- Wanawake wa Vanga wana nafasi muhimu katika biashara ya dagaa, kuanzia kuchemsha na kukaushwa hadi kusafirisha na kuuza samaki hao katika maeneo mbalimbali.
- Biashara ya dagaa huwasaidia wanawake kulisha familia, kulipia elimu ya watoto na kuajiri wengine, licha ya changamoto za kupata mtaji na vifaa bora vya kukaushia.
- Dagaa ni chanzo muhimu cha chakula na virutubishi kwa jamii za pwani, huku pia wakiwa sehemu muhimu ya mfumo wa ikolojia wa bahari.
- Wanawake wa Vanga pia wanashiriki katika uhifadhi wa mazingira kwa kupanda mikoko, kusafisha fukwe na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa bahari.
KWALE, Kenya – Wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali za dunia walipokongamana mjini Mombasa wakati wa Our Ocean Conference, suala la nafasi ya wanawake kama uti wa mgongo wa sekta ya bahari na uvuvi lilijitokeza pakubwa. Hii ilibainika huku utafiti kutoka WorldFish ukionyesha kuwa barani Afrika, asilimia 90 ya wanawake katika sekta ya uvuvi na ufugaji samaki wameajiriwa katika shughuli za uvunaji na uhifadhi wa samaki baada ya kuvuliwa.

Kwa baadhi ya wanawake katika kijiji cha Vanga, hili ni jambo la kawaida. Wengi wao wanajihusisha na biashara ya dagaa, ambapo kila asubuhi hukusanyika katika ufuo wa Vanga wakisubiri boti kutoka baharini. Wanawake hao huchukua dagaa hao kuwachemsha, kuwakausha na kuwauza katika sehemu mbalimbali nchini Kenya na nje ya nchi. Miongoni mwa dagaa hao ni katashingo (Sardinella neglecta), kimalawari (Stolephorus indicus) na simsimu (ecapterus macrosoma).
Kama wanawake wengine Vanga, Mwanakombo Shee alianza biashara yake takriban miaka nane iliyopita. Mtaji wake ulikuwa KSh10,000 ($77.36) ambao alipata kupitia chama cha kuweka na kukopa alichokuwa mwanachama pamoja na wenzake.
“Nilianza biashara hii nilipoona wenzangu kule Jimbo wakifanya biashara,” anasema Mwanakombo.
Sauda Hassan, mfanyabiashara wa dagaa kwa mwaka 10 sasa, na ambaye ni mwenyeji wa Jimbo, hakumbuki kiasi halisi cha mtaji wake. Hata hivyo, ni kupitia chama na akiba yake kidogo kidogo ambapo aliweza kuanzisha biashara yake. Biashara hii imemuwezesha kulipa karo ya shule na madrasa kwa watoto wake.
“Sikumbuki ni pesa ngapi lakini tulifanya mradi wa mikoko nikapata pesa, nikaongeza na zangu nyengine kidogo kidogo,” anakumbuka Sauda.
Kwa wanawake hawa, KSh10,000 ni mtaji muhimu, hasa kwa kuwa mara nyingi hawana taasisi rasmi kama benki au vyama vya kuweka na kukopa (SACCOs) vya kuwapatia mikopo.
Utafiti wa Umoja wa Mataifa uliochapishwa mwaka 2023 unaonyesha kuwa wanawake hutegemea biashara ya dagaa kulisha familia zao, kusomesha watoto wao na hata kuajiri wengine. Hata hivyo, wengi wao huachwa nje ya mfumo wa kupata fedha za kutosha za kuendeleza biashara zao.

Licha ya kwamba wanaume ndio wavuvi wa dagaa katika sehemu hiyo, wanawake ndio hushughulika kwa kiasi kikubwa na hatua za kuhakikisha samaki hao wanahifadhiwa salama na hawaharibiki.
Ferunzi Mohammed, mwanaharakati wa masuala ya mazingira jijini Vanga, anasifia nafasi muhimu ya wanawake katika usindikaji wa dagaa Vanga.
“Dagaa hao ni sehemu muhimu ya jamii ya Vanga, na wanawake ndio wana mchango mkubwa katika kuwahifadhi,” anasema.
Biashara ya dagaa inahusisha watu wengi Vanga, kutoka kwa wavuvi wanaowavua, wanawake wanaowatayarisha kwa kuwachemsha na kuwakausha, hadi vijana wanaowasafirisha na kuwabeba hadi maeneo mbalimbali. Dagaa kutoka Vanga hutumika kama kitoweo katika sehemu mbalimbali Pwani, katika maeneo kama Mombasa na Kilifi, na hata maeneo ya bara nchini Kenya. Pia husafirishwa hadi nchi za Rwanda na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo.
Faida za dagaa
Dagaa ni samaki wadogo wenye umuhimu mkubwa katika pwani ya Kenya. Wao ni chakula cha samaki wakubwa baharini, na pia ni chanzo muhimu cha chakula cha binadamu. Dagaa wana virutubishi muhimu na ni kitoweo cha aina yake kwa jamii zinazoishi pwani. Wataalamu wa bahari wanasema kuwa samaki hawa ni muhimu, si kwa usalama wa chakula tu, bali hata kwa mfumo wa ikolojia.
Prof Cosmas Munga, mwanasayansi wa masuala ya bahari na samaki, anasema kuwa dagaa wana virutubishi muhimu, ikiwemo asidi za mafuta aina ya omega-3, na viwango vya zebaki huwa chini ikilinganishwa na baadhi ya samaki wakubwa.
“Dagaa ni samaki wadogo, lakini wana virutubishi muhimu sana, viwango vya zebaki ni vya chini sana ukilinganisha na samaki wengine wakubwa,” anaielezea Mongabay.
Munga anasema yeye na wenzake wanaendelea na utafiti kuhusu jamii hiyo ya samaki, kwa kuwa tafiti kuhusu samaki hao katika Bahari ya Hindi ya Magharibi ni chache kwa sababu samaki hao huhamahama sana. Pia ni samaki wa msimu, hivyo basi kufanya utafiti wa muda mrefu huwa vigumu.
Hata hivyo, mabadiliko katika mazingira ya bahari yanaweza kuathiri mwani huo, ambao ni chakula cha dagaa, na hivyo kuathiri pia idadi ya dagaa.

Mabadiliko ya hali ya hewa pia yanaweza kuwaathiri wanawake hao. Wanasema wanakabiliwa na mvua zisizotabirika, jambo ambalo huathiri ukaushaji wa dagaa wao. Sauda anasema, “Wakati mmoja nilipata hasara baada ya dagaa wangu kuharibika walipokosa kukauka vizuri.”
Licha ya kwamba misimu haifanani, siku za nyuma, wanasema, walikuwa wakipata dagaa wengi kuliko sasa. “Miaka mitano nyuma hivi nilikuwa napata hata kilo 200. Lakini sasa huenda hata kilo 80 usifikishe,” ameongeza Sauda.
Bila vifaa maalum vya kukaushia, hawawezi kuepuka uharibifu kama huo. Sauda anasema kuwa walipata ufadhili wa kujenga sehemu za kukaushia dagaa. Hata hivyo, ziliharibika na pia hazikuwa za kisasa. Sasa hawana uwezo wa kununua vifaa vipya kwa sababu hawana mtaji wa kutosha.
Umuhimu wa kulinda mazingira
Wakitambua umuhimu wa kulinda mazingira ili kuendeleza biashara zao, wanachangia kuhifadhi mikoko katika maeneo yao. Wanawake hao hujishughulisha na kupanda mikoko, kusafisha fukwe za bahari na pia kuelimisha wenzao kuhusu umuhimu wa mazingira na bahari.
Hata hivyo, juhudi hizi si za wanawake wa Vanga pekee, bali zinaakisi baadhi ya juhudi zinazofanywa na wanawake katika sekta ya uvuvi na bahari.
Shamim Wasii Nyanda kutoka Hatch Blue Afrika anasema kuwa wanawake wengi barani Afrika tayari wanafanya biashara katika sekta ya uvuvi na bahari. “Biashara hizi zina mchango muhimu katika kuunda ajira, kuboresha usalama wa chakula na lishe, na kubadilisha jinsi biashara za baharini zinavyoendeshwa. Hata hivyo changamoto kuu ni kujiendeleza, kufikia na kusalia katika nyadhifa za juu za uongozi, na hata kupata mtaji zaidi wa kupanua biashara zao,” anasema Wasii.

Anaongeza kuwa iwapo masuala haya yatazingatiwa, wanawake wataweza kujua sehemu za kupata mtaji wa kuanzisha biashara zao ili waweze kujiboresha. “Hatua hii itaongeza usalama wa chakula, kutoa ajira zaidi na pia kuhakikisha wanawake wanapewa kipaumbele katika sekta ya bahari”.
Astrid Bergmål, katibu wa maendeleo ya kimataifa nchini Norway, anasema kuwa ni wakati sasa wa wanawake kuwa mstari wa mbele katika masuala ya bahari. “Badala ya kuangazia wanawake kama walinzi tu, ni muhimu wawe viongozi na washirikishwe tangu mwanzo wa shughuli yoyote,” anafafanua.
Picha ya bango: Boti zikiwa katika ufuo wa Vanga. Picha na Asha Bekidusa, Mongabay.