- Washitakiwa waliwasilisha hoja nane kupinga hatia na adhabu.
- Washitakiwa walifikishwa mahakamani mwaka mmoja baada ya kukamatwa.
- Upande wa mashitaka ulipinga rufaa na hoja za washitakiwa.
- Jaji asema upande wa mashitaka haukudumisha mnyororo wa utunzaji wa vielelezo .
Watu wanne, Jastine Balali na wenzake watatu waliotiwa hatiani kwa kukutwa na nyara za Serikali lakini wakapinga hukumu hiyo kwa kukata rufaa, wameshinda rufani baada ya Mahakama kukubali hoja zao kwamba kulikuwa na mapungufu makubwa kwenye mnyororo wa utunzaji vielelezo na walifikishwa mahakamani zaidi ya mwaka mmoja tangu walipokamatwa.
Washitakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na makosa mawili; kumiliki kinyume cha sheria nyara za Serikali, likihusisha vipande 450 vya nyama ya kiboko vilivyodaiwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani 1,500 pamoja na kumiliki silaha ndani ya hifadhi bila kibali.
Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro mbele ya Jaji Aisha Sinda baada ya kusikiliza rufani iliyotokana na kesi ya Uhujumu Uchumi namba 31.2022 iliyokuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kilombero, Ifakara.
Licha ya Balali, warufani wengine ni Mohammed Mekuso, John Nyange na Gabriel Emmanuel na wajibu rufani ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, tukio hilo lilitokea Juni 21, 2021, katika eneo la Mpanga, ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Wilaya ya Kilombero.
Mahakama ilielezwa kuwa askari wa uhifadhi walipokuwa wakifanya kazi ya kuweka mipaka kati ya vijiji na hifadhi walikutana na watu sita waliokuwa wakivuta baiskeli ya kubeba mizigo.

Watu hao walikamatwa na baada ya kupekuliwa, inadaiwa walikutwa na nyama ya kiboko pamoja na visu viwili vya porini, mshale mmoja pamoja na baiskeli tatu.
Utetezi wa washitakiwa
Washitakiwa walikanusha mashitaka yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka. Bilali licha ya kukiri kwamba alikamatwa na askari wa uhifadhi, akiwemo shahidi wa kwanza (PW1), wakati akirejea nyumbani kutoka Kikandekande alipokuwa amekwenda kukusanya mkaa, lakini alikanusha kwamba alikamatwa ndani ya Hifadhi ya Taifa. Pia alikanusha kuhojiwa na PW4 au kukutwa akiwa na nyama ya kiboko.
Alieleza kuwa alikamatwa akiwa peke yake na kwamba hati ya ukamataji ilisainiwa Udzungwa badala ya eneo ambalo tukio hilo lilidaiwa kutokea. Alidai kwamba kukamatwa kwake kulitokana na kinyongo kati yake na PW2, ambaye alisema alikasirika baada ya Balali kukataa kumpa mkaa.
Mshitakiwa wa pili, Mekuso alidai alikamatwa na PW1 wakati akirejea nyumbani kutoka Kikandekande aliko kwenda kukusanya mkaa. Hata hivyo alikanusha kukutwa akiwa na mzigo huo na kudai kwamba alilazimishwa kusaini hati ya ukamataji. Pia alipinga utambuzi uliofanywa na PW3 kuhusu nyama hiyo, akidai kuwa utambuzi huo ulifanyika bila kutumia vifaa vya kisayansi.
Mshitakiwa wa tatu, John Nyange alikanusha kuhojiwa. Pia alikanusha kukamatwa ndani ya Hifadhi ya Taifa, akisema alikamatwa eneo linalojulikana kama Kadenge. Mshitakiwa wa nne, Gabriel Emmanuel maarufu kama Yakobo, alieleza kwamba alikamatwa na askari wa uhifadhi Juni 21, 2021, wakati akirejea nyumbani baada ya kukata kuni.
Alikanusha kukutwa akiwa na mzigo uliokuwa na nyama ya kiboko na kudai kwamba alilazimishwa kusaini hati ya ukamataji. Mahakama ya Wilaya ya Kilombero baada ya usikilizwaji iliwatia hatiani na kuwahukumu kifungo cha miaka 20 jela.
Washitakiwa walipinga hatia na adhabu , waliwasilisha rufani wenyewe bila uwakilishi wa Wakili, wakiwa na hoja nane, zikiwemo kupinga uhalali wa ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), mnyororo wa utunzaji wa vielelezo, kucheleweshwa kufikishwa mahakamani, tofauti kati ya idadi ya watu waliokamatwa na waliotiwa hatiani, pamoja na madai ya kuwepo kwa utata katika ushahidi wa mashahidi wa Serikali.
Wakili wa Jamhuri
Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Daniel Makallo ambaye alipinga rufaa hiyo na kutoa ufafanuzi kuhusu mnyororo wa utunzaji vielelezo. Alisema ingawa PW1 na PW5 hawakueleza moja kwa moja nyara hizo zilikabidhiwa kwa nani, PW3, katika mwenendo wa kesi, alitoa ushahidi akithibitisha kwamba alipokea nyara hizo kutoka kwa Sajenti Charles (PW5) kwa ajili ya kuzitambua na kuzithaminisha.

Alisema upande wa mashtaka ulifanikiwa kuthibitisha chain of custody kupitia ushahidi wa PW1, aliyekamata vielelezo, PW2, shahidi huru wa ukamataji, PW3, aliyefanya utambuzi na kuthamini nyara,PW5, aliyewapokea washitakiwa pamoja na nyara zilizokamatwa na PW6, aliyeagiza nyara hizo zitupwe.
Alisisitiza kwamba hakukuwa na ushahidi wowote ulioonyesha kuwa nyara hizo ziliingiliwa au kubadilishwa. Kuhusu kuchelewa kuwafikisha washitakiwa mahakamani, Wakili wa Serikali Makallo alikiri kwamba washtakiwa walipelekwa mahakamani baada ya muda uliowekwa kisheria.
Uamuzi wa jaji
Katika uamuzi wake, Jaji Sinda alisema upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mnyororo wa utunzaji wa vielelezo kuanzia vilipokamatwa hadi vilipowasilishwa mahakamani.
Mahakama ilibaini kuwa shahidi wa kwanza (PW1), alieleza kuwa baada ya kuwakamata washtakiwa aliwapeleka katika Kituo cha Polisi Ifakara pamoja na vitu vilivyokamatwa, lakini hakueleza ni nani aliyebaki na vielelezo hivyo, vilihifadhiwa wapi na vilifikaje hatua ya kuwasilishwa mahakamani.
Kwa upande wake, PW5 pia hakueleza kama PW1 alimkabidhi washtakiwa au vielelezo hivyo, wala hakumtaja askari aliyekuwa na jukumu la kuhifadhi vielelezo baada ya kukamatwa.
Jaji Sinda alisema hakukuwa na nyaraka muhimu, kama daftari la vielelezo, linaloonyesha namna umiliki wa vielelezo hivyo ulivyohamishwa kutoka kwa askari mmoja kwenda kwa mwingine. “Mnyororo wa utunzaji wa vielelezo haukudumishwa na upande wa mashtaka,” alisema Jaji Sinda.
Alisema umuhimu wa mnyororo huo ni kuhakikisha kuwa kitu kinachowasilishwa mahakamani ndicho kilekile kilichokamatwa kutoka kwa mshtakiwa, hivyo kuondoa uwezekano wa kubadilishwa au kuchezewa.
Jaji Sinda alisema Mahakama ilibaini kuwa washitakiwa hawakufikishwa mahakamani ndani ya muda wa saa 48 uliowekwa na Kifungu cha 29(1) cha Sheria ya Udhibiti wa Uhalifu wa Kiuchumi na Kupangwa (EOCCA).
Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi, washtakiwa walikamatwa Juni 21, 2021, lakini walifikishwa mahakamani Julai 5, 2022, ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja baada ya kukamatwa.
Alisema upande wa Serikali ulidai kuwa ucheleweshaji huo ulisababishwa na jalada la uchunguzi kupelekwa kwa mwendesha mashtaka kwa ajili ya uchunguzi wa kisheria.
“Kupelekwa kwa jalada kwa mwendesha mashtaka kwa ajili ya kulipitia hakutoshi kuwa sababu ya kuridhisha ya kushindwa kuwafikisha washtakiwa mahakamani ndani ya muda uliowekwa kisheria,” alisema Jaji.
“Ucheleweshaji huo ulipaswa kuangaliwa pamoja na mapungufu mengine yaliyobainika katika ushahidi wa upande wa mashtaka, jambo ambalo liliongeza mashaka kuhusu uaminifu wa ushahidi uliotolewa dhidi ya washtakiwa,”alisema Jaji.
Hata hivyo, baada ya kuridhika kuwa rufaa imefanikiwa katika sababu ya pili na ya tatu, Mahakama ilisema haikuwa na ulazima wa kuendelea kuamua sababu tano zilizobaki.
Kuhusu sababu ya kwanza, Mahakama ilikataa hoja ya washitakiwa kwamba ridhaa na cheti cha DPP vilikuwa batili kwa sababu havikutaja majina ya makosa yaliyowakabili.
Jaji Sinda alisema ingawa majina ya makosa hayakuandikwa moja kwa moja katika nyaraka hizo, vifungu vya sheria vilivyotajwa vilikuwa vinaweka msingi wa kisheria wa makosa yaliyokuwa kwenye hati ya mashtaka.
Alisema hakukuwa na kasoro iliyobatilisha mamlaka ya Mahakama ya Wilaya kusikiliza kesi hiyo. “Mahakama Kuu inatengua hukumu za hatia na adhabu zilizotolewa dhidi ya washtakiwa katika kesi hiyo na kuamuru waachiwe huru mara moja, isipokuwa kama wanaendelea kushikiliwa kwa sababu nyingine halali kisheria,”alisema Jaji Sinda.
Picha ya Bango: Mwingiliano kati ya wanadamu na wanyama kuna wakati unaweza kusababisha madhara kwa pande zote mbili. Katika taarifa iliyochapishwa na gazeti la Mwananchi ilidaiwa kuwa kiboko aliingia kwenye makazi ya watu, na kujeruhi mtu mmoja katika Kijiji cha Mgonji. Picha kutoka kwenye mtandao wa gazeti la Mwananchi.