiki iliyokomaa.
“Pia, huhifadhi kaboni mara tatu hadi tano zaidi kwa eneo lenye ukubwa sawa kuliko misitu ya kitropiki. Sehemu kubwa ya kaboni ya buluu ya pwani huhifadhiwa kwenye udongo, badala ya kuhifadhiwa katika sehemu za mimea zilizo juu ya ardhi, kama ilivyo kwa misitu ya kitropiki”.
Tafiti za Global Mangrove Alliance zinaonesha kuwa mikoko huanza kufyonza kaboni tangu inapopandwa, ingawa kiwango hicho huongezeka kadri mti unavyokua na kukomaa. Zaidi ya hayo, pia hutoa bidhaa kama mbao, miti ya kujengea, kuni na malighafi nyingine.
Miche inayopandwa itaishi kwa muda gani?
Duniani, tafiti zinazotajwa na wataalamu wa urejeshaji wa mikoko, ikiwemo WWF, Wetlands International na machapisho kadhaa, kila moja kivyake, zinaonyesha kuwa hadi asilimia 80 ya miche inayopandwa bila kuzingatia miongozo bora ya urejeshaji huenda ikakosa kustawi.

Habari njema ni kwamba mikoko duniani inaanza kurejea baada ya miongo kadhaa ya kupungua. Utafiti uliochapishwa katika jarida la Science mwaka 2026, “Unexpected expansion and regrowth in Earth’s mangrove forests over the past four decades,” ulioongozwa na Zhen Zhang na Nicholas J. Murray, unaonyesha kuwa maeneo ya mikoko duniani yalianza kuongezeka baada ya takribani mwaka 2010, baada ya miongo kadhaa ya kupungua.
Kati ya mwaka 2010 na 2023, eneo la mikoko duniani liliongezeka kwa takribani kilomita za mraba 2,033, huku upanuzi wa asili kuelekea maeneo mapya ya pwani ukiwa chanzo kikuu cha ongezeko hilo.
Chini Kenya, licha ya juhudi nyingi za urejeshaji wa misitu ya mikoko, changamoto sasa ni kuhakikisha ile iliyopandwa inastawi na kurejesha mfumo wa ikolojia. Wakati rekodi zinahamasisha umma, hatua inayofuata baada ya sherehe na wapiga picha kuondoka ndiyo itakayoamua kama miche hiyo itageuka kuwa msitu wa mikoko unaotoa manufaa kwa mazingira na jamii.
Picha ya bango: Emmanuel Karisa akiwa na jamii wakipanda mikoko. Picha na Amina Chombo, Mongabay.
Nukuu
National Mangrove Ecosystem Restoration Guidelines 2025. https://www.kenyaforestservice.org/wp-content/uploads/2025/07/national-mangrove-ecosystem-restoration-guidelines.pdf
Mwongozo wa Kitaifa wa Urejeshaji wa Mfumo wa Ikolojia wa Mikoko (2026). https://wwfke.awsassets.panda.org/downloads/national-mangrove-ecosytem-restoration-guidlines-popular-version-english-kiswahili-a5_1.pdf
Global Mangrove Alliance, Best Practice Guidelines for Mangrove Restoration. Best Practice Guidelines for Mangrove Restoration
Urejeshwaji wa mikoko Bagamoyo waongeza kasi licha ya ukosefu wa takwimu